Friday, April 30, 2010

Usifikiri kuwa na mikono ndio kuweza kila kitu +Angalia Maajabu haya!!

Je ungekuwa mimi au wewe unayeangalia hapa ungeweza/tungeweza. Kujiamnini ni kitu kizuri sana.

Wednesday, April 28, 2010

Kuna wale wanaojikuta wanadanganya bila hiari!!!

Inasemekana wasichana wengi hudanganya juu ya umri wao

Inaweza ikatokea tukajikuta tumedanganya mahali ambapo wala hatukuwa na sababu ya kudanganya , tena mbaya zaidi tukawadanganya watu ambao ni wazi ingepaswa kutuuma sana kwa kuwafanyia hivyo. Watu ambao ni waelewa, wanaotuheshimu na kutupenda.
Hebu fikiria kuhusu bosi wako, mkeo, mumeo au hata rafiki tu ambaye anakuuliza juu ya jambo fulani ambalo ni wazi hata ukisema ukweli halitakudhuru wala kubadali chochote kwenye maisha yako. Unamwambia au kumjibu uongo, halafu baadaye anagundua kuwa ulimdanganya. Unaingia kwenye fedheha na aibu na kutokuaminika tena.

Kuna watu ambao wana laana ya uongo, yaani hujikuta tu wamedanganya juu ya jambo ambalo kwa kweli hawakupaswa kulidanganyia. Inaweza kuwa ni jambo dogo na la kawaida na watu wanaodanganya hawakupaswa kabisa kuwadanganya. Wenyewe (hao wanaodanganya) huwa wanajua kwamba wanafanya vibaya kwa kudanganya huko na kujisikiavibaya pia, lakini hawana uwezo wa kujizuia. Huwa wanajiuliza ni kwa sababu gani wamedanganya kuhusu jambo hilo na hujisikia vibaya.
Pengine kabla ya kuwazungumzia watu hawa wanaodanganya bilafaida au wanaodanganya bila hiari zao, ni vema tukabainisha kwamba kwa walio wengi kudanganya ni njia ya kuepuka matatizo. Mtu anapodanganya anafanya hivyo baada ya kuona kwamba bila kutumia uongo anaweza kuingia kwenye matatizo, ambayo angeweza kuyaepuka au kuyaepuka kwa muda kwa kusema uongo.
Uongo hata hivyo haupo kwa kila mtu. Kuna watu ambao hawawezi kabisa kudanganya, hata pale ambapo uongo mdogo ungeweza kuwaokoa kutoka kwenye adhabu kubwa. Lakini kuna wale ambao katika kauli zao kumi ni lazima zaidi ya tano zitakuwa za uongo.
Ni vizuri hata hivyo tutafafanua kwamba, hapa tunazungumzia kusema uongo na siyo kusema mambo ya uongo. Kuseama uongo ni kama huko ambapo mtu anaweza kusema kwamba alikuwa kwa dada yake wakati alikuwa kwa rafiki yake au kusema kwamba amelipia kitu fulani wakati hajafanya hivyo. Kusema mambo ya uongo ni kule ambako mtu anasema alipigana vita vya Kagera huku wakati huo hata meno alikuwa hajaota. Hivyo hatuzungumzii kusema mambo ya uongo, bali kusema uongo.
Kusema uongo ni tabia ambayo chimbuko lake kwa sehemu kubwa ni kutoka utotoni, kutoka katika malezi. Inaweza pia kuwa ni tabia ya kuiga, ambapo mtu huiokota katika mazingira anamokulia wakati wa makuzi yake. Hebu tuchukulie mtoto ambaye anakulia katika familia ambapo mzazi mmoja au wote ni wakali sana kwake. Kutokana na ukali huo, mtoto anajifunza kudanganya kama njia pekee ya kuepuka adhabu na kufurushwa mara kwa mara. Ni rahisi sana kwa mtoto huyu kuichukua hadi ukubwani amabako nako ataitumia kama silaha ya kujihami na adhabu au shutuma.

Kuna wakati tunajikuta tukidanganya katika mambo madogo na kwa watu ambao hatukuwa na sababu ya kuwadanganya kwa sababu ya kuhisi kwamba ukweli utatushushia hadhi na kuogopa kwamba watu hao wataanza kututazama vingine. Kwa mfano, mtu fulani ametuuliza kama tumefanya jambo fulani ambalo hatujalifanya, tunaweza kumdanganya, hata kama kusema kweli kusingesababishia lolote baya.
Tunadanganya kwa kutokuwa na uhakika kama kusema kweli kwetu tusingeweza kutuletea matatizo. Lakini hisia kama hizo haziji tu zinakuja kwa sababu ya uzoefu fulani wa utotoni. Huenda tulizoea kila tukisema ukweli tunapigwa au kuadhibiwa hata kama ukweli huo ndiyo hali halisi. Lakini pia inawezekana tulipokuwa wadogo, kauli na vitendo vya wazazi wetu vilituonyesha kwamba, mtu anapokuwa mkweli katika mazingira au uhusiano wa aina fulani anajiingiza matatizoni.
Kusema uongo ni udhaifu, kusema uongo kunaashiria mtu kuwa na mambo mengi, migogoro mingi, malimbikizo mengi ya shida za utotoni, ambazo zingehitaji msaada wa kiulaalamu kuweza kuondolewa. Kama mtu unajikuta huwezi kujizuia kusema uongo hata kwenye yale mazingira ambapo hukupaswa kudanganya, ni lazima ujue kwamba una matatizo mengi ya kisaikolojia ambayo yanaweza kuwa yanakuharibia maeneo yako mengine ya kimaisha.

Ni vigumu kusema ni kwa namna gani unaweza kujitoa kwenye tabia hii ya kusema uongo, hasa uongo ambao wala huna sababu ya kuusema na kuusema kwa mtu ambaye wala huna sababu ya aina yoyote kumdanganya. Uongo ambao baada ya kuusema huwa unakukera, lakini unashindwa kuuzuia. Hii ni kwa sababu, kama tulivyobainisha mapema, vyanzo na sababu za mtu kuwa na tabia ya uongo wa aina hii ni vingi.

Njia iliyo bora kabisa ni kwa mwenye tabia hii kuwa mkweli na mhusika, yaani aliyemdanganya. Kuwa mkweli kwa kumwambia kwamba, amemdanganya kuhusu jambo fulani ambalo hana sababu au hakuwa na sababu ya kumdanganya. Kujiadhibu kwa namna hii kwa kujishushua mwenyewe kwa mtu aliyemdanganya, huweza kumfanya mtu mwenye uongo huu kuanza kuichukia tabia yake, kwani itakuwa inamdhalilisha, hivyo uwezekano wa kuiacha huwa mkubwa. Tukumbuke kwamba kuwaambia ukweli waliowadanganya hakuwezi kuwaathiri chochote waongo hawa, kwani uongo wao huwa hauna maana na hauathiri chochote hata kama ungekuwa ni kweli.
Habari hii chanzo ni Gazeti la Jitambue.......

Tuesday, April 27, 2010

HONGERA KWA SIKU YA KUZALIWA DA MIJA/MWANAMKE WA SHOKA!!

Mwanamke wa shoka Da Mija Shija Sayi


Ni furaha kuwa na rafiki kama Da Mija na leo ni siku tukufu kwako. Ni siku ambayo ulitokea hapa duniani . Napenda kukutakia yote mema, uishi miaka mingi uwe bibi kizee na wajukuu wengi uwe nao. Mija, kama wote tunavyomfahamu alizaliwa hapa dunuani ili awe mwanamke wa shoka nakuheshimu na pia nakupenda sana .HONGERA KWA SIKU YA KUZALIWA RAFIKI YANGU na MWANAMKE WA SHOKA WETU!!!!!!

Monday, April 26, 2010

Jamani Elimu haina mwisho!!! Msikilize mwanamke huyu wa shoka asemavyo!!

TOVUTI/BLOG MPYA YA VIJANA FM !!

