Thursday, January 31, 2013

Neno La Leo: Mwaka Ni Kama Noti Ya Elfu Kumi Ya Bongo, Ukiichenji​, Inapukutik​a!



Ndugu zangu,
Leo ni mwisho wa mwezi wa mwaka mpya. Na mwaka ulivyo ni kama noti ya shilingi elfu kumi ya Bongo. Ukiichenji tu, utashangaa inavyopukutika!
Ukae sasa ukijua, kuwa kesho ndio Februari Mosi. Hivyo, mwaka mpya wa 2013, kama ilivyo kwa noti elfu kumi, ndio tutakuwa tumeuchenji. Subiri sasa uone siku, wiki na miezi inavyopukitika. Fumba na kufumbua utasikia tumeshaingia Juni tunaelekea Bajeti ya Serikali ya Julai, na ukitoka hapo utafikiri mwaka unateremsha milima ya Kitonga.
Inatukumbusha nini?
Umuhimu wa kupanga mambo yetu. Inahusu muda na matumizi ya muda. Na mwanadamu usipokuwa makini na muda, itakuwa sawa na kisa kile cha mzazi aliyeulizwa na wanawe; " Mbona nguo za Krismasi hatujanunuliwa?"
Mzazi akawajibu wanawe; " Jamani, Krismasi ya mwaka huu imekuja ghafla sana!"
Kana kwamba hakujua, kuwa kwenye kalenda ya mwaka tarehe ya Krismasi imeshawekwa, Desemba 25!
Ndio, Afrika mvua hainyeshi ghafla, huwa kuna dalili zake. Na katika maisha, mambo mengi hayaji ghafla, bali hutukuta tukiwa hatujajiandaa. Jiandae na mwaka unaoanza kupukutika kuanzia kesho, kama noti ya shilingi elfu kumi. Kila la kheri.
Nimetumiwa na kaka Maggid Mjengwa.

POLENI KWA MSIBA DADA MIJA NA WANANDUGU WOTE!!

Mwenzetu mwanablogu Mija Shija juzi amefiwa na mjomba wake mpendwa mzee Moses Tito Kachima (pichani juu)katika hospital ya Mama Ngoma iliyopo Mwenge Dar es salaam.Kwa habari zaidi mtembelee Mija Shija. Poleni sana, tuko pamoja.

Wednesday, January 30, 2013

LEO TUANGALIA HADITHI: MWENDO WA KINYONGA!!!

Hapo mwanzo, yasemekana kuwa Kinyonga alikuwa na mwendo wa haraka na hata kukimbia kwa kasi kama wanyama wengine. Hakuwa na mwendo wa kusuasua kama tumwonavyo siku hizi. Je, ni kitu gani kilichomfanya Kinyonga awe hivi alivyo?
Siku moja, lilipogwa la mgambo la kuwataka wanyama wote wakusanyike pamoja ili kuwe na mashindano ya kukimbia, wapate kujua ni mnyama gani hodari wa kuchanganya miguu kushinda wengine. Taratibu zilifanyika ili kuweka mambo yote sawa. Siku ya siku ilipowadia, mashindano ya kukimbia yakaanza: Msimamizi wa mashindano alianza kuhesabu: Moja, mbili, tatu! Loo, vumbi likaanza kutimka kutokana na kishindo cha mbio za wanyama wale. Kwa vile mbio zilikuwa za kasi sana, baadhi ya wanyama walioweka vitu mfukono mwao, vikaanza kudondoka, kimoja baada ya kingine. Kinyonga kutokana na ukali wa macho yake, akaviona vitu hivyo. Kadiri mbio zilivyozidi kupamba moto, na ndivyo vitu viliendelea kudondoka. Hatimaye, Kinyonga akashindwa kujizuia. Vitu vile vilimtinga sana. Akabadili uelekeo. Akawapisha wanyama wengine na kujifanya kama vile anakwenda kujisaidia. Kumbe, anarudi nyumba na kuanza kuokota vitu vilivyodondoshwa na wanyama wenzake. Kwa kuwa vitu vile vilikuwa vingi na vilidondoka ovyo ovyo bila mapangilio wowote, Kinyonga alianza kwenda polepole, kwa maringo na makini, ili aweze kuokota vizuri vitu vyote kisiachwe hata kitu kimoja. Alifanya hivyo sio kwa ajili ya kuwarejeshea wale waliopoteza, la hasha, bali kuweka kibindoni, ili vimfae mwenyewe maishani.
"Tamaa mbele, mauti nyuma." Sasa basi, kutokana na tamaa hiyo, alikiona cha mtema kuni. Jamaa tangu siku ile, hadi leo hii, hakuweza tena kutembea haraka wala kukimbia. Akawa "amejitaiti" mwenyewe. Halafu, akawa anabadilika badilika rangi kufuatana na mazingira ya sehemu anayokuwepo ili asije akaonwa na wenye mali zao. Vile vile, anazungusha zungusha macho huku na huko kana alivyofanya siku ili "alipookota" vitu vilinyodondoshwa na wanyama wenzake.
Na Kat.V.A. Ndunguru kutoka gazeti la Mlezi.
Je hadithi hii wewe msomaji inakufundisha nini?

