Thursday, April 30, 2009

SALAAM ZA MEI MOSI = SIKUKUU YA WAFANYAKAZI DUNIANI KOTE

Kufanya kazi si adhabu bali ni heshima, kwani kila mtu yampasa kuisha kwa jasho lake.

Kuwa na bidii kutampa mtu cheo, lakini uvivu utamfanya mtumwa.

Atafutaye mema kwa bidii hutafuta fadhila.
Atafutaye madhara, hayo yatamjia.

Kazi ndiyo msingi wa maisha. Maendeleo yanaletwa kwa kufanya kazi, tujenge tabia kujiajiri. Badala ya kujibweteka na kushinda vijiweni.
Nadhani wote tunajua ya kwamba ujuzi hauzeeki. Tunapaswa kuiga mifano ya wengine tufanyapo kazi zetu. Hata zikiwa za kawaida.

“Tazameni maua ya pirini jinsi yanvyomea. Hayafanyi kazi wala hayasokoti. Lakini, nawaambieni, hata Solomon mwenyewe na fahari zake zote hakupata kuvikwa vizuri kama au mojawapo. Ikiwa, basi, Mungu huvika hivyo jani la shambani ambalo leo liko na kesho hutupwa motoni, je, hatafanya zaidi kwenu niny? (Mt 6:28-30)

“Asiyefanya kazi na asile” (2Thes 3:10). Ili tupate maendeleo katika maisha ya jumuia na katika maisha binafsi kila mmoja inampasa kutumia vipawa vyake na kufanya kazi kwa ubunifu na bidii.

Kazi ni kazi. Hata kama ni kazi ya kutifua ardhi, cha msingi inampatia mtu riziki yake halali. Tufanye kazi kwa bidii na maarifa ili tujipatie mahitaji yetu kiuhalali.

MAENDELEO YA TEKNOLOJIA


Angalia jinsi hizo simu zinavyotofautiana ni maendeleo makubwa kutoka kwenye mraba wa sabuni (foma limau) mpaka size hiyo ndogo na nadhani kuna ndogo zaidi jina nisaidieni

UCHUNGU NA FURAHA

Kwa nini ni rahisi kuwa na furaha?
Kwa nini uchungu ni mzito?
Kwa nini kuna furaha kidogo?
kwa nini kuna uchungu zaidi?

Au kwa sababu tunathamini/pendezwa na furaha wakati tunapofikiwa na furaha?
Au kwa vile tunayanyenyekea maisha?
Au kwa vile tunalazimika kucheka?
Au Labda kwa vile tunalazimika kulia?

SIKUNJEMA KWA WOTE

Wednesday, April 29, 2009

BIKIRA

Mada hii nimeruhusiwa na http://mbilinyi.blogspot.com/ kwani nina imani wote tuna nia moja.
Mabinti wa kizulu huko Lamontville Afrika kusini wakisubiri kukaguliwa kama bado ni mabikira huku nyuso zikiwa zimepakwa udongo.
(Picha kwa hisani ya Ellen Emendorp wa NYT)

Kutokana na desturi za huko Sri Lanka bibi harusi ni lazima athibitishe kwamba ni bikira usiku wa harusi yake.
Kila bibi harusi hutakiwa kubeba kitambaa cheupe ambacho huwekwa chini wakati wa tendo la ndoa kwa mara ya kwanza usiku wa kwanza kwa maharusi ili kuthibitisha kwamba bibi harusi alikuwa bikira.
Kitamba kuwa na damu ni certificate kwamba bibi harusi alikuwa bikira.
Na wapo mabibi harusi hukutana na wakati mgumu baada ya kujikuta hawakutoa damu yoyote ingawa ni kweli wao ni mabikira.
Hii ni kwa sababu wasri Lanka kama jamii zingine duniani bado wanaamini bikira yeyote hutoa damu siku ya kwanza na Yule ambaye hakutoa damu huonekana alijihusisha na ngono kabla.

Hiki ni kipimo cha kitambaa kuwa na damu ni kipimo potofu kwani na unscientific, wanawake wengi innocent huumizwa na kuonekana hawana quality ya kuitwa bikira wakati ni bikira.
Ni vizuri watu kujua uhusiano uliopo kati ya kizinda (hymen) na ubikira (virginity)

Bikira ni nani?
Bikira ni mwanamke au mwanaume ambaye hajawahi kufanya mapenzi (penetrative sex) na si lazima awe mwanamke ambaye atatoa damu siku ya kwanza ya tendo la ndoa.
Ni vizuri kufahamu kwamba asilimia 20% - 25% ya mabikira huwa hawatoi damu yoyote kutokana na muundo wa kizinda (hymen)
Wakati mwingine kizinda huondolewa kwa kufanya mazoezi mazito, kupanda baiskeli, kukwea miti na ifahamike kwamba kufanya mazoezi hakuwezi kuondoa ubikira.
Kizinda ni nini?
Kizinda ni ngozi nyembamba sana (membrane) ambayo huziba entrance kwenye uke.
Ina matundu ambayo hutofautiana kwa size ambapo damu ya mwezi kwa mwanamke huweza kupita kila mwezi.

