Saturday, March 23, 2019

ASIFIWE TUTAMKUMBUKA DAIMA!

AHSANTE KAKA JACOB MAHOLIJA KWA KUMBUKUMBU  HII NZURI  NIMEONA NIIWEKA HAPA KIBARAZANI KWA VILE LEO NI MIAKA  9 SASA  IMETIMIA  HAUPO NASI KIMWILI ILA KIROHO.
Leo ni arobaini ya Mpendwa wetu Asifiwe Ngonyani alama ya upole na upendo iliyofutika ghafla tarehe 23/3/2011 kama imefanyika ilivyopangwa.
Pamoja na kuwa mila zetu wengi zinatueleza kuwa arobaini ni kuhitimisha msiba lakini ukweli itachukua muda huzuni kufutika katika mioyo yetu, hasa kwa tuliopata bahati ya kumuona binti huyo. Tunakubali kwasababu kazi ya mungu haina makosa. Bali Asifiwe Tutamkumbuka.

                      ASIFIWE TUTAMKUMBUKA!

Marehemu Asifiwe akiwa na baba
Kwa upande wangu nikiwa na siku kadhaa mbali na Jiji la Dar es Salaam katika Vijiji ambako network ya mawasiliano ni mtihani kidogo hali yangu ya kifikra ilikuwa tata kidogo, nahisi ilikuwa ishara ya taarifa ya kusikitisha.. nilipokuwa katika vijiji vyenye mtandao, niko bize, baadae nikaona Misscall ya Yasinta. Sikuwa na hela ya kutosha kwenye simu siku iliyofuata Simu iliita nikiwanayo mkononi nikapokea.
Tofauti kabisa na nilivyozoea napompigia au anaponipigia, habari niliyoipata ilininyong’onyesha!, Kwa sauti ya unyonge Yasinta alisema “Jacob nilikuwa nakutafuta ulikuwa hupatikani, nilitaka nikupe taarifa Asifiwe Hatunaye Tena” kwanza nilijipa moyo huenda sikuwa kwenye simu ni mawazo tu .. lakini kwanini niwaze hivyo?....ikabidi nimuulize “Unasemaji Yasinta?” .. “Asifiewa Amefariki” alirudia kunithibitishia … hatukuongea sana .. nilimwambia tutaongea .. bado nikiwa nahisi labda ni mawazo tu .. nikamtumia msg kumuuliza tena, alinijibu “ni kweli Jacob, Asifiwe Ametuacha” tuliendelea kuchati kwa muda kidogo lakini dakiki zilivyozidi nilizidi kuishiwa nguvu.. nikakata mawasiliano..maana taarifa zilikuwa zinazidi kuniumiza!
Nilikuwa namfahamu Asifiwe baada ya kumtembelea Nyumbani Ruhuwiko miezi michache baada ya kurudi Kutoka kwenye matibabu ya moyo Dar es Salaam mwaka jana.
Ktika picha ya pamoja na Marehemu Asifiwe
Kwa waliowahi kukutana na binti huyu kama kaka Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti aliyewahi kumtembelea pale Hospitali baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo, Shaabani Kaluse ambaye pia Jumamosi ya terehe 18/03/2011 alipata bahati ya kumuaga Asifiwe, na wengine waliowahi kumuonawataungana nami kuwa binti huyu alikuwa mpole, mtulivu mwenye sura ya heshima na upendo.
“Nilijikuta nikimwambia kuwa sasa anatakiwa kurudi Shule, akiwa na tabasamu pana usoni mwake alinijibu kuwa yuko tayari kurudi shule na ndipo baba yake akaniomba nimsaidie kumtafutia shule nzuri atakayosoma binti huyu” alisema Shaabani Kaluse, ambaye naungana naye mia kwa mia.
Asifiwe alikuwa na kiu sana ya kusoma, kama ilivyokuwa kwa Kaluse nilipomtembelea, katika mazungumzo alionyesha sana kiu ya kusoma, nilimuahidi kumsaidia atakapukuwa ametulia vizuri na nikampa kitabu kinachoitwa “Mpenzi wa Kweli” nilichokiandika kwa ajili ya vijana hasa wanafunzi kikizungumzia maadili na umuhimu wa kupenda Elimu. Alikipenda sana!.
Nasikitika nilichelewa kupata taarifa, nasikitika sikushiriki wakati wa msiba ila wanablog 53 kwa niaba ya wote walipata kushiriki vizuri msiba huu mzito online, wengine walitumia simu .. wengine wakaandika kwenye blog zao .. Yasinta hakuwa peke yake wakati huu mgumu.
“Dada Naomba uamini kuwa msiba huu sio wakwako peke yako ni msiba wetu sote, yaani familia ya Mzee Ngonyani na ya Mzee Mkundi au pengine na Wanablog wote wa ndani na nje ya nchi.
Ni msiba wetu kwa sababu wengi wetu tulikufahamu wewe kupitia maandishi yako katika Blog ya Maisha na Mafanikio ambapo pia tukaifahamu familia yako na familia ya Mzee Ngonyani” alisema Koero mkundi katika blog yake.
Baada ya kuongea mambo mbali mbali namna ya kumsadia asifiwe, nilipata picha na Mzee Ngonyani.
Binafsi nilitarajia kuhudhuria arobaini ya Asifiwe, lakini nasikitika nimekuwa na wakati mgumu kimajukumu. Hata hivyo leo usiku mdogo wangu anasafiri kuelekea Sweden atanifikishia Salamu zangu kwa Yasinta. Lakini pia nitakapokuwa Songea hivi karibuni nitamtembelea Mzee Ngonyani kumpa pole.

