Thursday, March 31, 2016

JE? WEWE UNGEFANYEJE?

Tumbili na sokwe walijikuta wamekaa pamoja kanisani. Mara Padre/Pastor akasema, mgeukie mwenzako na mwambie wewe ni mzuri. Tumbili akageuka na kumwangalia sokwe kisha akacheka na kumwambia Padre/Pastor mwambie mwenyewe mimi sitaki dhambi.
Je hiki ni kichekesho au?
NAWATAKIENI WOTE JIONI NJEMA

Tuesday, March 29, 2016

PICHA YA WIKI:- NI DADA MIJA WA MWANAMKE WA SHOKA NA MASANJA MKANDAMIZAJI WAKIWA NORWICH UK SIKU YA JUMAMOSI KUU

Pale unapokuwa na vyanzo vya habari  sehemu mbalimbali....hapa ni Masanja Mkandamizaji na Dada Mija (Mwanamke wa Shoka) Siku ya Ijumaa Kuu huko Norwich UK. Halafu wewe Mija una bahati sana kwani nilikuwa mbioni kukutangaza upo wapi ...hakika watu wengine wana machale...haya nashukuru unaonekana wa afya njema...

Monday, March 28, 2016

MAMBO HAYA KUMI(10) YANAWEZA KUOKOA MAHUSIANO AU NDOA YAKO


Katika pitapita nimekutana na hii mada hapa nikaona niwashirikishe na mwenzangu karibu upata hii elimu nawe hata kama wajua si mbaya kurudia.

Mahusiano sio jambo rahisi. Haishangazi kuona kwamba eneo la mahusiano ya binadamu, iwe ni kwenye ndoa, mapenzi, kazi, biashara na jamii ni mojawapo ya eneo linalopewa kipaumbele cha kila aina. Wataalamu wa saikolojia kila siku wanakesha wakijaribu kugundua mbinu mpya za kuboresha mahusiano ya binadamu.

Pamoja na “ugumu” wa mahusiano ya kibinadamu, yapo mambo kadhaa ambayo yanakubalika miongoni mwa wengi wetu kwamba yakifanyika kwa uwazi,upendo na bila hila, yanaweza kusaidia sana katika kuboresha mahusiano hayo. Haya hapa ni mambo 10 ambayo yanaweza sio tu kuboresha bali hata kuokoa mahusiano yako hususani mahusiano ya kimapenzi au ndoa.


1.Kuomba Msamaha (Samahani)- hakuna binadamu aliye kamili. Sote tuna mapungufu. Mapungufu hayo huja au kuwa dhahiri kwenye mahusiano na hata kwenye ndoa. Kuna kukosea. Kuna kumkosea mwenzako. Na mara nyingine unaweza kukosea kwa bahati mbaya tu bila kukusudia. Ukigundua kwamba mwenzako hajafurahishwa na ulichofanya au kutofanya, omba msamaha. Hata kama huelewi kwa undani kwanini mwenzako kakasirika au hata kama wewe unaona ni jambo dogo tu, omba msamaha.

2.Tumia Neno Tafadhali- Unapoomba kufanyiwa au kusaidiwa kitu, tumia neno tafadhali au naomba. Badala ya kusema Baba Nanihii, niletee maji ya kunywa,sema, “Baba nanihii tafadhali naomba niletee maji ya kunywa”. Ni maneno madogo tu lakini yanatosha kuonyesha heshima na upendo kwa mwenzako.

3. Sema Asante(Shukuru)- Kila unapopewa kitu, kufanyiwa jambo, kusifiwa nk onyesha upendo wako kwa kusema “Asante”. Usiposema asante usishangae siku nyingine usipopewa au kufanyiwa kitu fulani.

4. Mwambie mwenzako Unampenda- Anajua kwamba unampenda na pengine ndio maana yupo na wewe. Lakini hakikisha unamkumbusha. Usimchukulie poa tu. Hapana. Haya mwambie mwenzako unampenda sasa hivi.

5. Samehe na Sahau- Kama nilivyosema hapo juu, binadamu hatupo kamili. Tunakosea. Mara nyingine tunakosea kila mara na kwa jambo lile lile. Jifunze kusamehe na kusahau. Usisamehe kwa minajili ya kuzuga amani ili ulipize kisasi. Samehe na sahau. Usikumbushe yaliyopita. Jifunze kutokana na yaliyopita ila samehe na muombe Mungu usahau.