Shikamoo dada Yasinta,

Kwa niaba ya timu nzima ya Vijana FM nakuomba unisaidie kuitangaza tovuti/blog mpya ya www.vijanafm.com / www.vijanafm.blogspot.com.

Natanguliza shukrani za dhati na unakaribishwa kutoa maoni. Kama unaona kuna sehemu tunapaswa kuboresha zaidi usisite kuwasiliana nami.

Steven.
Kwa niaba ya Vijana FM.

Sunday, April 25, 2010

NGOJA LEO TUSALI KWA PAMOJA :- SALA YA ASUBUHI

Siku mpya inaanza, Nimuabudu Mungu kwanza,Mungu wangu baba yangu, upokee shukrani yangu. Wewe kwa usiku mzima, ulikuwa kwangu daima,kunilinda kwa amani na mitego ya shetani. Kwako baba wa milele, Ninaomba neema tele, Niepuke dhambi zote. Nikutumikie pote. Ubariki kazi yangu, Shida na furaha Zangu. Mama safi ee Maria, Nipe msaada wako pia. Ee malaika kiongozi, Nipeleke kwa Mwokozi. Yesu nijalie neema, Niwe daima mkristo mwema. Amina.

NA KUMBUKENI NI JUMAPILI YA 17 YA MWAKA. JUMAPILI NJEMAZ WOOOOTE!!!

Saturday, April 24, 2010

HONGERA KWA SIKU YAKO YA KUZALIWA MARIA FIDELIA NKUGI BINTI WA Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!


Nimeona nami nikuweka hapa mna kukutakia siku yako ya kuzaliwa. Napenda kukutakia siku hii maalum HONGERA sana kwa siku yako ya kuzaliwa na nakutakia maisha marefu na mema. Pia ukue, uwe na afya njema na uwatii baba na mama na watu wote katika dunia hii.

Friday, April 23, 2010

HIVI NI KWANINI TUWE WATU WA MAJUNGU?


“Wanawake wakipeana michapo”

Kuna mada moja nimeisoma katika blog ya Je huu ni uungwana, ya Mfalme Mrope. Mada hiyo imenivutia sana kwa kuwa yaliyoelezwa humo, ni mambo ambayo binafsi nimeyashuhudia huku ughaibuni. Kwa kuisoma mada hii unaweza kubofya hapa

Kwa kawaida zipo tabia mbazo katika kila jamii inajulikana kuwa nazo, kwanza zipo tabia za kimakabila, kiukoo na za kijamii yaani za nchi kwa ujumla. Kwa sisi Watanzania tunajulikana kwa wenzetu huku ughaibuni kuwa ni wakarimu, wapole na wanyenyekevu kupindukia, japokuwa unyenyekevu wenyewe hauna hata tija lakini kwa kweli tumevikwa sana kilemba hiki cha ukoka, tukitofautishwa na jirani zetu wa Kenya na Uganda.

Lakini sifa hizo zinavuma kwa kuwa aidha tunawafanyia wageni au zinaonyeshwa sana kwa wageni. Hata wewe unayesoma hapa unaweza kushangazwa na sifa hizo kwa kuwa huenda zikakuacha mdomo wazi kutokana na kile unachokishuhuda au ulichokishuhudia hapo nyumbani.

Hebu jiulize kwa nini siku hizi hapo nyumbani magazeti yanayoongoza kwa mauzo ni yale yanayoandika habari za umbeya na majungu yaani magazeti ya udaku? Tuache magazeti ya udaku tuje kwenye Mitandao, hivi umeshawahi kujiuliza ni kwanaini habari au mada zinazopata wachangiaji wengi kupindukia ni zile za majungu umbeya na fitina?

Labda kama hujui leo nitakujuza maana hili nimekaa nalo mwishowe nimeona potelea mbali ngoja niliseme.

Kuna baadhi yetu sisi Watanzania tuna tabia mbaya sana ya umbeya na majungu. Ndio lazima niseme ukweli. Kama huamini hebu fanya utafiti kwa kupitia magazeti ya udaku na mitandao yenye habari za udaku utakubaliana na mimi.

Kama hutakuta habari za kujadili maisha ya mtu, basi utakuta kuna mtu kazushiwa kashfa makusudi ili kumdhalilisha au kumshusha. Kutokana na magazeti hayo kuruhusu kuletewa habari, kuna watu wanakesha usiku kucha kutafuta namna ya kumkomoa mtu ili mradi apate jambo ambalo kama likiandikwa huyo muhusika ni lazima litamuharibia.

Wakati naondoka nyumbani miaka 15 iliyopita kuja huku Ughaibuni hali haikuwa kama ilivyo leo hii. Kulikuwa hakuna mitandao na wala magazeti ya udaku. Na sifa kuu niliyoondoka nayo ni ile ya ukarimu, upole na unyenyekevu tuliyo nayo Watanzania.

Kwa kawaida unapoishi mbali na nyumbani kwenu ulipozaliwa, hususana huku ughaibuni, unapata shauku sana ya kuwajua wenzako mliotoka nchi moja au hata mji mmoja, kabila moja na kadhalika lengo ni kukumbushana habari za nyumbani kubadilishana mawazo na kutembeleana.

Lakini kumbe kukaa kwangu huku sikujua kama mambo yamegeuka, kwani, nilishangaa sana kuona kuwa kila niliyejaribu kuwa naye karibu, mweh!. Mazungumzo niliyokutana nayo yalikuwa ni ya kujadili watu. Unaweza kumtembelea mtu kwa minajili ya kubadilishana mawazo tena ukiwa umeambatana labda na familia yako lakini utashangazwa na mazungumzo ya mwenyeji wako, unaweza kukuta muda wote tangu ufike hapo ni mazungumzo ya umbeya na majungu. Hapo watazungumziwa watu mwanzo mwisho, mpaka unajiuliza hivi na mimi kesho si itakuwa ni zamu yangu hapa akija mwingine.

Unaweza kushangaa mtu anaweza kumzungumzia mtu jinsi anavyoishi na familia yake huku ughaibuni mpaka hali ya kijijini kwao alikozaliwa utadhani wametoka kijiji kimoja, kumbe siyo.

Awali nilikuwa nikishangaa hii tabia imetoka wapi, lakini baada ya kuanza kublog na Kutembelea mitandao mbali mbali ndio nikaaanza kupambazukiwa. Nilipokwenda nyumbani likizo ndio nikakutana na magazeti ya udaku. Kuanzia hapo nikajua kumbe tatizo hili limeanzia nyumbani.

Kwa huko nyumbani inawezekana ni kutokana na watu kukosa shughuli za maana za kufanya, au kutokana na ulimbukeni wa uhuru wa vyombo vya habari, na kurasa za mitandaoni, hivi vitu bado ni vigeni kwetu, lakini je kwa sisi tunaoishi huku ughaibuni hili linawezekana kweli?

Mahali ambapo kuna ushindani mkubwa wa ajira na gharama za maisha zilivyokuwa juu, bado mtu unapata muda wa kukaa na kumchunguza mtu, maisha yake na kupata muda pia wa kumjadili. Huo muda kama ungetumika katika kubuni mambo yenye kuleta tija tungekuwa wapi kimaendeleo au tungekuwa tumewawezesha ndugu zetu au familia zetu huko nyumbani kwa kiasi gani.

Sikatai zipo baadhi ya familia na marafiki ambao wamestaarabika na wanajistahi, hawa wameendelea kuwa marafiki zetu wazuri huku tukitembeleana na kubadilishana mawazo.
Tumeendelea kushirikiana kwa kila hali na mali, bila kusigishana.

Nadhani kuna haja ya kujikagua na kujirekebisha, kwani tunatia sana aibu machoni mwa wenzetu. Nakubali kuwa kila jamii inayo mikabala tofauti, lakini mikabala hiyo inapokuwa ni ya kuoneana kijicho, husuda na kukashifiana, tutakuwa tunajifedhehesha bure.

