Monday, September 30, 2013

JUMATATU HII YA MWISHO WA MWEZI HUU WA TISA INATUKUMBUSHA AFRIKA....TANZAN IA NA MALIASILI YAKE...MBUGA!!!


Nawatakieni wote mwanzo mwema wa wiki hii. Binasi  nina furaha isiyo kifani leo kwani rafiki yangu mpendwa tumeongea leo..tulikuwa tumepoteana miezi kadhaa. AHSANTE MUNGU KWA HILI.

Friday, September 27, 2013

LEO NAPENDA NIWAPELEKE MPAKA NYUMBANI KWETU LITUMBAND´YOSI ..HAPA NI SHULE YA MSINGI AMBAYO MDADA MIMI NIMEWAHI KUSOMA ...

SHULE YA MSINGI LITUMBAND´YOSI
Leo nimekumbuka sana nyumbani yaani kule alikozaliwa baba yangu ndiko kwa mimi ni nyumbani kwangu....Nikakumbuka shuleni  hapa jinsi tulivyokuwa tukikutana shule nne kwa mashindano ya Kililupa..ikiwa na mana shule ya msingi Kingoli, Litumband´yosi,  Luhagara na Paradiso. Ilikuwa ni michezo ya kata. Najua wengi mliosoma shule hizi nayi mtakumbuka jinsi ilivyokuwa....Nawatakieni wote Mwanzo mwema wa mwisho wa wiki

Thursday, September 26, 2013

NIMELAZIMIKA KUVUNA NYANYA ZANGU KWA AJILI YA BARIDI KUWAHI MAPEMA KULIKO MATARAJIO YANGU....

 Hizi ni nyanya zangu ambazo zilikuwa bado kuiva kama mnavyoona ...nimeamka leo asubuhi  nimeshikwa na butwaa nyasi zote zilikuwa nyeupe theruji  kabisa kitu ambacho zikutarajia kwa haraka hivi. Kwa hiyo imenibidi kuzivuna kabla hazijaharibika sana na kuzihifadhi. Vipi SIJUI kwa kweli..Je nikizihifadhi kwenye boxi zitaiva? Maana hapa ni nusu ya tulizokula....
Hahahaaa:-)  na nikaamua nivune tu na vitunguu vilivyobakia ...mkulima wa ajabu anaanza kula kabla hajavuna na sasa vimebaki sita (6) tu....KARIBUNI KUNISAIDIA KULA NYANYA HIZO!!!

Wednesday, September 25, 2013

MSIFIKIRI NIMEPOTEA NIPO ILA MAJUKUMU YANAFANYA NIADIMIKE

....Nitarudi muda si mrefu kuwa nanyi, tena labda kesho tu......nawatakieni wote kila la kheri panapo majaliwa tutaonana kesho.  Kapulya

Monday, September 23, 2013

SIMTAKI......UAMUZI MZITO!!!

Leo nimeamaka nikiwa nikiwaza habari ambayo niliwahi kusoma.....Ilikuwa saa 11 jioni. Msichana mmoja kwa jina la Veronika alikuwa akitoka shuleni kwake. Alikuwa kidato cha nne. Alikuwa anaelekea kwenye shule ya Sekondari ya wavulana. Ilimbidi amwone Robert, rafiki yake wa kiume. Veronika alikuwa akifikiri moyoni: "Sina budi kumwona Robert leo. Siwezi kusubiri tena"

Wakati huo huo huo wavulani walikuwa wakitoka shuleni pia. Punde si punde alimwona Robert akitoka katika kikundi cha wavulana wengine akimji. Alikuwa akitabasamu lakini Veronika aliweza kuona kwamba Robert alikuwa na mshangao pia kumwona yeye pale. Kwa kawaida walikuwa wanakutana kwenye stendi ya basi. Na maongezi yaliendelea hivi:-

ROBERT: Habari za jioni  Veronika? Nina furahi kukuona .

VERONIKA: Sijambo, Robert ....ah.....Ninataka kuzungumza nawe. Je? kuna mahali pa faragha shuleni kwako- mahali ambapo tunaweza kukaaa na kuzungumza bila mtu kutubugudha?

Robert alimtazama kwa fadhaa kidogo lakini hakumuuliza zaidi.

ROBERT: Ndiyo, nadhani tunaweza kwenda kule maktaba. Leo ni ijumaa na ni mwanzo wa pumziko la wiki, hatuna masomo. Nina hakika hapatakuwa na mtu.

Veronika alimfuata bila kusema kitu. Waliketi mwishoni kabisa mwa chumba cha maktaba wakimpa kisogo mfanya kazi wa makataba ambaye alikuwa akishughulika na kadi za vitabu.