Tuesday, January 29, 2013

MILO AMBAYO NINGEPENDA SIKU YA LEO NILE NI HII HAPA...!!!

 
Chai ya rangi na ndizi mzuzu za kuchemsha
Mlo kama huu kwangu ni mali sana kuliko chai ya maziwa kwa mikate. Vyakula vyetu kama viazi, mihogo, magimbi na ndizi hakika jamani tuendelee kula kwanza unakula unashiba na halafu vina faida. Karibuni....na mchana...mmmmmhhh

 

Mchana, Nimekaa hapa naota mlo huu ugali, samaki, chuzi, mbogamboga na kachumbali kidogo bila kusahau pilipili... ila duh naona niishie kula kwa macho tu....au ...na jioni sijui itakuwaje ..hii ndiyo mara nyingi akina mama huwa tunawaza ili familia ipate chakula..tuna kazi kweli kweli......

Monday, January 28, 2013

KWANGU MIMI ILIKUWA NI KAMA NDOTO....!

Jana wakati nipo kazini nilipata nafasi kidogo na kupita hapa kwenye kibaraza cha kaka yangu mzee wa Utambuzi. Nikakutana na kisa hiki hapa kwa kweli kilinigusa sana kiasi kwamba nimeona niweke hapa na wengine msome...haya karibuni.......
...............................................................................................................................................
Hadi leo naona kama ndoto.............!
(Picha haihusiani na habari hii.)
Nakumbuka ilikuwa ni mwaka 1991 wakati huo nikiwa nafanya kazi kwa mtu binafsi, Muasia mmoja. Nakumbuka katika mojawapo ya majukumu yangu, nililazimika kwenda Nairobi nchini Kenya. Nilikwenda huko kikazi na nililazimika kukaa kwa mwezi mmoja. Nilipomaliza kazi ile, niliamua kukaa kama siku tatu zaidi ili kujionea hali ya Kenya ilivyo. Nilizunguka jijini Nairobi na kwenda maeneo ya karibu kama vile Thika, Kinangop na miji mingine iliyo karibu na jiji hilo maarufu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.
Siku moja wakati natoka kwenye matembezi yangu nje ya jiji hilo la Nairobi, nilikutana na mtu mmoja. Huyu bwana alikuwa anaonekana kuchoka sana, ama kwa kuumwa au kwa njaa. Nilikaa naye kiti kimoja kwenye Matatu, yaani daladala za Kenya. Huyu bwana alikuwa ananitazama mara kwa mara na kujitahidi kutaka kama kutabasamu, ingawa hakumudu sana.
Niliingiwa na huruma na kulazimika kumuuliza kama alikuwa yu mzima wa afya. Alisema anaumwa na hana hata senti tano ya kulipia matibabu yake. Nilimuuliza kama anao ndugu. Alisema hana na familia yake iko mashambani, ambapo haina kitu kabisa. “Nina watoto watatu mmoja amemaliza shule hana kazi na wawili wanasoma, lakini ni kwa mashaka sana, kwani mara nyingi hurudishwa nyumbani kutokana na kukosekana ada.” Aliniambia.
Ilibidi nimchukue yule bwana hadi hospitalini ambapo alichukuliwa vipimo. Aliambiwa arudi kesho yake kuchukua majibu yake. Tuliagana tukutane pale hospitalini kesho yake. Kwa kweli hakuamini kwamba, nilimfikisha hospitalini na kumlipia matibabu. Hakuweza hata kushukuru na nilielewa ni kwa sababu gani. Mshangao ulikuwa ni mkubwa sana kwa upande wake.