Ni vyema tukaunganisha nguvu na kuishi kama ndugu huku tukijadili matatizo ya nyumbani ili kusaidia kuleta maendeleo huko nyumbani tulipoacha familia zetu. Kwa mfano Blog na Mitandao ingetumika kama chachu ya kuhimiza maendeleo huko nyumbani kwa kuchukua yale mazuri ya wenzetu na kuwahabarisha watu wa nyumbani na kuibua mijadala yenye tija katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo huko nyumbani. Kama wote tunajenga nyumba moja kuna haja gani ya kugombea fito na kutiliana fitina miongoni mwetu?

Thursday, April 22, 2010

BWANA MATATA HAJUI KUSOMA+KUMBUKUMBU

Je? huyu naye ni bwana matata?


Mada hii nilishawahi kuiweka hapa kibarazani, lakini leo katika pitapita nimekukta picha hii nikakumbuka na nimeona si mbaya kama tukijadili tena kwa pamoja picha nimeipata hapa Haya soma haabari yenyewe hapa chini kuhusu bwana matata.

Namshukuru babangu kwa kutunza kitabu hiki leo nimefurahi sana nadhani hata wenzangu mtafurahi pia kukumbuka hadithi hii:-
Bwana Matata yupo mjini, anauliza uliza njia ya hospital. Kuna kibao hapo njiani, lakini haui kusoma kibao.Bwana Matata anaona aibu kuuliza njia tena, anaona aibu kwa sababu hajui kusoma. Sasa anafuata njia ya bomani
Bwana Matata amechoka sana. Amechoka na safari, pia amechoka kuuliza uliza njia. Amelala kwenye kibao, kibao kinasema HATARI. Lakini Bwana Matata hajui kusoma, tena amechoka mno. Amelala njiani kwenye kibao

Bwana Polisi anapita, anamwona Bwana Matata amelala kwenye kibao. Bwana polisi anamwita, mzee vipi? Kwa nini unalala hapa? Huoni kibao? Lakini Bwana matata amechoka sana amelele kama gogo. Polisi amawita tena, kwa nini unalala hapa kama gogo? Kuna hatari hapa. Lakini bwana matata hana habari ya hatari hajui kusoma.

Bwana Matata akaamka, akasimama na kumwambia polisi, nataka kwenda hospitali. Mtoto wangu yupo hospitali ni mgonjwa sana, lakini nimepotea njia. Bwana polisi akasema, umepotea njia? Fuata hii Bwana Matata akafuata njia ile. Kinachoendelea naadhani mnajua

Wednesday, April 21, 2010

Ngoja leo tuangalie baadhi ya Vitendawili/Mafumbo = Gåtor

KISWAHILI:- 1. Ni kitu gani chaweza/kinaweza kutembea lakini sio kukimbia?

KISWIDI:- Vad kan gå men inte springa?

KISWAHILI:- 2. Wakati tunapokuwa nje na miguu yetu tunajion kweli tupo ndani. Ni nini hicho?

KISWIDI;. Först när man är ute med fötterna är man riktigt inne. Vad är det?

KISWAHILI:- 3. Ni nini kinakuwa kikubwa na kikubwa zaidi wakati unataka kitoke/kukitoa?

KISWIDI:- Vad är det som blir större och större ju mer man ta bort?

KISWAHILI:- 4. Ni kitu gani cheusi na cheupe na kina miguu 236 na kinaruka angani/hewani?

KISWIDI:- Vad är det som är svart och vit och har 236 ben och flyger i luften?

KISWAHILI:- 5. Hivi kwa nini tunanunua nguo?

KISWIDI:- Varför köper vi egentligen kläder?

Tuesday, April 20, 2010

The Woman!!!


When God created woman he was working late in the 6th day.
An angel came and said..

"why sped so much time on that one?"

And the Lord answered..

"Have you seen all the specifications I have meet to shape her?, she must be washable, but not made of plastic, have more than 200 moving parts which all must be replaceable and she must be able to embrace several kids at the same time, give a hug that can heal anything from a bruised knee to a broken heart and she must do all these things with only two hands"

The angel was impressed

"Just two hands....impossible, and this is the standard model?!,too much work for one day...wait untill tomorrow and then complete her"

"I will not", said the Lord. I am so close to complete this creation, which will be the favourite of my heart, she cures herself when sick and she can work 18 hours a day"

The angel came nearer and touched the woman.

"But you have made her so soft Lord"

"She is soft", said the Lord, "But I have also made her strong, you can imagine what she can endure and overcome"

"Can she think?" the angel asked.

The Lord answered:

"Not only she can think, she can reason and negotiate"

The angel touched the woman's cheek..

"Lord it seems this creation is leaking, you have put too many burdens on her"

"She is not leaking...it is a tear" the Lord corrected the angel

"What's it for?" asked the angel

And the Lord said..
"Tears are her way of expressing her grief, her doubts, her love, her loneliness, her suffering and her pride"

This made big a impression on the angel.,

"Lord you are genius, you thought of everything. The woman is indeed marvellous!"

"Indeed she is, woman has strength that amazes man, she can handle trouble and carry heavy burdens. She holds happiness, love and opinions, she smiles when feeling like screaming, she sings when she feels like crying, crys when she feels she is happy and laughs when she is afraid, she fights for what she believes in, stand up against injustice, she doesn't take "no" for an answer when she can see a better solution. she gives herself so her family can thrive, she takes her friend to the doctor if she is afraid, her love is unconditional.
She cries when her kids are victorious, she is happy when her friends do well. She is glad when her friends do well.,she is glad when she hears of a birth or a wedding , her heart is broken when a next of kin or friend dies, but she finds the strength to get on with life, she knows that a kiss and a hug can heal a broken heart".

There is only one thing wrong with her...

"SHE FORGETS WHAT SHE IS WORTH"


Habari/tungo hii nimeidesa mtandaoni na nimeipenda na nikaona ni vema nikiweka hapa ili ujumbe uwafikie wengi. Bonyeza hapa.

Sunday, April 18, 2010

HUU NI UJUMBE WA JUMAPILI HII YA LEO!!!

Wapo watu ambao nyoyo zao ni kama lulu au almasi inayongáa kwa usafi, hazibebi chuki, choyo wala kejeli, bali hubeba mapenzi, imani na ukarimu. Hakika hata wewe unayesoma hapa ni mmojawapo. NAWAPENDA NYOTE.

Tufurahia jumapili hii kwa wimbo huu SISI SOTE NI NDUGU ulioimbwa na Innocent Galinoma....karibuni sana!!

NA NI DOMINIKA YA 16 TANGU MWAKA HUU UANZE.!!!!!

Saturday, April 17, 2010

Volkano yaendelea kukwamisha usafiri wa anga


Sehemu nyingi za bara Ulaya zitaendelea kukosa usafiri wa ndege mpaka alfajiri ya Jumamosi kutokana na anga kujaa majivu ya volkano yanayotimka kutoka Iceland, maafisa wameeleza.
Sehemu kubwa ya anga la safari za ndege maeneo mengi ya Ulaya kaskazini na magharibi limefungwa, huku pungufu ya nusu ya idadi za safari za ndege zikifanyika Ijumaa.

Maelfu ya abiria barani Ulaya na kote duniani wameathirika kutokana na athari za majivu hayo ambayo yanadaiwa yanaweza kuharibu injini za ndege zinapokuwa angani.

Wanasayansi wanasema volkano bado inatimka ingawa inatoa majivu kidogo ikilinganishwa na mwanzo.

Volkano ya Eyjafjallajokull ilianza kulipuka siku ya Jumatano kwa mara ya pili mwezi huu na kurusha majivu umbali wa kilometa 11 kwenda angani.