Friday, March 22, 2019

Friday, March 15, 2019

ZILIPENDWA- MOROGORO JAZZ BAND ATT RTD DAR ES SALAAM


NAWATAKIENI MWISHO MWEMA WA JUMA .
UJUMBE WANGU WA LEO:- AMANI, UPENDO NA FURAHA NDIYO VIVWE NGUZO YETU. Kapulya wenu.

Wednesday, March 13, 2019

PALE UNAPOSUBIRI KUSIFIWA!


Unapofanya jambo lolote, fanya tu kama nafsi yako inakubali na inafurahia jambo hilo.
Usifanye jambo kwa kutegemea kusifiwa. Kumbuka usiposifiwa itakuuma sana, lakini ukisifiwa bila kutegemea sifa hiyo, utajisikia furaha sana.

Bila shaka utakubaliana na mimi kuwa Binadamu ni kiumbe anayependa kusifiwa, lakini ikitokea ukawa na kiu kubwa ya kupenda kusifiwa , basi inabidi ujiulize, ni wapi pana kasoro kwenye fikra zako.

Haiyumkini katika malezi yako hukuwahi kusifiwa kamwe na maisha yako yalitawaliwa na kulaumiwa kwingi na kukosolewa, hivyo ukajikuta ukihitaji kukamilishwa.

Haya burudika na shairi hili la Malenga wa Mvita.

UWATAPO HAKI YAKO

Namba nawe mlimwengu, pulikiza matamko
Nikweleze neno langu, uzinduwe bongo lako
Nayo nda M'ngu si yangu, na ayani haya yako
Uwatapo haki yako, utaingiya motoni


Simama uitete, usivikhofu vituko
Aliyo nayo mwendee, akupe kilicho chako
Akipinga mlemee, mwandame kulla endako
Uwatapo haki yako, utaingiya motoni


Amkani mulolala,na wenye sikio koko
Isiwe mato kulola,natutizame twendako
Tuwate na kuduwala,usingizi si mashiko
Uwatapo haki yako,utaingiya motoni


Teteya kwa kula hali, usiche misukosuko
Siche wingi wala mali,sabilisha roho yako
Unyonge usikubali, ukaonewa kwa chako
Uwatapo haki yako, utaingiya motoni