ROBERT: Kuna matatizo gani Veronika? Mbona unaonekana kuwa na wasiwasi na huzuni?

Veronika alimtazama Robert, halafu aliinamisha kichwa .

ROBERT: Veronika kuna nini? huna budi kuniambia unajua mimi ni rafiki yako. Unahofu nini? labda umeshindwa mrihani wako wa katikati ya muhula?
Veronika: Hapana Robert. Ni kitu kikubwa kuliko hicho.... Ni ...nina mimba.

ROBERT: Nini? Una uhakika?
Robert alishikwa na bumbuwazi. Mawazo mengi yalipita ghafla akilini mwake.

VERONIKA:  Ndiyo, nina hakika. Lakini simtaki. Robert, simtaki mtoto huyu. Wazazi wangu wakisikia juu ya jambo hili hawatanipokea tena nyumbani kwetu. Pia itakuwa ni mwisho wa masomo yangu. Unajua, mwaka kesho ningeanza masomo ya uuguzi.

ROBERT: Najua.....Utafanya nini sasa? Ninaona njia moja tu: Ondelea mbali "kitu" hicho.

Veronika alifikiri:"kitu" hicho ni mtoto. Moyo wake ulikuwa unamwambia kuwa alichokuwa anapanga sasa ni jambo  baya sana. Lakini Veronika hakustahimili ile aibu wala wajibu wa tendo lake. Sasa alikuwa amekata shauri.

VERONIKA: Ninajua nitafanya nini. Nitakwenda kwa rafiki yangu Sarah. Yeye ni muuguzi kule hospitalini. Nitamwomba anipatie dawa ya kuondoa mimba, nina hakika atanisaidia. Hakuna mtu mwingine atakayejua. Hapo maisha yataendelea tena kama mwanzo.
Maneno haya ya mwisho Veronika aliyasema kwa sauti ya kunongóneza. Robert alikuwa ameshika kichwa chake kwa mikono yake miwili naye hakuthubutu kumtazama Veronika. Yeye pia alitambua kuwa anahusika lakini alifikiri: "Kwa kweli, hakuna njia nyingine, au sivyo? Hakujua. Lakini Veronika alikuwa amekwisha amua tayari. Basi, alimuuliza tu....

ROBERT: Utakwenda kumwona rafiki yako lini?

VERONIKA: Kesho......

Inasikitisha kweli kuona jinsi hali hii inavyorudiwa rudiwa mara nyingi siku hizi. Katika namna zoto za maisha kutoa mimba kumekuwa ni jambo la kawaida, jambo linalotokea mara kwa mara. Magazetini huandika kinaganaga jinsi watoto wanavyookotwa kwenye mapipa ya takataka, katika vyoo vya uma, n.k. Kutoa mimba kunaonekana kama njia ya kuondoa kitu kisichotakiwa ; njia ya kusahau kitu ambacho kisingelikuwa kimetokea.....ITAENDELEA......Habari hii nimeipata katika kitabu cha NJIA YETU KWA MAPENDO NA NDOA...



Sunday, September 22, 2013

JUMAPILI NJEMA KWA WOTE!!



Au pia tumsikiliza dada Jennifer Mgendi na wimbo huu Jaribu langu!!

NAWATAKIENI JUMAPINI NJEMA NA YENYE AMANI PIA UPENDO KWA WOTE NA BARAKA ZA MWENYEZI MUNGU ZITAWALE NYUMBANI MWETU/MWENU AU MWAKO...

Friday, September 20, 2013

MNAKUMBUKA NILIWAHI KUWAAMBIA NIMEPANDA DODOKI ? HAPA NI MAENDELEO YAKE!!!!!

 Hicho chungu cha bluu ndio mmea wa dodoki/madodoki mwenyewe umekuwa na umetambaa mpaka kwenye paa ya varanda...sasa leo  nimegundua -----
 Mmea huo umeanza kutoa maua na pia dodoki zimeanza kujitokeza hakika nimefurahi sana. Ila sasa najiuliza nitaumewka wapi maana kaubaridi kameanza na mmea huu unataka joto  ....maana mwisho wako
...ndo dodoki linakuwa hivi hapa tayari lishakomaa na kukauka tayari kwa kujisugulia mwilini. Hili nilinunu Songea Sokoni mwaka huu...Kweli hili hapo juu karibu na ua litakuwa kama hili?...Mwenye ushauri naomba  tafadhali!! Nawatakieni jioni yenye upendo na amani.