Kuna aina Nne za vizinda
1. Kizinda cha kawaida (normal hymen),
2. Kizinda kisicho na tundu lolote [huhitaji surgery wakati mwingine] (Imperforated hymen),
3. Kizinda chenye tundu dogo sana (Microperforated hymen)
4. Kizinda chenye tishu za ziada na kufanya matundu mawili (septate Hymen)

Bado haijajulikana kazi ya kizinda ni nini, kwani baada ya sex mara ya kwanza huchanika na kuachana na kubaki historia.

Kizinda kiligunduliwa mwaka 1544 na Daktari wa kiarabu Ibn Sinna hata hivyo kufika karne ya 16 watu walikuwa wana imani potofu kwamba kizinda ni ugonjwa na dawa yake ilikuwa ni sex inayofuatana na mwanamke kuolewa.

Kutokuwa na kizinda au kutokutoa damu siku ya kwanza ya sex si evidence kwamba mwanamke si bikira wapo wanazaliwa hawana wengine nyembamba sana na wengine huweza kutoka kutokana na aina ya mazoezi au accidentally.Damu ambayo hutoka siku ya kwanza ya sex ni kidogo sana linaweza kuwa tone hakuna mwanamke amewahi kutoa damu na kulazwa au kuhatarisha maisha yake kwa sex mara ya kwanza.
Pia ifahamike kwamba mwanamke huweza kujisikia maumivu kidogo au discomfort wakati wa tendo la ndoa.
Hata hivyo maumivu mengi huhusiana na woga na ignorance (knoweledge is power), wakati mwanamke anakuwa na hofu, woga wakati wa tendo la ndoa misuli ya uke hukaza na uke huwa tight na mwembamba na wakati mwingine hushindwa kutoa lubricants kwenye uke kutokana kuwa na hofu na matokeo yake ni kusikia maumivu wakati wa penetration.
Pia inawezekana mwanaume hakumuandaa vya kutosha na pia inawezekana wakati wa kumuandaa mwanamke mwenyewe hakuwa relaxed na kuwa tayari kupokea tendo zuri la sex akihofia kuumizwa.

Je, mwanamke kutunza bikira hadi wakati wa kuolewa kuna heshima au fahari yoyote?

Kwa nini suala la kuwa bikira kwa wanaume katika jamii zote linakuwa halina uzito bali wanawake tu?

Je, wakati wa kuoa au kuolewa karne hii ya 21 suala la bikira ni muhimu kuzingatiwa?

Tuesday, April 28, 2009

MAVAZI NA MITINDO YA KISASA=MAISHA

Hili gauni nimelipenda sana na nalitafuta
Na hii begi ndo basi tu naipenda sana

mavazi haya yamenipendeza sana, huu ndio utamaduni mzuri



BAADHI YA MISEMO NA METHALI TOKA TANZANIA

1. Acha kukuna makovu ya mende (Kichaga)
Maana yake ni kwamba uache kukumbuka taabu ya wakati uliopita. Methali hii itafahamika vizuri kama tukielewa kwamba hapo zamani katika jamii zetu, mende walikuwa wanaonekana kwa wingi katika nyumba. Nao mende ni hodari wa kuuma watu wakati wa usiku wakiwa wamelala. Na pale walipouma hubaki kovu ambalo hukuna. Lakini pia ambaye ameshaumwa na mende hao itakuwa ni kazi bure kama atakalia kuyakuna makovu hayo.
Methali hii hutumika kwa kuwaonya watu wasikalie kufikiria makosa au taabu za wakati uliopita.

2. Afadhali kuchakaza nguo kuliko akili (Kipare)
Maana yake ni kuwa hakuna kitu bora kama akili (hekima). Mtu ambaye hana hekima ya uchi kuliko uchi wa aina yoyote ile. Kuwa uchi kinguo, mtu anaweza kununua zingine. Lakini mtu anapokuwa uchi kiakili, hakuna maarifa.
Methali hii hutumika kwa kumhurumia mtu ambaye ameharibikiwa na akili na anafanya majambo isivyotakiwa katika jamii.

3. Amekufa hata Mwakafwile aliacha mwana alipokufa (Kinyakyusa)
Methali hii inatokana na mila za kibantu kukosa mrithi ni mwisho wa ukoo na jina la ukoo. Mtoto wa kiume huendeleza ukoo. Ni jambo la kusikitisha sana kutokuwa na mwana mrithi.
Maana ya methali hii ni kwamba mtu anayehusika hana msaada wowote kutoka kwa ndugu, jirani au mahali penginepo.
Hutumika na mtu binafsi aliyezama ndani ya kilindi kikubwa cha matatizo, wala hana mtoto au mtu wa karibu naye ambaye angeweza kumsaidia. Ni methali ya watu maskini na wanyonge katika kuhurumiana shidani. Kama kuunguliwa nyumba, kufiwa nk.

4. Anayetaka usawa mwisho wake uchawi (Kikerewe)
Methali hii ina maana kwamba tukubali kuwa binadamu budi kutofautiana. Fulani kapata baiskeli – lazima nami nipate, fulani kapata nyumba – lazima nami nipate nk. Maneno kama haya mwishowe humsukuma mtu kutumia hila mbaya au njia zisizo za kawaida kama vile uchawi.
Methali hii hutumika katika kuwaonya wanopenda kujikweza.