Siche kifaru na ndovu, wangazidi nguvu zako
Wapempe kwa uwekevu, unusuru haki yako
Siandame wapumbavu,kilicho chako ni chako
Uwatapo haki yako, utaingiya motoni


Cha mtu hakifitiki,kikafungiwa kiliko
Huzuka kikawa hiki,kazana utwae chako
Uwatapo yako haki,fahamu ni dhara kwako
Leo na kwa Mola wako,utaingiya motoni



Fumbuwa unyang'arize, uone duniya yako
Bure sijiangamize,kuangalia wendako
Utatupa upoteze,wende ambapo si pako
Uwatapo haki yako,utaingiya motoni


Kadhalika nako pia,huko ambako sikwako
Huwezi kujitetea,wala huwi na mashiko
Basi iwaze duniya,kwani ya kale hayako
Uwatapo haki yako ,utaingiya motoni


Kadi tamati shairi,sitii la ongezeko
Mwanati iwa tayari, utete haki yako
Unyonge usiukiri,Jifunge ufe kwa chako
Uwatapo haki yako, utaingiya motoni

Shairi hili limetungwa na Ahmad Nassir wa Malenga wa Mvita

Monday, March 4, 2019

BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO IMETIMIZA MIAKA KUMI NA MOJA MWAKA HUU TAREHE 23/2/2019

Hapa ni mwenyewe mamaMaisha na Mfanikio AKA Kapulya
Blog ya Maisha na Mafanikio kama mchezo mwaka huu  yatimiza miaka kumi na  (11). Napenda kuchukua nafasi hii na kusema:- Hii yote ni kutokana na uwepo wenu ulioambatana na upendo pia ushirikiano mzuri mlio nao. Na kubwa zaidi ni kwa familia yangu kwa kuwa bega kwa bega nami. Pia napenda kusema kwa kupitia michango ya wasomaji na wanablog wenzangu nimeweza kijifunza mambo mengi sana. Na ndiyo kwa sababa hii napenda kusema:- AHSANTENI SANA KWA USHIRIKIANO WENU NASEMA TENA KWANI NAAMINI BILA NINYI, NISINGEFIKA HAPA NILIPO LEO. KWA KWELI NAAMINI KUWA SISI SOTE NI NDUGU NA NI WATOTO WA BABA MMOJA. UPENDO NA UMOJA WETU UDUMU DAIMA NA PIA MILELE!!!!!......Halafu la kufurahisha siku niliyoanza kublog ilikuwa ni JUMAMOSI na mwaka huu pia  ni JUMAMOSI... HAYA NIWATAKIENIAMANI NA FURAHA  KWA WOTE MTAKAOPITA HAPA NA WENGINE WOTE.

Monday, February 25, 2019

MLO WANGU WA JIONI YA LEO UTAKUWA HUU NA CHA KUTEREMSHIA NI MAJI...

Karibuni tujumuike ndugu/rafiki zangu ni samaki kwa viazi....Nimekumbuka sana kule nilikozaliwa Nyasa ila kule kwetu kungekuwa na ugali wa muhogo weeeee

Wednesday, February 13, 2019

UJUMBE WA LEO- TOFAUTI BAINA YA SHULE NA MAISHA.....

Shuleni unajifunza somo/masomo na baadaye unapata mtihani. LAKINI- Katika maisha , kuna mitihani ambayo tunajifunza masomo.
PANAPO MAJALIWA , Kapulya wenu!