TUIANZE IJUMAA/MWISHO WA JUMA NA ZILIPENDWA...


Hakika vya zamani ni vizuri na vinadumu  hizi tulikuwa tukizisikia tangu tupo migongoni wa mama zetu .....Nafurahi zimetunzwa na leo watoto wetu wanaweza kusikiliza...IJUMAA NJEMA KWA WOTE...

Wednesday, September 18, 2013

NILIKUWA NATEGEMEA KULA HAYA MABOGA LEO KUMBE....HAYALIWI .....

Mavuno ya maboga..Nimepata manne na leo nilipanga iwe siku ya kuyala nilitaka kutengeneza supu, kuchemsha na futari. Lakini wifi yangu kaniambia hayaliwi eti ni chakula cha nguruwe tu na yeye ndiye alinipa mbegu. Sasa hapa najiuliza kama nguruwe anakula na kupona kwanini binadamu asile...Kuyatunza kwote nilikofanya yaani ni kazi ya cheka bure kweli???,,Na ndo nikaamua niwaulize ndugu zanguni je ni kweli?...Maana majani yake yana  mibamiba zikukuchoma zinawasha na majani ni mapana kuliko ile mboga ya maboga ya Njombe na ile ya kawaida...Au sijui ni mabuyu/ yale ya kutekea maji au kunywea maji yaani kata?...Duh kaaaazi kwelikweli hapa sasa nimekwama inabidi nianza upya kuwaza cha kula:-(.

Tuesday, September 17, 2013

UJUMBE /SWALI WA/LA LEO!!!

Kama huwezi kujisamehe mwenyewe na uliyoyafanya, utawezaje kuwasamehe wengine?
NAWATAKIENI WOTE JUMANNE NJEMA SANA NA KUMBUKENI TUPO PAMOJA DAIMA!!!Kapulya!

Friday, September 13, 2013

MDADA KAPULYA SI MTU WA KUTULIA ..MSIMU WA BUSTANI UNAKARIBIA KWISHA NA SASA WAJA MSIMU KUCHUMA UYOGA NAYE NI MPENZI SANA WA KAZI HII KWA HIYO LEO ALIKWENDA MSTUNI NA HAPA NI MATOKEO YAKE....

 Kuchuma uyoga ni kitu ambacho nakipenda sana , unakuwa na wakati mzuri wa kutafakari, pia mazoezi nahalafu unapata mboga ..Mboga hii mimi nimeipata bure leo mstuni lakini kama ningekwenda kuinunua dukani kwa kilo ni kama kwa kila shilinga 23000/= . Nami nilipata lita kama tano hivi. Sasa kazi nyingine unaporudi nyumbani ni kuusafisha na ndio hapo nafanya kutoa mchanga na takataka nyingine,,,,
 Baada ya masaa matatu uyoga tayari umetolewa takataka zote na upo safi kwa kuliwa.....
 ...Uyoga upo kwenye plain pan tayari kwa kuandaliwa kwa ajili ya mlo wa jioni......
 .....baada ya dakika tano umepungua kiasi hiki na maji mengi yamejitokeza ..naendelea kukausha maji...
 ---Maji yamekakamia na hapa sasa ni kuweka chumvi, sukari kiduchu kwa ajili ya ladha..na pilipili manga kidogo na kikubwa zaidi siagi kama kijiko kimoja cha mezani unakaanga kwa dakika kumi....
 ...baada ya hapo unaweka krimu ya maziwa na kama huna krimu basi weka unga wa ngano kijiko kimoja cha mezani na maziwa kikombe cha chai,,,,
Na mwisho mlo ukapatikana hivi:- Wali, kuku, uyoga uloungwa kama nilivyosema hapo juu  ikiwa na nyanya kutoka bustanini  kwetu, tango na majani ya ruccula. Na hivi ndivyo ilivyoisha IJUMAA YA KAPULYA na mpishi ni YEYE MWENYEWE KAPULYA:-) TUTAONANA TENA PANAPO MAJALIWA !!

IJUMAA YA LEO NIMEFIKA HADI IRINGA NA NIMEONA NIWAONYESHE KILE NILICHOKIONA NA KUKIFURAHIA:- NGOMA YA ASILI YA WAHEHE/WABENA KARIBUNI!!!


NAPENDA KUWATAKIEWNI WOTE IJUMAA NJEMA NA KUMBUKENI TUPO PAMOJA. Kachiki upu nawe mtani wangu Fadhy na wengine wote jiungeni nasi najua kaka S na  dada mkuu msaidizi mnakumbuka kitu hapa...

