Monday, October 31, 2011

LAITI KAMA NINGEKUFAHAMU KABLA.........HADITHI YA KUFIKIRIKA

Miaka mitano iliyopita nilikuwa natafuta mke wa kumuoa ambaye angekuwa na sifa nizitakazo. Nilikuwa natafuta msichana mzuri wa wastani maana sikutaka kuoa mke mzuri kupindukia asije niua bure kwa presha na jakamoyo. Nilikuwa natafuta binti atakanikubali kama nilivyo na mapungufu yangu na mimi niliahidi kumkubali na mapungufu yake ili mradi asiwe ni mwenye tamaa ya kupenda sana pesa na mfujaji. Awe na staha na anayeweza kukabiliana na hali yoyote, niwe nacho, nisiwe nacho au kwa kifupi tupendane kwa shida na raha. Pamoja na sifa nyingine ndogo ndogo, lakini muhimu ni upendo na amani vitawale nyumbani kwangu. Hatimaye nilimpata Binti Yasinaty, na kukutana kwetu kulikuwa ni kama muujiza, nakumbuka siku hiyo nilipanda daladala nikielekea kazini na kwa bahati kiti nilichokalia kilikuwa ni cha mwisho upande wa dirishani. Wakati nakaa nikahisi kukalia kitu kigumu, nilipopapasa ilikuwa ni simu mpya kabisa tena ya bei mbaya kama sikosei wakati huo ilikuwa inauzwa shilingi laki nne kwa wakati huo, kumbuka kwamba hapa nazungumzia habari ya miaka mitano iliyopita. Kwa bahati mbaya simu ile ilikuwa imezimwa, na nilipojaribu kuiwasha iliwaka na kuzima kuashiria kwamba betri yake iliisha chaji. Niliiweka mfukoni na kujiuliza kuwa ile simu ilikuwa ni ya nani, sikusikia mtu kulalamika kwamba amepoteza simu na niliogopa kuuliza maana nilichelea mtu kujitokeza na kusema kwamba ni yake ilihali sio ya kwake. Nilifika ofisini na kuanza kazi, baadae nilimuita katibu muhtasi wangu na kumwomba anisaidie kutafuta chaji ya ile simu kwa kuwauliza wafanyakazi pale ofisini, nilikuwa na shauku ya kumfahamu mwenye simu ile ili nimrudishie, kwani nilikuwa namuoana dhahiri akisikitika kwa kupotelewa na simu yake, kwa jinsi ilivyoonekana ilikuwa bado ilikuwa ni mpya kabisa na ilikuwa haijatumika zaidi ya wiki. Katibu wangu muhtasi hakufanikiwa kuipata ile chaja ya ile simu. Niliweka ile simu kwenye droo ya ofisini kwangu ili jioni nikitoka nipitie nayo kariakoo ninunue chaja yake.Ilipofika jioni alikuja mchumba wangu ambaye tulitofautiana wiki iliyopita na kuamua kutengana naye. Sikutaka kuonana naye na nilimwambia katibu wangu muhtasi amwambie kuwa niko bize na sitaki afike tena pale ofisini kwangu. Ukweli ni kwamba nilimpenda sana lakini kitendo chake cha kukuta mwanaume mwingine chumbani kwake tena akiwa amelala kitandani kwake halafu anajidai kunidanganya kuwa eti ni binamu yake hakikunifurahisha kabisa. Nakumbuka nilisafiri kikazi kwenda Mbeya, na ilikuwa nikae kule kwa wiki moja, lakini ilitokea dharura huku Makao makuu Dar ikabidi nirudi baada ya siku mbili tu na nilipofika kwa kuwa ilikuwa ni usiku kama saa mbili niliamua kupitia kwa mchumba wangu ambaye alikuwa akiishi Mwenge ili kupata chakula cha jioni kabla sijaenda kwangu Maeneo ya Sinza. Nilipofika nilimkuta akiwa nje akipika, lakini aliponiona alishtuka sana akabaki kinywa wazi, hakunipokea alibaki ameduwaa, nikahisi kuna jambo. Nilimsalimia alijibu kwa wasiwasi nilipotaka kuingia ndani, alinizuia, na huku akiongea kwa sauti yenye kutetemeka aliniambia eti ndani kuna binamu yake kaja na amejipumzisha kitandani kwake, nilishtuka. Niliiingia ndani moja kwa moja na kumkuta kijana amelala kitandani nilipomuhoji kuwa yeye ni nani na anafanya nini pale akaniambia kuwa yuko pale kwa girlfriend wake na alitaka kujua eti mimi ni nani. Sikutaka kuzua ugomvi, nilimwambia kuwa pale ni kwa dada yangu na nilifika kumsalimia, nilimuomba radhi kwa kuingia bila hodi, ila nilimshauri aharakishe kulipa mahari ili tujue kuwa dada yetu anaye mtu, ili wakati mwingine tubishe hodi, niliongea kwa utani, yule kijana alimsifia sana mchumba wangu kuwa ni mzuri hasa na anajua kupenda, alibwabwaja mambo mengi na upuuzi wao wanaofanya nikiwa sipo, niliongea naye kwa utani mwingi na kuaga na kuondoka, lakini moyoni roho ilikuwa ikiniuma kweli. Nilikuwa nampa yule binti karibu kila kitu alichohitaji, lakini kumbe hakuridhika bado akawa na mwanaume mwingine.Nilitoka na nilimkuta kajiinamia pale nje, sikumuaga nikaondoka zangu. Nilipofika nyumbani nilimtumia ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani nikimwambia kuwa kuanzia siku hiyo ilikuwa ni mwisho wa uhusiano wetu. Hakijibu na siku iliyofuata alipiga simu lakini sikupokea, alibadilisha namba na nilipopokea na kugundua kuwa ni yeye nilikata simu, baadae zilifuata ujumbe kadhaa wa simu yake ya kiganjani akitaka tuonane ili tuyamalize. Sikumjibu. Na ndio akaamua kuja ofisini. Nilimpigia simu katibu muhtasi wangu na kumuamuru amwambie yule binti aondoke pale ofisini. Niliambiwa kuwa amekataa, nilimpigia simu dereva wangu na kumuuliza kama gari limeshatoka gereji, akanijibu kuwa gari litatoka baadae kidogo, nikamwambia akitoka gereji aende nalo nyumbani kisha kesho asubuhi anifuate. Gari langu liliharibika siku mbili zilizopita, hivyo nililazimika kupanda daladala au taxi kama nikiwa na dharura. Niliondoka pale ofisini nikimuacha akiongea na katibu wangu muhtasi na kuondoka zangu. Nilikodi taxi na wakati niko njiani nikakumbuka kuhusu ile simu, lakini niliisahau ofisini, kwa hiyo sikupitia kariakoo tena. Nilikwenda moja kwa moja hadi kwa rafiki yangu anayeishi maeneo ya Kijitonyama na kupoteza muda huko hadi usiku ndio nikarudi nyumbani. Siku iliyofuata dereva alinifuata na kunipeleka ofisini, nilipofika nilimpa ile simu na kumtuma akanitafutie chaja ya ile simu. Baadae alirudi akiwa na chaja ya simu ile na kunikabidhi. Niliichaji na ilipojaa niliiwasha ziliingia ujumbe kadhaa kutoka kwa watu waliokuwa wakimtafuta mwenye simu ile, nilipozisoma niligundua mwenye simu ile alikuwa anaitwa Yasinaty, nilikata shauri nimpigie mmoja wa watu waliokuwa wametuma ujumbe ambaye alionekana kuwa ni mama yake. Nilipompigia simu na kuuliza kama anamjua mwenye simu kwanza alitaka kujua mimi ni nani na kwa nini simu ya mwanaye ninayo mimi. Nilimsimulia kila kitu na nilimuomba ampe mwanae namba yangu ya simu na kumuomba amwambie awasiliane na mimi ili nimpe simu yake. Yule mama alifurahi sana na kunishukuru sana, kumbe ile simu Yasinaty alitumiwa na kaka yake aishie Ughaibuni. Mchana nilipigiwa simu na Yasinaty na tuliongea mengi na alionekana ni binti mchangamfu kweli, alinimbia kuwa anafanya kazi kwenye Hoteli moja ya kitalii maarufu iliyoko katikati ya jiji, nilimuahidi kumpitia kazini kwake jioni nikitoka ofisini. Nilimpitia jioni na kama alivyonielekeza kuwa yuko reception nilimkuta pale akimalizia kazi na aliniomba nimsubiri kweye kijimgahawa kilichopo pale ndani, kwa kuwa mimi sio mnywaji wa pombe niliagiza juisi ili kumsubiri. Baadae alinipitia pale nilipokaa na kunimbia kuwa anatoka hivyo tukutane nje kwani anakwenda kubadili sare za kazini. Alitoka na kunikuta nje nikimsubiri, alipanda kwenye gari na nilimuomba dereva wangu atupeleke Hoteli nyingine ya kitalii maarufu pale hapa jijini ili tupate kahawa na Yasinaty. Tulifika pale tuliagiza vinywaji. Nilitumia wasaa ule kumtazama vizuri Yasinaty, alikuwa ni binti mrembo sana, na mchangamfu hasa, naamini alistahili kufanya kazi reception. Nilimkabidhi simu yake na yakafuata maongezi mengine ya kujuana na simulizi za hapa na pale. Huo ndio ukawa mwanzo wa kujuana na Yasinaty, ambaye baadae alikuja kuwa mke wangu mpenzi. Laiti kama ningekufahamu kabla Yasinaty………………….Habari hii nimetumiwa na msomaji wa blog hii ya MAISHA NA MAFANIKIO ambaye anasheherekea ndoa yake kutimiza miaka mitano leo. Na nimeona si vibaya kama nikiweka hapa kibarazani.

