Wapendwa wasomaji wa blog hii na wanablog wenzangu nimekuwa nikipokea email nyingi toka kwa wasomaji wa blog hii wa huko nyumbani Tanzania, wengi wakielezea uzoefu wao na wakitaka niziweke hapa ili tujadili kwa pamoja, na mimi sina kinyongo kwa kuwa blog hii inazungumzia Maisha, basi nitakuwa nikiziweka hapa ili wasomaji wengine wapate kujifunza
Leo nimewaletea kisa cha kusikitisha cha binti aitwae Katarina, naomba muuangane na msimulizi wa kisa hiki.
**********************************************************************
Alikuwa ni mtumishi wa nyumbani na alikuwa na umri wa miaka 14 wakati huo, nakumbuka ilikuwa ni mwaka 1993, ndio aliletwa kufanya kazi kwa shemeji yangu.
Nakumbuka nilikuwa naenda kwa shemeji yangu kila baada ya wiki kumjulia hali yeye na wanae.
Huyu Binti ambae alikuwa akijulikana kwa jina la Katarina mwenyeji wa kule Iringa alitokea kunipenda kweli na hakuficha hisia zake, kalikuwa ni kabinti kazuri na kadogo sana na kalikuwa na heshima kweli.
Siku moja shemeji yangu aliniambia kwa utani lakini, kuwa Katarina ananipenda na Kama nikitaka kuoa basi nisitafute mwanamke mwingine bali Katarina angenifaa zaidi.
Sikutilia maanani kauli ya shemeji yangu, na niliichukulia kama utani tu. Nilikuwa kila nikienda kwa huyo shemeji yangu Katarina atahakikisha ananipikia na kuniandalia maji ya moto ya kuoga tena kwa heshima kweli na nikishaoga kama nitalala pale alipenda sana kupiga soga na mimi na alikuwa akivutiwa sana na simulizi zangu za uongo na kweli.
Ilitokea nilipata kazi moja ya muda mfupi ambapo nililazimika kwenda Msolwa Morogoro ambapo nilikaa kwa miezi sita niliporudi nilikaa kama mwezi mmoja kabla sijaenda kwa shemeji yangu ambaye alikuwa akiishi Mbezi kwenye nyumba yake mwenyewe kumjulia hali.
Siku moja nilijikuta nikipata hamu sana ya kwenda kumuona shemeji yangu na nakumbuka ilikuwa ni mwaka 1994 mwishoni. Nilipotoka kibaruani jioni nilikwenda kwa shemeji yangu, lakini nilipofika nilikuta kuna mtumishi mwingine pale nyumbani, nilikaribishwa na kwa bahati mbaya shemeji yangu hakuwepo nyumbani alitoka kidogo kwenda kwa shoga yake aishiye mtaa wa pili.
Kumbuka kwamba kipindi hicho kulikuwa hakuna simu za mkononi, ilibidi nikae pale sebuleni peke yangu kwani hata watoto wa shemeji walikwenda kwa marafiki zao kusoma tuisheni.
Nilikaa pale sebuleni peke yangu kama saa moja na nusu na ndipo shemeji akarudi na aliponiona alifurahi sana. Tulizungumza mambo mengi sana lakini sikumsikia akimzungumzia Katarina, mwishowe ikabidi nimuulize. “Shemeji, tangu nimefika hapa sijamuona Katarina, mchumba wangu, je yuko wapi?” niliuliza kwa utani.
Niliona uso wa shemeji yangu ukisawajika kwa huzuni na alinyamaza kimya kwa sekunde kadhaa, kabla hajasema kitu alimuomba yule binti aliyenipokea ambaye niliambiwa ni mtumishi wa pale nyumbani amletee maji ya kunywa.
Muda wote tukisubiri maji yaletwe tulikaa kimya na alionekana kuwaza sana, hali ile ilinitisha sana. Mara maji ya kunywa yakaletwa, alikunywa funda kadhaa za maji kisha akaweka ile glasi chini na kushusha pumzi ndefu, kisha akasema.
“Shemeji ni jambo la kusikitisha kukujulisha kuwa Katarina alifariki wiki iliyopita na taarifa hizo tumezipata juzi” Alisema shemeji yangu kwa upole, niliposikia taarifa ile kuna kitu kilinichoma moyoni kama msumari wa moto na nilijihisi kama natetemeka na kijasho chembamba kilinitoka.
“Amefia wapi, aliugua nini, na amezikwa wapi?” yalinitoka maswali mengi mfululizo.
Shemeji yangu alinisimulia kuwa, aliamua kumtafutia shamba boy wake wa zamani kibarua katika kiwanda fulani cha wahindi kwa kuwa alitarajia kuoa na kabla ya kuanza kazi alimtuma kwao Singida akamletee shamba boy mwingine ili amfundishe kazi awe ni mrithi wake kabla hajaanza kazi yake mpya.
Alikwenda Singida na akaja na huyo kijana na baada ya kumfundisha alikwenda kuanza kazi na kumuacha yule kijana mpya pale nyumbani.
