Wednesday, January 23, 2013

Nimeshindwa vumilia !!!!

Siwezi siwezi tena, siwezi kuvumilia,
Hali miye tena sina, sinayo menizidia,
Usiku nao mchana, nazidi tu kuumia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Mejaribu kujikaza, kinywa nikakizuia,
Mezidi moyo umiza, nafuu h’ijatokea,
Moyo pendo mekoleza, mekolea kuzidia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Mejaribu kutosema, moyo haujatulia,
Juu juu ninahema, kama nataka jifia,
Kwako nilishatuwama, sina ninalosikia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Usingizi siupati, wewe tu nakuwazia,
Nipo hoi hatihati, hatihati kuugua,
Nawaza kila wakati, ni vipi nitakwambia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Nimechoka nimechoka, nimechoka vumilia,
Leo nakwita itika, moyo upate kutua,
Maana ushaniteka, na moyo usharidhia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Nipo hoi taabani, moyo kwako umetua,
Nitakuwa furahani, wewe kinikubalia,
Nimekuweka moyoni, uniweke nawe pia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Chonde chonde muhashamu, nifanye moyo tulia,
Nikupe pendo adhimu, pekee hii dunia,
Pendo liso na awamu, kila siku lachanua,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Nikupe pendo la huba, pendo nalosisimua,
Pendo tele na si haba, moyoni ‘shakujazia,
Pendo mara saba saba, mahaba yalozidia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Siwezi tena kungoja, kusubiri kukwambia,
Moyoni ipo haja, zaidi nitajifia,
Nakupenda wewe mmoja, hakuna nokufikia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Uwe wangu wa milele, name niwe wako pia,
Nikupe mapenzi tele, nawe tayafurahia,
Pamoja huku na kule, kwa raha ilozidia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Nimeshindwa vumilia, nd’o ma’na nimekwambia,
Kwamba ninakuzimia, juu yako naugua,
Natumai mesikia, kisha tanikubalia,
Kwani siwezi himili, kutosema nakupenda.

Shairi hili kutoka kwa mtani wangu Fadhili Mtanga
NAWATAKIENI WOTE KILA LA KHERI..PAMOJA DAIMA.

Tuesday, January 22, 2013

SIKU YA MWAKA MPYA 1/1/2013 ILIVYOKUWA HAPA KWETU SONGEA/RUHUWIKO NA MZEE UHAULA NDANI YA MAPISHI!!!

Hapa pilau likiandaliwa na mpishi maalumu, kwa jina anaitwa mzee Edward Uhaula ni mkazi wa Matetereka..tulikuwa tukiishi nashi enzi hizo. Kwa hiyo siku hii ya mwaka mpya 2013 alikuja kutusalimia na hakukosa kukumbushia enzi yaaani kupika. Maana si unajua ukiwa na familia kubwa..halafu tena ni sikukuu ya mwaka mpya inapendeza kukutana pamoja kula na kucheza/kuongea..kubadilishana mawazo. ilikuwa safi sana kwa kweli
Hapa ni nyama ya ngómbe ikiandaliwa ..muda si mrefu itatengenezwa kwa viungo na baadaye kuliwa....

Sunday, January 20, 2013

NAPENDA KUWATAKIENI WOTE MTAKAOPITA HAPA JUMAPILI NJEMA SANA!!!!! MICHEZO NI FURAHA!!!!

Licha ya kuwafundisha watoto elimu ya kitabuni, wanahitaji pia michezo ili waweze kujengeka kimwili, kiakili, kiroho na kuwa na maadili mema.. JUMAPILI NJEMA SANA....

Friday, January 18, 2013

IJUMAA YA LEO NA MWANAMTINDO WETU NDANI YA KITENGE TUDUMISHE HILI VAZI!!!