Tuesday, February 12, 2019

KUMBUKUMBU: NI SHAIRI LA SIKU NYINGI SANA NILIIMBA NIKIWA DARASA LA NNE



Nililiimba kipindi niko shule ya msingi ,nakumbuka ni darasa la nne na mpaka leo takribani miaka 30 zaidi bado nalikumbuka. Bila shaka shairi hili litakukumbusha yaliyo mema ya kipindi cha nyuma. Na cha kufurahisa zaidi kitabu hiki ambacho hili shairi lipo ninacho:-)

Monday, February 11, 2019

HIZI ZITAKUWA PICHA ZA MWZI HUU WA PILI

Nimeamka asubuhi ya leo na nikawa na hamu ya kula yai  kwa kawaida huwa napenda kula yai moja tu lakini lakini leo macho yangu yakakutana na maajabu haya katika yao moja nikaona ni mawili. Cha ajabu yao halikuwa kubwa kuliko kawaida....nimeyale yote :-)  Mara nikakumbuka kuna mtu alinitumia picha ....
...picha maajabu yaliyotokea mgomba mmoja umezaa mikungu minne ya ndizi. Hakika hii ni kali ya mwezi ..

Monday, February 4, 2019

TUANZE MWEZI HUU WA PILI KWA PICHA HII:-UMOJA NI NGUVU

 Kuna wengi watakumbuka hii kazi ya kutwanga  sio hapo zamani tu hadi sasa hasa vijijini bado wana enzi utamaduni huu. Lakini jamii ya sasa sijui kama kuna anayejua kinu   na mwichi ni nini...najivunia kuwa mmoja ninayeuenzi utamaduni huu pia hata kizazi changu. NAWATAKIENI MWEZI MPYA HUU UWE MWEMA.


Thursday, January 31, 2019

SI KILA MARA UNAPASWA KUUSIKILIZA



Ni mara nyingi sana tumeshindwa kufika mahali tulipopaswa kufika kwa wakati. Ni mara nyingi pia labda tumefanya makosa makazini au kwenye shughuli zetu za kila siku,yote hii ni kwasababu ya kuusikiliza kila wakati. Tumeshindwa kuwa na sauti kwake,unatupelekesha sana....

Maisha yanakwenda kwa kasi kweli kweli. Kila siku shughuli na mahitaji yetu yanaongezeka. Muda wa kufanya kazi unaongezeka....

Kadiri muda wa kufanya kazi unavyoongezeka ndivyo muda wa kupumzika nao unapungua,mahitaji mapya yanaongezeka. Kadiri siku zinzavyokwenda ndivyo mahitaji mapya yanaibuka zaidi kila siku,vile tulivyo navyo leo  tunaviona havifai tena tunataka vipya....

Ni kweli miili yetu nayo inachoka sana na kuhitaji pumziko kwa mfano ili kukusanya nguvu mpya ya kuendelea kuwajibika. Lakini jambo moja kubwa pengine tusilolijuwa ni kwamba mwili haujawahi kuridhika na chochote,kila siku/saa utahitaji kitu kipya. Ukipumzika leo kesho mwili utataka kupumzika tena na kesho kutwa hivyo hivyo na siku inayofuata,hakuna mwisho....

Wengi tumeshapata hasara au pengine kushindwa kutimiza mambo fulani fulani katika maisha  kwasababu ya mwili. Tunashindwa au tulishindwa kwasababu ya kuusikiliza mwili na kuupa kila utakacho lakini bahati mbaya sana mwili unaendelea kuhitaji tu. Unatufurusha tu kila siku....

Wapendwa,kama nilivyosema huko juu,mwili nao una mahitaji yake lakini mwili huu huu hauridhiki,hakuna wakati utasema hapana,ukiupa kuku leo kesho utatamani Sato. Hautaishia hapo keshokutwa utataka dagaa wakavu,siku inayofuata utataka nyama ya kukaanga na mlolongo unakuwa mreefu sana,hakuna kukoma labda afya iwe na kasoro....

Mwili ni kama mtoto mdogo. Mtoto anapoamka anataka kitumbua hapo hapo atataka kwenda kucheza. Kuna wakati tunawazuia watoto kutenda mambo fulani kwasababu tunajuwa yanaweza kuwadhuru au hayana faida kwao. Miili yetu nayo ni hivyo hivyo,si kila utakachohitaji basi uhangaike kuupa....