Habari hii nimeipata kutoka BBC nimeona ni vizuri wengi tujue.zaidi unaweza kusikilöiza hapa http://www.bbc.co.uk/swahili/news/story/2010/04/100416_ndege_ulaya.shtml

Thursday, April 15, 2010

Ubakaji unavyodidimiza elimu Karagwe

Watoto wa kike kama hawa wapo hatarini
kubakwa kama hawatopata ulinzi wa kutosha
kutoka kwa jamii



SUALA la ubakaji kwa wanafunzi ni kosa la jinai kisheria na ki jumla linadidimiza maendeleo ya wanafunzi wa kike ambao ni waathirika wakuu.
Wanafunzi hawa huishia kupata mimba au magonjwa mbalimbali hali ambayo huwaathiri kitaaluma na hata na kjamii kwa ujumla. Haja ya kulipinga suala hili hasa kipindi hiki ambacho serikali inapigania kwa nguvu zote haki za mtoto wa kike awapo shule na pindi apatapo mimba akiwa shuleni.
Serikali ilishapitisha pia utaratibu wa kumruhusu mwanafunzi apatapo mimba kurejea masomoni pindi anapojifungua kwa minajili ya kunusuru maendeleo yake kielimu.
Suala la ubakaji katika wilaya ya Karagwe iliyopo mkoa wa Kagera bado lipo juu hivyo kutishia maendeleo ya elimu kwa mtoto wa kike.
Takwimu zinaonyesha kuwa watoto zaidi ya 54 walibakwa katika kipindi cha mwaka 2009, takwimu hizo kwa mujibu wa wakazi wa karagwe wanadai ni ndogo sana ukilinganisha na idadi halisi ya kesi zinazotokea hasa vijijini.
Mbali na ubakaji, wanafunzi kupewa mimba na wengine kuolewa kwa mwaka 2009 pekee walifikia 44 Karagwe ikiwa wilaya ya pili kwa ukubwa wa tatizo hilo ikitanguliwa na wilaya ya Chato yenye wanafunzi 74 waliopata mimba kwa kipindi hicho hicho.
Kwa mkoa wa Kagera kwa ujumla, Katika kipindi cha Januari 2009 hadi Desemba 2009 jumla ya wanafunzi 365 walipata mimba katika kipindi cha Januari mpaka Desemba 2009 kati ya hao wanafunzi 148 walikuwa ni wa shule za msingi na 217 walikuwa wa sekondari.
Wilaya pia ina jumla ya shule za msingi 212, kati ya hizo, shule 204 ni za Serikali na 8 za binafsi zenye jumla ya wanafunzi 105,229 wasichana wakiwa 53,491 na wavulana 51,738.
Shule za sekondari katika wilaya ya Karagwe zipo jumla ya 43 (zikiwemo 34 za serikali na 9 za binafsi). Ongezeko hili limeenda sambamba na sera ya nchi lengo likiwa ni kuchukua ongezeko la watoto wanaomaliza darasa la saba.
Mbaraka Ismaili mkazi wa kijiji cha Kagenyi wilayani Karagwe ambaye mtoto wake wa miaka 14 Fatuma Mbaraka alibakwa na mzee wa miaka 54 Ali Migeyo mwishoni mwa mwaka jana anasema kesi nyingi za kubakwa watoto zinafichwa na kuzimaliza kimila bila kufikishwa mbele ya sheria.
“Kesi za kubakwa wanafunzi hapa kwetu Karagwe zinaishia huko mitaani, aidha wanakubaliana na kumalizana kwa kuoana au kulipana kiasi fulani cha fedha, suala hili linajumuisha uongozi wa vijiji na kata ambao ndio wapo mstari wa mbele kushauri watu wamalizane,†anasema Mbaraka.
Mbaraka pia anasema kuwa “imezoeleka kusikia kesi za wanafunzi kubakwa au kupewa mimba katika maeneo yetu, na hakuna mtu anashangaa hilo, ni tabia mbaya ambayo serikali lazima ichukue hatua ili kunusuru watoto wetu wa kike.†Kwa hapa shule ya msingi Kagenyi tu kwa mwaka jana tulishuhudia kesi tatu za watoto wadogo kubakwa na kupewa mimba, kesi mbili kati ya hizo wazazi walimalizana wao kwa wao kulipana kwa kushirikiana na polisi na ni moja tu ndiyo ilipelekwa mahakamani.
Mbaraka aliwalaumu polisi na viongozi wa vijiji kuwa kikwazo kikubwa katika upatikanaji wa haki za wanafunzi wanaobakwa na wale wanaopewa mimba kwani ndio waliokua mstari wa mbele kuwashawishi wazazi kuyamaliza bila kupelekana mahakamani.
Fatuma Mbaraka anayesadikiwa kubakwa na mzee wa miaka 54 Novemba mwaka 2009, anasema watoto wanaobakwa wengi wao huacha shule kutokana na aibu wanayoipata.
“Mimi mwenyewe baba ndiye ananilazimisha kwenda shule, ila nina mazingira magumu sana kwani kila niendako nachekwa na wenzangu na wananiita mzazi, walimu toka nimebakwa sijawahi kusikia waseme kitu wala kuniita na kuniuliza,†anasema Fatuma huku akitoa machozi.
Mkurugenzi wa wilaya ya Karagwe Consolata Kamuhabwa anasema kuwa tatizo la ubakaji kwa wanafunzi ni sugu ingawa hatua kali zinachukuliwa dhidi ya watuhumiwa pindi wanapofikishwa mbele za sheria.
Kamuhabwa anasema moja ya sababu ya kuongezeka kwa ubakaji kwa wanafunzi ni imani kuwa wanafunzi hawana magonjwa ya zinaa hasa ukimwi, hili ni tatizo kubwa katika wilaya ya Karagwe.
“Watu wengi wanaamini kuwa kumbaka mtu mzima wanajiweka katika hali ya hatari kwa kupata ukimwi lakini kwa mwanafunzi inakua si rahisi kupata magonjwa kama ukimwi,†anasema Kamuhabwa.
Kamuhabwa anatoa sababu zingine zinazosababisha kuongezeka kwa matukio ya kubakwa kwa wanafunzi kuwa ni imani za kishirikina, matumizi makubwa ya madawa ya kulevya kama bangi na pombe kali aina ya gongo.
Anasema “mkuu wa wilaya hii kanali Fabiani Masawe amekuja na mikakati mikubwa ya kutokomeza tatizo hili kwa njia ya adhabu kali, kutoa elimu kwenye vyombo vya habari hasa redio za hapa Karagwe kama radio Karagwe na Fadeco FM ambazo zinasikilizwa zaidi na wakazi wa wilaya hii."
Afisa ustawi wa jamii wa wilaya Mary Kashaija anasema changamoto kubwa inayoikabili wilaya ni wazazi wa watoto wanaobakwa na wale waliobakwa kukaa pamoja na kuelewana kutoyafikisha masuala hayo mbele ya sheria.
“Tabia hiyo inachochea kuongezeka kwa tatizo la ubakaji kwani wanajua hata wakibaka basi watamalizana au kulipa fedha kwa wazazi na hivyo kutochukuliwa hatua, hali hiyo inaturudisha nyuma katika mapambano dhidi ya ubakaji kwa wanafunzi,†anasema Kashaija.
Kashaija alisema "tatizo hili ni kubwa sana, huwezai kaa wiki tatu bila kusikia kesi ya kubakwa wanafunzi,kesi zipo nyingi sana ukilinganisha na zile ambazo hazitufikii, kesi za kubaka na kutokuletwa kwetu ni nyingi kuliko zile zinazoletwa."
Inafikia hatua hata wazazi kuharibu ushahidi kwa kutokutoa ushahidi ili masuala hayo yaishe kwa wao kulipwa, kesi nyingi zinaisha bila adhabu yoyote kwa kukosa ushahidi, hali inatisha kwa kweli lakini tunakabiliana nayo kupitia elimu kwa njia ya vyombo vya habari, alisistiza afisa huyo wa ustawi wa jamii wilaya.
Mkazi wa kayanga wilayani karagwe Ester John alisema kuwa jamii inapaswa kutafakari kwa kuangalia suala zima la ubakaji ili kutafuta ufumbuzi kwani watoto wengi wa kike ndoto zao za elimu zinazimwa kwa tamaa ya baadhi ya wanaume kwa kuwabaka na kuwapa mimba wangali shule za msingi.
“hapa Karagwe tatizo la ubakaji ni kubwa sana mpaka sasa inaonekana kama ni kawaida jambo ambalo linasikitisha kwa kweli, tunaomba serikali itusaidie watoto wetu wanaangamia jamani,†anasema Ester.
Kesi kukosa ushahidi.
Sheria ya Kujamiiana ya mwaka 1998 inaeleza wazi kuwa kufanya mapenzi na mtoto, chini ya umri wa miaka 18 ni kitendo cha ubakaji, kwa kuwa kinafanywa kwa ulaghai na si hiari ya mtoto huyo.
Hivyo, kumfukuza mtoto huyo shule ni kumuadhibu kwa mara nyingine, kwani adhabu ya kwanza kapewa na yule aliyefanya naye mapenzi kwa nguvu au kwa ulaghai na kumpa mimba na ya pili ni kufukuzwa shule.
Kesi nyingi za kubaka wanafunzi wilayani Karagwe huisha kwa watuhumiwa kuachiwa huru kutoikana na kukosa ushahidi wa kutosha kwani wakazi wengi hawana mazoea ya kutoa ushahidi pindi kesi zifikapo mahakamani.
Kashaija anasema kesi nyingi hukosa ushahidi kutokana na gharama kubwa za mashahidi kusafiri kutoka kijijini mpaka wilayani kipindi cha kutoa ushahidi jambo ambalo linakatisha tamaa wazazi kutokana na kuelemewa na gharama na hivyo kuamua kulipana bila kufika mahakamani.
“Wilaya hii ni kubwa sana, utakuta mtu anatoka umbali wa kilometa 100 ili kufika mahakama ya wilaya kutoa ushahidi, kutokana na gharama za nauli kutoka huko mpaka mjini, mashahidi hao hushindwa kusafiri na hivyo kesi kuwa na ushahidi hafifu,†anasema afisa huyo wa Ustawi wa Jamii.
Raisi Jakaya Mrisho kikwete na Mkewe Mama Salma Kikwete wamekuwa mstari wa mbele katika kupigania haki za mtoto wa kike kielimu nchini kote huku raisi akiwataka wakuu wote wa wilaya na mikoa kuhakikisha wanakomesha tabia hizi za mimba kwa watoto wa kike.
Mapambano hayo yanaenda na sera ya kumlinda mtoto wa kike inayomtaka mwanafunzi aliyepata mimba kurudi shule na kuendelea na masomo pindi wajifunguapo ingawa wengi wao wamekuwa hawapendi kurudi shule kutokana na kuona aibu.
Vincent Mnyanyika, HakiElimu (Gazeti la Mwananchi)