Wednesday, September 11, 2013

KATIKA MAISHA NI VIZURI KUWAFARIJI MWENYE MATATIZO

Huu ni ushauri wangu mimi kwa wewe uliye na rafiki aliye na matatizo:-

1) Kama rafiki yako ana matatizo usiogope kumwuuliza hali yake kwa ujumla hata kama hali yake inaonekana si nzuri. Kama una matatizo halafu watu/marafiki wanakuuliza U HALI GANI utajisikia amani yaani kuna watu ambao wanakujali haupo peke yako.

Wakati mwingine kunatokea mambo ambayo si kweli na watu wanafikiri kuwa tayari yule mwenye matatizo amepata msaada mtu wa kuongea naye, wakati kumbe wewe upo peke yako kwa hiyo kuuliza ni muhimu sana.

2) Piga simu au nenda ili kujua mpatwa matatizo ana hali gani. Pia pika chakula, nenda kwake na mle pamoja. Wakati matatizo yanapotokea, inakuwa ngumu kuelezea vitu ulivyozoea kufanya kila siku. Kama una watoto inakuwa ngumu zaidi kuwatunza wakati upo kwenye matatizo/majonzi.

3) Onyesha upendo wako, bila kuonekana ni usumbufu kwa mpatwa matatizo, uwe nusu nusu. Usizidishe au usipunguze. HAPO NDIPO UTAWEZA. ......Huu ni mtazamo na ushauri wangu ...PAMOJA DAIMA,.

Monday, September 9, 2013

PALE INAPOFIKIA MSIMU WA BUSTANI KUVUNA/KWISHAKWISHA KWANI MSIMU WA BARIDI UNAKARIBIA SASA

 Hapa ni maboga yanakaribiwa kuwa makubwa na tayari kwa kuliwa..kwa uzowefu wangu inabidi yawe na rangi ya njano kidogo ili kujua yamekoma ..ila sijui ni kweli naomba ushauri wenu....
 Hapa ni mboga ya maboga mnaona inakaribia kufa/ kwisha ila nimekula sana na akiba nimeweka kwa hiyo karibuni sana .
 Nyaya ndo bado, zinaendelea kuiva  kila siku ila nasikitika  sina sehemu ya kuzihifadhi hapo baridi itakapozidi
 Mchicha nao umechokachoka na pia umeanza kuchanua na hapo ndipo nitakapopata mbegu za mwakani ila sijui kama zitawahi kukauka...Je naweza kuzitoa kabla ya kukauka na kuhifadhi sehemu ..akina bwana shamba na wataalamu naomba ushauri....
 Na hapa ni ile figiri niliyowaambia nitapanda nyingine imekuwa kufikia hapa. Ni kwamba natumia ujanja wa kufunika na kitambaa fulani chembesi sana ili wale viwavi jeshi wasile na naona inakuwa vizuri. Kwa figiri huwa inavumilia sana baridi maana hizi mbegu nimepata Njombe na baridi ya Njombe ni sawa na hapa mwanzono mwanzoni....
 Kapulya si mpenzi wa kulima bustani za mboga tu ni mpenzi wa bustani wa maua na maua ya kupanda kwenye makopo...Ua hili huwa linanikumbusha shule nyingi za msingi na secondary nyumbani Tanzania.

Hapa pia ni ua ambalo nimelitunza na limenipita hadi urefu mimi mwenyewe ..mnaona kazi hiyo...hapa huwa nakaa na kutafakari mengiiiii nikiliangalia hili ua.
HAYA NAWATAKIENI WOTE JUMATATU IWE NJEMA NA PIA WOTE MNAPENDWA...KAPULYA WENU

Sunday, September 8, 2013

NAPENDA KUWATAKIENI JUMAPILI NJEMA NDUGU ZANGUNI WOTE!!

Nachukua nafasi hii na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunilinda, kuniongoza, kunifanya nipate chakula, na kuniepesha na yasiyo mema. Nakutumaini wewe Mungu wangu , eh Mungu, wewe ni mwamba imara katika maisha yangu ...... Pia napenda kuwaombea familia, ndugu, wazazi/walezi, marafiki, majirani, wafanyakazi wenzangu pia hata madui zangu. Mwenyezi Mungu na atushushie wote baraka na upendo pia amani ...AMINA. . NA UJUMBE WA LEO NI:- SISI SOTE NI NDUGU,WATOTO WA BABA MMOJA.

Friday, September 6, 2013

NAWATAKIENI WOTE MTAKAOPITA HAPA MWANZO MWEMA WA MWISHO WA JUMA ......SEHEMU FUALANI NDANI YA AFRIKA...