6 Ongea Lugha Ya Umoja Badala ya Umimi- Binadamu tu-wabinafsi. Ni hulka. Tunajiangalia sisi kwanza kabla ya kumwangalia mtu mwingine hata akiwa mpenzi, mume au mke. Lakini ukitaka mahusiano yadumu, ni muhimu kubadili “lugha”. Badala ya kuongelea mambo katika umimi, ongea katika wingi(sisi). Kwa mfano badala ya kusema,’ nyumba yangu au gari langu” (hususani kwa walio kwenye mahusiano ya ndoa) sema, “nyumba yetu na gari letu”. Hutopungukiwa kitu ila utaijaza akaunti yako ya mahusiano mema.

7. Muite kwa Jina Lake- Ushakwenda mahali kama benki vile ukasoma jina la mhudumu aliyepo mbele yako kupitia kitambulisho chake kisha ukamuita kwa jina? Uliona jinsi alivyokupa huduma nzuri zaidi? Binadamu (hususani wanaume) tunapenda kusikia majina yetu yakitajwa. Ni hulka. Hakikisha unamuita mwenzako kwa jina lake. Litumie katika mazungumzo ya kila siku na kila mara.

8. Sikiliza- Kuna nyakati mpenzi wako anachotaka ni sikio lako tu. Sikiliza kwa makini anachokuambia. Onyesha wazi kwamba unasikiliza. Epuka na tabia ya “kumsikiliza” mwenzako huku unachezea simu yako au unakodolea macho televisheni.

9. Mheshimu- Hili linaonekana kuwa la wazi, si ndio? Kwa bahati mbaya mahusiano mengi yanavunjika huku wanaoachana wakisema “kutoheshimiwa” ndio sababu kubwa ya wao kuamua kujitoa. Kila mtu ana jinsi yake ya kuona anaheshimiwa au kudhauraliwa. Kwa makini jaribu kujua mambo yanayomfanya mwenzako aone umemdharau au kutomheshimu. Ikiwezakana muulize. Msome. Kisha yaepuke kama ukoma.

10 Msaidie Mwenzako- Ni muhimu sana kusaidiana. Hata pale ambapo mwenzako hajaomba msaada, fikiria kama Ingekuwa wewe ungehitaji msaada? Kama ni ndio, basi msaidie. Kwa mfano, msaidie kupika, kufua, kusafisha gari, kununua mahitaji ya Nyumbani, kusafisha nyumba, kuvalisha watoto. Kila inapowezekana (na mara nyingi inawezekana) msaidie.
KILA LA KHERI WOTE!

Sunday, March 27, 2016

KUTOKA MAISHA NA MAFANIKIO TWAWATAKIENI WOTE PASAKA NJEMA SANA

Katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye alitoa uhai wake kwa ajili yetu, imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ua hao ndugu. Yoh. 3:16.
Pasaka njema na jumapili njema sana !!!

Friday, March 25, 2016

NAWATAKIENI PASAKA NJEMA YA KHERI NA BARAKA TELE.......!!


NI IJUMAA KUU BASI NA TUTIMIZE YALE YOTE YANAYOTAKIWA KWA SIKU HII YA IJUMAA KUU. IJUMAA KUU IWE NJEMA KWA KILA ATAKAYEPITA HAPA NAWE MTAKIE IJUMAA NJEMA MWINGINE NA PIA PASAKA NJEMA.