Unapopata zawadi unapaswa kuchukuru ahsante Dada mkuu msaidizi..Mija na hii ni kazi ya mikono ya shemeji Manju...kuona kazi zake zaidi unaweza kuingia hapa
Mimi ndani ya kitenge ..huwa kila niendapo kunyumba nashona kitenge ..napenda sana vazi hili. Kitu kimoja huwa kinaniletea taabu pale nishindwapa kuchagua mshono/mtindo..huu nimechaguliwa na fundi kama kuna mtu anaweza kunipa mbinu naomba...
Hapa ni zawadi kutoka kwa dada Ester Ulaya nilipata ile siku tuliyokutana,,Ahsante sana Dada Ester na Shemeji ..nimeipenda sana zawadi hii..si unajua mwanamke kanga/kitenge..kudumisha utamaduni wetu ni msingi mzuri..mpiga pcha ni dada Camilla. NAWATAKIENI WOTE MTAKAOPITA HAPA IJUMAA NJEMA NA PIA MWANZO WA MWISHO WA JUMA UWE WENYE FURAHA..PAMOJA DAIMA...

Thursday, January 17, 2013

Wanawake hupenda kuonewa wivu……!

Kama ulikuwa hujui, ni kwamba wanawake hupenda kuonewa wivu, lakini kwa kiasi kidogo tu. Lengo lake hasa ni kutaka kujua kama unamjali kwa kiasi gani. Wakati mnapoingia kwenye mghahawa ama kwenye Baa, mwanamke angependa ugundue kwamba kuna mtu amevutiwa naye, hata kama mtu huyo ni muhudumu. Pia wakati wanaume wengine wanapowakodolea macho unapokuwa naye barabarani, ama wafanyabiashara wa mitaani wanapopiga kelele na miluzi ya kumsifia, angependa kuona utalichukuliaje hilo. Unapoonekana kutofurahishwa na vitendo hivyo na kumtaka mtafute sehemu nyingine ambayo haitakuwa na rabsha, ama nawe utakapoonekana kuona fahari ya kuwa na mwanamke anayevutia watu, basi mpenzi wako huyo naye ataona kwamba yeye ni muhimu kwako. Lakini ni lazima uwe mwangalifu usije ukajenga ama kuonesha wivu wa kupindukia, kwani hilo litamfanya mpenzi wako ahisi unamuona yeye si mwaminifu, au ni Malaya. Kumbuka wivu ukizidi sana huwa kero. HABARI HII NIMEIPATA UTAMBUZI NA KUJITAMBUA....

Wednesday, January 16, 2013

HONGERA KWA SIKU YA KUZALIWA KAKA SIMON KITURURU/KADODA..BABA MAX!!!

KAKA SIMON KITURURU /BABA MAX HONGERA SANA KWA SIKU YAKO YA KUZALIWA Mwezi huu ni kumbe tupo wengi tuliozaliwa mojawapo mimi mwenyewe ambaye nimevunja makumi kadha, Na leo kaka Simon Kitururu naye kavunja kalenda na wengine wote kama vile shemeji Isaac mume wa dada Rachel, kaka Haki Ngowi, baba wa mzee wa Changamoto, na mtoto wa kaka yangu Sam Mbogo, mtoto Oskar..na wengine wote wanaotimiza miaka/mwaka mwezi huu HONGERA SANA KWA MWEZI WETU...!!!

UJUMBE WA SIKU YA LEO!!

Watu wengi Binadamu wachache!! TUWE NA SIKU NJEMA!!!

Monday, January 14, 2013

SIKU HIZI SITAZISAHAU ..HATIMAYE TUMEKUTANA USO KWA USO..