Sunday, October 30, 2011

NINAWATAKIENI JUMAPILI NJEMA, NINAPENDA KUMSHUKURU MUNGU KWA KUFIKA JUMAPILI YA MWISHO YA MWEZI HUU!!!

Hapa katika picha ilikuwa mwezi wa saba wakati nikiwa Ruhuwiko. Kama kawaida Kapulya hakukosa kumdadisi BABA PADRE wakati alipofika nyumbani kwake kusoma misa ya kumkumbuka mpendwa wetu Asifiwe.

Jumapili ya leo nawaomba muungane nami na kuimba wimbo ni katika nyimbo za zamani za Bikira Maria...ambazo ni nyimbo maarufu sana ziliimbwa sana karibu na kila mwumini, naamini mtakuwa mnaufahamu ni huu hapa haya tuimbe pamoja moja, mbili, tatu :- "Sisi wana wadunia tukumbuke maneno aliyosema Bikira Maria, alipo watokea watoto wa Fatima; Lucia, Francisco na Yasinta, alisema tusali....tusali rozari na tupate amani, na tuwaombee wale wakosefu wasio na mwombezi". Ahsante kaka Baraka Chibiriti kwa kunikumbusha wimbo huu:-)

Hata hivyo naona tusikilize na nyimbo nyingize za zamani pia....

JUMAPILI NJEMA KWA WOTE!!!!!

Friday, October 28, 2011

Thursday, October 27, 2011

UJUMBE WA LEO UKUTOKAO KWA KAPULYA NI HUU HAPA!!!

Ndoto zetu zote zinaweza kutimizwa ikiwa tutakuwa na ujasiri wa kutimizwa.

Ngoja Kaka Sam amalizie na wimbo huuu...


ALHAMIS NJEMA JAMANI NA TUSISAHAU KUMSHUKURU MUNGU KWA KILA JEMA NA KILA SEKUNDE ATUPAYE NA KILA ATUJALIALO.

ELIMU:- EBU TUSIKILIZE SIMULIZI YA DADA YACINTA, HAKUNA KISICHOWEZEKANA!!


Kila la kheri Yacinta...hakuna kabisa lisilowezekana kama unapenda. Mvumilivu hula mbivu.

Wednesday, October 26, 2011

Up date/ kuhusu ajali ya kaka Shaban Kaluse!!

Habari za jioni ndugu zanguni ..kama wote mjuavyo rafiki, mwanablog na kaka yetu Shaban Kaluse alipata ajali ya gari jana asubuhi wakati akiwa anaenda kazini. Baada ya kuwasilliana na kwa kutaka kujua anaendelea? Ni kwamba bado ana maumivu kifuani na mbavuni. Amesema kwamba kwa vile mkono huu amekwisha vunja mara moja na hii ni mara ya pili. Kwa hiyo kesho alfajiri atafanyiwa upasuaji kwenye mkono ili kuweka vyuma.

Pia anasema ya kwamba Dereva kakimbia, mwenye gari kamfuata ili wayamalize nje ya Mahakama. Trafik ameshauri kwamba ni vema wayamalize kwa sababu maswala ya bima huchukua hata miaka mitatu na malipo yako ni kidogo sana. Pia wanamuomba atoe ruhusa gari liachiliwe. Ametuomba sisi ndugu/wanablog wenzake ushauri au labda nisema je ?tuna mtazamo gani kwa hili?

Hii ni Zawadi niliyotumiwa leo na Mtani wangu Fadhy Mtanga ni DAGAA NYASA!!!

Si muda mrefu uliopita nimerudi toka katika majukumu yangu. Na nikwa nafikiri nipike nini mchana huu mara naangalia Mwananchi mimi nakutana na hii zawadi. Jamani watu wachokozi kwelikweli...Nimebaki mate yanadondoka maana ile kumbukumbu ya tangu utoto na pia juzi tu nilipokuwa MATEMA BEACH nilikula hawa dagaa tena wale waliovuliwa muda huohuo ila si wabichi kabisa. Waliokwa/chemshwa (lighanda) eeeeehhh, eeehh bwana wewe niliwakula na pilipili (sobola) pia chumvi na limao kwa mbali....sasa leo natamanishwa hivi kweli...kazi kwelikweli AHSANTE KWA ZAWADI MTANI FADHY MTANGA:-)

UKIONA MWANAUME ANALIA UJUE...

NI JUMATANO YA KIPENGELE CHETU CHA MARUDIO......Kama kawaida Kapulya ametembea na kukutana na hii....HABARI HII nimeipata kwa kaka Mbilinyi

Ni mara chache sana utakutana na mwanaume akitoa chozi la uhakika hivi!
(http://www.democracyfornewmexico.com/)
Wanawake kweli ni viumbe wa thamani ambao wakati mwingine hushangaza; hata hivyo yote ni kwa utukufu wa Mungu aliyetuumba tuwe tofauti ili kukamilishana.
Machozi ni moja ya vitu ambavyo mwanamke huhusika moja kwa moja hata katika malezi wazazi wetu walikuwa wanatuonya watoto wa kiume tusilie tukikutana na jambo kubwa au gumu kwani walisema kulia ni mwanamke na si mwanaume.
Mwanaumke huweza kutoa machozi akifurahi, akihuzunika, akikutana na rafiki au ndugu ambaye walioachana muda mrefu, hata wakati mwingine hutoa machozi ili kupata kitu na wakati mwingine hutoa machozi kwa kupoteza kitu katika miliki yake yaani moyo, na kwenye misiba basi huko usiseme maana ukichanganya na mila inakuwa shughuli nzito.Kwa maelezo zaidi ya machozi na mwanamke soma hapa
Pia machozi ni moja ya silaha mwanamke hutumia hasa kujilinda kwani anaweza kujieleza kwamba tafadhari “Usiniambie mapungufu yangu la sivyo nitaaza kutoa machozi sasa hivi”Hata hivyo kazi kubwa ya mwanaume ni kutofautisha machozi ya hisia, msongo wa mawazo na uchoyo, ni kweli mwanamke ni emotional creature ambaye mwanaume lazima uwe makini to handle with care.
Hata hivyo Watafiti wengi wanakubaliana kwamba mwanamke anayetoa machozi ni mzuri sana lipokuja suala la hisia katika maeneo yote ya maisha hii ina maana kwamba mwanamke mwenye kumwaga chozi mara kwa mara ni mtamu chumbani kwa sababu anaweza kujieleza katika lugha ya mapenzi (love making, act of marriage) Na mwanamke mwenye macho makavu maana yake ni mgumu kuji –express wakati wa kuwa mwili mmoja.
Wanawake wenye machozi ni mara chache sana kuwa baridi (frigid) wakati wa kuwa mwili mmoja kwani ukimwandaa ni rahisi kuwa connected kihisia.
Pia kujua machozi ni dawa soma hapa.
TUKUTANE TENA JUMATANO IJAYO KATIKA KIPENGELE HIKI CHA MARUDIO.KILA LA KHERI!!
Ebu tumalie na kaka Kidumu na wimbo huu...