Wednesday, March 23, 2016

SABABU 4 AMBAZO KAMWE HUPASWI KUACHA KWENDA HAJA NDOGO PALE MAUMBILE YANAPOTAKA UFANYE HIVYO…


ANAHITAJI KWENDA HAJA NDOGO
Wote tunajua kwamba pale tunapokuwa tumebanwa  kweli kweli na haja ndogo(mkojo).
Wakati mwingine huwa tunalazimika kwa muda mrefu kukaa bila kwenda haja ndogo na
hata mwishowe kuhisi kana kwamba kibofu kinataka kupasuka.
Wakati mwingine tunakuwa katika sehemu ambazo hakuna maliwato yaliyoko karibu na
wakati mwingine huwa tunakuwa na marafiki tukipiga soga kiasi kwamba hutuwia
vigumu kuacha kukatisha mazungumzo ili kukidhi hitaji hilo la kimaumbile, lakini pia
wakati mwingine huweza kuwa na foleni ndefu kwenda maliwato hasa katika maeneo ya
Mighahawa au maeneo ya jumuia.
Zipo sababu nyingi kwa nini wakati mwingine yatupasa kuvumilia/kutunza  mkojo kwa
muda mrefu iwezekanavyo kutokana na maeneo tuliyopo kutokuwa rafiki katika kukidhi
hitaji hilo la kimaumbile lakini ni vyema tukijua kwamba jambo hilo lina athari kubwa
kiafya kwetu.
Kwa nini inasisitizwa kwamba tunapokuwa na hitaji hilo la kimaumbile tutafute mahali pa
kujisitiri haraka iwezavyo. Ni kwamba kibofu cha mkojo ni chombo ambacho kinaweza
kubeba/kutunza hadi lita 0.5 za mkojo. Wakati kibofu kikiwa kimejaa kama theluthi mbili
ubongo huwa unapata hisia kwamba ni lazima ukojoe. Lakini kwa sababu mawasiliano
kati ya kibofu cha mkojo na ubongo ni sehemu ya mfumo wa neva involuntary, unaweza
kuamua ni muda gani unaweza kukojoa - hivyo kuna wengi ambao wanaweza kukaa na
mkoja kwa muda mrefu, lakini hata hivyo ni vyema tukijua kwamba jambo hilo ni hatari
kwa afya zetu.
Hizi hapa ni sababu nne(4) kwa nini hupaswi kukaa na mkojo kwa muda mrefu.
1. Unaweza kupata maambukizi kwenye njia ya mkojo
Kama hukojoi kuna hatari bakteria kuwa wengi/kuzidi katika mkusanyiko wa mkojo huo 
watafiti wa (illusterad vetenskap) wanasema wakati unapokojoa bakteria wanatoka nje
ya vimelea(bomba la mkojo). Bakteria, mara nyingi koli bakteria kutoka kwenye utumbo
inaweza kusababisha magonjwa ya maambukizi kwenye njia ya mkojo ambayo inaweza
kukua na kuwa hatari kwa figo. Hii kwa upande mwingine inaweza kusababisha sumu
kwenye damu utafiti umegundua hivyo.
2. Kibofu cha mkojo chaweza kuvuja mara kwa mara.
Kama unatunza mkojo mara nyingi kibofu cha mkojo wako kitatanuka na kuwa kilegevu.
Hii inaweza kusababisha tatizo la udhaifu wa kibofu kuwa mtepetevu ambapo mkojo
unaweza kuwa unatoka wenyewe matone  matone  kila wakati na matone huishia
kwenye nguo ya ndani na hapo ndipo mtu hujikuta unanuka mkojo mara kwa mara.
3. Unaweza kusababsha uharibifu wa figo:-
Mkojo unaozalishwa katika figo wakati unapoutunza mkojo huo kwa muda  mrefu kiasi 
cha kibofu cha mkojo kukaza kwa kuzidiwa basi figo hufanya kazi ya kupeleka mkojo
katika njia ya bomba la mkojo kwa shinikizo (presha) na unapoendelea kuzuia ndipo
unaposababisha athari kiafya. Utafiti wa Illustrared Vetenskap umebainisha kwamba hali
hiyo inaweza kusababisha uharibifu wa figo.
4. Kibofu cha mkojo kinaweza kupasuka na tumbo lako kujaa mkojo.
Kibofu cha mkojo kinaweza kupasuka. Lakini ni nadra, kwa kawaida watu ambao
wamepata tatizo la kibofu cha mkojo au ulevi ambapo mwili waweza "kusahau" kukojoa.
Wakati kibofu cha mkojo kikipasuka mkojo hutawanyika katika tumbo na unaweza
kueneza maambukizi na pia huwa na maumivu makali sana na athari nyingine kiafya.
NIMEONA NIWASHIRIKISHE HABARI HII ILI TUWE MAKINI KWENDA DAIMA HAJA
NDOGO PALE TUNAPOHITAJI, ILI KUEPUKA HIZI HATARI.
CHANZO: NEWSNER VATENSKAP.