Ngoja tumaliza na kumsikiliza dada yetu Saida Karolina wimbo huu (nkyalimuto)

Wednesday, April 14, 2010

KWA NINI WATU WANAOANA?

Kama ukimuuliza au ukiwauliza watu wanaooana, kwamba kwa nini wanaoana au ni kwa nini wako kwenye ndoa? Utapata majibu tofauti tofauti kulingana na namna watu hao wanavyotafsiri neno ndoa. Mimi sitajibu swali hilo lakini labda kile ninachokusudia kukiandika hapa huenda kikakusaidia kupata jibu la kwa nini watu wanaoana.

Kuna ukweli kwamba binadamu wamefanya kuoana kama jambo la kimaumbile, na wakilifunganisha na tendo la ndoa. Mtu anajikuta akioa au kuolewa tu. Hana haja ya kujiuliza ni kwa nini anaoa au kuolewa, kwa sababu anaona watu wanoa na kuolewa na akiangalia umri wake anaona kwamba amefikia umri wa kuoa au kuolewa hana haja ya kutaka kujua sababu. Hivi ni nani aliyepanga umri wa kuoa au kuolewa? Na umri wa kuoa au kuolewa umapangwa kwa kuzingatia vigezo gani? Je kupitisha umri huo kuna athari gani?

Ipo sababu nyingine inayotajwa kuwa watu wanoana kwa sababu wamependana, upendo ninaouona hapa ni wa mtu kumtamani mwenzie awe mwanamke au mwanaume, kwani kwetu sisi tunaamini kuwa kutamani ndio kupenda.

Hivi kama watu wanoana kwa sababu ya kupendana kungekuwa na talaka kweli? Naamini kama kungekuwa na talaka basi zingekuwa ni chache sana, na wanaoachana wasingeachana kwa ugomvi na visasi, bali wangeachana kwa upendo na wangeendelea kupendana na kuheshimiana, kwa sababau upendo ni tofauti na kutamani, upendo upo na utaendelea kuwepo na si vinginevyo.

Utakuta wanandoa wanasema “sisi tumeoana kwa sababu tunapendana” lakini baada ya mwaka wanandoa hao hawaelewani na wanakuwa na ugomvi wa mara kwa mara mpaka kufikia mmoja kumuua mwenzie, huu ndio upendo wa aina gani?

Ndoa za namna hii, hazikuwa ni za upendo bali watu kutamaniana au mtu kutamani mwili wa mwenzie, lakini kulikuwa hakuna upendo miongoni mwao.

Wengi wameoana kwa kufuata mnyororo ule ule wa kuoana kwa kufuata dhana iliyowekwa na jamii kuwa ni lazima watu waoana bila kutafuta tafsiri ya kufanya jambo hilo. Na mara waingiapo katika ndoa huona kama wamejitwisha mzigo mzito wasioweza kuubeba. Kuna zile kauli zinazotolewa ambazo wengi huita usia kwa wanandoa kwamba ndoa ni kuvumialiana, lakini watu hawajiulizi ni nini maana ya kuambiwa ndoa ni kuvumiliana, kuvumiliana kwa lipi? Kuna kitu gani katika ndoa kinachohitaji watu kuvumiliana?

Haya maswali inapaswa watu wajiulize kabla hawajaingia katika ndoa maana kuna mambo mengine hayafai kuvumilia, sasa itakuwaje nikishindwa kuvumilia? Na kuvumilia huko ni mpaka wapi?

Kuna watu wengi wanapata shida katika ndoa kwa sababu hawakujua ni kwa nini wanaoa au kuolewa, inawezekana, waliunganishwa na tendo la ndoa zaidi na sio upendo, na hapo ndipo wanpokuja kugundua kuwa walifanya makosa.

Nadhani imefikia wakati sasa ya watu kujiuliza ni kwa nini wanaoa au kuolewa, kwani ni hii itapunguza magomvi na talaka katika ndoa.Inabidi kila mtu awe na sababu yake mwenyewe ya kuamua kufanya hivyo sio kwa kuangalia sababu zilizowekwa na jamii au kusukumwa na matakwa ya jamii bali uwe ni uamuzi wake mwenyewe bila kushurutishwa au kusukumwa na matakwa ya jamii.

Kama hujaoa au kuolewa isikupe shida tulia, na ukitaka kuoa au kuolewa ufanye hivyo ukiwa na sababu yako binafsi.

Tuesday, April 13, 2010

UJUMBE WA LEO:- NI VYEMA KUIJUA SIRI HII!

Huu ndio ukweli, ukitaka kupata furaha ya maisha

1.Sema kweli
2.Furahia maisha na furahisha wengine, Penda kwa dhati bila unafiki na bila masharti
3.Jiamini
4.Chukia kusema uongo
5.Tetea unachokipenda na kukiamini
6.Ukiwa dhaifu wa kukumbwa na mawazo potofu usichukie kumbuka mawazo pototfu yameumbiwa Binadamu
7Jitahidi kufikiri na kuwaza vyema ili uzidi kujiamini, kujipenda na na kuwapenda wengine. Yote yanawezekana.