Kesho yake alipata majibu yake ambayo yalionyesha kwamba alikuwa na maji kwenye pafu moja pamoja na kifua kikuu. Ilibidi aandikiwe dawa. Hakuwa na fedha kabisa. Ilibidi nitoe fedha zote za matibabu yake. Ilikuwa kama silimia 20 ya pesa zote nilizozipata pale Nairobi kama posho. Lakini hiyo haikunisumbua. Nilikuwa najisikia vizuri kuona angeweza kupona.
Ilibidi niombe ruhusa ya siku saba zaidi ili nikae Nairobi kukagua hali ya yule jamaa. Wakati huo huo nilimwambia kwamba, kama anaweza kumwita mkewe akae naye pale mjini wakati anatibiwa ingekuwa vizuri. Nilimwambia ningemsaidia pesa kidogo za kumwezesha mkewe kukaa naye angalau kwa siku kadhaa. Alikubali na kumwita mkewe. Mkewe alipofika hakuamini kwamba niliweza kumsaidia mumewe vile. Yule mama alilia sana na aliniombea sana kwa kikwao, yaani Kikikuyu kwa majina ya mizimu yote. Nilijisikia furaha kwa namna mke wa jamaa alivyojisikia vizuri kuona mumewe amepata matibabu.
Niliondoka Nairobi siku ya tatu tangu mkewe kuja. Niliwaachia hela kiasi cha shilingi 14,000 za Kenya, ambazo nilimwambia yule mama zingemsaidia kufanyia shughuli yoyote ambayo ageona inafaa. Niliondoka bila hata kuwaachia anuani yangu wala simu yangu. Labda wao walitegemea ningewapa anuani yangu, lakini sikufanya hivyo. Mimi sikuona sababu ya kuwapa kwani, niliwasaidia kama binadamu ambao wanahitaji msaada wangu, siyo ili wanijue au tuwe marafiki.
Hivyo ndivyo nilivyo hata leo. Sijisifu kwa sababu sioni kuwa ni sifa, bali naona kila binadamu angetakiwa kuwa hivyo, ila basi tunazuiwa na choyo ya kufundishwa. Sikuwahi kusoma kuhusu masuala ya kusaidia na kupata furaha wala kumsikia mtu. Tabia hii nilitoka nayo kwetu, niliitoa kwa baba yangu ambaye, alikuwa mtu wa kusaidia sana bila kujali malipo. Hilo nalijua.
Mambo yangu yalienda vizuri hadi mwaka 1994. Mwaka huo nilipoteza kibarua change na hata shughuli zangu zikawa zimepoteza umaarufu kutokana na mabadiliko ya teknolojia. Ilibidi nianze kuhangaika. Kufikia mwaka 1996, nilikuwa hoi bin taabani kiuchumi. Watoto wangu watatu wakawa hawaendi tena shule, hakuna ada. Tulishindwa kulipa kodi ya nyumba, ambapo ilibidi tufukuzwe na kwenda kuishi kwa ndugu wa mke wangu. Huyu naye hatukukaa hata mwezi masimango yakaanza. Siwezi kumlaumu, kwani kusaidia siyo jambo rahisi, ingawa naamini ndipo mahali furaha ya binadamu ilipo.
Tulilazimika kuhama na kwenda kuishi Mtoni Kijichi. Huko hatukuwa tumepanga. Jamaa yangu mmoja alikuwa anajenga kule na alikuwa anataka mlinzi, ambapo nilimwambia ningefanya kazi hiyo. Hivyo tukawa tunaishi kwenye kibanda cha mtumishi. Lakini tulihisi nafuu. Hata hivyo watoto wote walisimama shule, kwani hata nauli ya kuwapa ili waende shule ilikuwa ni vigumu.

Sunday, January 27, 2013

UJUMBE WA JUMAPILI HII YA NNE YA MWAKA 2013 NI KAMA IFUATAVYO!!

Unapotafakari mema ya Mungu ya leo:-

WASAMEHE WALIOKUKOSEA,
WAKUMBUKE WALIOKUSAHAU na UILINDE AMANI YA MOYO ISIPOTEE.
Kwani utakuwa na furaha daima!!!
JUMAPILI NJEMA NDUGU ZANGUNI!!!!