Tuesday, March 22, 2016

JINSI TUNAVYOSONGEKA KIMAISHA

Nimeamka leo nikakumbuka kitabu MAISHA NA MAFANIKIO KILICHOANDIKWA NA MUNGA TEHENNA. Baada ya kukirudia tena kusoma nikakutana na habari hii, binafsi nimeipenda na kuelimika. Nikaona si mbaya kama na mwenzangu ukapata elimu hii...KARIBUNI.
------------------------------------------------------------------------------------------------------------

YUPO NDANI YA MSONGO MKALI
Shirika la Afya Dunian (WHO) linaeleza kwamba, msongo ndiyo utakaokuwa unashika nafasi ya pili kwa kusababisha vifo kwa watu katika nchi zinazoendelea kufikia mwaka 2020. Siyo vifo tu bali hata kusababisha kuondoka kwa uwezo wa watu katika kuwajibika.
Kwa sasa zaidi ya watu milioni 340 duniani wanasumbuliwa na msongo. Kwa ujumla tatizo hili limevuruga zaidi  ya moja kwa kumi (10%) ya muda wa uzalishaji duniani. Zaidi ya nusu ya wale wenye tatizo hili  huwa hawajui kwamba wanalo na hata walio karibu yao kiuhusiano huwa pia hawajui kwamba, wenzao wako kwenye tatizo. Je, sisi tuko kwenye usalama kiasi gani? Je, tunajua au hatujui kwamba tuko kwenye kusongeka? Na tukijua kwamba tunalo tatizo hilo tutatoka vipi?...

Mara nyingi tunakereka, kuvunjika moyo, kuhuzunika na kusononeka, lakini maisha yanaendelea, hayasubiri. Kipitia kusononeka na kusongeka kwwenye maisha tunapoteza uwezo wetu wa kuiona na kuikubali hali halisi na hatimaye pia tunaweza kupateza maisha yetu....
Hebu tuangalie baadhi ya dalili zifuatazo ambazo  huwa zinatusumbua  katika msongo:-

*Kuwa kwenye huzuni ya muda mrefu kunahesabiwa kama dalili ya sononi.
*Kukosa nguvu kwa maana ya mtu kuhisi hana uwezo wa kufanya shughuli au mambo mengi.
*Kupoteza matumaini na hisia kwamba mtu hana thamani.
*Kushindwa kufurahia mambo au shughuli zile ambazo hapo nyuma mtu alikuwa anazifurahia.
*Kushindwa kuzingatia mambo, iwe masomo, mazungumzo au shughuli.
*Kulia bila sababu za msingi na pengine kukosa au kushindwa kuzuia uliaji huo.
* Ugumu katika kufanya uamuzi wa aina yoyote hata ule mdogo au unaohusu mambo madogo
    madogo.
* Kuhisi kukosa amani na kuwa kama vile mtu anawashwa kwenye hisia zake, hivyo kuhisi kukereka
   tu.
*Kulala kwa ziada, yaani kuwa na ongezeko la kiwango cha usingizi. Tunasema, kulala-lala. Lakini   
  kwa wengine, badala ya kuwa na usingizi wa ziada, hupoteza usingizi kabisa. Hivyo, tunasema
  kukosa usingizi.
*Maumivu ya maeneo mbalimbali ya mwili ambayo hayana maelezo ya chanzo chake hasa.
*Matatizo ya tumbo, hasa udhaifu wa usagwaji wa chakula. Kukosa choo huweza kujitokeza.
*Kupungukiwa na hamu ya tendo la ndoa kwa kiwango kikubwa.
*Kuumwa na kichwa mara kwa mara na wakati mwingine kwa kiwango kikubwa.
*Kubadilika kwa hamu ya kula na mara nyingi kupoteza hamu ya kula kunakopelekea udhaifu wa
  mwili.
*Kuwa na mawazo ya kutaka kujiuwa kwa sababu mtu haoni kwa nini aishi. Wengine wanaofanya
  majaribio ya kujiuawa huwa wanakabiliwa na kusongeka kimaisha.
PANAPO MAJALIWA!

