Nadhani wengi hasa mlio na umri wangu mnakumbuka kitabu hiki au vitabu hivi ya TUJIFUNZE LUGHA YETU. Leo nimekumbuka shairi hili...haya fuatana nami......Karudi baba mmoja, toka safari ya mbali,
Kavimba yote mapaja, na kutetemeka mwili,
Watoto wake wakaja, ili kumtaka hali,
Wakataka na kauli, iwafae maishani.
Akatamka mgonjwa, ninaumwa kweli kweli,
Hata kama nikichanjwa, haitoki homa kali,
Roho naona yachinjwa, kifo kinanikabili,
Kama mwataka kauli, semeni niseme nini.
Yakawatoka kinywani, maneno yenye adili,
Baba yetu wa thamani, sisi tunataka mali,
Urithi tunatamani, mali yetu ya halali,
Sema iko wapi mali, itufae maishani.
Baba aliye kufani, akalibi lile swali,
Ninakufa maskini, baba yenu sina hali,
Neno moja lishikeni, kama mnataka mali,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.
Wakazidi kumchimba, baba mwenye homa kali,
Baba yetu watufumba, hatujui fumbo hili,
Akili yetu nyembamba, haijajua methali,
Kama tunataka mali, tutapataje shambani?
Kwanza shirikianeni, nawapa hiyo kauli,
Fanyeni kazi shambani, mwisho mtapata mali,
Haya sasa burianai, kifo kimeniwasili,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.
Alipokwisha kutaja, fumbo hili la akili,
Mauti nayo yakaja, roho ikaacha mwili,
Na watoto kwa umoja, wakakumbuika kauli,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.
Fumbo wakatafakari, watoto wale wawili,
Wakakata na shauri, baada ya siku mbili,
Wote wakawa tayari, pori nene kukabili,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.
Wakazipanda shambani, mbegu nyingi mbalimbali,
Tangu zile za mibuni, hata zitupazo wali,
Na mvua ikaja chini, wakaona na dalili,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.
Shamba wakapalilia, bila kupata ajali,
Mavuno yakawajia, wakafaidi ugali,
Wote wakashangilia, usemi wakakubali,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.
Wakawanunua ngómbe, majike kwa mafahali,
Wakapata na vikombe, mavazi na baiskeli,
Hawakuita pombe, sababu pombe si mali,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.
Wakaongeza mazao, na nyumba za matofali,
Pale penye shamba lao, wakaihubiri mali,
Walikiweka kibao, wakaandika kauli,
KAMA MNATAKA MALI, MTAYAPATA SHAMBANI.
NA HAPA NI MWISHO....!!!!