Kumbuka usemi huu “ukivuliwa nguo chutama. Ukikosea tubu haraka.
Wastara huwa haumbuki……………

Sunday, April 11, 2010

Nakuomba Mola Wangu

mke mwema

Nimechoka nimechoka, nimechoka peke yangu,
Mwenzenu nataabika, nahisi dunia chungu,
Nimechoka hangaika, namhitaji mwenzangu,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Nahitaji nami oa, kwani muda umefika,
Nimpate aso doa, mke alokubalika,
Niwe nayo njema ndoa, siyo ya kukurupuka,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Binti ntayempata, ajue kumcha Mungu,
Asiwe mwenye kunata, awe'shimu ndugu zangu,
Aitike nikimwita, hata mbele ya wenzangu,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Ajaaliwe nidhamu, nidhamu ya kwelikweli,
Ajawe na ufahamu, kufikiri mara mbili,
Hekima nayo muhimu, mazingira kukabili,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Sitaki mwenye kiburi, huyo ataniumiza,
Sitoitoa mahari, mwenye kukiendekeza,
Napenda ajidhihiri, hivyo asije nitweza,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Awe amefunzwa vema, awe na njema tabia,
Yawe maisha salama, asiruke na dunia,
Mola 'tatupa uzima, tutamtumainia,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Awe na uvumilivu, majira hayafanani,
Siku tukila pakavu, asizue tafrani,
Asitende jambo ovu, kuniweka matatani,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Sitochagua kwa dini, kabila ama kwa rangi,
Nitampenda moyoni, yeyote mi' simpingi,
Anifae maishani, ndilo jambo la msingi,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Na watoto tuwazae, Mungu akitujalia,
Tasa 'simnyanyapae, dunia kuichukia,
Kwa dhiki nikamfae, apate kujivunia,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Kuna kitu namwahidi, kwake nitakuwa mwema,
Sitofanya ukaidi, nitamw'eshimu daima,
Kwani kwake sina budi, kumwongoza kwa hekima,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Nitakuwa mwaminifu, kamwe sitomwumiza,
'Tamjali mara alfu, dhikini kumliwaza,
Na watu watamsifu, maana atapendeza,
Nakuomba Mola wangu, nipatie mke mwema.

Kaditama nimalize, kwa beti zangu dazeni,
Afaaye 'jitokeze, nimweke mwangu moyoni,
Mmoja tu nimtuze, huyo huyo maishani,
NAKUOMBA MOLA WANGU, NIPATIE MKE MWEMA.
Shairi limetungwa na Fadhy mtanga nami nimevutiwa nikaona niweka hapa ili tujifunze kwa pamoja. NA NAPENDA KUWATAKIENI WOTE JUMAPILI/DOMINIKA NJEMA. NI JUMAPILI YA 15 YA MWAKA HUU!!!!


Thursday, April 8, 2010

Hospitali ya Ludewa/ Mambo ndio haya!!

Akina mama ambao wanawauguza ndugu zao katika hosptali ya Wilaya ya Ludewe wakisonga Ugali nje ya wodi ya akina mama wanaosubiri kujifungua, kati ya akina mama 100,000.wajawaito 200 hupoteza maisha katika Wilaya hiyo kutokana na ukosekanaji wa miundombinu.
Wanawake wajawazito toka katika vijiji 76 vinavyo zunguka Wilaya ya Ludewa wakiwa wamelala na wengine wakila chakula huku wakiwa wamesubilia siku zao za kujifungua katika hospitali ya Wilaya ya Ludewa Mkoa wa Iringa kati ya akina mama 100,000 wajawazito 200 hufariki kutokana na ukosefu wa huduma.

Inasikitisha: Baadhi ya akina mama wajawazito wakiwa nje ya wodi ya wazazi katika hospitali ya Wilaya ya Ludewa ambapo jengo hilo lina vitanda 6 na kila kitanda hutumiwa na akina mama wajawazito wawili. Wengine hulazimika kulala chini. (picha na Albart Jackson).

Wednesday, April 7, 2010

Maisha ya uzeeni/Kuishi nyumbani au kituo cha kulelea/kutunzia wazee!!!



Nasi twaelekea huku!!!



Makala hii hapa chini http://tustaarabike.blogspot.com/2010/04/nikionacho-darubini.html nimeipenda ndiyo maana nikaamua kuichukua na kuiweka hapa kwangu kwani taratibu za huko Marekani ni sawa na za hapa Sweden Nami nataka kuongezea ni . Nashukuru kwa kuiweka hii mada -
Kwani najua nakamilisha lengo lake la kuifanya isomwe na wengi. Ni hivi hata mimi nilikuwa nikijiuliza hivi kwanini watu hapa Sweden, kila wakati wanaonekana wapo na shughuli tu kiasi kwamba wanashindwa hata kuwatunza wazazi wao- Kwa nini hawapo karibu sana na wazazi/ndugu zao.

Sijui kama ningeweza kumpeleka mmzazi wangu kwenye kituo cha kulelea/kutunza wazee. Napenda zaidi utamaduni/mila zetu za kiafrika na naomba Mungu tusiige kabisa tamaduni/mila hii. Sijui ni tabia gani? Maana kuna wengine ukiwauliza ni lini wameenda kuwasalimia mama/baba zao wanasema mwaka jana kweli huu ni upendokweli?

Zaidi soma hapa nimevutiwa na hii makala hii na nimeona niwaonyeshe na wenzangu ili tujadili kwa pamoja.


Nikionacho kwenye darubini.......