5.Fimbo ya jirani haiui nyoka (Kiiraqw)
Ujirani ni jambo jema lakini si vizuri kutegemea misaada yote toka kwa majirani. Methali hii inafundisha umuhimu wa kujitegemea na si kutazamia kupata misaada kila uhitajipo.Pia, ni lazima ieleweke kwamba hakuna sheria inayomfanya jirani atoe msaada hata kama anaweza, yote hutegemea matakwa yake na huwezi kubashiri ni lini atakataa kutoa msaada.

6. Fungo alikosa mkia kwa kulala (Kizigua na kinguu)
Ipo hadithi katika hadithi za Kizigua na Kinguu isemayo kuwa kwa sababu ya usingizi wake Fungo alikosa au aliupoteza mkia wake. Methali hii inaonyesha hasara ya uzembe na kuchelewa mara nyingi. Hali hii inaweza kumkosesha mtu mambo mengi mazuri au kupoteza maslahi yake ambayo yangemfaa baadaye. Hutumika kama onyo kwa wazembe.

7. Anayelala na mgonjwa ndiye anayejua miugulio (Kisambaa)
Maana yake ni kwamba huwezi kujua undani wa mtu mpaka uwe naye karibu katika uhusiano. Hutumika kwa mtu anayejitia kujua sana mambo ya ndani ya wengine kuliko wenyewe wanaohusika.

8. Hohehahe hakosi siku yake (Kiha)
Maana yake ni kuwa kila mtu ana bahati yake. Hata maskini ana siku yake ya bahati. Hutumika kama onyo kuwa inafaa kuthamini watu kwa utu wao na wala si kwa mali walizonazo. Mtu ni utu.

9. Kondoo wa madoadoa hawako katika jamii ya wanadamu (Kimasai)
Wanadamu wote hawahitilafiani sana kwa maumbile yao, na ndio maana tunaweza kusema, binadamu wote ni sawa. Tusikiapo kitu kisicho cha kawaida kuhusu mtu tunaweza kutumia msemo huu kumaanisha kwamba tumestaajabishwa na habari hizo. Msemo huu unatumika pia katika kukanusha habari zisizoaminika.

10. Kucheka chongo ya mwenzio na hali yako umefunika (Kisukuma)
Maana yake ni kuwa si vizuri kucheka makosa ya wengine kwani huenda ukafanya makosa yale yale na pengine una udhaifu wako ambao wengine wanakucheka. Hutumika katika kuwaonya watu wanaocheka dosari au udhaifu wa watu wengine na pengine watu wanaocheka wenzao waliopatwa na maafa k.m. kufilisika.

11. Mbwa mwenye mnofu mdomoni hapigi kelele (Kifipa) Maana yake ni kama methali ya kiswahili isemayo:- Mwenye shibe hamjui mwenye njaa. Methali hii hutumiwa kwa kuwasema watu ambao wana kitu na huwasahau wale ambao hawana kitu. Zaidi, huweza kutumika kwa kuwaonya viongozi wanaosahau kuwatetea wenzao baada ya kupata madaraka na shibe.

12. Mwenda usiku amesifiwa kulipokucha (Kikwere) Mwenda usiku hapa ni sawa na mtu ayetenda jambo ambalo kwa wakati ule wengine hawalielewi. Lakini mwishowe jambo hilo lilipoonyesha mafanikio ndipo watu wakaanza kumsifu. Hutumika kwa mtu anayechekwa na wenziwe juu ya jambo alitendalo iwapo wakati ule wale wamchekeo hawaelewi usahihi wa lile alitendalo.

13. Nguo ya mzee haikosi chawa (kimeru) Maana yake, mzee hakosi akiba. Maana ya methali hii itafahamika zaidi si kwa vile hali ya uchafu ndiyo iletayo chawa, bali kwamba kwa mzee huwa na akiba za aina aina nayo maana yake ni ile nzuri. Methali hii hutumika wakati mtu anapozungumzia utajiri wa mtu mzee. Ni kama njia ya kuwakoga wengine kwamba wakati wote utazamie kumkuta mzee katka hali nzuri, anayo akiba yake ambayo ameihifadhi.

14. Usidharau wakunga uzazi ungalipo (Kibena) Wakunga ni watu wenye kuheshimiwa sana kwa sababu ya ufundi na ujuzi wao wakati wa kuzalisha. Kwa kuchukua umuhimu wao huo, wanawake hushauriwa kutowadharau maadamu wangali wanazaa, isijeikawa wakti wa kujifungua wakakosa msaada. Matumizi ya methali hii ni kuwaonya watu kwa ujumla wasiwe na dharau kwa kitu ambacho kitawafaa katika maisha yao. Zaidi kwamba, kitu kilichokusaidi wakati uliopita usikidharau kwa vile hukitumii kwa wakati huu.