Monday, March 21, 2016

KUTOKANA NA BEI YA EMBE KUWA KUBWA NIMEONA BARA NIANZE KULIMA MWENYEWE...FUATANA NAMI KATIKA SAFARI HII NA KUKUZA MTI HUU WA EMBE....

 Mwezi mmoja uliopita bei ya embe ilikuwa nafuu nikanunua na baada ya kula nikawekeza kokwa/koko na tarehe 3/2/2016 nikaatika...Na sasa miezi miwili na siku kumi na nani zimepita na  mche wa embe yangu upo hivi  UJANJA  eeh:-). Kwa pamoja tuufuatilie MWEMBE HUU NA KUONA UTAISHIA WAPI....

Saturday, March 19, 2016

UJUMBE WA JUMAMOSI YA LEO!

"utajiri wa leo ni uzima , na wala sio vipande vya dhahabu au shaba" Na Mahatma Ghandhi.
NAWATAKIENI WOTE JUMAMOSI NJEMA SANA.

Thursday, March 17, 2016

PICHA:- HILI LITAKUWA CHAGUA LA MAISHA NA MAFANIKIO KUWA NI PICHA YA WIKI...PIPA KICHWANI

UJASIRIAMALI:- Ama kweli kutafuta pesa kwataka uvumilivu. Nakumbuka miaka si mingi sana mama yangu alikuwa akifanya hii kazi ya kupika pombe za kienyeji. Alikuwa hana pipa lake binafsi la kupikia pombe. Kulikuwa na kikundi cha akina mama walichanga pesa na kununua pipa. Kwa hiyo hilo pipa lilikuwa la umoja. Lilikuwa halikaa sehemu moja tu lilikuwa likizunguka. Na kwenda kulichukua basi ilikuwa kwa mtindo huo, ila sasa mama yangu alikuwa akitembea kwa mguu kwenda kulichukua hilo pipa. Hapa huyu mama kidogo afadhali. Ila najiuliza swali moja tu  je? hapo kukikutokea kitu cha hatari  au mbele yake kuna watu ambao inabidi awape ishara kuwa yupo nyuma yao na anahitaji kupita atafanyaje? ataachilia huo mkono alioshikilia pipa au? 

Wednesday, March 16, 2016

PALE MTU UNAPOTAMANI MATUNDA UYAPENDAYO LAKINI BEI NAYO INAKOMOA MPAKA HAMU INAKWISHA

Ni juzi tu nilikuwa dukani kapata mahitaji kama kawaida binadamu lazima ale/tule..Nikafika kwenye matunda nikakutana na matunda ya kila aina mojawapo lilikuwa tunda la  EMBE,  nikapata hamu LAKINI KUJA KUANGALIA BEI NIKANYWEA...EMBE MOJA NI Tsh. 4868...mmmhhh nikakumbuka nyumbani jinsi miti ya miembe ilivyozunguka nyumba nikaacha.....nikaendelea na matunda mengine.......
 Nikakutana na karakara (Passion) nikaangalia weee nikapumua kwa hiyo bei tena ...Tsh. 1696 kwa karakara (passion) moja nikaanza kukumbuka.....
Kazi ya mikono yangu...mikarakara yangu(mapassion)

........karakara (passion) zangu nilizonayo nyumbani Ruhuwiko-Songea. Ambazo ni freshi kabisa yaani kutoka tu nje na kuchuma. Nakwambia nusu nilie:-(  Ebu angalia  hapa...basi nikaamua kufanya ubahili. Yaani sikununua nimepata hasira  ya kuanza kuongeza kupanda miche ya mikarakara (mipassio/mipasheni) zaidi... Nguja niache  niwaachie na wengine wasema...panapo majaliwa wapendwa.

Tuesday, March 15, 2016

MAISHA:- JAMBO LA KUKUMBATIANA NA FAIDA ZAKO.........