NAWATAKIENI IJUMAA NJEMA NA MWANZO MWEMA WA JUMA TUWE NA AMANI NA KILA LA KHERI KWA KILA KITU TUKIFANYACHO...NA KUMBUKENI WOTE MNAPENDWA....Sisi sote ni ndugu na ni watoto wa baba mmoja ....Kapulya

Wednesday, September 4, 2013

LEO TUANGALIA JIOGRAFI,HISTORIA YA MJI WETU WA SONGEA!!!

Leo tuangalia mji wa SONGEA:-
Songea ni mji nchini Tanzania ambao ni makao makuu ya Mkoa wa Ruvuma. Kulingana na sensa ya mwaka 2002 idadi ya wakazi wake ilihesabika kuwa 131,336. Kuna barabara ya lami kutoka Songea kupitia Njombe hadi barabara kuu ya Dar es Salaam - Mbeya. Barabara ya kwenda pwani kupitia Tunduru na Masasi ni mbaya mara nyingi haipitiki wakati wa vua haswa..ila sasa iko mbioni kutengenezwa...
JIOGRAFIA KIDOGO:-
Mji wa Songea uko kimo cha M 1210 juu ya UB katika nchi ya Ungoni kwenye nyanda za juu za kaskazini za Tanzania. Chanzo cha mtu Ruvuma kipo karibu na mji.
HISTORIA:-
Jina Songea ni kumbukumbu ya chifu Songea wa Wangoni aliyekuwa na ikulu yake hapo wakati wa kuenea kwa wa ukoloni wa Ujerumani akauwawa na Wajerumani wakati wa vita ya majimaji.
Mji wa Songea (iliandikwa Ssongea wakati ule) ulianzishwa mwaka 1897 kama kituo cha kijeshi cha Kijerumani. Ukakua kuwa makao makuu ya utawala wa mkoa wa Songea wa Afrika ya Mashariki ya Kijerumani.
Mazinginra ya mji yaliathiriwa vibaya na vita ya majimaji na ukandamizaji wake na Wajerumani.
Songea ikaendelea kuwa makao makuu ya mkoa wakati wa utawala wa Uingereza katika Tanganyika na baada ya uhuru katika Tanzania huria.....HII NI HISTORIA/GEOGRAFIA YA MJI WA SONGEA...

Tuesday, September 3, 2013

TUSISAHAU METHELI ZETU ZA KISWAHILI....!!!!!

1. Yaliyopita si ndwele, tugange yajayo.
2. Yote yangáayo usidhani ni dhahabu.
3. Ungelijua alacho nyuki, usingelionja asali.
4. Radhi ni bora kuliko mali.
5. Ndugu wakigombana, chukua jembe ukalime, wakipatana chukua kapu ukavune.
NAWATAKIENI JUMANNE NJEMA WOTE NA KAMA UNA METHALI PIA ONGEZEA:-)

Sunday, September 1, 2013

NAWATAKIENI JUMAPILI HII YA 22 YA MWAKA C IWE NJEMA !!

Mdada katoka kanisani hapa
 
Sala ya leo kwa ajili ya kuwaombea watu wote:
Salamu, Maria, umejaa neema, Bwana yu nawe,
umebarikiwa kuliko wanawake wote, na Yesu,
mzao wa tumbo lako amebarikiwa.
Maria mtakatifu, Mama wa Mungu,
utuombee sisi wakosefu, sasa na saa ya kufa kwetu.
Amina.
NA TUSISAHAU KUWAOMBEA JT. YUSTO, INGRID, JN GREGORI MKUU , SOFIA
JO ..ROSALIA, IRMGARD, AL.. ROMULO, ROSWITA...IJ ...MAGNUS, ALEX, JS YIDITH.
TUPO PAMOJA. AMINA

. 

Friday, August 30, 2013

IJUMAA YA LEO TUSIKILIZE ZILIPENDWA ...MAYASA

NAWATAKIENI WOYE MWANZO MWEMA WA MWISHO WA JUMA HILI. NA NAPENDA KUMSHUKURU MWENYEZI MUNGU KWA WEMA WAKE KWA WATU WOTE. ....IJUMAA NJEMA SANA!!

Wednesday, August 28, 2013

PALE WAZAZI WANAPOWACHAGULIA WOTOTO/MABINTI ZAO WACHUMBA!!!