Nimekaa nimejiinamia huku mawazo kibao yakiwa yamenizonga. Nilimtupia jicho la haraka binti yangu mdogo ambaye ndio kwanza katimiza tumiezi kadhaa karibia na nusu mwaka. Mojawapo ya swali lililonizonga ni je kweli binti huyu na dada yake watanipeleka katika vituo vya kulelea wazee (nursing homes) pindi nitakapokuwa mzee na sijiwezi? Heh! Mungu na apishie mbali walah mimi nitaenda kuzeekea nyumbani kwetu bongo, labda nitazeeka kwa heshima astahiliyo mzee.
Kwa wale ambao hamjanipata vema nitawaelezea ili nanyi muelewe ni nini hasa kinachonikera. Hapa Marekani kama nchi nyingi za Ulaya kuna kasumba ya kuwapeleka wazee wasiojiweza katika vituo vya kulelea wazee. Vituo hivi vinaendeshwa kwa mfumo wa utoaji huduma za afya na masuala mengineyo. Wazee huishi katika vituo hivi na kupata huduma zote za kijamii na kuangaliwa kwa karibu afya zao. Chimbuko hasa la vituo hivi ni kutokana na mfumo wa kiuchumi uliopo katika maisha ya familia ya kila siku. Familia nyingi huwa ziko bize na maisha ya kila siku. Wengi makazini na wengine katika biashara huku wajukuu wakiwa wameshatawanyika aidha kwenda mashuleni au kuhamia majimbo mengine. Sababu hizi na zinginezo nyingi husababisha wanandugu kukaa na kuamua kuwapeleka wazazi wao katika vituo hivi.
Lengo huwa ni zuri tu kwasababu kama hauna nafasi ya kumtunza baba au mama yako ( dah!) pengine shangazi au mjomba na kuna sehemu ambayo kwa malipo ya bima basi atatunzwa basi ni vema kufanya hivyo. Lakini tatizo linakuja wapi??? Tatizo ni pale ambapo wazee hawa wanapogundua kuwa its about time. Hakuna anayependa kutenganishwa aidha kutoka nyumbani kwake na kwenda sehemu ngeni ifananayo na hospitali na kugundua wanatakiwa kupaita nyumbani. Wazee hawa hudhoofika kiafya haraka sana kwani hawaipendi hali hii na mara zote huonekana wamekuwa depressed. Magonjwa ya akili mara nyingi huwaandama na kuathiri afya zao na kusababisha urahisi wa kushambuliwa na magonjwa mengine. Kumbuka unapokuwa depressed muda wote huathiri kinga ya mwili hivyo kusababisha magonjwa kukushambulia kirahisi. Hali hii husababisha wazee wengi kudhoofika na hata kama walikuwa wazima vipi! Ni hoja tu jamani...
Tukirudi upande mwingine, vituo hivi vya kulelea wazee huendeshwa kwa mtindo wa kibiashara hasa chini ya mfumo wa kibepari. Faida kubwa ndio lengo na si vinginevyo. Ahadi kem kem hutolewa na pia kuna sheria maalum za kuwalinda wazee hawa. sheria hizi zimetungwa na serikali na zingine zimetungwa na majimbo. Vema basi kuna sheria kibao za kuwalinda wazee alright? Wrong! Kwanini basi nasema hivyo? Wale ambao wamepata kufanya kazi kwenye vituo hivi watakubaliana nami kuwa wazee hawa hunyanyaswa sana na wafanyakazi. Manyanyaso haya husababishwa na hasira za wafanyakazi kwa kufanyishwa kazi za watu wawili watatu bila hiari yao. Upungufu wa wafanyakazi katika vituo hivi ni jambo la kawaida kabisa ambalo huelekea kukosekana kwa ufanisi na morali za kufanya kazi. Mara nyingi upungufu huu husababishwa na mishahara midogo wanaolipwa wafanyakazi au menejimenti ipuuzavyo masuala ya ajira. tatizo hili husababisha wafanyakazi kubadili mwajiri kila mara hivyo vituo kukosa wafanyakazi wa uhakika. Utakuta kisheria mtu anatakiwa labda ahudumie wazee wanne mpaka watano kwa ufanisi lakini kutokana na upungufu basi mtu huyo huyo atapewa watu kumi mpaka kumi na tano wa kuwahudumia na hivyo kusababisha ufanisi kutoweka. Wafanyakazi mara kadhaa hasira zao huzimalizia kwa wazee hawa ambao maskini ya Mungu hawastahili haya kwani ni akina babu na bibi zetu na wanastahili mema toka kwetu. Hili ni tatizo sugu ambalo wamiliki wa vituo haliwasumbui sana kwani kwao ni faida kubwa sana kimapato. Familia nyingi zinafahamu tatizo hili na mara nyingi watembeleapo vituo hivi hutaka kujua rashio ya wafanyakazi (staff ratio).
Ninawaza sana, bora tu mfumo wetu wa nyumbani kwetu bongo. Tuendelee kuwalea wazee wetu na kuwathamini kwani ndio waliotufikisha hapa tulipo. Mfumo wa umimi na amerikani drimu usituingie kamwe kwani baadae utakuja kuturudi na kujikuta tunapambana na wanetu ili watupe haki yetu ya kututunza kwani nao tuliwatunza...

Monday, April 5, 2010

NIMEZISHITUKIA OFA ZA WANAUME!!!!!!!

Tumezishitukia ofa zao

Kwa huku kwetu ni wanaume wachache sana wanaomsaidia mwanamke bila lengo la kumpata mwanamke huyo, na akimtaka, mwanamke anaweza kujisikia vibaya wakati mwingine kwa kudhani kwamba misaada hiyo itakoma haraka kwa sababu hakuna jambo lenye kuwashika, yaani tendo la ndoa, hivyo hulazimika kukubali kutoa tendo la ndoa ili misaada isikome.


Hata hivyo sio wanawake wengi wanaokubali kulipa fadhila kwa njia hiyo, lakini wanaume wengi hutumia misaada au ofa kama chambo cha kuwanasia wanawake.

Kwa wanawake kusaidiwa ni kusaidiwa tu huwa hakufungwi na kutakiwa kimapenzi, lakini kwa wanaume kusaidia huwa kunafungwa pamoja na mapenzi.

Je sababu ni nini?

Wanaume wamelelewa na kufanywa kuamini kwamba wanatakiwa kuonesha sifa fulani kwa wanawake kabla hawajawatongoza.

Kwa hiyo mwanaume kabla hajatongoza huanza kujisifu kwanza, ili mwanamke amuone kama mtu anayeweza, hivyo mwanaume anapotoa msaada kwa mwanamke kuna mawili kama sio matatu, ama anataka kusifiwa au anamtaka mwanamke huyo, au vyote.

Lakini pia wanaume wengi huamini kwamba kwa kutoa ofa, mwanamke atajua kwamba anamtaka, hivyo kwa wanaume hao ofa ndio kutongoza kwenyewe. Kwa hiyo mwanume kama huyu anapotoa msaada kwa mwanamke anatarajia kumpata kimapenzi mwanamke huyo.

Kwa mijini kwa mfano mwanamke anayepewa lifti ni yule mzuri kwa sura na umbo, ukweli nikwamba hakuna msaada hapo bali mwanaume anaanza kununua penzi ambalo hajalipata.
Mwanaume akimpa lifti mwanamke na kumtongoza, na mwanamke huyo akakataa, basi huo msaada unafutwa mara moja.

Kwenye baa, mwanaume anaweza kumtuma mhudumu ampe pombe mwanamke fulani. Hajui mwanamke huyo kaja hapo baa na nani na anafanya kitu gani. hiyo ofa sio ya urafiki bali ni ombi la mwili wa mwanamke huyo, kwani hiyo ni hatua ya awali ya kuwa karibu nae.

Kuna idadi kubwa ya wanaume ambao hujitolea kuwasomesha, kuwapa au kuwatafutia ajira wanawake, lakini nyuma ya kujitolea huko, kuna agenda ya kuutaka mwili wa huyo mwanamke.
Mara nyingi mwanamke anakuwa hajui kwamba misaada mingi ya wanaume imefungwa pamoja na mapenzi. Ni wanaume wachache sana waliolelewa tofauti wasiofanya hivyo.

Ukweli ni kwamba wanawake wengi wamekuwa wahanga wa misaada .
Utakuta mwanaume anamsaidia mwanamke, mwanamke anapokea misaada hiyo akijua ni ya kibinadamu, kumbe akilini mwa mwanaume ni kwamba amewekeza. kwa hiyo anapokuja kumtongoza mwanamke huyo akakataa basi vita huanza.

Mwanaume anaweza kukumbushia misaada aliyotoa. na katika hali ya kushangaza mwanamke huyo hushikwa na butwaa. kwani hakujua kwamba alikuwa anapewa misaada ili atoe mwili wake.

Kuna wanaume wengi tu ambao wanaweza kumpa mwanamke soda kama taarifa kwamba amempenda, na mwanamke anaweza kupokea soda hiyo akijua kwamba ni ofa ya kawaida, lakini baadae hushangaa akija kutongozwa, na akikataa, anadaiwa soda aliyokunywa.

Nawasihi wanawake wenzangu wawe makini na ofa za wanaume kwani nyingi zimejaa utata mkubwa.



Habari ndiyo hiyo.......
Mada hii nimeichukua kutoka kwenye kibaraza cha VUKANI, cha dada Koero, nami nimevutiwa nayo nikaona sio vibaya kuirejea ili kujikumbusha.

Sunday, April 4, 2010

PASAKA NJEMA !!

Katika hili tumelifahamu pendo, kwa kuwa yeye alitoa uhai wake kwa ajili yetu, imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ua hao ndugu. Yoh. 3:16-
Pasaka njema na jumapili njema sana yaani jumapili ya kwanza ya mwezi wa nne na ya 14 ya mwaka!!!

Saturday, April 3, 2010

Heri ya Pasaka kwa watu wote/Glad Påsk alla!!!

Påskgubbe
Påskkäringar

Haya wasomaji naona sasa pasaka inakaribia. Nimeamua niwaeleze kidogo mila na desturi wakati/kipindi hiki cha pasaka huku ninakoishi ni tofauti sana na nyumbani TZ. Ngoja nianze kuwaeleza kuliko kuanza kuwachosha. Ni hivi alhamisi kuu ni kama kawaida au nimesahau sijui yaani watu wanakwenda kazini kama kawaida. Ijumaa kuu baadhi ya watu hawafanyi kazi na JUMAMOSI KUU hapa ndio sikuuu kubwa sio kama nyumbani TZ sikukuu ni jumapili.