Kukumbatiana husaidia uzalishaji wa homoni ya "oxytocin" ambayo husaidia sana mwili kuondoa tatizo la kuhisi upweke, hasira na kutengwa.
Unapomkumbatia mtu, unaupa mwili hali ya kujihisi salama na huru pia. Kukumbatiana hufanya misuli isinyae hivyo kuondoa/kupunguza baadhi ya maumivu ya mwili na kuufanya uwe huru. Kukumbatiana huboresha mahusiano ya watu wanaopendana, kwani unapomkumbatia mtu unaonyesha hali ya kupenda, usalama na mapenzi ya dhati. Pia kukumbatiana huondoa wasiwasi. Kama ulikuwa unajiona si wa thamnai, basi ukikumbatiwa unajiona wa thamni. Kumbuka tulipokuwa wadogo, wazazi wetu walitukumbatia na tukajiona tunapendwa na tuko mahali salama. Upendo ule tulioonyeshwa na wazazi wetu unakuwepo ndani yetu kadiri tunavyokuwa watu wazima. Pia unapomkumbatia mtu inakufanya uhisi kupendwa na kuwa wa thamani. Kukumbatia/wa huleta usawa kwenye mfumo wa fahamu kwani wengi wetu tunaishi mazingira yanayoufanya mwili kuwa katika hali ya kujihami muda wote. Hivyo unapomkumbatia/wa mtu mwili husinyaa na kurudi katika hali yake ya kawaida. Kukumbatiana hutufundisha kutoa na kupokea. Kukumbatiana hushusha shinikizo la damu mwilini, mguso wa mwili husababisha neva za kwenye ngozi zinazoitwa "pacinian corpuscles" kupeleka habari kwenye sehemu ya ubongo inayo husika kushusha shinikizo la damu.
Ndio maana watoto wanaokumbatiwa kwa kiasi kikubwa wakiwa wadogo huwa katika hatari ndogo zaidi ya kupata msongo wa mawazo kuliko wasio kumbatiwa vya kutosha.

Friday, March 11, 2016

NAWATAKIENI MWISHO MWEMA WA JUMA HILI...

Juma/wiki hii imekuwa ndefu na majukumu mengi sana. Ila sasa nitapumzika siku mbili tatu na ninaamini nawe unayesoma hapa utapata nafasi ya kupumzika na kuwa na familia/ndugu, jamaa na  marafiki kwani ni jambo nzuri kufanya. Karibuni tujumuike...Nilikuwa nyumbani Ruhuwiko/Songea. IJUMAA NJEMA. Kapulya.

Thursday, March 10, 2016

LEO TUWE KWETU RUVUMA:- NYUMBA YA GHOROFA MOJA KATIKA KIJIJI CHA LIPUMBA WILAYA MBINGA MKOA WA RUVUMA

Nyumba hii ya ghorofa moja imejengwa katika kijiji cha Lipumba katika Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma ambayo Rais wa kwanza wa Tanzania alimsaidia mwenye nyumba bati kwa ajili ya kuipaua, baada ya kuwa imeezekwa kwa nyasi ...inasadikiwa

Wednesday, March 9, 2016

AFYA:- KAMA UANATAKA KUACHANA NA POMBE ZINGATIA HAYA.....

Kama ni mlevi  na unahisi huwezi kuacha kunywa  kwa siku moja, anza kwa kupunguza kiwango cha kunywa, yaaani kama unakunywa bia tatu kwa siku , anza kunywa moja,  baadae  moja kwa siku mbili mpaka utakapozoea kuishi bila pombe/kileo.
Epuka kuweka kilevi au pambe nyumbani au sehemu ya kazi ili kuepuka majaribu.
Usipende kuruka mlo, kula chakula mara tatu (3) mpaka mara nne (4) kwa siku ili kuupatia mwili virutubisho vyote muhimu.
Ondoa dhamira potofu kwamba huwezi kuishi pasipo kunywa pombe. Kumbuka mwili wako umeumbwa kikamilifu kukabili hali zote za maisha, hivyo usihisi kuwa pombe ndio kichochea chako kila unapotaka kufanya jambo fulani.
Zingatia mlo kamili, na jifunze kula matunda kwa mwingi. Hasa kama ulikuwa huli.
Anza kufanya mazoezi na upange ratiba yako ule muda ambao ulikuwa ukitumia kunywa pombe.
Kumbuka mambo mabaya yaliyokutokea kutokana na pombe katika maisha yako. Hii itakusaidia kutothubutu tena  kunywa pombe.
Ongeza unywaji wa maji, jiwekee mazoea ya kunywa maji angalao glasi tano (5)  kwa siku.
Kuwa na tabia ya kujizawadia/kujipongeza kutokana na uamuzi wako mzuri wa kutokunywa pombe.
Ni muhimu kuwashirikisha ndugu, jamaa na marafiki wa karibu kuhusu uamuzi wako wa kuacha pombe/kileo na pia usijione mjinga kwa wale watakao kucheka.
PANAPO MAJALIWA.KAPULYA WENU!