Sunday, April 26, 2009

BINADAMU NA MAZINGIRA:- INAPENDEZA WATU KUWA NA MALENGO KATIKA MAISHA

Bila shaka haijawahi kutokea mtuakapanda garimoshi au ndege bila kujua anakwenda wapi na kwa nini anakwenda huko. Lakini kwenye maisha ndivyo ilivyo kwa wengi. Wengi wamepanda garimoshi la maisha lakini hawajui wanaelekea wapi na kwa nini?

Hivi sasa vijana wengi ambao wanalalamika kwamba hawana ajira au hwana la kufanya, watu wengi ambao wanalalamika kwamba mambo yao au kila jambo wanalofanya linakataa, wanakabiliwa na tatizo hili. Wengi wamepanda garimoshi la maisha lakini hawajui hasa wanakwenda wapi.
Kwenye maisha hakuna tofauti. Mtu ambaye hajui hasa anataka kufanya nini au anataka kuwa nani maishani, hawezi hata siku moja kutulia na kupata mafanikio. Bila shaka atakuwa ni mtu wa kuhangaika kwa kufuata harufu au uzuri bila kujua kwamba hivyo sivyo anavyovitaka.

Mahangaiko hususani shughuli:- Kuna wengi sana miongoni mwetu ambao hufanya shughuli hii kidogo na kuiacha na kurudia ten hii hadi wanazeeka na kufa. Kuna watu ambao wana vipaji na ujuzi wa mambo fulani, lakini watu hawa ni kama vipepeo, wanatua ua hili na huruka tena kwenda ua lile na tena na tena. Kwa nini? Ni kwa sababu hawajaamua mahali pa kwenda, ingawa wako kwenye garimoshi wanasafiri. Kwa sababu tu wana ujuzi au vipaji wanadhani na kuamini kwamba hawapaswi kujiuliza wanataka nini maishani na wanaelekea wapi hasa.

Kila binadamu anatakiwa ajue anakoelekea, ajue anataka kuwa nani. Kwa mtu kujua anataka kwenda wapi au anataka kuwa nani, anajiweka kwenye nafasi ya kuwa na malengo na mipango maishani.Malengo na mipango hiyo ndiyo ambayo inaweza kumsaidia kuwa na dira.

Kama ilivyo kwenye garimoshi. Abiria anayejua kwamba anakwenda mahali fulani hata kama garimoshi litafia njiani, hatakwama kwani anajua safari yake ni ya kwenda mahali maalum, hayo yote ni matatizo ya safari. Lakini yule asiyejua anakoenda anaweza kudandia garimoshi lolote na kushuka popote. Kwa kushindwa kwetu kujua hasa tunakwenda wapi tunataka kuwa nani ndiyo unakuta mtu anafanya shughuli fulani, akitetereka kidogo anaiacha na kuanza nyingine ambayo wala haijui vizuri na wala hajawahi kuifikiria. Akikwama kigogo anakata tamaa na kuacha na kuingia kwenye shughuli nyingine ngumu zaidi.

Kutokujua tunataka nini maishani na tunataka kuwa nani ndiyo maana tunajikuta tunahama na kubadili shughuli kila siku na bado miaka nenda rudi tuko palepale. Kwa sababu hatuja mipango na malengo kuhusu uamuzi wa kile tunachokifanya, tunakuwa ni watu wa kubahatisha maisha tu.

Utakutaa mtu ana genge mahali, lakini hajui kama anataka kuwa na genge kwa sababu kichwani mwake anataka kila kitu. Akiona watu wanapata fedha kwenye biashara ya kuchoma mahindi anaacha genge na kwenda huko. Kesho akiona watu wanauza korosho na wanapata fedha, anaacha kuchoma mahindi na kuhamia huko. Anakuwa ni mtu wa kubahatisha maisha. Unaweza kuhusisha mifano mingi ya aina hii ambayo inatokea katika jamii tunamoishi, iwe katika familia, utawa na hata vyuoni, mtu anabadili masomo ghafla bila maandalizi ya kina.

Kufanya uamuzi ni muhimu:- Maisha hayaendi hiyo na hata siku moja haijatokea mtu asiyejua anataka nini maishani kufanikiwa au kutulia. Kama mtu ameamua kufanya biashara ya genge anashauriwa kuishikilia biashara hiyo na kuipangia mipango yote ya kuikuza. Kama wewe umeamua kusoma masomo fulani au kufanya kazi aina fulani, basi zingatia hilo wala usiyumbe. Kila siku huwa tunasikia watu wakisema “yule jamaa alianza kuuza ndizi na nyanya tu, sasa ametajirika ana maduka ya vyakula mji mzima”. Au utasikia wakisema “yuke jamaa alianza masomo yake kwa njia ya posta tu lakini sasa yuko chuo kikuu” Huwa tunatamka sana kauli hizi lakini bila shaka hatujawahi kujiuliza inakuwaje hadi mtu kama huyu kufikia juu kiasi hicho kutokea chini chini chini sana ambako kunadhalauliwa.