Friday, January 25, 2013

NAWATAKIENI WOTE IJUMAA NJEMA KWA WIMBO HUU:- MOYO WA SUBIRA NA LINEX!!!!


IJUMAA NJEMA JAMANI ...TUWE NA MOYO WA SUBIRA HATA KAMA TUMEUMIA/UMIZWA....KAPULYA

Thursday, January 24, 2013

HABARI YA KUSIKITISHA SONGEA:- MWANAFUNZI WA KIDATO CHA SITA SONGEA BOYS AJINYONGA

MWANAFUNZI wa kidato cha sita katika shule ya sekondari ya wavulana ya Songea mkoani Ruvuma amekutwa amekufa baada ya kujinyonga kwenye mti uliopo kandokando ya njia kwenye eneo la milima ya matogoro ya hifadhi ya msitu ya taifa nje kidogo ya manispaa ya Songea.
Kaimu kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma mrakibu mwandamizi wa polisi George Chiposi alisema kuwa tukio hilo lilitokea januari 21 mwaka huu majira ya 12.30 asubuhi huko katika eneo la milima ya matogoro
Kaimu kamanda Chiposi alimtaja mwanafunzi huyo aliyekutwa amekufa baada ya kujinyonga kuwa ni Ahabu Richard Ng’ondya (21) wa kidato cha sita katika shule ya sekondari ya wavulana ya Songea ambapo alidai kuwa siku hiyo ya tukio watoto wawili ambao walikuwa wakipita njianimajira ya saa za asubuhi ghafla waliona kama kuna mtu ananing’inia kwenye mti mrefu ambao upo kandokando ya njia hiyo.
Watoto hao baada ya kuona hali hiyo walikimbia na kukutana na mtu aliyejulikana kwa jina la Osward Kahongo walimwonyesha tukio hilo ambaye nae pia aliwasiliana na polisi ambao walifika kwenye eneo la tukio wakiwa wameongozana na daktari.
Alisema baada ya polisi kufanya uchunguzi ulibaini kuwa alikuwa ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya wavulana ya Songea ambaye anadaiwa aliondoka kwenye eneo la shule katika mazingira ya kutoroka siku chache kabla ya kutokea tukio hilo.
Alibainisha zaidi kuwa upelelezi wa awali wa polisi umebaini kuwa chanzo cha kujinyonga kwa mwanafunzi huyo ni kwamba alikuwa amefukuzwa shule na uongozi wa shule baada ya kutofanya mitihani ya majaribio hivyo uongozi  wa shule ulimtaka arudi nyumbani kwao Matamba Uwanji wilaya ya Makete mkoani Njombe ili akamlete mzazi wake.
Alieleza zaidi kuwa baada ya kuambiwa hivyo mwanafunzi huyo alitoeka kwenye eneo la shule na kwenda kusikojulikana hadi hapo alipokutwa akiwa amekufa kwa kujinyonga, hata hivyo alieleza kuwa mwili wa marehemu umesafirishwa kwenda Matamba Uwanji nyumbani kwa wazazi wake kwa ajili ya mazishi
CHANZO:- Songea yetu.

LEO:- TUSISAHAU VITENDAWILI VYETU/ JE UNAVIKUMBUKA HIVI?

1. Chini chakula, juu chakula, katikati kuni. Nini hicho
2.  Nimefika ugenini, ameniamkia mtoto. Mtoto huyu ni nani?
3.  Mtu anabadilika badilika
4.  Watoto wawili wanapigana kila wakati. Watoto gani hao?
5.  Ndege wangu ametagia kwenye miiba. Ndege gani huyyo?
6.  Shamba langu nimelima kubwa, nimepanda mbegu zangu tatu: Mbegu hizo ni nini?
7.  Mgeni yupo ndani nyumbani, hasemi, mimi simwogopi
8.  Nje kukavu, ndani maji. Nini hicho?
9.  Nyumba yangu ina nguzo mbili, kama zinaanguka siwezi kuzisimamisha.
10. Nimekata tete, nimevuka mto mkubwa. Tete hili ni nini?
11. Natoka kwa mama, naenda kufa.
12. Ugonjwa wa watu wote ni nini?
NAWATAKIENI KILA LA KHERI KWA KILA JAMBO...!!!!!!!