Tuesday, October 25, 2011

KAKA SHABAN KALUSE APATWA NA AJALI YA GARI/DALADALA NA KUVUNJIKA MKONO WA KULIA!!!

Nimeamka asubihi hii na kukutana na ujumbe huu kwenye simu yangu ya kiganjani kutoka kwa kaka yetu na wanablog mwenzetu Shaban Kaluse, ujumbe unasema hivi:- Dada Yasinta nimegongwa na gari. Naomba uwajulishe wanablog kwamba nimepata ajali na niko AMANA ILALA kwa matibabu. Nimevunjika mono wa kulia. Nilikuwa navuka barabara maeneo ya Tabata Mawenzi ili kupanda daladala, nikagongwa na daladala lingine ambalo lilikuwa likiovertake kushoto ili kuwahi abiria, mimi sikuliona kabisa. Namba za hiyo daladala ni T 837 AUK.

Monday, October 24, 2011

Siku ya Umoja wa Mataifa/FN DAGEN

Muda si mrefu kijana wetu Erik amerudi kutoka shule. Baada ya kumuuliza za shule akanijibu safi sana. Na baadaye akawa anisimulia kuwa kwa kuwa leo ni SIKU YA UMOJA WA MATAIFA/FN DAGEN. Basi huko shuleni katika darasa lake,walikuwa huru kuchagua cha kufanya. Na baadaye wakawa wanaimba na moja ya wimbo ulikuwa huu hapa.

JUMATATU NJEMA JAMANI!!!

CHUMBANI/CHUMBA CHA KULALA KIWEJE?

Habari zenu ndugu zangu natumaini wikiendi yenu wote imekuwa sio ya pilikapilika sana.

Haya mwenzenu leo nina swali ambalo limekuwa likinikera muda sasa. Lakini jana nilishindwa kuvumilia na wakati nipo kazini nikawauliza wafanyakazi wenzangu. Jambo lenyewe ni kuhusu chumba cha kulala. Na swali lenyewe ni hivi je? chumba cha kulala kinatawa kiweje? Yaani pembeni mwa chumba kuwa na vimeza na je hapa kwenye vimeza kuwe na nini? na je? kuwa na TV? Computer? na aina nyingine ya vitu? au kuwa na kitanda tu?...na baadaye baada ya pitapita /udadisi wangu nikakutana na habari hii hapa chini ambayo nimeiunganisha. haya tusaidiana kupeana ushauri.
---------------------------------------------------------------------------------------------

naamini baadaya ya siku ndefu kutafuta riziki, na baada ya siku ndefu kuongea na watu tofauti, kukasirishwa na watu tofauti na wakati mwengine inafika mda mwili wako unakuwa umechoka unachohitaji na kupumzika katika kitanda chako cha nyumbani.. wengi nimesikia wakisema huwawia vigumu kupumzika vizuri kitanda kingine tofauti na alichonacho nyumbani.. sababu ni kwamba labda godoro la nyumbani ni zuri kuliko sehemu nyengine ama tu ukilala nyumbani unapumzika vizuri zaidi ukiwa pembeni ya mtu aliyekaribu na moyo wako..

ndio swala la chumbani linapoingia, sehemu ya kulala hupaswa kukufanya uchovu uliokuwa nao wote kutoweka, chumba cha kulala hakitakiwi kuwa na vitu vingi vya kufanya hata hewa isiingie, sijui viatu, kapu la nguo chafu, ma vengine vingi.

hupendeza chumba chako cha kulala kiwe na kitanda tu peke yake, lakini kwa watu ambao nyumba zao ni ndogo basi kabati ndani ya chumba sio vibaya lakini muda eote liwe limefungwa, na hata kama umeweka viatu kwenye chumba chako basi hakikisha kabla hujavipeleka chumbani viatu vyako unaviweka kwanza sehemu ya hewa nje ili uvundo na jasho viweze kutoka ndio uvipeleke chumbani, na wenye makapu ya nguo chafu chumbani akikisha makapu hayo yanamifuniko kuzuia harufu mbaya ya nguo zilizovaliwa siku za nyuma kabla ya kufuliwa.

chumbani mambo mengi sana hufanyika ukiacha kulala, hata kupumzika tu na mwenzi wako mkiongelea mambo fulani ya maisha yenu. kwahiyo hutaki kufanya hivyo na harufu mbaya ikiwapitia pembeni. Habari hii nimekutana nayo hapa.

Sunday, October 23, 2011

JUMAPILI YA LEO EBU TUSIKILIZE KWAYA HII YA WATOTO HAWA!!


Nimeipenda kwaya hii watoto wanaimba vizuri pia wana sauti nzuri.Nikaona tusiwasahau watoto na ndio nikaona wao watupe raha jumapili ya leo. JUMAPILI NJEMA SANA KWA WOTE.

Saturday, October 22, 2011

Nilikwenda kumtembelea Da´Subi ndipo nilipokutana na hii...AMA KWELI DUNIA HII!!!



Nimekutana na habari hii kwa Da Subi nami nikasema nawletea hapa pia muone...inasikitisha kwa kweli.

Je umewahi kukisikia kisa cha mnyamwezi kupigwa na mzungu???!!!

Mzungu alikuwa hajuwi aendako yupo kwenye gari alipofika njiani akaona aombe msaada wa mtu wa kumsindikiza kule aendako. Basi mzungu alipoona wamekwenda mbali kiasi akamuliza kijana bado kilometa ngapi" akamwambia twente tu ,basi mzungu akaongeza mwendo kwavile bado kilometa nyingi alipiga mwendo kilometa 22 zikapita akamwuliza tena,bado kilometa gapi ?? Yule kijana kama kawaida akajibu twente tu ,, akiwa namaanisha twende tu hapo mzungu akakasirika akashuka na kumshusha mnyamwezi na kupiga makofi akimwambia kilometa ishirini na mbili ngapi zimepita kila mara unaniambia twenty two why fulish man go out akamwacha pale na mzungu akaendelea na safari akilalamika njia mzima. Nakwambia nimecheka yaani na nadhani hata wewe utacheka na JUMAMOSI YAKO ITAKUWA MURWAAAAAAAAAAA. JUMAMOSI NJEA JAMANI...

Friday, October 21, 2011

Ijumaa ya leo inatupeleka mpaka Afrika kwetu sio kwingine bali ni Botswana na kipande hiki


Jionee mwenyewe burudani iliyomo katika nyimbo hii yaa Tsabana kutoka katika kundi mahiri la Makhirikhiri la nchini Botswana, ambalo kwasasa bado lipo nchini likiendelea kukonga nyonyo za wapenzi wa burudani. Kwa sababu hii kwa mimi inanikumbukumba LIZOMBE sijui wewe mwenzangu. Afrika ni Afrika na mimi ninapensa sana mambo ya asili.

Thursday, October 20, 2011

KATIKA KUWAZA NIPIKE NINI JIONI HII? GHAFLA NIKAJIKUTA NATAMANI KWELI CHAKULA HIKI...