Tukianza kujiuliza tutajua kwamba sababu kubwa ni mipangi inayotokana na kujua kwao wanataka kitu gani maishani mwao. Kwa sababu wanajua wanakokwenda na wanachokitafuta, hata mambo yakienda kombo watangángánia tu kwenye shughuli zao. Wale wasiojua wapokwenda ndiyo ambao wakiyumba kidogo tu huacha kile wakifanyacho na kukimbilia kingine.

Ebu muulize jirani yako:- Hapo ulipo, wakati ukiyasoma makala haya kama kuna mtu unayemfahamu muulize anataka kuwa nani au kwenda wapi kwenye maisha yake? Ni lazima atakuambia, “mahali popote mambo yakikubali naenda...”
Mtu unatakiwa kuwa na malengo kwenye maisha hata kama malengo hayo yatafikiwa baada ya miaka kumi. Kwa kuwa ni malengo ndiyo ambapo utaweza kwanza kutulia na baadaye kufika kule unakokutaka.

Bila shaka unajua wengi ambao wamejaribu kila kitu kuanzia kulima mchicha, biashara ya magari, uongozi hadi uuzaji wa madawa ya kulevya, na bado wanahangaika. Haiwezekanai wakatulia kwa sababu ndivyo ilivyo, hawajui wanakoelekea maishani, ingawa wako safarini. Je?, wewe msomaji wangu unajua ukoelekea maishani?

Friday, April 24, 2009

BINADAMU KATIKA MAISHA YA ULAFI NA ULEVI


maneno ”mlafi” na ”mlevi”:- Walafi na walevi wapo, au tuseme tupo. Walafi wapo majumbani mwetu na huonekana pia kwenye sherehe ama sikukuu. Huonekana kwenye mazishi kunakotolewa chakula, nyama na pombe, huonekana kwenye matanga, maulidi na kadhalika. Si haba wanaokula kwa pupa na kupita kiasi wali, pilau, nyama, mikate, maandazi na matunda mbalimbali hasa ndizi, machungwa, embe na mapapai.

Wakati wa vyakula vipya au mavuno mapya, kesi za kuvimbiwa hujitokeza. Vyakula hata kwa kuvimbisha watu ni pamoja na maboga, matikiti na mahindi mabichi. Wengine huvimbiwa hata kufikia hatua ya kulazwa hospitalini ama kuchunguliaa kaburi kabisa. Walafi wengine walio wakristo hifikia umahututi hata wa kusaabisha kupewa hata sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa. Aibu kweli.!

Walevi nao ni wengi hapa duniani. Hata kama wapo walevi wa kujisifu kwa maneno tu, wapo wanofanya kweli. Hao wanaweza kuzikata pombe na vileo vya aina mbalimbali. Wao wanaweza kutembea pote. Wanaweza kubugia pombe yoyote iliyo karibu yao tangu ulanzi karanga, myakaya, wanzuki, chibuku hadi bia. Nazo bia ni aina zote, tangu Kilimanjaro, Ndovu, Tusker, Serengeti, Castle, Safari hadi Bingwa. Na katika uwanja wa pombe kali wamo pia. Wanaweza kuikata tangu konyagi, gongo hadi ”whisky” kali kama John walker na Vodka na zaidi.

Wednesday, April 22, 2009

WATOTO WA NYERERE NA AMIN WAKUTANA

Bofya HAPA kusikia mazungumzo yao.

Jaffar Amin mwana wa Idi Amin aliyekuwa rais wa Uganda, na Madaraka Nyerere mtoto wa rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere, wamekutana kwa mara ya kwanza kijiji Butiama.

Tuesday, April 21, 2009

MASUALA YA UBAKAJI NA KUPIGA WANAWAKE LINAZIDI KUWA KUBWA

Dunia imeharibika watu wanazidi kupotoka, angalieni haya mambo yanavyozidi kuenea. Mambo kama vile unyanyasaji, kuna ukatili mwingi sana hapa duniani ambao zaidi ni juu ya wanawake na watoto. Hao ndio wanaopata shida zaidi. Ukatili ni kinyume na haki za binadamu na uko ukatili wa aina mbalimbali. Kuna vipigo, matusi, kulazimishwa kufanya mapenzi, kuna baadhi ya mila potofu kama vila ndoa za lazima, kuolewa ukiwa na umri mdogo, kurithi wajane nk.

Bado sijaelewa ni kitu gani kinawafanya wanaume wengine wawapige wanawake. Kwanini umpegi mwenzi wako? Je usipompiga uanaume wako utapotea? Na kuna raha gani kumpiga mwenzako kama mnyama? Na hata mnyama hairuhusiwi kumpiga. Hili suala la kubaka utasikia raha gani wakati mwenzako anapata maumivu yasiyo kifani. Na pia hajapenda.

Je? Mnafikiri hii inaweza kutokana na wengi wanaume wanafikiri wao ndio waamuzi wa kila kitu ndani ya nyumba? Na kwa nini watu wawili waliooana wasikaa chini na kujadiliana na kuona kosa liko wapi. Je? Ingekuwa kinyume ingakuwa sawa?

Au labda wengi wanafuata maandishi haya:- Mwanzo 3:16 Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako, kwa uchungu utazaa watoto na tamaa yako itakuwa kwa mumea, naye atakutawala.