Habari za jioni ndugu zanguni....Hivi karibuni nimetumiwa email kutoka kwa msomaji wa maisha na mafanikio kutoka huko nyumbani Tanzania ikiwa na ujumbe huu na kuniomba kama naweza niuweka hapa kibarazani ...karibu tujadili kwa pamoja
--------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
Kuna mdada mmoja ambaye ni miongoni mwa watu wasomi sana. Amemaliza chuo hapa mlimani. Wakati alipokuwa chuoni alibahatika kupata mchumba ambaye walikubaliana kuoana. Na walikuwa katika maelewano mazuri katika uchumba waoi.

Baada ya uchumba huo kuendelea, aliamua kumpeleka kwa wazazi wake na kuwafahamusha kuwa mimi nimepata mtu ambaye naona atanifaa katika maisha yangu. Baada ya kuwafahamisha jambo hili, mama dada huyo alikubaliana na wazo lake la kutaka kuolewa na huyo mchumba wake lakini upande wa baba yake kulikuwa na shaka. Huyo binti alikuwa karibu sana na baba yake na aligundua kuwa baba yake hataki kukubaliana na wazo lake. Baada ya mazungumzo ya hapa na pale na baadaye mvulani yule kuondoka, binti alimfuata baba na kuzungumza naye na akasema kwa jinsi nilivyomwona huyo mvulana hakufai. Binti akamwambia si vizuri kumhukumu mtu kwa kumwangalia tu. Mimi nimekuwa naye muda mrefu namfahamu vizuri sina shaka naye. Baba yake bado hakukubalina na hilo lakini upande wa mama yake hakukuwa na shida.

Uchumba uliendelea na yule mvulana akasema inaonyesha baba yako hataki kabisha, lakini nitaumia sana endapo kama bado ataendelea na msimamo wake huo. Ni mtu ambaye nimekuzoea, tumeheshimiana sana. Yule binti akamwambia kila kitu kinawezekana na itawezekana tu.

Siku moja yule binti akiwa katika mizunguko yake ya hapa na pale akiwa mjini, alikutana na kaka mmoja akiwa katika mavazi ya kijeshi, na alikuwa na mwonekano mzuri sana, lakini cha kushangaza yule kaka baada ya kumwona binti yule aliduwaa. Baada ya kuduwaa kwa kipindi aliamua kumfuata binti na kumsalimia na kumuuliza kila kitu, na baadaye walianza kuwasiliana mawasiliano ya kawaida kabisa lakini mwanajeshi huyo alikuwa na mawazo tofauti, na ndipo siku moja akamweleza kuwa angetamani siku moja awe mke wake. Yule binti akamwambia hapana, mimi tayari nina mtu wangu na tunaheshimiana sana, akamwambia sawa. Kwa vile  ni watu marafiki alimrudisha mpaka kwao, kumbe lengo lake yule kijana ni kutaka kujua binti anaishi wapi.
Na ndipo siku hiyo yule kijana aliamua kwenda peke yake nyumbani kwa wazazi wa binti huyo na kukutana na baba yake (Baba wa binti). Na ndipo alipozumza ukweli wa kile alichokiona na lengo lake ni lipi. Na mzee aliweza kumdadisi kijana na kumweleza kila kitu. Kwa  wakati huo yule binti pamoja na mama yake walikuwa hawapo na binti aliporudi akamweleza akaelezwa na baba yake kuwa kuna kijana mmoja alikua yuko hivi na hivi akanieleza kila kitu, nadhani huyo ndiye atakayekufaa. Binti akamwambia hapana, wewe ndiye umemwona na mimi itabidi nimwone. Baadaye yule mjeshi akaja wakazungumza.

Baada ya mazungumzo marefu ya hapa na pale yule kijana mjeshi aliamua kuondoka, na kwa kuwa binti hakutaka kukorofishana na baba yake aliamua kukubaliana na mawazo yake na baadaye wakamwita tena kijana huyo mjeshi. Baadaye taratabu zote za kuoana na mjeshi huyo zikafanyika, kisha binti huyo alienda kwa mchumba wake wa kwanza na kumweleza yote yaliyotokea na kumrishia pete ya uchumba waliyovishana hapao awali. Kijana huyo alisikitika sana kwa uamuzi aliouchukua lakini hakuwa na jinsi aliamua kufuata shinikizo la baba yake. Hatimaye baadaye yule binti aliolewa na mwanajeshi na ndoa ilifungwa kanisani.

Baada ya ndoa tu kinachotokea sasa hivi ni kwamba kosa kidogo tu anaambulia kipigo ambacho hajawahi kukipata, kiasi kwamba inampelekea kumkumbuka yule wa kwanza ambaye walikuwa wakiongea naye kwa utaratibu kabisa.