Yasinta na Kaka Albano Midelo Ruhuwiko/Songea Ilikuwa ni mwaka mpya huu 2013 kwa mara ya kwanza kaka Albano Midelo alikuja kututembelea kwetu Ruhuwiko yeye ni mmiliki wa blog ya Maendeleo ni vita
Yasinta na kaka Shaban Kaluse wakiwa Jangwani beach Dar es Salaam Haikuishia kukutana na kaka Midelo tu, pia kwa mara ya kwanza nikakutana na kaka yangu wa hiari kaka Shaban Kaluse Mzee wa utambuzi. Ilikuwa ni furaha ya ajabu sana kukutana na kaka huyu ...kwa kumfahamu zaidi unaweza kumsona hapa
Yasinta na Dada Ester Ulaya wakiwa wametulia ndani ya Savanah Lodge Sikuishia kukutana na hao akina kaka tu ..Nilipata bahati ya kukutana na Dada Ester Ulaya pia nadhani safari yangu safari hii ilikuwa yenye baraka sana kuweza kukutana na ndugu hawa..hapo tupo sehemu tuliyofikia Savanah Lodge ambayo ipo maeneo ya Banana..kuweza kumfahamu dada huyu ingia kwenye blog yake Rular and Urban
Na hapa ni picha ya pamoja hicho kiti kisicho na mtu ni cha mpiga picha ambaye ni mr. wangu, anayefuatia ni mmiliki wa hotel ya Savanh Lodge, halafu anafuatia kaka Kinunda, na halfu anafuatia ni mume wake dada Ester Cathbert Angelo Kajuna na ni mmiliki wa blog HABARI NA MATUKIO na pembeni yake ni mwenyewe dada Ester na halfu mimi nipo ila sijaonekana hapo na bila kusahau kaka Chacha naye tulikuwa naye ila alifika baadaye na katika kunogewa na hadithi tukasahau kupiga naye picha.Na halafu nisisahau tulikuwa na dada mkuu msaidizi katika maongezi yetu yaani kwa simu..si mwingine tena ni mwenyewe mwanamke wa shoka Dada Mija. Yeye anapatikana zaidi hapa. Tuulikuwa na wakati mzuri sana kwa ujumla.

Hivi tunawezaje kuishi kwa matumizi yafuatayo kila mwezi?