Tuesday, March 8, 2016

PALE WATOTO WANAPOSHIRIKI KAZI KAMA HIZI.....

Hapa tunaona jinsi watoto hawa wannavyobeba matofari  na kupanga  tanuru la matofari. Je? hapa ni kujifunza kazi au ajira mbaya kwa watoto. Maana nina uhakika kwa umri wao ilibidi wawe darasani.Au unafikiri labda ni kazi tu za ziada baada ya shule kujitafutia pesa za kununua daftari na kalamu? ..mmmhh Kweli watu tumetoka mbali....
Mtoto huyo na jembe begani, hii imenikumbusha mbali sana...maana nilikuwa nikitoka tu shuleni najificha kukwepa kwenda shambani kupalilia viazi (mbatata):-) Naona nisiseme sana... TUPO PAMOJA...KILA LA KHERI!

Monday, March 7, 2016

JUMATATU HII TUANZE HIVI! MUHIMU:- FAIDA KUMI ZA KUNYWA MAJI MOTO YENYE LIMAO KILA UNAPOAMKA

1. Huongeza kinga yako ya mwili hasa kupambana na magonjwa madogo madogo kama vile mafua  na kikohozi kutokana na kuwa na vitamini C
2. Husafisha mfumo wako wa chakula, kuondoa sumu mwilini na kuzuia gesi kujaa tumboni mara kwa mara.
3. Huleta hewa safi kinywani.
4. Hukuongezea uchangamfu na kufanya siku yako ianze vizuri sana.
5. Husaidia majeraha kupona kwa haraka kutokana na kuwa (ascorbic acid) asidi  ya kutosha. Pia huimarisha mifupa.
6. Husaidia mmengènyo wa chakula utakachokula asubuhi au mchana kwa kuondoa vikwazo vyote vinavyoweza kuzuia umengényaji wa chakula.
7. Huimarisha ngozi yako, kuondoa makunyanzi na kukupa muonekano mzuri.
8. Husaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uzito kwani maji moto ya limao huyeyusha mafuta ya kutosha
9. Huyapa macho yako afya nzuri na kuimarisha kuona
10. Huondoa hali ya kuhitaji kahawa kila asubuhi ambayo si nzuri kiafya.

Friday, March 4, 2016

IJUMAA YA LEO TUPO KATIKA SOKO LA NAMTUMBO NJE KIDOGO YA MJI WA SONGEA

Hebu angalia hapa vyakula vyetu vya asili yaani hata kuangalia tu unashiba... umeona eehh. Nyanya, Tangawizi na vyakula vingine kwa wingiiii...Mmmmhhh ngoja NIWATAKIENI IJUMAA NJEMA. PANAPO MAJALIWA TUTAONANA.

Tuesday, March 1, 2016

NI MWEZI MPYA, SIKU MPYA YA JUMANNE NA JIKONI LEO ILIKUWA HIVI:-.....

 Nilianza kwa kuandaa saladi ya karoti- ambayo ilikuwa na karoti 3-4, nusu kitunguu maji, mbegu za maboga zilizokaushwa vijiko viwili vya mezani, vijiko viwili vya mezani mafuta upendayo chumvi kidogo na pilipili manga kidogo pia limau kwa mbali.  Unaweza kula kama ilivyo au mkate kidogo lakini mimi/sisi tuliamua....
... sahani iwe hivi samaki, njegere, viazi vya kuponda  na hiyo saladi ya karoti ikawepo. Na kuteremshia ni gilasi ya maji. .....KARIBUNI TUJUMUIKE.....