Ni mara nyingi sana tumeshindwa kufika mahali tulipopaswa kufika kwa wakati. Ni mara nyingi pia labda tumefanya makosa makazini au kwenye shughuli zetu za kila siku,yote hii ni kwasababu ya kuusikiliza kila wakati. Tumeshindwa kuwa na sauti kwake,unatupelekesha sana....
Maisha yanakwenda kwa kasi kweli kweli. Kila siku shughuli na mahitaji yetu yanaongezeka. Muda wa kufanya kazi unaongezeka....
Kadiri muda wa kufanya kazi unavyoongezeka ndivyo muda wa kupumzika nao unapungua,mahitaji mapya yanaongezeka. Kadiri siku zinzavyokwenda ndivyo mahitaji mapya yanaibuka zaidi kila siku,vile tulivyo navyo leo tunaviona havifai tena tunataka vipya....
Ni kweli miili yetu nayo inachoka sana na kuhitaji pumziko kwa mfano ili kukusanya nguvu mpya ya kuendelea kuwajibika. Lakini jambo moja kubwa pengine tusilolijuwa ni kwamba mwili haujawahi kuridhika na chochote,kila siku/saa utahitaji kitu kipya. Ukipumzika leo kesho mwili utataka kupumzika tena na kesho kutwa hivyo hivyo na siku inayofuata,hakuna mwisho....
Wengi tumeshapata hasara au pengine kushindwa kutimiza mambo fulani fulani katika maisha kwasababu ya mwili. Tunashindwa au tulishindwa kwasababu ya kuusikiliza mwili na kuupa kila utakacho lakini bahati mbaya sana mwili unaendelea kuhitaji tu. Unatufurusha tu kila siku....
Wapendwa,kama nilivyosema huko juu,mwili nao una mahitaji yake lakini mwili huu huu hauridhiki,hakuna wakati utasema hapana,ukiupa kuku leo kesho utatamani Sato. Hautaishia hapo keshokutwa utataka dagaa wakavu,siku inayofuata utataka nyama ya kukaanga na mlolongo unakuwa mreefu sana,hakuna kukoma labda afya iwe na kasoro....
Mwili ni kama mtoto mdogo. Mtoto anapoamka anataka kitumbua hapo hapo atataka kwenda kucheza. Kuna wakati tunawazuia watoto kutenda mambo fulani kwasababu tunajuwa yanaweza kuwadhuru au hayana faida kwao. Miili yetu nayo ni hivyo hivyo,si kila utakachohitaji basi uhangaike kuupa....
Wakati wa kuamka asubuhi unaweza kufika lakini mwili unakataa huku unafahamu kabisa kuwa ni lazima uamke ili ukawajibike,ukiusikiliza mwili wako utaharibu kazi. Mwili unaweza kukuharibia malengo yako na zaidi maisha kwa ujumla wake....
Si kila unaomtamani mwanamke/mwanaume basi uupatie mwili unachokitaka. Haitatokea ukaridhika,ukiupa mwili utakacho leo kesho utataka tena kwa mwingine mwishowe utaharibu ndoa yako na familia kwa ujumla....
Si kila unapotamani bia basi unywe. Si kila unapotamani nguo basi ununue. Utaharibu bajeti za mambo mengine halafu mwili hautakoma kutaka vingine....
Tujifunze kuukatalia mwili na vurugu zake. Upatie mwili yale ya muhimu tu. Kama unahitaji kulala,lala kwa muda sahihi na baada ya hapo amka ukafanye kazi. Mwili utakutaka uendelee kulala tu,ukiusikiliza inakula kwako. Utaharibu kazi na matokeo yake utaishia kufukuzwa kwenye nyumba uliyopanga au utashindwa kuihudumia familia yako....
Uvivu ni matokeo ya kuusikiliza mwili. Karibia tabia zote hasi ni matokeo ya kusikiliza mwili kuliko pindukia. Tabia kama ulevi,umalaya,matumizi ya madawa ya kulevya n.k ni matokeo ya jambo hili....
Kuanzia leo sema hapana kwa mwili wako. Kataa kuwa mtumwa wa mwili wako leo na maisha yako yatabadilika kabisa....
Uwe na wakati mwema......
Chanzo:- nimetumiwa na rafiki nikaona sio vema kubaki na ujumbe mzuri wa burasa kama huu peke yangu. Elimu ni kugawana.