Wednesday, January 23, 2013

Nimeshindwa vumilia !!!!

Siwezi siwezi tena, siwezi kuvumilia,
Hali miye tena sina, sinayo menizidia,
Usiku nao mchana, nazidi tu kuumia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Mejaribu kujikaza, kinywa nikakizuia,
Mezidi moyo umiza, nafuu h’ijatokea,
Moyo pendo mekoleza, mekolea kuzidia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Mejaribu kutosema, moyo haujatulia,
Juu juu ninahema, kama nataka jifia,
Kwako nilishatuwama, sina ninalosikia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Usingizi siupati, wewe tu nakuwazia,
Nipo hoi hatihati, hatihati kuugua,
Nawaza kila wakati, ni vipi nitakwambia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Nimechoka nimechoka, nimechoka vumilia,
Leo nakwita itika, moyo upate kutua,
Maana ushaniteka, na moyo usharidhia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Nipo hoi taabani, moyo kwako umetua,
Nitakuwa furahani, wewe kinikubalia,
Nimekuweka moyoni, uniweke nawe pia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Chonde chonde muhashamu, nifanye moyo tulia,
Nikupe pendo adhimu, pekee hii dunia,
Pendo liso na awamu, kila siku lachanua,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Nikupe pendo la huba, pendo nalosisimua,
Pendo tele na si haba, moyoni ‘shakujazia,
Pendo mara saba saba, mahaba yalozidia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Siwezi tena kungoja, kusubiri kukwambia,
Moyoni ipo haja, zaidi nitajifia,
Nakupenda wewe mmoja, hakuna nokufikia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Uwe wangu wa milele, name niwe wako pia,
Nikupe mapenzi tele, nawe tayafurahia,
Pamoja huku na kule, kwa raha ilozidia,
Nimeshindwa vumilia, kutosema nakupenda.

Nimeshindwa vumilia, nd’o ma’na nimekwambia,
Kwamba ninakuzimia, juu yako naugua,
Natumai mesikia, kisha tanikubalia,
Kwani siwezi himili, kutosema nakupenda.

Shairi hili kutoka kwa mtani wangu Fadhili Mtanga
NAWATAKIENI WOTE KILA LA KHERI..PAMOJA DAIMA.

Tuesday, January 22, 2013

SIKU YA MWAKA MPYA 1/1/2013 ILIVYOKUWA HAPA KWETU SONGEA/RUHUWIKO NA MZEE UHAULA NDANI YA MAPISHI!!!

Hapa pilau likiandaliwa na mpishi maalumu, kwa jina anaitwa mzee Edward Uhaula ni mkazi wa Matetereka..tulikuwa tukiishi nashi enzi hizo. Kwa hiyo siku hii ya mwaka mpya 2013 alikuja kutusalimia na hakukosa kukumbushia enzi yaaani kupika. Maana si unajua ukiwa na familia kubwa..halafu tena ni sikukuu ya mwaka mpya inapendeza kukutana pamoja kula na kucheza/kuongea..kubadilishana mawazo. ilikuwa safi sana kwa kweli
Hapa ni nyama ya ngómbe ikiandaliwa ..muda si mrefu itatengenezwa kwa viungo na baadaye kuliwa....

Sunday, January 20, 2013

NAPENDA KUWATAKIENI WOTE MTAKAOPITA HAPA JUMAPILI NJEMA SANA!!!!! MICHEZO NI FURAHA!!!!

Licha ya kuwafundisha watoto elimu ya kitabuni, wanahitaji pia michezo ili waweze kujengeka kimwili, kiakili, kiroho na kuwa na maadili mema.. JUMAPILI NJEMA SANA....

Friday, January 18, 2013

IJUMAA YA LEO NA MWANAMTINDO WETU NDANI YA KITENGE TUDUMISHE HILI VAZI!!!