..ugali na kumbikumbi/mbulika ambacho mara ya mwisho nilikula 2009 nilipokuwa Lundo kando ya ziwa Nyasa . Mwaka huu nilipokuwa nyumbani msimu ulikuwa si mwenyewe. Pia nimetamani kweli ugali na LIKUNGU sijui wangapi mmewahi kula au tu kujua/kuona ? Likungu ni mboga, ni "wadudu/aina ya kama mbu". Huwa wanajitokeza ziwani na watu wanawakamata na kuwakanda kama vile unakanda unga wa mkateau maandazi pamoja na chumvi na pilipili na baadaye wanachoma ili kuhifadhi au unaweza kukanda na chumvi na pilipili na kuchemsha na kulamoja kwa moja. Bahati mbaya sina picha ya LIKUNGU. Ila rangi yake ni nyeusi. Kweli nyumbani kuna vyakula vingi vya asili na vitamu...Sijui sasa nipike nini? maana kupata vyakula hivi hapa itakuwa ngoma ..unga ninao ila...Ushauri jamani?

NGOJA LEO TUPATE CHANGOMOTO KIDOGO!!

Ni hivi:- Maria na kaka yake mdogo aitwaye Juma wanataka tuhesabu miaka /umri wao. Juma anasema ukizidisha umri wangu mara mbili halafu jumlisha jawabu na umri wa Maria na pia zidisha mara mbili, jawabu litakuwa 7148.
Na Maria naye anasema ukizidisha umri wangu mara mbili halafu jumlisha na jawabu la umri wa Juma pia zidisha mara mbili, jawabu litakuwa 5274. Je? Maria ana umri gani? na Juma ana umri gani?....Nawatakieni kila la kheri kwa changamoto hii pia Alhamis njema....Kapulya.

Wednesday, October 19, 2011

HOSPITAL YA LITEMBO YATIMIZA MIAKA 50!!!

Tarehe 10/6/2011 Litembo Hospital ilitimiza miaka 50 ya kutoa huduma ya afya . Ashukuriwe Mungu. Picha hizi nimetumiwa na Padre Raphael Ndunguru ambaye tulisoma pamoja shule ya msingi Lundo.

Hospital ya Litembo
Hapa huyu mwenye kanzu nyeupe ni mhashamu Askofu mpya wa jimbo la Mbinga John Ndimbo.
Sr. Maria Meiss avishwa taji:- Ametumikia Litembo kama muuguzi kwa muda wote wa miaka 50.
Hapa akina mama kwa furaha wameungana kusherehekea.

Ugonjwa wa kifafa washambulia kijiji kizima!!!!!

Leo ni ile JUMATANO ya KIPENGELE CHETU CHA MARUDIO YA MATUKIO/MADA/AMAKALA NA PICHA MBALIMBALI NA LEO TUELEKEE KATIKA MKOA WETU WA RUVUMA. HABARI HII NIMEIPATA HAPA na Albano Midelo

Wananchi wa Kijiji cha Mtua ambacho kinapakana na pori la wanyamapori la Liparamba wilayani Mbinga mkoani Ruvuma wapo katika hatari baada ya ugonjwa wa kifafa kushambulia karibu kijiji kizima.
Uchunguzi umebaini kuwa katika kijiji hicho chenye wakazi zaidi ya 1,600 watu 200 wanadaiwa wanaugua kifafa ambapo kila nyumba kuna mgonjwa mmoja wa kifafa na baadhi ya nyumba zina wagonjwa wawili hadi watatu hali ambayo inasababisha wananchi wa kijiji hicho kuhitaji msaada mkubwa kutoka wizara ya afya na ustawi wa jamii kwa lengo la kukinusuri kijiji hicho.

Kijiji cha Mtua kipo katika kata ya Mpepai ambapo inadaiwa ugonjwa huo ulianza kuwashambulia watu wachache mwaka 1996 ambapo hivi sasa umeenea katika kiwango cha kutisha ukilinganisha na vijiji vingine vya Lipilipili,Kihungu na Changarawe, hivyo kukifanya kijiji hicho kuongoza katika wilaya ya Mbinga na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.

Samweli Matembo ni mwenyekiti wa kijiji cha Mtua anasema tatizo la kifafa ni kubwa katika kijiji hicho ambapo idadi ya wagonjwa inazidi kuongezeka siku hadi siku na kusisitiza kuwa wananchi wengi wanaamini ugonjwa huo ni wa kurithi na kwamba inadaiwa ugonjwa huo unasababishwa na ulaji wa nyama ya nguruwe ambayo haijaiva vizuri,imani za kishirikina,unywaji wa pombe kupita kiasi na kuoa au kuolewa katika ukoo ambao umeaathirika.

“Tatizo hilo lilianza polepole mwaka 1996 na linazidi kuongezeka kwa kasi ambapo hivi sasa wananchi wanashindwa kufanya kazi zao za kiuchumi na kubakia masikini kutokana na muda mwingi kutumia nyumbani kuwaangalia wagonjwa wa kifafa ambao wanahitaji uangalizi wa hali ya juu hasa kwenye moto na maji,hivi sasa wagonjwa wanatumia dawa za hospitali lakini bado tatizo ni kubwa,tunawaomba watalamu wajitahidi kufika hapa ili watusaidie’’, anasema mwenyekiti mstaafu wa kijiji John Nchimbi.

Kondrad Nyika mzee wa miaka 70 anasema katika nyumba yake wapo wagonjwa wa kifafa watatu akiwemo mke wake ambaye anasema kifafa kilimuanza wakati anapika ugali ambaye hivi sasa anatumina dawa za hospitali na hali yake inaendelea vizuri na kwamba watoto wake wawili bado wanaendelea kuugua kifafa bila kupata nafuu licha ya kutumia dawa za hospitali.

Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mtua wilayani Mbinga wakimwelezea mwandishi wa habari hizi kuhusu tatizo la ugonjwa wa kifafa lilivyoathiri kijiji kizima kutokana na kila nyumba kuwa na mgonjwa wa kifafa

John Nchimbi anasema idadi kubwa ya wanafunzi wa shule ya msingi Mtua wanadaiwa wanaugua ugonjwa wa kifafa hali ambayo inasababisha wengi kuwa watoro na kuacha shule hata wale ambao wanasoma wameathirika na kushinda kufuatilia masomo kutokana na ugonjwa huo kuathiri ubongo.
Denis Nchimbi mwanafunzi anayeugua kifafa aliungua moto baada ya ugonjwa kumuanza akiwa jirani na moto na wazazi wake walikuwa shambani
Lauriano Komba mkazi wa kijiji cha Mtua anasema wagonjwa wa kifafa 33 hadi sasa wanadaiwa wameungua na moto baada ya kuanguka kifafa wakiwa peke yao na kusisitiza kuwa kifafa kilichopo katika kijiji hicho ni cha ajabu kwa kuwa katika vijiji vingine idadi ya wagonjwa hawazidi wane ambapo katika kijiji hicho karibu kila nyumba kuna mgonjwa.

Wakizungumza kwa niaba ya wenzao Maria Komba, Juliana Hyera na Flora Nchimbi walisema wanashinda kwenda shambani kutokana na muda mwingi kuutumia kuwaangalia watoto wao wanaugua kifafa kuhofia kuangukia kwenye moto au maji endapo ugonjwa huo unawaanza bila kuwa na mwangalizi.

Takwimu za ugonjwa wa kifafa katika mkoa wa Ruvuma zinaonesha kuwa katika kipindi cha mwezi Julai hadi Desemba 2009 kulikuwa na wagonjwa 1072 kati yao wanaume 639 na wanawake 433 ambapo wilaya ya Mbinga inaongoza kwa wagonjwa 337,Songea manispaa 309,Songea vijijini 217,Namtumbo 62 na Tunduru 147 takwimu hizi ni wale walioripoti kwenye vituo vya afya.

Baadhi ya wanawake katika kijiji cha Mtua baada ya kutoa maoni yao kuhusu tatizo ka kifafa linavyowaandama.

Mratibu wa magonjwa ya akili na kifafa mkoa wa Ruvuma Talumba Gullum anasema wagonjwa wengi wa kifafa hawajitokezi kwenye vituo vya afya na hasa waliopo vijijini ambao kutokana na kukosa elimu sahihi dhidi ya ugonjwa huo wanaamini ugonjwa huo ni ushirikina na wa aibu hali inayowafanya wagonjwa kuwaficha majumbani na tatizo kuongezeka.