Wakati wa kuamka asubuhi unaweza kufika lakini mwili unakataa huku unafahamu kabisa kuwa ni lazima uamke ili ukawajibike,ukiusikiliza mwili wako utaharibu kazi. Mwili unaweza kukuharibia malengo yako na zaidi maisha kwa ujumla wake....

Si kila unaomtamani mwanamke/mwanaume basi uupatie mwili unachokitaka. Haitatokea ukaridhika,ukiupa mwili utakacho leo kesho utataka tena kwa mwingine mwishowe utaharibu ndoa yako na familia kwa ujumla....

Si kila unapotamani bia basi unywe. Si kila unapotamani nguo basi ununue. Utaharibu bajeti za mambo mengine halafu mwili hautakoma kutaka vingine....

Tujifunze kuukatalia mwili na vurugu zake. Upatie mwili yale ya muhimu tu. Kama unahitaji kulala,lala kwa muda sahihi na baada ya hapo amka ukafanye kazi. Mwili utakutaka uendelee kulala tu,ukiusikiliza inakula kwako. Utaharibu kazi na matokeo yake utaishia kufukuzwa kwenye nyumba uliyopanga au utashindwa kuihudumia familia yako....

Uvivu ni matokeo ya kuusikiliza mwili. Karibia tabia zote hasi ni matokeo ya kusikiliza mwili kuliko pindukia. Tabia kama ulevi,umalaya,matumizi ya madawa ya kulevya n.k ni matokeo ya jambo hili....

Kuanzia leo sema hapana kwa mwili wako. Kataa kuwa mtumwa wa mwili wako leo na maisha yako yatabadilika kabisa....

Uwe na wakati mwema......

Chanzo:- nimetumiwa na rafiki nikaona sio vema kubaki na ujumbe mzuri wa burasa kama huu  peke yangu. Elimu ni kugawana.

Friday, January 25, 2019

HEBU LEO TUANGALIE BAADHI YA MANENO LA HEKIMA....!

1. Kila jambo na wakati wake
2. Aba na haba hujaza kibaba
3. Maji hayatoki yakishushwa kwa moto.
4. Siku njema huonekana asubuhi.
5. Dalili ya mvua ni mawingi
6. Dawa ya moto ni moto
7. Fimbo ya mbali haini nyoka
8. Asiyefunzwa na mamaye hafunzwa na ulimwengu
BASI  NIWATAKIENI IJUMAA NJEMA NA MWISHO MWEMA WA JUMA.

Thursday, January 24, 2019

KUMBUKUMBU .....ENZI HIZOOO! WATU TUMETOKA MBALI KWA KWELI

Aina za mafuta ya kupikia pa kupaka kwenye mkate nadhani PRIDE na SUPA-GHEE
Aina nyingine ni tan bond
Dada ana mzinga wa redio/ kaseti ili kupata pozi
Basi la Iringa enzi hizo

Thursday, January 10, 2019

VIFAA MBALIMBALI VYA KUTUNZIA MAJI/KWENDA KUCHOTA MAJI KISIMANI AU SEHEMU NYINGINE

 Hapa ni ndoo tena za aina tatu au nne hivi 
 Hapa ni VIBUYU
 MTUNGI
Hapa ni kabila la wamasai wao hubeba mgongoni na hutumia madumu/madungu .
Binafsi nimezoea tumia ndoo na mtungi na kubeba kichwani. Je wewe mwenzangu?

Wednesday, January 9, 2019

UJUMBE WA LEO : TUYAKUMBATIE MALENGO/MAWAZO MAPYA ILI KULETA UHALISIA ....

Ukikumbatia ulicho nacho utaona mafanikio yake. NAWATAKIENI SIKU HII YA JUMATANO IWE NJEMA SANA.  PAMOJA DAIMA. Ni mimi Kapulya wenu.