Unapopata zawadi unapaswa kuchukuru ahsante Dada mkuu msaidizi..Mija na hii ni kazi ya mikono ya shemeji Manju...kuona kazi zake zaidi unaweza kuingia hapa
Mimi ndani ya kitenge ..huwa kila niendapo kunyumba nashona kitenge ..napenda sana vazi hili. Kitu kimoja huwa kinaniletea taabu pale nishindwapa kuchagua mshono/mtindo..huu nimechaguliwa na fundi kama kuna mtu anaweza kunipa mbinu naomba...
Hapa ni zawadi kutoka kwa dada Ester Ulaya nilipata ile siku tuliyokutana,,Ahsante sana Dada Ester na Shemeji ..nimeipenda sana zawadi hii..si unajua mwanamke kanga/kitenge..kudumisha utamaduni wetu ni msingi mzuri..mpiga pcha ni dada Camilla. NAWATAKIENI WOTE MTAKAOPITA HAPA IJUMAA NJEMA NA PIA MWANZO WA MWISHO WA JUMA UWE WENYE FURAHA..PAMOJA DAIMA...

Thursday, January 17, 2013

Wanawake hupenda kuonewa wivu……!

Kama ulikuwa hujui, ni kwamba wanawake hupenda kuonewa wivu, lakini kwa kiasi kidogo tu. Lengo lake hasa ni kutaka kujua kama unamjali kwa kiasi gani. Wakati mnapoingia kwenye mghahawa ama kwenye Baa, mwanamke angependa ugundue kwamba kuna mtu amevutiwa naye, hata kama mtu huyo ni muhudumu. Pia wakati wanaume wengine wanapowakodolea macho unapokuwa naye barabarani, ama wafanyabiashara wa mitaani wanapopiga kelele na miluzi ya kumsifia, angependa kuona utalichukuliaje hilo. Unapoonekana kutofurahishwa na vitendo hivyo na kumtaka mtafute sehemu nyingine ambayo haitakuwa na rabsha, ama nawe utakapoonekana kuona fahari ya kuwa na mwanamke anayevutia watu, basi mpenzi wako huyo naye ataona kwamba yeye ni muhimu kwako. Lakini ni lazima uwe mwangalifu usije ukajenga ama kuonesha wivu wa kupindukia, kwani hilo litamfanya mpenzi wako ahisi unamuona yeye si mwaminifu, au ni Malaya. Kumbuka wivu ukizidi sana huwa kero. HABARI HII NIMEIPATA UTAMBUZI NA KUJITAMBUA....

Wednesday, January 16, 2013

HONGERA KWA SIKU YA KUZALIWA KAKA SIMON KITURURU/KADODA..BABA MAX!!!

KAKA SIMON KITURURU /BABA MAX HONGERA SANA KWA SIKU YAKO YA KUZALIWA Mwezi huu ni kumbe tupo wengi tuliozaliwa mojawapo mimi mwenyewe ambaye nimevunja makumi kadha, Na leo kaka Simon Kitururu naye kavunja kalenda na wengine wote kama vile shemeji Isaac mume wa dada Rachel, kaka Haki Ngowi, baba wa mzee wa Changamoto, na mtoto wa kaka yangu Sam Mbogo, mtoto Oskar..na wengine wote wanaotimiza miaka/mwaka mwezi huu HONGERA SANA KWA MWEZI WETU...!!!

UJUMBE WA SIKU YA LEO!!

Watu wengi Binadamu wachache!! TUWE NA SIKU NJEMA!!!

Monday, January 14, 2013

SIKU HIZI SITAZISAHAU ..HATIMAYE TUMEKUTANA USO KWA USO..

Yasinta na Kaka Albano Midelo Ruhuwiko/Songea Ilikuwa ni mwaka mpya huu 2013 kwa mara ya kwanza kaka Albano Midelo alikuja kututembelea kwetu Ruhuwiko yeye ni mmiliki wa blog ya Maendeleo ni vita
Yasinta na kaka Shaban Kaluse wakiwa Jangwani beach Dar es Salaam Haikuishia kukutana na kaka Midelo tu, pia kwa mara ya kwanza nikakutana na kaka yangu wa hiari kaka Shaban Kaluse Mzee wa utambuzi. Ilikuwa ni furaha ya ajabu sana kukutana na kaka huyu ...kwa kumfahamu zaidi unaweza kumsona hapa
Yasinta na Dada Ester Ulaya wakiwa wametulia ndani ya Savanah Lodge Sikuishia kukutana na hao akina kaka tu ..Nilipata bahati ya kukutana na Dada Ester Ulaya pia nadhani safari yangu safari hii ilikuwa yenye baraka sana kuweza kukutana na ndugu hawa..hapo tupo sehemu tuliyofikia Savanah Lodge ambayo ipo maeneo ya Banana..kuweza kumfahamu dada huyu ingia kwenye blog yake Rular and Urban
Na hapa ni picha ya pamoja hicho kiti kisicho na mtu ni cha mpiga picha ambaye ni mr. wangu, anayefuatia ni mmiliki wa hotel ya Savanh Lodge, halafu anafuatia kaka Kinunda, na halfu anafuatia ni mume wake dada Ester Cathbert Angelo Kajuna na ni mmiliki wa blog HABARI NA MATUKIO na pembeni yake ni mwenyewe dada Ester na halfu mimi nipo ila sijaonekana hapo na bila kusahau kaka Chacha naye tulikuwa naye ila alifika baadaye na katika kunogewa na hadithi tukasahau kupiga naye picha.Na halafu nisisahau tulikuwa na dada mkuu msaidizi katika maongezi yetu yaani kwa simu..si mwingine tena ni mwenyewe mwanamke wa shoka Dada Mija. Yeye anapatikana zaidi hapa. Tuulikuwa na wakati mzuri sana kwa ujumla.