Kulingana na watalaamu wa afya kifafa (Epilepsy) kinatokea kunapokuwa na mapungufu katika seli za ubongo na kwamba kunapokuwa na hitilafu katika huu mfumo kifafa kinaweza kutokea ambacho dalili zake ni kuona maluwe luwe (aura), kiasha kupoteza fahamu, kuanguka na kutupa miguu na/au mikono, kukaza mdomo, kutoa povu na wakati mwingine na kutoa haja ndogo au kubwa.Hata hivyo watalamu wa ugonjwa huo wanasisitiza kuwa kifafa sio ugonjwa wa kuambukiza, mara nyingi unakuwa kwenye familia kwa kurithi toka kwa mzazi au wazazi, na kwamba wakati mwingine inaweza tokea baada ya kuumia ubongo kutokana na ajali, kiharusi (stroke), kuumia wakati wa kuzaliwa (birth injuries) na kwamba Kifafa cha aina hiyo ni tofauti na ‘dege dege’ kwa watoto au kifafa cha mimba (Eclampsia).

Kulingana na wataalamu kifafa hakitibiki na mgonjwa kupona kabisa bali kuna dawa za kupunguza au kuzuia kifafa kutokea mara kwa mara na kwamba dawa hizo zinapatikana katika vituo vya afya na hospitali ambapo mgonjwa atakunywa kwa maisha yake yote ambapo dozi inategemea na hali ya mgonjwa anapoonwa mara kwa mara kwenye kliniki zao maalum.

Tuesday, October 18, 2011

NAPENDA KUTOA SHUKRANI ZANGU KWA WOTE KWA MAOMBI YENU/ JIONI HII NINAJISIKIA NAFUU NA NAAMINI NIPO SALAMA..AHSANTENI!!!


Kwa ajili yenu wapendwa

Napenda kuwashukuruni wote kwa maombi yenu mazuri.Kweli nasema upendo wenu na mshikamano ni mafanikio makubwa kwa mimi na pia kwenu. . Kwa hiyo kwa jambo hili napenda KUWASHUKURUNI WOTE. NA NASEMA PAMOJA DAIMA bila kusahahu UPENDO DAIMA!!!!!

Monday, October 17, 2011

LEO KAPULYA AMEPATIKANA /MWILI UNAPOSHINDWA KUVUMILIA!!!

Nimeamka asubihi nikawa najisikia uchovu uchovu nikadharau na kudhani ni uchovu tu wa kawaida. Lakini nikaona nazidi kuchoka na mwili wote unauma na joto kali ....Kama kungekuwa na mbu basi ningesema malaria lakini sasa....NAUMWA:-(

MICHEZO/HIVI NDIVYO WIKIENDI YANGU ILIVYOKUWA!!

Kuwa na watoto ni raha sana, ila kua wakati unaweza kusema kaaazi kwelikweli. Maana hakuna kupumzika. Kama uonavyo hapa hivi ndivyo wikiendi yetu ilivyokuwa da´Camilla alikuwa katika mechi, hapa yeye ni huyo karibu na kipa huyo mwenye jezi nyeupe na nywele nyeusi ...bahati mbaya timu yake ilishindwa ila kwa kweli walijitahidi na mchezo ulikuwa mzuri sana. Ni handboll/mpira wa mikono.

Saturday, October 15, 2011

MAJIBU KWA NDUGU MANGI NA KAKA SIMON KITURURU!!!

Kutokana na maoni ya ndugu zangu Mangi na kaka Simon Kitururu ambayo yanatoka katika picha hizi nimeona niweke hii picha labda itasaidia. Maoni yenye yalisema hivi:Ndugu Mangi anasema "Akina msitudanganye kabisa!Tuonyesheni kitu kipya na kamili kwa kuvaa mavazi ya wanawake katika picha kamili kuanzia juu kwenda chini mkionyesha uwakilishi wa kitanzania." Na kaka Simon naye anasema "Ghafla naamia upande wa mtani wangu MANGI ,...... nahisi kuna kitu hamjatuonyesha. Na neno la MANGI liheshimiwe nanyi. Amen.
JUMAMOSI NJEMA WAPENDWA!!!!!

Friday, October 14, 2011

UJUMBE WA IJUMAA YA LEO:- UPENDO HUWEZA!!

Upendo /mapenzi ni kama maji tu ambayo yawezayo kuizima kiu ya moyo!!! IJUMAA NJEMA WAPENDWA!!

Thursday, October 13, 2011

PICHA YA/ZA WIKI:-SARE SARE MAUA ASIYEJUA KUCHAGUA KABILA YAKE ....

Dada Rachel

Hapa ni mama/dada wa Swahili na waswahili yupo ndani ya T-shirt ya TANZANIA na ......


Dada Yasinta/Kapulya
...ni mama/dada wa Maisha na Mafanikio naye hayupo nyuma tena kavilia hadi kitambaa/bendera kichwani..wamependeza :-)

HIKI NI KIFUNGUA KINYWA CHANGU CHA ASUBUHI YA LEO NI UJI WA ULEZI KARIBUNI!!

Karibuni tujumuike jamani ni uji wa ulezi...na wala msiwe na wasiwasi kuwa labda hautoshi kuna zaidi!!!



Wednesday, October 12, 2011

ETI MALI NI YA MWENYEWE?

Kipengele cha JUMATANO cha MARUDIO YA MADA, baada ya kuweka hiyo hapo ya kaka Kitururu nikawa natembea tembea tena mitaani nikakutana na hii hapa kaaazi kwelikweli ebu tujadili kwa pamoja hii nayo nimeikuta kijijini kwetu

Inaonekana kuwa mara baada ya kufa mfanyibiashara mkubwa basi aghalabu biashara hiyo huenda sawa.

Hivi majuzi nilipanda moja ya mabasi mabasi ya safari ndefu ambayo wakati wanaanza safari zao ilikuwa na huduma mbalimbali kama za kutoa maji, kuonyesha sinema/video, pipi, biskuti nk.

Huduma kwa wateja pia zilikuwa safi ambapo mlikuwa mwatangaziwa mlipofika na kadhalika. Nilishangazwa na hali ya sasa ya basi hili na nilipouliza nkaambiwa...'huna habari? Mwenye mali keshakufa so watoto ndo wanaoendesha kampuni'

Swali: kwani mwenye kampuni asipokuwepo ndo mambo yaende ndivo sivo?

Je yawezekana yatokeayo Tanzania kwa sasa ni kwa kuwa mwenye mali-Mwl. Nyerere-hayupo? Je kuna siku nasi biashara ya kulinda rasilimali zetu na kuiongoza nji vema ikawa swafi kama biashara nyingine?

HALI YA MTOTO CECILIA NI MBAYA ARUDI BILA KUFANYIWA OPERESHENI

Mtoto Cecilia wakati akiwaomba wasamalia wema waweze kumsaidia.



Hapa Mtoto Cecilia akitoka Hospital ya Regency Dar akiwa ameshikwa mkono na afisa mmoja wa Channel Ten tayari kwa kuelekea Airport kuanza safari ya kwenda India.

Mtoto Cecilia alitangazwa hivi karibuni na Vituo mbali mbali vya habari akiomba msaada wa kusaidiwa pesa za matibabu ambazo zingeweza kumwezesha kufanyiwa operesheni ya moyo ambao umempelekea mpaka Tumbo lake kuvimba kama unavyoliona.

Taarifa za Cecilia ziliweza kutolewa na Miss Tanzania wa mwaka 2006 Bi .Hoyce Temu pale alipoamua kujitokeza na kumtangaza Cecilia akiomba msaada huo. Wasamaria wema walijitokeza na kumsaidia Cecilia mpaka akaweza kwenda India kwa matibabu, cha kusikitisha sana ni kwamba matibabu yake kwa njia ya operesheni yameshindikana kutokana na moyo wake kwa upande mmoja kuathirika na sumu ambayo madaktari wa India wamesema inasababishwa na Sumu ambayo ipo kwenye Mihogo, sumu hiyo huwaathiri sana watoto wenye umri kama wake.

