Ni hatari kwa mtu kudhani kwamba, anajua kila ambacho kinaendelea kwenye mawazo au hisia za mpenzi wake. Kuna uwezekano mkubwa hisia zako zinaweza zisiwe sahihi, kama ambavyo mara nyingi imekuwa ikitokea. Kuna migogoro mingi ambayo chanzo chake ni hisia potofu, hisia zitokanazo na mtu kujaribu kuingia kwenye mawazo au hisia za mwenzake.
Hebu fikiria, umeingia ndani mwako kutoka huko utokako. Unamkuta mumeo/mkeo akiwa amekunja uso. Kabla hujamuuliza chochote unaanza kufikiria kwamba, amekasirika kwa sababu leo umechelewa kurudi nyumbani kwa nusu saa tu. Unaanza kuwaza kwa kulaani kwamba, mumeo/mkeo siyo mtu wa maana kwa sababu ya wivu. Unaweza kufikiria kwamba, usiku huo utamwambia ukweli na kama ni kugombana ni afadhali iwe hivyo, halafu unamuuliza "Vipi mbona uko hivyo, nini tena?"
Mumeo/mkeo anakujibu "Hapana, nina taarifa mbaya, nimesimamishwa kazi kutokana na tuhuma fulani...." Unabaki ukiwa umepanua mdomo, kwa sababu uliingia kwenye mawazo yake na ukawa umekosea sana. Mfano huu ni wa jambo dogo, kuna wakati tunaweza kuingiza mawazoni mwetu fikra kwamba, wenzetu hawatupendi kwa kudhani kwetu kwamba tunaweza kujua yale yanayoenda mawazoni mwao. Kutokana na kufikiri kwetu hivi, tunaweza kuanza kufanya mambo ambayo sasa ndiyo yatapelekea wapenzi wetu kuacha kutupenda.
HABARI HII NIMEITOA KWENYE KITABU CA MAISHA NA MAFANIKIO KILICHOANDIKWA NA MUNGA TEHENAN...JITAMBUE
--------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
Hii huwa inatokea mara nyingi sana na watu wengi wamepoteza marafiki zao kwa hili jambo la kusoma mawazo...ni bora kuuliza....