Hivi tunawezaje kuishi kwa matumizi yafuatayo kila mwezi?

Fikiri, matumizi nyumbani: chakula, umeme, gesi, maji, soda/juisi za wageni. Ada za watoto zinazolingana na za chuo kikuu. Matibabu hospitalini, pesa ya walinzi kwa mwezi, sherehe za kuaga na kukaribisha mwaka mpya; Zaka ya kanisani na misikitini, Kupanda Mbegu/ Sadaka, Shukurani ya Neno, Ahadi na Collect, shukrani ya Chakula cha Bwana church, marekebisho ya kitasa cha mlango kabla mwenye nyumba hajashtuka, gharama za marejesho ya mkopo wa saccos kazini. Tozo za Flying (wazoa taka wa mikokoteni ambao huzit...upa hapo hapo), Madalali wa nyumba/viwanja, Pango la nyumba, Fremu ya biashara/ofisi, Mazakayo wa mitandao ya simu [airtime vouchers]; Mafuta ya gari, Walinda/waosha magari (oya sista/blaza, mdogo wako nipo apaaa); Tozo za kuegesha magari, Makato ya Mikopo, Tozo za internet cafe ili uweze ku-surf. Rambirambi ya mfiwa mtaani kwetu, Harusi ya ndugu yako wa ukoo na zawadi, Sendoff ya mtoto wa mdogo wake rafiki yako na zawadi, Kumuaga mfanyakazi mwenzetu na zawadi, Michango ya komunio ya 1 & 2 na kipaimara; Michango ya besdei party na zawadi; Ndugu wa kule kijijini, Mshahara wa Hausigeli na hausiboi; Bodaboda, teksi na bajaj; Duka la dawa kwa Mchaga, Tuisheni ya mtoto, Kuchangia wahanga wa mabomu na mafuriko. Kwenda kumuona mtoto aliyezaliwa, Kununua CD/DVD ya Uzinduzi wa Kwaya yetu. Chakula cha mbwa, Machango wa Ujenzi wa Kupanua Kanisa, Kuchangia Uinjilisti Masasi, outing ya kitimoto, Ujenzi wa Nyumba Mabwepande, Kuendeleza shamba mkuranga (linalotaka kutaifishwa kwa kutoendelezwa). Na kwa wale wenzetu wanaokwenda umbali wa Viti Virefu, moja moto moja baridi. Maji ya Traffik, Chai ya Nesi na Daktari, Kahawa ya Hakimu, Karani na PP. Vishoka waunganisha maji na umeme; Kidogodogo cha mjumbe na mtendaji wa mtaa, makaribisho ya get together na dinner kwa rafiki wa kikazi ambaye hamjuani ila kweye simu tu, Mchango wa matibabu ya mtoto Nyumba ndogo kule Ngusero, mchango kidogo kwa rafiki aliyevamiwa na Vibaka na kuumizwa vibaya, gharama za malipo ya mtura Mkulima Bar Moshi, manunuzi ya maji ya Kilimanjaro Uwanjani Sheikh Amri Abeid Ukicheck mechi ya Yanga na JKT Oljoro, malipo kwa ajili ya Uji wa Shanga baada ya kazi Njiro jioni ya Alhamisi, Vipi manunuzi ya kandambili kwa ajili ya matumizi ya home.Hivi hali inakuwaje? Mia mbili ya watoto wa mtaani/ombaomba, kitu kidogo cha wale wanaolazimisha kuosha kioo cha gari kwenye foleni. umeme uliopanda bei, gesi iliyopanda bei, maji yaliyoadimika, bado contingency mana huu usafiri unaotembelea ball joint, bush, feni belt havijafa - hapo bado service. Bado msosi wa mchana kazini esp kama maofisi yetu mama ntilie wanakaribiana bei za restaurants, bado mchango wa kitchen pati na sare, baby shower. Na hapo bado hujatoa watoto outing jumapili, Upo wapi uwezekano wa kununua laptop mpya ambayo ni muhimu katika mfumo wa maisha ya kisasa, desktop nyingine kwa ajili ya watoto at home, rim mpya za gari ambazo zimeingia ku modernize gari lako kuu kuu, vipi kuhusu gharama za kujipendekeza kwa kimwana wa job ambaye amekubali kwenda nawe out leo, gaharama za matibabu ktk hospitali binafsi kwa kuwa madaktari wa serikali wapo ktk mgomo, Dogo naye “bro ninunulie basi japo kasimu ka promosheni, ile yangu imedondoka chooni” Mara “Bro/Sister Next week on sato shuleni tunavisit snake Park na sina shilingi 3000 za mahudhurio”, Wife naye “ Daddy leo Mwakasege yupo relini, vipi tutapitia? Hapo ujue kichwani gharama ya taxi baada ya semina, vipi tozo za toyo kwa kuwa nimeachwa na gari la staff. Dullah the balhead kama kawaida anakusubiri uwajibike kwa gharama zako. Mama yangu!!!!!!!! Hapo mwajiri amekuongezea mshahara kwa 7% tu wakati inflation ni above 19%. Ukifikiri kwa makini, unajiuliza watanzania wana-survive vipi kwa style hii??? Ndipo unapoimba "Mwokozi nitoe roho niepuke, hili balaaa" Napenda msomaji utafakari mwenendo wako wa matumizi kulingana na hali hali ya uchumi wa nchi na jamii yetu. Kama ukiyumba kwenye suala la kuweka akiba, basi maisha yako yatakuwa yanakabiliwa na ukosefu wa msingi wa muongozo au utakuwa unatumia gharama kubwa kwa mambo yasiyoweza kusaidia familia yako.