Kwa hiyo imekuwa ni vigumu kumfanyia operesheni hiyo, wakashauri atumie dawa tu ili kuweza kuitoa sumu hiyo, Mtoto Cecilia mpaka sasa hali yake sio nzuri anawaomba watanzania mumuombee ili aweze kupona na aweze kutimiza azma yake ya kuwa Mwalimu. Watanzania tunashauriwa tukiona hali ambayo ni tofauti kwa watoto wetu tuwawaishe Hospitali mapema kwa uchunguzi tunaweza tukawaepusha na hali kama hii aliyofikia Cecilia.
HABARI NIMEIPATA KWA KAKA:
Henry Kapinga wa KAPINGAZ Blog

VILEVI VYA AKILI!!!

Ni JUMATANO nyingine tena na ni kile KIPENGELE CHETU cha marudio..Leo Kapulya katika pitapita na kupekua amekutana na hii mada nadhani wengi wetu hatujawahi kuisoma nimeipata hapa
Kilevi kikubwa kisicho cha kawaida ni dini. Pombe kwa Wabongo, na karibu kila kabila lina vyake. Bangi Wahindi. Wajamaika nk....Pombe kali, Warusi, Wafini nk.........Bia, Wajerumani. Wana viwanda zaidi ya 1200 vya kutengenezea kifyonzo hiki.nk..........Sigara, Wahindi wekundu, dunia, nk.........Ngono, Dunia.nk......Elimu, dunia. nk.........Je umelewa? Kilevi chako ni nini? Je ni ngono?
TUKUTANE TENA JUMATANO IJAYO....!!!!!

SAFARI YETU YA NYUMBANI TANZANIA HATUKUKOSA KUWASALIMIA MARAFIKI/WENYEJI WETU PIA:SHAMBA LA KAKAO HAPA NI MATEMA BEACH

Hapa ni mwenyeji wetu Mr. Mgaya ,akitutembeza katika moja ya shamba lake la kakao. Kwa sisi ilikuwa ni mara ya kwanza kuona ZAO hili la kako ni vipi linalimwa na linaonekana vipi. Maana tulikuwa tunaona kako ipo kwenye kopo tu tayari kwa kunywewa.

Na hapa ni mti wa kako na hizo unazoona zimeningínia ndizo kakao zenyewe hapo bado hazijaiva bado.
Ukimwa mdadisi basi utajifunza mengi ...Yaani nina maana tuliuliza kama kakao zinaliwa kkama zilivyo ..hapo ni matokeo yake tukatafutiwa maoja iliyoiva ikabanguliwa na tukaonja ..sikuwahi kuonja kakao freshi maishani ...ulikuwa msafara ambao tulijifunza mengi sana....

Hapa ni kako zimeanikwa na baadaye zitakuwa tayari kwa kuwa kakao ya unga ..tulishindwa kusubiri mpaka kunywa...Safari nyingine labda.... tembea uone mengi, uliza jifunze mengi nk nk, haya ndio maisha ... kuna mengi yanakuja!!!

Monday, October 10, 2011

MALI NA FEDHA NI KITU GANI KWA MWANAMKE?

Kuna jambo moja leo nataka kulizungumzia, nalo sio jingine bali ni hili la wanaume kutokujua hasa sisi wanawake tunawapendea nini katika ndoa au mahusiano.
Katika maisha yangu ya ndoa nimekuja kugundua mambo mengi sana ambayo huenda wanaume wengi hawayafahamu juu yetu sisi wanawake.

Kuna ujinga mkubwa sana ambao huwa unawasumbua wanaume. Wanaume wengi, sijui ni kutokana na malezi huwa wanadhani kwamba sisi wanawake tunahitaji fedha na mali ili kufurahia maisha ya ndoa au mahusiano.

Na dhana hii ambayo mimi naiona kama ni potofu, huwafanya wanaume kuamini kwamba wakiwa na fedha watakuwa wamemaliza matatizo yote ya mwanamke, na hivyo kuwa na ndoa au mahusiano yenye amani na utulivu.

Na kwa kuwa wanaamini hivyo, basi wakiishiwa ndani hapakaliki, wanahangaika kutafuta fedha ili kuzihami ndoa zao au mahusiano yao na wapenzi wao, kwani wanaamini kuwa bila fedha kutakuwa hakuna upendo tena kutoka kwa wake zao aua wapenzi wao.
Katika kipindi hicho cha ufukara ndipo mwanaume atakuwa karibu zaidi na mke au mpenzi wake kwa hofu ya kuogopa kuachwa, lakini baadae akizipata anakuwa hana muda na (bize)unajitokeza kwani wanakuwa na imani kuwa fedha ipo kwa hiyo uwezekano wa kuachwa na wake au wapenzi wao nao unakuwa haupo.

Sikatai wanaume kutafuta fedha kwa bidii ili kuondokana na umasikini na kuweza kijikimu kifamilia, lakini inapokuja kuonekana kuwa sisi wanawake tunawapenda wanaume kutokana na kuwa na fedha, hilo nalipinga kabisa.
Tuachane na zile dhana zilizojengeka siku hizi kuwa, wanawake wa siku hizi eti wanafuata pesa tu (after money) na wanathamini sana wanaume wenye fedha. Hilo inawezekana lipo lakini hebu tujiulize, hivi mwanamke anayempenda mwanaume kwa ajili ya fedha, hata akiolewa, unadhani atakuwa na amani kweli?

Kama mwanaume huyo atakuwa (bize) hana muda na shughuli zake, halafu anadai kuwa ana amani, basi labda atakuwa anaipata mahali pengine na sio kwa mume huyo, na hiyo ni hatari sana.
Kuna haja ya wanaume kujiangalia mienendo yao, je wanakuwa na muda na wake au wapenzi wao? Na wanatenga muda maalum wa kuzungumzia matatizo ya familia yao na kutafuta suluhu kwa pamoja?

Kuna haja ya wanaume kujikagua na kuangalia upya mahusiano na wake au wapenzi wao yakoje kabla mambo hayajaharibika

Sunday, October 9, 2011

Mahojiano na Upendo Nkone, Upendo Kilahiro na Christina Shusho

Habari hii nimetumiwa na mzee wa Changamoto ...hapa http://changamotoyetu.blogspot.com/




Au labda tusikilza na hapa pia nayo nimetumiwa na kaka Mubelwa pia...
Nyerere Day 2011 in Washington DC.

JUMAPILI NJEMA KWA WOTE NA UJUMBE HUU KUTOKA KWA KAPULYA!!!

Kwa vile mikono yangu haiwezi kukufikia huko uliko. Hebu basi sala zangu zikukumbatie kwa upendo wa MWENYEZI MUNGU .Ukiongozana na baraka, afya njema na sio leo tu bali siku zote!
Basi ngoja tuimalizie jumapili hii kwa wimbo huu wa mpanzi!!!


Au labda twaweza pia kusikiliza redio maria basi bonyeza hapa....http://tunein.com/radio/Radio-Maria-Tanzania-891-s6424/
KRISTU.....TUMAINI LETU!!UWE NA JUMAPILI NJEMA!!!


Saturday, October 8, 2011

UNAMFAHAMU MWANAMTINDO HUYU WA JUMAMOSI HII!!!





Kaka Sam upo? au bado unataka nivae LOL.......hapo kwenye deshi jaza wewe LOL... mdada huyu ni mpezi sana wa sketi ndefu. Sketi ya kitenge hii imeshonwa Songea, top nyeusi imenunuliwa Vila, blauzi kijana /maji ya bahari imenunuliwa H&M. Na nyuma yake nadhani mnaona baiskeli nyekundu hiyo ndiyo inayomfikisha kila aendako...ni usafiri wa haraka sana...


Hapa pia yupo kakaa chini na sketi yake imetanda kama gauni la bibi harusi... LOL.