Fikiri, matumizi nyumbani: chakula, umeme, gesi, maji, soda/juisi za wageni. Ada za watoto zinazolingana na za chuo kikuu. Matibabu hospitalini, pesa ya walinzi kwa mwezi, sherehe za kuaga na kukaribisha mwaka mpya; Zaka ya kanisani na misikitini, Kupanda Mbegu/ Sadaka, Shukurani ya Neno, Ahadi na Collect, shukrani ya Chakula cha Bwana church, marekebisho ya kitasa cha mlango kabla mwenye nyumba hajashtuka, gharama za marejesho ya mkopo wa saccos kazini. Tozo za Flying (wazoa taka wa mikokoteni ambao huzit...upa hapo hapo), Madalali wa nyumba/viwanja, Pango la nyumba, Fremu ya biashara/ofisi, Mazakayo wa mitandao ya simu [airtime vouchers]; Mafuta ya gari, Walinda/waosha magari (oya sista/blaza, mdogo wako nipo apaaa); Tozo za kuegesha magari, Makato ya Mikopo, Tozo za internet cafe ili uweze ku-surf. Rambirambi ya mfiwa mtaani kwetu, Harusi ya ndugu yako wa ukoo na zawadi, Sendoff ya mtoto wa mdogo wake rafiki yako na zawadi, Kumuaga mfanyakazi mwenzetu na zawadi, Michango ya komunio ya 1 & 2 na kipaimara; Michango ya besdei party na zawadi; Ndugu wa kule kijijini, Mshahara wa Hausigeli na hausiboi; Bodaboda, teksi na bajaj; Duka la dawa kwa Mchaga, Tuisheni ya mtoto, Kuchangia wahanga wa mabomu na mafuriko. Kwenda kumuona mtoto aliyezaliwa, Kununua CD/DVD ya Uzinduzi wa Kwaya yetu. Chakula cha mbwa, Machango wa Ujenzi wa Kupanua Kanisa, Kuchangia Uinjilisti Masasi, outing ya kitimoto, Ujenzi wa Nyumba Mabwepande, Kuendeleza shamba mkuranga (linalotaka kutaifishwa kwa kutoendelezwa). Na kwa wale wenzetu wanaokwenda umbali wa Viti Virefu, moja moto moja baridi. Maji ya Traffik, Chai ya Nesi na Daktari, Kahawa ya Hakimu, Karani na PP. Vishoka waunganisha maji na umeme; Kidogodogo cha mjumbe na mtendaji wa mtaa, makaribisho ya get together na dinner kwa rafiki wa kikazi ambaye hamjuani ila kweye simu tu, Mchango wa matibabu ya mtoto Nyumba ndogo kule Ngusero, mchango kidogo kwa rafiki aliyevamiwa na Vibaka na kuumizwa vibaya, gharama za malipo ya mtura Mkulima Bar Moshi, manunuzi ya maji ya Kilimanjaro Uwanjani Sheikh Amri Abeid Ukicheck mechi ya Yanga na JKT Oljoro, malipo kwa ajili ya Uji wa Shanga baada ya kazi Njiro jioni ya Alhamisi, Vipi manunuzi ya kandambili kwa ajili ya matumizi ya home.Hivi hali inakuwaje? Mia mbili ya watoto wa mtaani/ombaomba, kitu kidogo cha wale wanaolazimisha kuosha kioo cha gari kwenye foleni. umeme uliopanda bei, gesi iliyopanda bei, maji yaliyoadimika, bado contingency mana huu usafiri unaotembelea ball joint, bush, feni belt havijafa - hapo bado service. Bado msosi wa mchana kazini esp kama maofisi yetu mama ntilie wanakaribiana bei za restaurants, bado mchango wa kitchen pati na sare, baby shower. Na hapo bado hujatoa watoto outing jumapili, Upo wapi uwezekano wa kununua laptop mpya ambayo ni muhimu katika mfumo wa maisha ya kisasa, desktop nyingine kwa ajili ya watoto at home, rim mpya za gari ambazo zimeingia ku modernize gari lako kuu kuu, vipi kuhusu gharama za kujipendekeza kwa kimwana wa job ambaye amekubali kwenda nawe out leo, gaharama za matibabu ktk hospitali binafsi kwa kuwa madaktari wa serikali wapo ktk mgomo, Dogo naye “bro ninunulie basi japo kasimu ka promosheni, ile yangu imedondoka chooni” Mara “Bro/Sister Next week on sato shuleni tunavisit snake Park na sina shilingi 3000 za mahudhurio”, Wife naye “ Daddy leo Mwakasege yupo relini, vipi tutapitia? Hapo ujue kichwani gharama ya taxi baada ya semina, vipi tozo za toyo kwa kuwa nimeachwa na gari la staff. Dullah the balhead kama kawaida anakusubiri uwajibike kwa gharama zako. Mama yangu!!!!!!!! Hapo mwajiri amekuongezea mshahara kwa 7% tu wakati inflation ni above 19%. Ukifikiri kwa makini, unajiuliza watanzania wana-survive vipi kwa style hii??? Ndipo unapoimba "Mwokozi nitoe roho niepuke, hili balaaa" Napenda msomaji utafakari mwenendo wako wa matumizi kulingana na hali hali ya uchumi wa nchi na jamii yetu. Kama ukiyumba kwenye suala la kuweka akiba, basi maisha yako yatakuwa yanakabiliwa na ukosefu wa msingi wa muongozo au utakuwa unatumia gharama kubwa kwa mambo yasiyoweza kusaidia familia yako.

Saturday, January 12, 2013

BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO HEWANI TENA...AHSANTENI KWA MAOMBI YENU...!!!

Nimetulia nakula embe karibuni si mwaona zilivyo nyingi:-)


Blog ya Maisha na Mafanikio inapenda kuawataarifu kuwa sasa itakuwa nanyi hewani tena kama kawaida. Napenda kuwatakeni samahani kwa usumbufu wa kutopata matukio kama ilivyozoeleka. Pia nachukua nafasi hii kuwa-SHUKURUNI KWA MAOMBI YENU kwa safari yangu na familia yangu. Tumesafiri salama na hii nina imani ni kutokana na maombi yenu. AHSANTENI SANA PAMOJA DAIMA....KAPULYA...

Saturday, January 5, 2013

LEO NI SIKU YANGU YA KUZALIWA ....MIAKA INAKWENDA JAMANI

Leo ni tarehe/siku ambayo familia ya Mzee Ngonyani ilikuwa kumpati binti huyo ambaye alizaliwa siku hii ya leo. Na leo ameongoza mwaka tena na kuzidi kuzeeka. Lakini hata havyo anapenda kuwashirikisha ndugu, jamaa na marafiki kwa siku hii ili tumsaidie kusherekea. Na wote manakaribishwa..sana. NAWATAKIENI SIKU NA WAKATI MWEMA. WOTE MNAPENDWA SANA ...KAPULYA

Wednesday, January 2, 2013

BADO NIPO SONGEA NA NIPO SALAMA..KHERI YA MWAKA MPYA 20113!!!!