Ndugu wasomaji/wanablog naomba mnisaidie kunipa jibu.

Monday, April 20, 2009

NGOMA YA MGANDA YA KUNYUMBA "LIVE"

Mwenzenu leo nimefurahi kweli kuona ngoma hii"live" Yaani angalia hizo stepu raha sana. Picha hii nimeichukua toka kwa kaka MICHUZI http://issamichuzi.blogspot.com

Sunday, April 19, 2009

JE? UMEGUNDUA HAPA NI NINI KATIKA PICHA HII?

Siku hii ilikuwa ni siku ya kupita kwa ustadi ili hii picha isianguke. Na kulikuwa hamna amani kwani ilichukua siku nzima. JUMAPILI NJEMA KWA WOTE!!!

Saturday, April 18, 2009

MAVAZI YA WANAWAKE

Nimelipenda shairi hili kwani linasema ukweli limeandikwa na Katekista Rafael Mlelwa katika gazeti la Mwenge:-

Natembea natazama, ni hali ya kushangaza,
Mitaani akina mama, mambo wanayoigiza,
Wengine watuwazima, inakuwaje nawaza,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Vazi la Mtanzania, tangu kale heshima,
Watu walijivunia, wa lika zote nasema,
Haya nawasimulia, walivaa akina mama,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Suruali mwavalia, mfanane na wazungu,
Asili mwaikimbia, mnanitia uchungu,
Watu wote angalia, mnamdharau Mungu,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Vimini mwajibalia, mwana kama vikatuni,
Nyingine mnapasua, makusudi mapajani,
Mapaja twaangalia, pia na nguo za ndani,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Siketi taiti pia, mitaani mwavalia,
Hiyoni ya kulalia, maungo yaoneshea,
Mitaani mwatembea, watu kwa kuangalia,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Kweli mwatia karaha, moyoni nasononeka,
Singerendi mwavalia, maziwa yanaonekana,
Mitaani mnahaha, kutwa nzima mwazunguka,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Kwa umbo mmeumbika, kwa uzuri asilia,
Uarabu mwautaka, tena kwa kujichubua,
Kama Mungu angetaka, mngekuwa Saudia,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Wengine watu wazima, tena ni wake za watu,
Watoto wenu lazima, watawaigeni tu,
Malazi yao lazima yatakuwa yenye kutu,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama.

Hapa mimi nasimama, naomba mnisikie,
Wanamama wenye hekima, hali hii tukemee,
Hakika mimi nasema, tena isiendelee,
Mavazi mnayovaa, ya aibu kinamama-

Friday, April 17, 2009

GHAFLA SIKU MOJA TULIINGILIWA NA HAWA WAGENI "SIAFU"

Ruhuwiko/Songea 2009 mwezi wa pili . Siku hii ghafla tulifikiwa na wageni bila kutegemea. Ni wadudu hatari sana lakini bahati nzuri tuliwashtukia na kuwasaidia waendelee na safari yao. Ila wangeingia ndani basi leo tungeongea mengine.

MNAONAJE?IJUMAA YA LEO TUCHEZE BAO/NCHUA AU KWA JINA UJUALO WEWE


Lakini hapa uchezi tu kuna kitu pia unajifunza natumai wato mmenielewa vizuri tu.

Thursday, April 16, 2009

MAISHA/KUTEMBELEANA NA KUTAKANA HALI

Haya sasa wasomaji hapa duniani watu tumeumbwa tofauti kwa kila kitu. Kwani mimi nilikuwa nadhani watu wote tuna mawazo sawa hasa katika jamii. Kama nilivyosema tangu mwanzo kabisa nilipoanza kublog, kama wote mmesoma tangu mwanzo. Vipi tunalea watoto wetu. Yaani haya maisha ya baba, mama na watoto inanisumbua sana akili yangu. Ukizingatia vipi sisi waafrika tunavyolelewa. Kwa kweli mimi inanipa shida sana, ni vigumu kuelewa kwa nini dunia nzima wasiishi kama sisi waafrika. yaani kuwatembelea wazazi, ndugu na marafiki mara kwa mara. Yaani huku watu wanathamini zaidi pesa/kazi kuliko jamii. Utakuta mtu anamwacha mama yake baba yake mzazi kwenye nyumba ya wazee ili atunzwe na watu wengine kwa sababu yeye ana shughuli nyingi. Nimewauliza mara nyingi je? wangeacha hao wazazi wako leo ungekuwa wapi? Lakini wao wanasema kila mtu na maisha yake. Na nimejiuliza je? hii ni haki au vipi? Kwani najua sisi Afrika tunaweza tukaishi pamoja ukoo mzima na tunatunzana. Ndugu wasomaji mnasemaje mnaonaje upi ni utaratibu mzuri?

Jambo jingine ni kwamba nina nusu mwaka sijaonana na majirani zangu lakini leo ghfla wakati nipo nje nafanya usafiwa mazingira. Amekuja jirani yangu na kunisalimia na pia nia yake kubwa ni kuonyesha ya kwamba amepata mjukuu. Yaani huyo tunaishi pua na mdomo lakini kuonana ni kasheshe. Inawezekana wakati mwingine jirani anakufa na usiwe na taarifa. Huwezi kujua, na pia kuna mila/tabia huwezi tu kwenda msibani bila kualikwa. Sasa kwa vile kajua kanaanza kujionyesha basi kuku wote wamefunguluwa. Ukizingatia wakati huu ndo kuna kuwa na ile michomo ya kitimoto na bila kusahau bia (ulanzi). Mmhh. Maisha haya kazi kwelikweli.