Swali je? unafikiri ni mpiga picha ni mmoja au ni tofauti? kama ni tofauti hiyo picha ya kwanza nani kapiga na hii ya pili nani kapiga?


JUMAMOSI NJEMA KWA WOTE NA KUMBUKENI MNAPENDWA SANA!!!

Friday, October 7, 2011

MICHEZO: MPIRA WA MIGUU SWEDEN FINLAND 2-I!!

Jioni hii kulikuwa na mechi katio ya Sweden na Finland na Sweden imeshinda na mabao 2. na Finland 1. Mechi/mchezo ulichezwa nchini Finlanda. Hongera Sweden!!!!

IJUMAA NJEMA PIA MWISHO WA JUMA MWEMA!!!



Nikiwa natoka kazini kwenye baiskeli yangu ghfla nikajikuta naimba wimbo huu nikaona niuweke hapa ....TUPO PAMOJA!!!

BABA ASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI MKOANI MBEYA KWA KOSA LA KUMSHINIKI​ZA MKEWE KUNYWA SUMU HADI KUFARIKI

01.Mtuhumiwa Bwana Mohamed Mwawipa ambaye alimshinikiza mkewe Nuru Masuba kunywa sumu baada ya kumtuhumu kuwa amemwibia fedha taslimu shilingi laki nne na elfu hamsini akionesha askari wa upelelezi eneo alilonywea sumu mkewe

02. Mweyekiti wa kijiji cha Ijumbi kata ya Ruiwa wilaya ya Mbrali Bwana John Mkalimoyo akimfariji dada wa marehemu Nuru Masuba aitwaye Stumai Wilson ambapo marehemu alikuwa akiishi naye Kijiji cha Mapogolo kapunga.

03.Mwili wa marehemu Nuru Masuba aliyeshinikizwa kunywa sumu baada ya kutuhumiwa kumwibia fedha shilingi laki nne na elfu hamsini na Mumewe Mohamed Mwawipa akipelekwa kuhifadhiwa kaburini, baada ya uchunguzi wa daktari na polisi kukamilika.
Picha na habari na- Mbeya yetu Blog

Mohamed Mwawipa mwenye Umri wa miaka 50 mkazi wa kijiji cha Ijumbi kata ya Luwiwa wilayani Mbarali mkoani Mbeya ameshikiliwa na Jeshi la Polisi wilayani humo kwa tuhuma za kumshinikiza mkewe kunywa sumu baada ya kumtuhumu kumwibia shilingi laki nne na elfu hamsini.
Habari kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa marehemu Nuru Masuba alikuwa na ugomvi kwa kipindi kirefu na mumewe hali iliyopelekea wakatengana lakini October 4 walirejeana upya mahusiano yao hadi kifo kilipomfika.
Akiongelea tukio hilo mwenyekiti wa kijiji cha Ijumbi John Kalikumoyo amesema mtuhumiwa alikiri kutenda tukio baada ya kuhojiwa na uongozi wa kijiji na kwamba endapo mwanamke huyo asigekubali kunywa sumu angetumia silaha ya jadi aina ya kisu kumuangamiza kama fedha hizo hazitoonekana.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Advocate Nyombi alipomuulizwa juu ya kukamatwa kwa Mohamedi Mwawipa alisema kuwa taarifa hizo bado hazijamfikia na kwamba atazitolea ufafanuzi pindi atakapo pata taarifa kamili kutoka kwa mkuu wa polisi wilaya ya Mbarali.

Thursday, October 6, 2011

FIKRA/WAZO LA JIONI HII!!!

1. Je?Kuna mtu yeyote amewahi kukuambia ni jinsi gani una umuhimu kwa wengine?
2. Unajua ya kwamba kuna mtu/watu wanatabasamu kwa upendo wako wa kweli?
3. Je kuna mtu yeyote amewahi kukueleza ni kiasi gani anakupenda? Basi, leo rafiki yangu nakuambia.

Naamini ya kwamba bila kuwa na rafiki utakosa mengi.
Uwe na jioni/siku njema , nina furaha ya kuwa sisi ni marafiki.
URAFIKI UENDELEE NATUMAINI SIKU YAKO ITAKUWA/IMEKUWA NJEMA..NA ITAENDELEA KUWA NJEMA.

Wednesday, October 5, 2011

Sasa tunakaribia Miaka 50 ya uhuru na mfumo huu wa upishi?

Huyu ni kati ya wanake aliyekutwa katika Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma akipika ugali wa mahindi kwa mtindi wa wa kutumia mafiga matatu,kutumia kuni ambazo zinatoa moshi mwingi kwa mama huyu. Katika karne hii ya 21 ambayo inasisitiza maendeleo katika teknolojia Je? huu ni uungwana kweli? au Je una maoni gani katika hali hii? picha kutoka HAPA

Muhimbili, Prof. Masangu Matondo, Mubelwa Bandio, Yasinta Ngonyani, Simon Kitururu...

Kama kawaida KIPENGELE CHETU CHA MARUDIO YA MATUKIO, MADA/MAKALA PICHA NK KITUJIACHO SIKU HII YA JUMATANO. NA LEO KINATUKUMBUSHA MAKALA HII AMBAYO INATOKA KWA DA`YETU SUBI.

Juzi kaka mdogo Mubelwa Bandio aliandika habari ya kumshukuru Dk. A. Kinasha na wengine wote katika hospitali ya Muhimbili na kwingineko ambao walishughulikia suala la afya yake iliyokuwa halijojo hadi kupata ahueni.

Ni mara ya tatu sasa ninasoma mrejesho wa waliopatiwa huduma katika sekta ya afya kwa njia ya blogu. Kwanza nilisoma kutoka kwa Prof. Matondo na pili ikawa ile ya dada Yasinta akisimulia na kushukuru kuhusu mdogowe Asifiwe. Napenda kuamini kuwa wapo watu wengine wengi tu waliofanya hivi kwa njia mbalimbali ikiwemo ya barua, maneno ya mdomo, kupiga simu, kwenye redio, televisheni na hata kuandika magazetini na kwenye vijarida kadha wa kadha.

--------------------------------------------------------------------------------
Yasinta Ngonyani Ninaafiki kuwa si watu wote wanaweza kuwa wamezisoma (kama ilivyo habari za kwenye blogu na tovuti, si wote wanaozipata). Lakini faida ya kuandika mrejesho kwa huduma alizopewa mtu zina umuhimu wa hali ya juu kwa wale wote wanaojali na kuzingatia maana na dhana ya neno 'huduma' na katika hilo nikimulikia sekta ya Afya ambayo imekuwa mojawapo ya sekta zinazolalamikwa sana, niliziandika katika posti iliyopita (unaweza kubofya hapa kuirejea).

Kilichonigusa katika posti ya Mubelwa, si tu maandishi yake ambayo niliyapeleka kunako jiko, bali pia maoni yaliyotolewa na wadau, mosi kutoka kwa Kaka Simon Kitururu na pili toka kwa Kaka Prof. Matondo.


--------------------------------------------------------------------------------
Kwa mfano, katika sehemu ya maoni yake, Simon anaandika, "...Huwa unanifanya nifikirie ni WANGAPI maishani mwangu ambao sijawashukuru na WASTAILIO shukurani za DHATI ."
Maneno haya ni kama vile Simon aliyasema kwa niaba yangu (na pengine wengi) kwamba katika kusoma habari za watu wengine, je, tunapata kujifunza kutokana na maneno yao? Kama kuna jambo la pekee sana kutoka kwa Mubelwa ambalo mtu aweza kujifunza, basi ni utamaduni wa KUSHUKURU na kusema ASANTE. Kwa hili Mubelwa ameendelea kunikumbusha tena na tena. Nami kwa sina budi kusema Asante Mubelwa kwa kunikumbusha kushukuru.