Nataka kuwafahamisha ya kwamba nilisafiri salama na nipo salama. mAJUKUMU YALIZIDI...Na pia NAWATAKIENI WOTE KHERI SANA KWA MWAKA MPYA 2013...BADO NIPO SONGEA..TUTAONANA MUDA SI MREFU....KAPULYA

Friday, December 14, 2012

BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIA KUTOKUWA HEWANI KWA MUDA ..NAKWENDA KULA LIKOLO LA NANYUNGU:-)NYUMBANII NI NYUMBANI!!!

Hali ya hewa ndivyo ilivyo leo  DAKIKI/DAKIKA MBILI ZILIZOPITA...yaani mtu unaonekana mnene kama vile tembo kwa ajili ya kuvaa mingua mingi ili usisikie baridi. Nina furaha kuachana na hali hii kwa muda .. nisemapo hivi ni kwamba BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIA INATAKA KUSEMA HAITAKUWA HEWANI KWA MUDA KUTOKANA NA MAMA WA MAISHA NA MAFANIKIO ATAKUWA SAFARINI. Nachukua nafasi hii kuwatakieni wote CHRTITMAS NJEMA NA PIA MWAKA MPYA NA PANAPO MAJALIWA TUTAONANA TENA HAPO MWAKANI 2013.
Labda tu Remmy Ongala afichue wapi nakwenda..... na kipande hiki cha mziki..

Narudi nyumbani eeeeh nakwenda kula likolo la nanyungu....wangoni wote myumwike..nyumbaniiiiiii

Wednesday, December 12, 2012

NIMEUPENDA UBUNIFU HII ...AKILI NI MALI KILA MTU ANA ZAKE/USITUPE VIZIBO VYA BIA/SODA NI MALI!!!

Mwaka jana nilipita Mikumi katika maduka waozayo mambo ya urembo na vitu vingine..Nilishikwa na mshangaO baada ya kuona hizi heleni zilizotengenezwa na vizibo vya sodana bia (visoda). Nilipenda sana ubonifu wao na binti yangu akaniambia twaweza pia kufanya kazi hiyo kwa mikono yetu. Lakini, kumbe si kazi rahisi. Nawasifu watu waliofanya kazi hii kwa mikono yao. kunywa soda au bia yako na vizibi ( visoda ) usitupe ni mali... NAWATAKIENI WOTE SIKU HII YA JUMATANO IWE NJEMA SANA NI SIKU MAALUMU MAANA NI TAREHE 12-12-12..KILA LA KHERI!!!

Tuesday, December 11, 2012

KUMBUKUMBU .....TANZANIA!!!!!

 Shamba la katani ...ni Morogoro karibu na mlima wa Uluguru


Twiga wa Serengeti
Ngorongoro Crater

Sunday, December 9, 2012

JUMAPILI YA LEO NI JUMAPILI AMBAYO IMEANGUKIA SIKU AMBAYO TULIPATA UHURU 9/12/1961...


Nami nimea si wimbo huu wa maombi unafaa sana kwa siku ya leo. NACHUKUA NAFASI HII NA KUWATAKIENI WOTE JUMAPILI NJEMA NA PIA SIKU HII KWA UJUMLA

Friday, December 7, 2012

SALAMU/UJUMBE KUTOKA BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO IJUMAA YA LEO NI:-

Kila CHOZI ni ishara ya MAUMIVU. Kila ukimya ni ishara ya UPWEKE, kila TABASAMU ni ishara ya FURAHA, lakini kila ujumbe ni ishara ya kum-mis/kumtamani mtu. NAWATAKIENI WOTE MTAOPITA HAPA  ASUBUHI ,MCHANA, JIONI AU NISEME TU IJUMAA NJEMA.....KAPULYA!!!!

TUANZE MWISHO WA JUMA HILI NA WIMBO HUU MALAIKA NAKUPENDA NA MIRIAM MAKEBA....