Wednesday, April 15, 2009

MGANDA+BURUDANI/UTAMADUNI=MAISHA

Kucheza ngoma za asili sio suala la mabududisho tu, bali ni sehemu mojawapo ya kudumisha utamaduni wetu.

Tuesday, April 14, 2009

MAISHA YA BINADAMU YANA UTAMU NA UCHUNGU WAKE

Maisha ni yenye ladha ya aina yake. Kwa upande mmoja maisha hayo ni yenye ladha ya utamu na upande mwingine yana ladha ya uchungu na ukakasi. Utamu au uchungu wa maisha hutokana na mambo kadha wa kadha ambayo hutokea maishani.

Maisha huwa na ladha ya utamu pale mtu anapokuwa mwenye siha njema, maelewano mema na wengine, mafanikio katika maisha, hali njema kiuchumi nk. Maisha hayohayo hubadili ladha yake pale mambo yanapokuwa magumu na kukuendea kombo. Ugumu huo wa maisha hutokea pale mtu anapokuwa katika afya mbaya,katika majonzi, msiba, mahusiano mabaya na wengine, kuwa katika mfadhaiko na kushindwa katika mambo mbalimbali ya maisha. Pia mambo mengine yanayosababisha ladha ya maisha kwa amani na upendo katika nchi, vita, hali ya ukimbizi nk.

Mambo kama hayo na mengine ya mtindo huo husababisha maisha kuonekana magumu kubadili ladha yake. Pia yanapomkabili mtu katika nafasi yake mtu huyo hushikwa na mfadhaiko na kusongwa nafsi yake hatimaye hupatwa na jakamoyo na kukata tamaa ya kuishi.

Katika ulimwengu tunaoishi kuna fujo tele. Fujo hizo husababisha ladha ya maisha kuchachuka. Ladha hiyo huyafanya maisha yaonekanane kuwa magumu na yenye kukatisha tamaa. Sasa hivi kuna vilio mbalimbali kutoka kona zote za dunia vitokanavyo na mwenendo wa maisha. Sio mara moja tunasikia redioni na kusoma katika magazeti juu ya kumomonyoka kwa maadili. Kuna maonevu mengi ambayo sasa yanaelekea kwenye kuhalalishwa kama sehemu ya maisha ya kisasa.Ubakaji leo hii umekuwa tu kama hadithi za kuburudisha. Utoaji wa mimba unaoendana bega kwa bega na utupaji wa watoto ni kama vitendewili vya kutengwa na kutegeliwa.

Dunia yetu imetawaliwa na vita na magomvi yasiyo kifani. Vita hivyo husababisha maafa, hali ya ukimbizi na shida nyingine za aina aina. Mfano mzuri ni vita vile vya Demokrasia ya Kongo ilivyosababisha lukuki ya wakimbizi. Tena yapo magonjwa ambayo hayana tiba na ambayo husababisha vifo visivyo na idadi kila siku. Magonjwa hayo huwafanya watu kukosa raha ya kuishi.

Tatizo sugu la madawa ya kulevya linazidi kuota mizizi, pamoja na vyombo vya dola kupiga vita dhidi ya mambo haya ya madawa ya kulevya, wahusika wameziba masikio, hawasikii na wala hawaelewi kitu. Kadiri wanavyozidi kutafuta mbinu za kupunguza au kuthibiti ndiyo kadiri hiyo hiyo biadhara inavyoshika kasi yake. Aidha, matukio ya vifo vya watu wanaojinyonga au kujiua wenyewe kutokana na mifadhaiko ya maisha waipatayo yanazidi siku hadi siku. Ukienda mjini, nako ongezeko la vichaa ni kubwa kiasi cha kutishia amani. Hali ya uchumi nayo huzidi kuwa ngumu siku hadi siku. Wenye uwezo wanazidi kujilimbikizia mali na makabwela wanazidi kudidimia. Rushwa tatizo sugu linazidi kupenyeza zaidi, watoa na wapokea rushwa ni wengi. Katika mtumbwa wa rushwa wako mameneja, madaktari, polisi, wakuu wa vyuo, makarani na hata wangoja malango, hapa ni baadhi tu. Bila rushwa huwezi kupata huduma. Haki iko wapi?

Mambo hayo na mengine mengi ya mtindo huo yanakatisha tamaa ya kuishi. Mtu wa kwanza kukatishwa tamaa ni kijana ambaye ndio kwanza anayaibukia maisha. Kijana anapoibukia maisha anakuwa na ndoto nyingi sana. Matarajio yake hutegemea namna gani ulimwengu utampokea. Lakini sasa anapokumbana na mambo ya aina hiyo ambayo yanakatisha tamaa, kijana anabadilika kabisa na kuwa kama vile hana akili nzuri. Hayo ni masumbuko, mateso, adha na kero kwa walio wengi. Siku za matumaini haziji bali bughudha nyingi zinazidi kila siku.!!!!!!