Saturday, January 12, 2013

BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO HEWANI TENA...AHSANTENI KWA MAOMBI YENU...!!!

Nimetulia nakula embe karibuni si mwaona zilivyo nyingi:-)


Blog ya Maisha na Mafanikio inapenda kuawataarifu kuwa sasa itakuwa nanyi hewani tena kama kawaida. Napenda kuwatakeni samahani kwa usumbufu wa kutopata matukio kama ilivyozoeleka. Pia nachukua nafasi hii kuwa-SHUKURUNI KWA MAOMBI YENU kwa safari yangu na familia yangu. Tumesafiri salama na hii nina imani ni kutokana na maombi yenu. AHSANTENI SANA PAMOJA DAIMA....KAPULYA...

Saturday, January 5, 2013

LEO NI SIKU YANGU YA KUZALIWA ....MIAKA INAKWENDA JAMANI

Leo ni tarehe/siku ambayo familia ya Mzee Ngonyani ilikuwa kumpati binti huyo ambaye alizaliwa siku hii ya leo. Na leo ameongoza mwaka tena na kuzidi kuzeeka. Lakini hata havyo anapenda kuwashirikisha ndugu, jamaa na marafiki kwa siku hii ili tumsaidie kusherekea. Na wote manakaribishwa..sana. NAWATAKIENI SIKU NA WAKATI MWEMA. WOTE MNAPENDWA SANA ...KAPULYA

Wednesday, January 2, 2013

BADO NIPO SONGEA NA NIPO SALAMA..KHERI YA MWAKA MPYA 20113!!!!

Nataka kuwafahamisha ya kwamba nilisafiri salama na nipo salama. mAJUKUMU YALIZIDI...Na pia NAWATAKIENI WOTE KHERI SANA KWA MWAKA MPYA 2013...BADO NIPO SONGEA..TUTAONANA MUDA SI MREFU....KAPULYA