NAPENDA KUWATAKIENI WOTE MWISHO MWEMA WA JUMA NA MATUMAINI YANGU TUPO PAMOJA...KAMA UTAKUWA UNAENDESHA WALE WENYE THERUJI ENDESHENI TARATIBU MAANA KUNA AJILI NYINGI ZIMETOKEA MPAKA SASA..IJUMAA NJEMA....

Nilipoendelea kutafuta zaidi wimbo huu wa MALAIKA...nikakutana na hawa nadhani ni wachina nao wanaimba ebu wasikilize ukipata muda....

Kweli kiswahili sasa kinaenea dunia nzima....haya kila la kheri!!!!

Thursday, December 6, 2012

JINSI WATOTO WA KIKE WANAVYOJIFUNZA MAISHA ...

....mtoto umleavyo ndivyo akuavyo..ila kuna wakati katika jamii yetu huwa tunazidisha kidogo..mtoto anakuwa kama mtu mzima kabisa. Kwa maana hiyo anakosa ule muda wa kuwa mtoto. Ila tumejifunza mengi na tumekuwa kwa kiutu uzimauzima si kama sasa..au wenzangu mliopitia maisha haya mnasemaje?..Duh!  siku zinakimbia tayari leo ni Alhamisi ya tarehe 6/12/2012..KILA LA KHERI WANDUGU!!!!

Wednesday, December 5, 2012

MCHANA WA LEO NINGEPATA MLO KAMA HUU NINGEFURAHI SANA LAKINI SASA ITANIBIDI NILE KWA MACHO....

Ni ugali kwa mlenda uliochanganywa kwawa majani ya maboga na ambayo bamia. Halafu  bakuli la (ma)tembele la kuchemshwa kwa nyanya na kitunguu. Bila kusahau pilipili shamba.
Hakika hapa ni utamu, na tena ule wa asili kabisa ,yamu yamu yamu....NAWATAKIENI WOTE SIKU /JUMATANO NJEMA SANA.

Tuesday, December 4, 2012

NIMEUPENDA UJUMBE HUU:-)

Nimeupenda ujumbe huu kwa kweli ...nahisi nawe unayesoma umeupenda pia basi ngoja niwatakieni wote mtakaosoma siku njema.PAMOJA DAIMA...

Monday, December 3, 2012

HIVI NDIVYO HALI YA HEWA ILIVYOKUWA FINLAND LEO!!!

Hali ya leo Finland...hapa kwetu bado haijaangua kihivyo ila kuna baridi kali sana kiasi kwamba ile kutoka tu nje pua inasinyaa kabisa....Mwaka huu itakuwa kali kwelikweli...JIONI NJEMA KWA WOTE.....

MWANAFUNZI ABAKWA MPAKA ANAPOTEZA FAHAMU MKOANI RUVUMA!!!

JESHI LA POLISI mkoa wa Ruvuma limefanikiwa kumtia mbaroni Daud Ndunguru (19) wa mtaa wa Hoahoa uliopo Mbinga mjini na linaendelea kumsaka na mwingine jina lake ambaye halikufahamika mara moja linaendelea kumsaka kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa kike wa umri wa miaka 12 (jina lake limehifadhiwa) anayesoma darasa la nne katika moja ya shule za msingi zilizopo Mbinga mjini na kumsababishia maumivu makali na kupoteza fahamu.

Habari zilizopatikana jana mjini hapa ambazo zimethibitishwa na kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Deusdedit Msimeki zimeeleza kuwa tukio hilo lilitokea desemba 2 mwaka huu huko katika mtaa wa Kihaha nje kidogo ya Mbinga mjini ambako mwanafunzi wa kike inadaiwa alibakwa na watu wawili akiwemo Daud Ndunguru ambaye alikamatwa muda mfupi baada ya kumfanyia kitendo cha kinyama msichana huyo na mwenzake ambaye jina lake halikuweza kufahamika alikimbia na kutokomea kusikojulikana.