Saturday, January 5, 2019

LEO NI SIKU YANGU YA KUMBUKUMBU YA KUZALIWA

 Namshukuru  mwenyezi kwa kunipa afya njema mpaka leo nimeiona kumbukumbu  yangu ya kuzaliwa. Pia napenda kuwapa hongera kwa wote waliozaliwa mwezi  huu wa kwanza  na watakaozaliwa mwezi huu.
 Kwa vile nilikuwa mwema familia, ndugu na marafiki wamenipondeza kwa zawadi.HONGERA SANA KWA SIKU YA KUZALIWA MIMI.

Monday, December 31, 2018

UJUMBE WA MWISHO WA MWAKA 2018 KUTOKA KWANGU KUJA KWENU

UJUMBE :-
HATA SURA NZURI ITAZEEKA, NA MWILI MZURI UTACHOKA, ILA ROHO NZURI HUBAKI  KUWA NZURI MILELE NA MILELE.
NACHUKUA NAFASI HII KUWASHUKURUNI SANA KWA MWAKA HUU 2018 KWA USHIRIKIANO WENU. AHSANTE SANA SANA . NI MIMI KAPULYA WENU.

Wednesday, December 26, 2018

MWOKOZI YESU AMEZALIWA


NI MATEGEMEO YANGU KUWA SIKUKUU HII YA KUZALIWA MWOKOZI WETU IMEKUWA NJEMA KWA WENGI WETU. NAMI NACHUKUA NAFASI HII NA KUSEMA NAWATAKIENI  WOTE NOELI NJEMA

Monday, December 17, 2018

LEO NIMEKUMBUKA MITINDO YA ZAMANI JINSI WATU WALIVYOKUWA WAKIPEANA HISIA ZAO

Hapa itakuwa anaenda kisimani ndoo kaficha sehemu, hivi unafikiri kwa nini hawaangaliani?
Hapa yaonekana mdada anaenda kutafuta kuni

...na mtindo huu ni kiboko wote wanaonekana kuwa na aibu ...


....hii ni  baadhi ya mitindo ya hapo kale.  Au pia watu walikuwa wakiandika barua au kumtuma mtu. Siku hizi eti mtu anatuma sms ya kawaida au WhatsApp

Thursday, December 13, 2018

TAREHE HII HAPA LEO NI SIKUKU YA MTAKATIFU LUCIA...

Kwa hiyo mimi nimeona itapendeza zaidi kama nikiitumia mikono yangu kwa kutengeneza aina hii maalumu ya mikate(LUSSEKATTER)  ili kujumuika ndugu, marafiki pia majirani kwa kusherehea siku hii....


.....pia aina hii ya biskuti (pepparkaka) GINGERBREAD


Na hapa ni maagizo  jinsi inavyokuwa. Nakumbuka binti yetu aliwahi kuigiza duh! niliogopa sana maana hiyo mishumaa inawaka kwa ukweli ......ila walijiandaa na ndoo za maji...

Monday, December 10, 2018

HAPO KALE KARIAKOO YETU ILIVYOKUWA........

NAWATAKIENI WOTE JUMATATU NJEMA SANA. PANAPO MAJALIWA TUTAONANA TENA!

Wednesday, December 5, 2018

NIMEYATAMANI SANA HAYA MATUNDA...............


Hapa ni mbula au sisi wangoni twasema  mabuni ni matamu sana pia juisi yake ni tamu mno.
Na hapa ni masuku, sasa ndio msimu wake 

Tuesday, December 4, 2018

NI MWEZI MPYA TENA ...TUANZE NA MSEMO HUU KUUANZA MWEZI HUU WA KUMI NA MBILI!

Msemo/ujumbe wa leo:-
Njia bora ya kuacha kuwaza ni jinsi gani unafikiri ya kwamba unajifahamu/jijua ni kuzingatia kile unachokijua, unajua.
TUKUTANE TENA PANAPO MAJALIWA!