Kumbe kuna siku yule kijana shamba boy mpya alimbaka Katarina, lakini alimtisha kuwa akisema atamuua na kukimbilia kwao Singida asionekane tena.
Katarina aliogopa kusema na akabaki kimya akiugulia maumivu baada ya kitendo kile. Haikupita muda , yule binti alianza kuumwa umwa na kutapika kusikoisha, ikawa kila anachokula anatapika. Utendaji wa kazi ukapungua na akawa anatumia muda mwingi sana kulala. Shemeji yangu akajenga wasiwasi ikabidi amdadisi kama ana mimba.
Awali Katarina alikataa katakata kuwa ni mjamzito, lakini shemeji alimtishia kuwa atampleke Hospitali kesho yake akapime ili kujiridhisha Katarina alikiri kuwa ni mjamzito. Sasa Shughuli ikawa kwenye kumtaja mhusika, Katarina alikataa kabisa kumtaja mhusika shemeji ilibidi atumie mbinu ya kumtisha kuwa atampeleka Polisi na ndio akamtaja yule kijana lakini alisema kuwa alitishwa sana kuwa akimtaja atamuua ilibidi shemeji amfuate yule kijana chumbani kwake ili kumdadisi lakini kumbe yule kijana alikuwa akifuatilia ule mzozo kupitia dirishani na aliposikia jina lake likitajwa kuhusika na ile mimba alitoweka haraka sana asijulikane alipokwenda.
Ilibidi shemeji abaki na ule mzigo, kwanza alikuwa ni mjane pili hakuwa na mfanya kazi wa Ng’ombe maana yule kijana katoweka na pia mtumishi wake wa ndani yaani Katarina ndio huyo ni mjamzito, na yeye ni mtumishi serikalini, ilikuwa ni kaazi kweli kweli.
Ilibidi afanye mawasiliano na marafiki zake na kwa kushirikiana na yule boy shamba wake wa zamani alifanikiwa kupata mfanyakazi wa ng’ombe mwingine, na baada ya wiki akapata House girl mwingine.
Baadae alimshauri Katarina arudi kwao Iringa na alimuahidi kumpa pesa ya kutosha ili imsaidie kujifungua na akijifungua alimtaka arudi kwake ili aendelee na kazi.
Ni kweli Katarina alikubali japo shingo upande na alikuwa na wasiwasi jinsi atakavyopokelewa nyumbani kwao na wazazi wake.
Baada ya wiki moja Katarina alipakiwa ndani ya basi na kurudishwa Iringa na yule Shamba Boy wa zamani. Shemeji aliandika barua ndefu kueleza mkasa uliompata Katarina ili wazazi wake wasije kumuadhibu.
Aliporudi kutoka Iringa yule shamba boy aliyempeleka Katarina alisimulia kuwa walipokelewa lakini kwa wasiwasi kutokana na hali aliyokuwa nayo Katarina. Na kama si ile barua alioandika shemeji, basi yule shamba boy angelipishwa mahari na kuozeshwa yule binti, lakini ile barua iliposomwa ndio wakaamini japokuwa wapo walioitilia mashaka kuwa huenda imetengenezwa makusudi ili kumnasua yule kijana. Hata hivyo yule binti alikanusha kuwa yule kijana aliyefuatana naye hahusiki.
Baada ya kupita mwezi mmoja shemeji yangu alipokea taarifa kuwa Katarina alifariki wiki moja iliyopita baada ya jaribio la kutoa mimba kushindikana.
Taarifa zaidi zilisema kuwa alipata manyanyaso pale nyumbani kwao kwa wazazi wake kutokana na kwamba walikuwa wanamtegemea na baada ya kurudi pale nyumbani wakawa wana hali ngumu na hivyo kumtupia Katarina lawama kuwa amekuwa mzembe kaharibu kazi kwa umalaya.
Katarina alikusudia kuitoa mimba ile ambayo ilishatimiza miezi sita na ndipo ikashindikana na akapoteza maisha yeye na kiumbe kilichokuwa ndani.
Nilishikwa na butwaa wakati wote shemeji yangu alipokuwa akinisimulia mkasa huo wa Katarina.
Ni miaka 15 sasa tangu binti huyu afariki Dunia, lakini leo katika hali ya kushangaza nimetokea kumkumbuka, sijui ni kwanini.
Dada Yasinta nakuomba uuweke mkasa wa binti huyu katika blog yako kama Dedicationa kwa binti huyu ambaye alifariki mwezi huu wa Disemba japo tarehe siikumbuki.
Ni mimi msomaji wa blog yako Miki Malissa
9 comments:
,habari yako dada yasinta,ni mara yangu ya kwanza kuacha comment humu ila ni msomaji mzuri wa hii blog,hii habari imenisikitisha sana na imeniliza ila hatuna cha kufanya .mungu amrehemu katarina wetu.Amin
mara nyingi wazazi pia wanachangia kuharibu maisha ya watoto. Najiuliza, je alipokufa walilia????
kama wlililia walikuwa wanaliaje? je ni kama wale professional mourners wa kule akina nanihiiino ama ni tofauti.... :-(
Hapa kuna msururu wa makosa ya kijamii, naamini kama Katarina angekuwa ameandaliwa kisaikolojia mapema jambo hili lilipotokea angesema na kuhakikisha sheria inachukua mkondo.
jamii nayo yaani familia yake ilitakiwa kumfariji kipindi hiko cha ujauzito wa kubakwa na sio kumnyanyasa kwa ni hata yeye hakufanya bali alibakwa
Walakini hata mwana wa adamu ahijui siku ile, kwakuwa yeye aliyejuu aijuaye siku ndiye muweza wa yote.