Habari zaidi za tukio hilo zimefafanua zaidi kuwa watu hao wawili akiwemo Ndunguru majira ya saa 4:30 usiku walimvizia njiani msichana huyo na kumlazimisha atoe nguo alizokuwa amevaa na kisha kumfanyia kitendo cha ubakaji jambo ambalo limesababisha msichana huyo kupata maumivu makali sehemu za siri na kusababisha kupoteza fahamu.

Hata hivyo kamanda Msimeki alisema kuwa kufuatia kuwepo kw purukushani hizo majirani watoka na kwenda kwenye eneo la tukio ambako walifanikiwa kumkamata Ndunguru na mwenzake alikimbia huku msichana huyo akiwa amepoteza fahamu na walimchukua na kwenda nae kituo cha polisi cha kati cha polisi ambapo walichukua hati ya polisi ya matibabu (PF3) na kwenda nae hospitali ya serikali ya wilaya ya Mbinga ambako amelazwa na anaendelea kupata matibabu na hali yake inaendelea vizuri.
Kamanda Msimeki alisema kuwa mtuhumiwa Ndunguru anatarajiwa kufikishwa mahakamani pindi upelelezi wa tukio hilo utakapo kamilika na jeshi la polishi mkoani Ruvuma linaendelea kumsaka mtuhumiwa mwingine wa tukio hilo anayedaiwa kukimbia na kutokomea kusikojulikana baada ya kumfanyia kitendo cha kinyama msichana huyo
Habari hii nimeipata hapa

Saturday, December 1, 2012

SIKU YA LEO NIMEKUMBUKA LUNDO MBAMBA BAY 2007

Hapa kutoka kushoto ni kaka yangu wa mwisho Philoteo, katikati ni mjomba wangu mwl. John Bosco Ngonyani anajulikana zaidi kwa jina la JB na mwisho ni mwenyewe Kapulya. Siku hii ilikuwa siku ya furaha sana katika maisha yangu kwani nilikuwa sijaonana na mjomba wangu mpendwa karibu mika ishirini ...Muwe na  WAKATI MZURI PIA JUMAMOSI NJEMA YA MWEZI HUU WA KUMI NA MBILI AMBAYO NI YA KWANZA  NA KESHO NDO TUNAANZA KUSUBIRI ULE UJIO /KUZALIWA WA/KWA BWANA YESU KRISTU.

Neno La Leo: Fikiri Kuwa, Sayari Tunayoishi ( Dunia) Ni Jehenamu Ya Sayari Nyingine..​.!

Ndugu zangu,

Kwamba kuna viumbe kwenye sayari nyingine wenye kukesha wakiomba kwenye nyumba zao za ibada, kuwa Mungu wao awaepushe na balaa la kuwaleta kwenye sayari dunia. Dunia iliyo zaidi ya tambala bovu. Dunia iliyojaa wanadamu wenye roho za wivu, kinyongo, inda, husda na nyinginezo. Wanadamu wenye kutakiana mabaya badala ya mema.

Na mfano ni huyu aliyeomba sana kwa Mungu ashushiwe rehma. Siku moja akashukiwa na malaika. Akaambiwa, kuwa Mungu amepokea maombi yake. Kwamba anamtaka mwanadamu huyu achague jambo moja ili ashushiwe. Na akishachagua moja, basi, Mungu atampa jirani yake mara mbili ya kitu alichochagua.

Mwanadamu yule akamwambia malaika; " Basi, niache kwanza nitafakari". Baada ya kutafakari kwa muda,mwanadamu yule akatamka; " Namwomba Mungu anipe chongo!" Kwamba kwa vile alimwonea kinyongo jirani yake apate mara mbili ya atakachokipata, mwanadamu yule aliona ni heri Mungu amtoboe jicho lake moja, awe chongo, na jirani yake atobolewe mawili, awe kipofu!

Naam, fikiri kuwa sayari tunayoishi yaweza ni jehenamu ya sayari nyingine. Kumbuka, nimesema fikiri, hivyo basi fikiri kwa bidii...yaweza kukusaidia kupata jibu la kwanini nchi yetu ni masikini, na watu wake pia.

Na hilo ni Neno La Leo.

Maggid Mjengwa
Iringa.
0788 111 765
Nimetumiwa na http://mjengwablog.com.