Haya sikiliza sasa siku ile ya jumamosi watu wote ni lazima kula mayai kadiri unavyopenda bila mayai basi si pasaka tena. Wana mila hii ya kula mayai kwa sababu hapo zamani kuku waliacha kutaga mayai. Na ghafla walianza tena kutaga na siku ile ya waliyoanza kutaga ilikuwa JUMAMOSI KUU. Hii ndio sababu siku hii ni lazima kuwe na mayai mazani.

Halafu kitu kingine siku hii ya JUMAMOSI KUU watoto wadogo wanavaa kama mababu na mabibi hapo zamani. Pia wanajichora usoni na kalamu za rangi .Na pia wanakuwa na barua ambazo wameziandika/chora wenyewe kwenye vikapu. Na wanapita kila nyumba na kubadilishana na pipi. Ni mila yaani ni kama jambo la kutakiana pasaka njema. Kwa hiyo kipindi kama hiki kila kaya inabidi iwe na pipi au matunda kama huna hivyo viwili basi uwe na hela. mwanzoni nilishangaa lakini sasa nimezoea. HERI KWA PASAKA WOTE!! GLAD PÅSK ALLA!!

Thursday, April 1, 2010

KAMA MVI NI KIPIMO CHA BUSARA, NI KWA NINI ZIFICHWE??

Mbona Profesa Mbele anazo mvi lakini hazifichi?



Mvi ni dalili ya uzee au ni kitu gani? Kwa zamani ingekuwa ni muhali mkubwa mtu kuuliza swali la aina hii, kwa sababu mvi zinahesabiwa kama dalili ya busara, bila shaka zikihusianishwa na kuona mengi ambayo ni wenye umri mkubwa tu waliokuwa na nafasi hiyo.
Lakini leo, mvi ni kisirani na karibu kila mtu anajaribu kuzikimbia, kwani kuendalea kuwa kijana ni sifa kubwa. Kwa sasa uzee unanuka na kila mmoja anajaribu kuukimbia kwa njia mbalimbali ikiwemo ya kukana umri na kujirudisha nyuma kimatendo. Kwa kifupi hii ndiyo historia ya mvi, usiziogope bure!
Karibu rangi zote asilia za nywele zinatoka kwenye kitu kiitwacho melanin, ambacho huzalishwa na mwili kutokana na seli zinazofahamika kama melenocytes. Nywele zinapobadilika na kuwa nyeupe ina maana kwamba, melenocytes haizalishi tena melanin. Mabadiliko haya ya nywele kutoka rangi nyeusi na kukosa rangi (mvi) siyo hatua ya siku moja bali mwaka na miaka, kwani nywele moja hubadilika baada ya muda mrefu na nyingine na nyingine. Siyo hatua ya siku moja tu.
Kwa kadiri mtu anavyozeeka ndivyo ambavyo uwezo wa mwili kuzalisha melanin unavyopungua. Uwezo huu huanza kupungua mtu anapofikia umri wa miaka 35 au 40. Lakini watu wengine huanza kuota mvi wakiwa na umri wa miaka hata 20 tu. Je, hii nayo inatokana na nini?
Hili kusema kwali siyo jambo la ajabu. Ingawa kuna watu ambao huwa wanalishangaa. hata hivyo wana sayansi wanasema kwamba hawajaweza hasa kujua ni kwa sababu zipi uwezo wa mwili kuzalisha melanin huwa unashuka. Lakini wana uhakika kwamba wale wanaoanza kuota mvi kabla hawajafikisha umri wa miaka 35, kwa sehemu kubwa wanaathiriwa na urithi au kizalia.
Kama mtu ataona kwamba anaanza kupata mvi mapema sana ni dhahiri kwamba akiangalia kwenye familia yao atakuta kuna mtu ambaye naye alianza mapema kuwa na mvi. Hii itasaidia kumuonyesha kwamba mvi zake ni matokeo ya kizalia.
Pengine ni jambo la ajabu kwamba kuvuta sigara kunatajwa kama sababu ya kuchochea mtu kupata mvi akiwa na umri mdogo. Ukiwachunguza wavuta wazuri, utagundua kwamba wameanza kuota mvi mapema kuliko umri wa miaka 35 au 40.
Matatizo kwenye kiungo kinachodhibiti ukuaji mwilini, yaani thyroid huweza pia kusababisha mtu kupata mvi kabla ya kufikisha umri wa miaka 35. Pia ukosefu wa vitamin B12 unatajwa kwa sababu nyingine.
Kuna watu ambao hata kama wana umri wa miaka 60 bado hawataki kuona nywele nyeupe vichwani mwao . Watu hawa huangaika huku na kule kutafuta dawa kuondoa mvi na pengine kutumia rangi ya nywele ili kufanya rangi ya nywele nyeupe zisionekane. Huu ni kama mwendawazimu kwa kiasi fulani. Kwanini?
Kwanza kuna ukweli kwamba nyingi kati ya hizo zinazodaiwa kuwa rangi za kuondoa mvi, zina athari katika mwili wa mtumiaji. Lakini wendewazimu mkubwa zaidi ni kitendo chao cha kukataa ukweli ambao inabidi waujivunie.
Mvi bado ni dalili ya busara. Kama umefikia umri wa kuota mvi na hujafanya jambo lolote la maana na hujatoa mchango wowote wa maana kwa familia yako au jamii unamoishi ni lazima utaficha mvi zako. Kwanini?Kwa sababu utaona haya sana kuonekana kwamba umri wako ni mkubwa lakini hujafanya lolote. Tunaposema mchango wa maana hatuna maana ya fedha au mali, bali zaidi tuna maana ya mawazo ya kujenga na pengine kuandaa misingi ya kujenga kwa nia ya kuleta maendeleo baadaye.
Hebu chunguza kwa makini, utagundua kwamba watu wote wanaojaribu kuficha mvi ni wale watu ambao wametawaliwa sana na vionjo na tamaa ya miili yao kuliko maendeleo ya binadamu. Ni wale watu ambao hata kama wana fedha, hawajajua hasa wako hapa duniani kwa sababu gani. Hivi ndivyo ilivyo kwa sababu watu wa aina hii huhofia sana umri, huhofia sana kufa kwa sababu hawajakamilisha walichokuja kukifanya duniani kwasababu hawajajua bado.
Kukosa kujiamini na kujikubali kwamba wewe ni fulani na uko katika hali fulani na kiwango fulani hupelekea watu wengi kubadili majina, kuchukua makabila yasiyo yao, kujiita maarufu au kuongopa kuhusu maisha yao kwa ujumla. Mtu anayejaribu kuficha mvi ili asijulikane kwamba ana umri mkubwa hana tofauti na watu hawa.
Mtu ambaye anajiamini hawezi kuogopa kutaja umri wala kuonyesha kwamba ana umri mkubwa. Na mtu hawezi kujiamini kama hajijui yeye ni nani na kujijua kunataka mtu asiishi kwa kutazama wengine watamuonaje, bali anajionaje.
Kuficha mvi inaweza kuwa ni dalili ya mtu kuvuka kipindi fulani bila kufanya mambo ambayo kisaikolojia alitakiwa kuyafanya wakati huo. Kama mtu alitakiwa kufanya mambo hayo katika umri wa miaka 20 hadi 25 na hakufanya, kuna kawaida ya mtu kama huyo kuja kutaka kuyafanya akiwa na umri wa juu zaidi.
Kwa kuwa wakati huu mvi ni dalili kwamba ameshapita umri wa kufanya mambo hayo, atahakikisha kwamba dalili hii inafunikwa au kufutwa ili isimfedheheshe. Wengi wetu tunawajua wa waficha mvi na vituko vyao huko mitaani kwetu. Habari hii chanzo ni Jitambue.......