--------------------------------------------------------------------------------
Mfano mwingine ni maoni ya kaka Matondo, ambapo sehemu katika maoni yake kwenye posti hii anauliza, 'Hivi madaktari bingwa kama hawa wakistaafu wanakwenda wapi?..." na kisha anamalizia, '...Ningekuwa "serikali", ningewapa kila kitu wanachohitaji na kuwaomba wabakie kazini mpaka umri utakapowaamuru kuacha." na hapa ndipo aliponikumbusha juu ya maisha ya wasomi na wastaafu wetu. Ananikumbusha habari niliyowahi kuisoma katika jarida pepe la IRINnews.org (TANZANIA: Pensioners step in to plug medical gaps) kuhusu baadhi ya wastaafu hawa katika sekta ya Afya nchini Tanzania.
Kisha, upo mjadala uliowahi kujadiliwa na redio ya BBC katika kipindi chake cha Africa Have Your Say (bofya hapa kusikiliza) ambako nako walisikika wastaafu na wasio wastaafu wakizungumza kuhusu faida ama/na hasara ya kuendelea kuwa na watu wa umri ambao unadhaniwa kuwa ni wa kustaafu, wakiendelea kushika nafasi zao za kazi kadiri ya uhitaji si wao binafsi tu, bali kwa taifa lao pia.



Kuna jambo ambalo umewahi kufanyiwa na kuridhika hata ukatamani urejeshe shukrani? Fanya hivyo.

Je, lipo jambo ambalo umewahi kufanyiwa likakuudhi na ukakereka sana hata ukatamani utoe dukuduku ambayo itaonya na kusababisha wahusika wajirekebishe? Liseme.

Hii ni karne ya TEKNOHAMA, wakati muafaka kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano kusema ili usikike.

Elimu, Maarifa, Wajibu, Shukrani... katika maisha ya Mwanadamu.

Tuambizane. Tusemezane.

Tuesday, October 4, 2011

HONGERA KAKA DISMAS NGONYANI/BABA NOELA NA GIVEN KWA KUTIMIZA MIAKA

HONGERA KWA SIKU YA KUZALIWA KAKA DISMAS
Sijui ni uzee au kutingwa? Nilitaka kusahau kuwa kuna kaka anatimiza miaka leo. Nimerudi toka kazini nafungua kitabu changu cha kumbukumbu na kukuta kuwa tarehe ya leo kuna binadamu alizaliwa. Hapo juu ni kaka yangu Dismas akiwa na mjomba wake Erik mwaka huu mwezi wa saba. Wakichezea simu nadhani. Siku kama ya leo kijana huyu alizawa kwa hiyo anapenda kumshukuru Mungu kwa kuwapa nguvu wazazi wake kwa kumlea mpaka kufikia miaka 31 leo. Ukizingatia kwamba na yeye sasa ni baba wa watoto wawili. HONGERA KWA SIKU YA KUZALIWA KAKA DISMAS AU SIKU HIZI TUNAMWIITA BABA NOELA AU PIA BABA GIVEN.!!!!!!!

PICHA YA WIKI...MAZOEZI NI MAHIMU KWA AFYA YAKO!!!

Picha hii imenikuna sana na pia nimejikuta natamani pia kukimba kwani nimekuwa mzembe sana. Ngoja nikurudi kutoka kazini nami nikimbie. Safi sana ..ila sasa usiache endelea hivyo hivyo :-)

Monday, October 3, 2011

TUIANZE JUMATATU HII YA KWANZA YA MWEZI NA HADITHI:- JINSI SUNGURA ALIVYOPATA MAJI


Hapa zamani za kale, kulikuwa na shida Kubwa sana ya maji katika nchi zote. Kwa bahati, likabakia ziwa moja tu. Wanyama wengi wa kila aina walipata maji yao kwenye ziwa hilo. Wanyama wakubwa kama vile Tembo, Simba na Chui; waliwanyanyasa sana wanyama wadogo waliofika kunywa maji kwenye ziwa hilo. Wakawa Hawana raha. Walipata maji kwa shida sana baada ya manyanyaso makali.

Sungura alipoona hivyo, alianza kukuna kichwa akifikiri jinsi ya kuepukana na adha hiyo. Akapata njia. Alitengeneza ngoma na kucheza kwa siri nyumbani kwake. Wanyama wengine waliposikia sauti ya ngoma ile ilivyosikika vizuri, wakavutika nayo. Wa kwanza kuvutika, walikuwa wanyama wakubwa. Wakamwendea Sungura ili wapate kuiona ile ngoma inayotoa sauti nzuri. Sungura akawaambia: “Mimi napiga ngoma hiyo na kucheza pake yangu kwa siri. Ninyi mkitaka kuiona, naomba mje moja moja, nami nitawaonyesha.” Hiyo ilikuwa mbinu yake tu kutaka kujua nani atakuwa wa kwanza na wa mwisho kuja kwake ili apate kuwatenda vibaya.


Tembo alikuwa wa kwanza kwenda kwa Sungura. Akamwambia: “Ingia nyumbani mwangu”. Tambo bila kukawia akaingia ndani. Loo, maskini Tembo! Sungura akafunga mango kwa Nguvu, mara akachoma nyumba yote. Tembo akafa.

Akaja Chui, bila kufahamu kilichotekea kwa Tembo. Yeye akapelekwa kwenye mlima wa mawe wenye mtelemko mkali. Sungura akamwambia: “Hapa wanapatikana wanyama wengi sana. Unisaidie kuwinda ili upate kula karamu kabla ya kucheza ngoma. Wanyama wanapatikana kwa urahisi sana ukifuata taratibu nitakayokuelekeza. Nayo ni hii: Ufumbe macho mpaka mnyama anapoanza kukupita. Kisha, ufumbue macho na umfuate kwa nyuma. Ndipo utakapofaulu kumkamata”.

Chui akakubali. Sungura akapanda mlimani kuporomosha jiwe kubwa. Likaja moja kwa moja kutoka juu na kumponda Chui aliyefumba macho kungoja mnyama. Sungura akamchukua Chui na kumchuna ngozi. Zamu ya Simba ilifika, akamwmbia: “Ngoma hii kila atazamaye, lazima achunwe ngozi kama walivyofanya wenzako. Tazama, ngozi hii ni ya nani? Si ya Chui?” Simba akakubali. Akachunwa kwa tamaa ya kutazama ngoma, akafa. Sungura Akava ngozi hizo kwa zamu ili kwenda ziwani kuwatishia wanyama wadogo. Sungura akatawala maji yale, wakati Wote wa shida, kutokana na werevu wake.

Fundisho
Hadithi hii inawahusu wanyama. Kadiri ya maelezo, unaweza kufikiri kuwa wanyama waliouawa hawakuwa na akili. Hiyo ni hadithi. Na kila hadithi inalo jambo la kujifunza. Kwa mfano:-

Sentensi ya mwisho ya hadithi: “Sungura akatawala maji yale, wakati wote wa shida, kutokana na warevu wake. Werevu wa sungura ulikuwa kuwahujumu wenzake. Hujuma sio kitu kizuri maishani. Ni dhambi. Sisi tusiwe werevu wa kuwahujumu na kuwaonea wenzetu. Mamoja wakiwa wakubwa au wadogo.Katika jambo hilo, Yesu anasema: “Kila kitu mlichomte-ndea mmojawapo wa hawa ndugu zangu wadogo, mlinitendea mimi” (Mt.26:40)
Werevu wetu uwe katika kuwapenda wenzetu na kuwatendea mema.

Hadithi hii imeandikwa na Kat.V:A Ndunguru . Mimi katika pitapita zangu nilikuwa hapa Peramiho basi nikawa nimenunua mkate na nikafungiwa gazeti na baada ya mkate kwisha nikawa naangalia gazeti au kipande cha gazeti na kukutana na hadithi hii nikawasoma wanangu na nimeona niiweka hapa Nayni msome na mcheke kama sisi. Na gazeti lenyewe linaitwa MLEZI.

Halafu hadihi hii imenikumbusha nilipokuwa darasa la kwanza na pili tulikuwa tukiimba sana nyimbo na moja ya nyimbo ni kama hii. Sungura Sungura mjanja wee X2 Ingawa mdogo hushinda wakubwa X2 Akili akili zatoka wapiX2 Ingawa mdogo hushinda wakubwa……