Ndipo baadaye binti (ambaye sasa ni mke wa mwanajeshi) akamtafuta yule mchumba wake wa kwanza na kumweleza kila kilichotokea. Lakini kijana huyo alijaribu kumweleza namna ya kufanya ili waendelee kuishi vizuri na mume wake na kuzidi kumwombea ili waishi vizuri.

Kwa wakati huu kijana huyo bado hajaoa na anamweleza binti itachukua muda mrefu kwa sababu kwanza itabidi nikusahau wewe pili nikae chini nitulie tatu nijianze upya hivyo itachukua muda sana.
Kikubwa zaidi ni kuwa binti huyo amekubali kuolewa na mwanajeshi kwa shinikizo la baba yake, lakini kinachoendelea ni kwamba kosa dogo tu anaambulia kipigo kisicho cha kawaida na kinachomuuma zaidi zaidi huyo dada ni kuwa siku moja walipotoka NJE walienda sehemu ile ile ambayo walikuwa wakienda na mvulana yule wa kwanza na hivyo hii humuuma zaidi.
Sasa dada huyu anaomba mawazo, ushauri na maoni afanyeje???

Tuesday, August 27, 2013

MKWAWA SHUJUA!!

KAMA UNAKUMBUKA DARASA LA TANO WALE WENYE UMRI KAMA WANGU BASI UTAKUMBUKI UKURASA HUU WA KITABU HIKI CHA TUJIFUNZE LUGHA YETU! KITABU CHA SITA(6) KARIBU UKUMBUSHIE ENZI HIZOOOO
 
Hapo zamani palikuwa na mzee aliitwa Muyugumba. Mzee huyo alikuwa mtemi wa Wahehe. Alikuwa akipendwa sana na watu wake.

Mtemi Muyugumba alikuwa na watoto wengi. Wawili kati yao walikuwa Mkwawa na Muhenga. Siku moja aliwaita watoto hao wawili ili kuzungumza nao. Walipofika aliwaambia, "Wanangu, nimewaiteni usiku huu huu wa leo niwaeleze habari muhimu sana. Kwanza, mnajua kwamba mimi nimekuwa mtemi wa nchi hii kwa muda mrefu. Nimeweza kuwaunganisha watu wangu mpaka tumekuwa na kauli moja. Kwa ajili ya umoja wetu, tumeweza kuwashinda maaduni wetu. Tumeweza kuhifadhi uhuru wetu. Sasa mimi ni mzee. Nguvu zinaanza kumalizika taratibu. Nimetazama katika watoto wangu wote sikumwona ambaye ataweza kuendesha kazi yangu ila ninyi. Hivyo leo nimewaita kuwapeni usia wangu.

"Mimi karibuni nitakufa. Nitakapokufa nanyi mtaitawala nchi hii. Kwa hiyo, wewe Mkwawa utakuwa mtemi wa Kaskazini; nawe Muhenga utakuwa mtemi wa Kusini ya Iringa. Ninaigawa nchi sehemu mbili ili kazi yenu iwe rahisi. Jambo kubwa ninalotaka mlikumbuke wakati wotw ni kudumisha uhuru, heshima na umoja katika nchi ya Uhehe. Msiposhirikiana hamtaweza kufanikiwa; na kazi yenu itakuwa ngumu sana." Mkwawa na Muhenga wakajibu wote kwa pamoja, "Asante baba. Tutafanya kama ulivyotuagiza."

Haukupita muda mrefu, Mtemi Muyugumba akashikwa na ugonjwa, akafa. Wahehe wakawa na huzuni sana kwani walimpenda sana kiongozi wao. Matanga yalipokwisha Mkwawa aliwekwa kuwa mtemi wa kaskazini ya Iringa na Muhenga kusini kama walivyousiwa na baba yao. Kwa bahati mbaya Muhenga alikuwa mchoyo. Hakuridhika na sehemu yake ya utawala. Hivyo aliyaamrisha majeshi yake yamvamie Mkwawa; nayo yakamvamia. Lakini Mkwawa hakukubali. Alipigana kiume, mwisho akamshinda nduguye akawa mtemi wa nchi yote ya Iringa kama ilivyokuwa wakati wa marahemu baba yake.

Wakati wa utawala wa Mkwawa, kulitokea wageni weupe kutoka Ulaya. Wageni hao walikuwa ni Wajerumani. Walifika katika nchi yetu ili kuondoa utawala wetu wa jadi na kuweka utawala wao wa kigeni. Kwa kweli wageni hao walikuwa katili sana. Waliwaua babu zetu bila kosa lolote. Waliwapiga bakora kama wanyama. Walifanya kazi katika mashamba yao, wakatengeneza mabarabara na kujenga majumba yao makubwa makubwa. Yote haya yalikuwa kwa ajili ya manufaa yao. Jambo lililokuwa baya zaidi ni kuwa waliwafanya babu zetu kuwa si binadamu kamili kama wao. Walitunyangánya nchi yetu kushibisha matumbo yao.