Naaam amin nakwambia alilopanga mola katu halitopingwa....subiri, naijua roho yako, nayajua matendo yako...bali ni mwenyezi mungu tu ahukumuye hayo.
mwana wa adamu alikuja kwa wazima na wafu kwa masikini na matajiri.
LAKINI
alihimiza kuwa hakuja KUVUNJA TORATI.
JAMANI
wako wapi TAMWA? wako wapi watetezi wa wanawake jamani msinilize bureeeeeeeeeeeeeeeeeee! ndiyo maana nasema hawa siyo watetezi kabisa ni majangili tupu.
wanawake amkeni kitisho ni nini jamani, msiogope mwana wa adamu yuaja awaokoe ilmradi mifunga malngo wenu mpate amani.
ee mola ikumbuke siku ya kubakwa na kufa binti huyu.
Mimi sijui niseme nini, lakini naamini kuwa hili sio tukio la kwanza kuwatokea mabinti hawa wanaoitwa ma house girl.
Sio kubakwa tu na maboy shamba, bali pia hubakwa na akina baba wenye nyumba, kuna simulizi nyingi zinazowahusisha mabinti hawa na matukio ya aina hiyo na haiyumkini kuwa hata hawa watoto tunaowaita watoto wa mitaani ni zao la mabinti hawa, baada ya kubakwa na wenye nyumba na kisha kufukuzwa na kutelekezwa.
Je taasisi kama hizi za TAMWA, WILAC, TAWLA, CHODAWU nk. zimechukua hatua gani katika kutetea maslahi na madhila wanayoyapata mabinti hawa?
Sitaki kuamini kuwa hawafahamu juu ya tatizo hili.
Mimi ninafahamu mengu juu ya matatizo wanayoyapata mabinti hawa, kwani nilishawahi kuandika pale kibarazani kwangu.
Niliwahi kufanya kazi kwa muda katika taasisi inayofanana na hizo nilizozitaja hapo juu, nilichokishuhudia pale, mpaka leo kinaniumiza moyo, kesi zinazopewa nafasi na kufanyiwa kazi ni zile tu zinazochukua nafasi katika vyombo vya habari ambazo zitakuwa ni kama supporting documents wakati wa kuombea fedha kwa wafadhili.
Wafadhili huangalia zile kesi kubwa zinazochukua nafasi katika media. Kama kesi yako ni ya kutiwa mimba na mwenye nyumba au kubakwa na house boy, ni media gani itaipa uzito kesi hiyo, labda kama tukio hilo litakuiwa limefanywa na hao wanoitwa Vigogo, na tena katika kubalance stori mtuhumiwa akitoa mlungula, basi imekwisha hiyo, binti atajikuta yuko ndani kwa tuhuma za kumuibia tajiri yake.Kesi itamgeukia.
Matukio ya aina hiyo yako mengi na jamii na serikali kwa ujumla haijawa serious katika kushughulikia janga hilo linalowakumbwa watumishi hao wa majumbani.
Dada Yasinta vilio vya akina Katarina viko vingi, sema tu kuwa ni kama sauti ya mnyonge nyikani.
MUNGU AILAZE ROHO YA KATARINA MAHALI PEMA PEPONI....AAAMEN
Baada ya mie kuupata ujumbe wa hii habari nijiulizacho pamoja na mengine ni :
Katarina kwa KUFARIKI umepumzika machungu yaendanayo na MAISHA na kuwa hai?
Katarina wakati tunakukumbuka hivi ni kweli marehemu husikia waongeayo walio hai au walio hai kwa kuongelea au tu kuongea na walio wafu ni jinsi tu ya WALIO HAI kujaribu kukabili kuwa hai kwao?
@Mt Simon: :-(
Kamala na Kaluse wana majibu yooote kwa maswali yako!!!!!!!!!
Kwanza napenda kukukaribisha Saabado, karibu sana na sana na sana.Na pia Ahsanteni wengine wote. Ni kweli hii simulizi ni kusikitisha sana na ni kweli mara nyingine ni wazazi wenyewe wanasababisha vifo vingi vya wasichana kma Katarina. Kwa kutupiwa mzigo waote. Wazazi hawataki hata kujua ilikuwaje mpaka ikawa hivi. Isipokuwa kumpa lawama na tena wengine wanawafukuza kabisa. Nami pia najiuliza kama wazazi wa Katarina walilia kweli waliaje?
kyrie 9
goyard store
golden goose outlet
a bathing ape
off white outlet
hermes outlet
palm angels hoodie
fear of god essentials
goyard handbag
off white outlet
Post a Comment