Mkwawa hakuweza kuvumilia ukatili wa Wajerumani. Hakupenda watu wake watawaliwe na wageni. Kwa hiyo, hakuwa na njia nyingine ya kufanya ili kuyakabili majeshi ya Wajerumani. Jamboo la kwanza alilofanya ni kuimarisha majeshi yake. Vijana wa Kihehe walijiandikisha kuwa askari kwa wingi sana. Ili Mkwawa awape askari wake mafunzo bora ya kivita, alijenga kambi kubwa mahali pamoja panapoitwa Kalenga. kambi hii ilizungukwa na ngome kubwa sana. Katikati ya ngome hiyo palijengwa nyumba kubwa. Hiyo ndiyo ilikuwa makao makuu ya Mkwawa. Pia mlikuwemo nyumbo za askari, mifugo na mashamba ya vyakula. Ngome hiyo ililindwa barabara na askari wa zamu usiku na mchana. Ilikuwa ikiitwa "Liringa", yaani "ngome kuu ya Vita." Kila kijiji kilikuwa na ngome za aina hii ili kuwalinda wananchi.

Baada ya kupigana kwa muda mrefu, na Wajerumani wengi kuuwawa, Mtemi Mkwawa aliweza kushinda Wajerumani. Lakini majeshi yake yalianza kudhoofika kwa sababu askari wake wengu waliuwawa. Wajerumani walipowashika viongozi wa Wahehe waliwanyonga hadharani!

Mkwawa alipoona kwamba Wajerumani wanazidi kuimarisha majeshi yao, na kwamba walikuwa wanamtafuta ili wamuue, alitoroka na kwenda msituni. Alitoroka na askari wake wawili ambao walikuwa wamekula kiapo cha uaminifu cha pamoja naye. Mara siku moja Mkwawa akajiona amezungukwa na majeshi ya Wajerumani. Alikuwa mtu shujua ambaye hakupenda kukamatwa mateka wala kuacha mwili wake uguswe na mzungu . Hivyo alijiua mwenyewe kwa bunduki kabla Wajerumani hawajawahi kumgusa.

Kweli Mkwawa alikuwa shujua. Anatukumbusha kuwa babu zetu hawakupenda kutawaliwa na wageni. Hawakupenda kupuuzwa. Hivyo walikuwa tayari kufa kuliko kutawaliwa.

Monday, August 26, 2013

HUU NI MCHANA MWINGINE YA JUMATATU .....KARIBU TUJUMUIKE HAPA JAMANI....

Picha hii imenikumbusha mbali sana huu ni mtindo mzuru sana kula hivi sahani moja ....Ila kuna kitu kimoja kilikuwa kinanishinda hapa nilikuwa nakula taratibu mno na ninaposhtuka ugani umeisha. Ni mtindo mzuri maana hapo ndipo wote mnaweza kukusanyika na kuongea pia ila si sana maaana kila mtu anakuwa hana nafasi ya kuongea.....isipokuwa kushiba....Je nawe msomaji unakumbuka hii?
JUMATATU NJEMA!!!!

Sunday, August 25, 2013

NI DOMINIKA YA 21 YA MWAKA C..WATOTO


Watoto wana hali ya kimbingu. kwani wana kila sababu: unyofu. utulivu. amani, upendo, furaha, mapatano. umoja, ushirikiano. usikivu na unyenyekevu. Ndiyo maana hata Bwana wetu yesu Kristu alisema: "Waacheni wadogo waje kwangu." Hali hii inatakia kwa kila mmoja wetu ili baada ya maisha haya ya sasa tukafurahi pamoja na Mungu katika utatu, milele yote mbinguni.
JUMAPILI NJAMA

Friday, August 23, 2013

TUANZA MWISHO WA JUMA NA UJUMBE HUU MUWE NA WAKATI MWEMA!!


 NA MSANII MRISHO MPOTO....

AU LABDA TUENDELEEE NA UJUMBE HUU

Tumkomboe mwanamke mimi na wewe tukomboe Taifa, kwani ni yeye mama ni yeye mwanzo Taifa...taifa bora huanzia tumboni mwa mama.....endeleee  yaani hapa nipo hoi maana  mapigo ya ngoma yanafanana na ngoma ya lizombe......
IUJUMAAA NJEMA KWA WOTE:-)