JINSI YA KUBEBA WATOTO KWENYE TOROLI AU MGONGONI (2)

Angalia hapa mtu unakuwa huru na pia umnaweza kutumia mikono kufanya kitu kingine.

JINSI YA KUBEBA WATOTO KWENYE TOROLI AU MGONGONI (1)


Angalia jinsi anavyopata shida kuingia ndani ya basi na hili toroli. Swali je wewe ungependa njia ipi ya kubaba watoto?

Monday, April 13, 2009

UTAMBUE UGONJWA WA SARATANI YA KIBOFU

Ugonjwa wa Saratani ya kibofu (Prostate Cancer) unabaki kuwa kitendawili kwani Waafrika na kwa walio wengi. Kutokana na kutokuwa na uwezo, watu wengi wanaishia kuugua kimyakimya.
Kwa kawaida, ugonjwa huu unapokuwa umefikia kiwango cha juu huonyesha kuwepo kwa uvimbe hatari katiak tezi zilizo chini ya kibofu cha mwanaume kwa kiingereza prostate glands. Kutokana na uvimbe huo, tezi huongezeka ukubwa na kuubana mrija wa mkojo (urethra), hivyo husababisha matatizo katika utoaji wa haja ndogo.

Saratani ya kibofu ni nini?
Chembechembe za mwili huzaliwa na kufa kila siku pia, chembechembe zinazounda tezi za prostate hufa na nyingine kuundwa kila mara kwa ajili ya kuchukua ya nafasi ya zilizokufa. Kama hakuna tatizo lolote basi kitendo hiki hufanyika mara kwa mara.

Kama chembechembe zilizozaliwa zinakuwa nyingi kuliko zilizokufa basi hutokea tatizo. Hali inakuwa mbaya zaidi pale chembechembe zinazozaliwa zinapokuwa haziko sawa na zile za awali, hali ambayo hujulikana kama Saratani ya chembehai. Kwa hiyo Saratani ya kibofu ni saratani inayoathiri tezi za prostate.

Asili ya saratani ya kibofu
Chanzo chake ni uhusiano mkubwa wa ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi pamoja na kuongezeka kw homoni za uzazi ya testosterone.
Ugonjwa huu huwakumba zaidi wanaume wenye umri zaidi ya miaka 75. Ni mara chache sana wanaume chini ya miaka 40.

Hivi karibuni watafiti wamebaini kuwa wakulima, wafanyakazi wa viwanda vya magurudumu,wapakaji rangi, pamoja na wanaume wanaofanya kazi katika mazingira yenye kemikali aina ya Cadmium ambayo ni aina ya metali.

Aina za saratani ya kibofu
Saratani ya kibofu imegawika katika aina nne:-
1. Uvimbe usioonekana lakini unaweza kubainiwa kwa kutumia darubini.
2. Uvimbe dhahiri chini ya kibofu
3. Uvimbe ulioenea kutoka eneo la chini ya kibofu lakini bila kusambaa zaidi sana
4. Saratani inayotokea na kusambaa ndani ya majimaji ya mwili, yajulikanayo kama lymph.
Ugonjwa huu hujitanua kwa kusambaa katika vilengelenge vilivyomo katika majimaji yabebayo mbegu za kiume, kibofu, pamoja na mvunguni mwa tumbo. Kama uanachelewa kmwona daktari mapema huweza kusambaa hadi kwenye mfumo wa lymph, mifupa, mapafu, ini na figo.
Dalili za saratani ya kibofu
Kuna dalili nyingi za saratani ya kibofu. Dalili hizo ni matatizo katika kukojoa ikiwa ni pamoja na mkojo kutoka taratibu, maumivu wakati wa kukojoa, maumivu ya sehemu ya chini ya mgongo na maumivu ya sehemu za tumbo.

Dalili nyingine ni kukojoa mara kwa mara usiku, kutokwa jasho, kushindwa kuzuia kutoka kwa mkojo, mkojo kuwa na rangi isiyo ya kawaida, kuwepo mchanganyiko wa damu katika mkojo, maumivu ya tumbo, maumivu ya mifupa, kupungua kwa uzito wa mwili na upungufu wa damu.

Saturday, April 11, 2009

UBUNIFU WA MICHEZO +KUWAFURAHISHA WATOTO


Tazama hapa mtoto alivyo na furaha kwa mchezo huu wa kukaa kwenye plastiki chakavu na kuvutwa na kamba kama yupo kwenye gari vile. Lisifuni jina lake kwa michezo, mwimbieni kwa ngoma na zeze. Zab 149:3

Friday, April 10, 2009

UJUMBE WA LEO IJUMAA KUU NI:-

Yesu Kristo mwenyewe alichukua dhambi zetu katika mwili wake msalabani, tupate kufa kuhusu dhambi, na kuishi kwa ajili ya uadilifu. Kwa majeraha yake niny mmeponywa (1 Pet 2:24)

Na pia tukumbuke kuwa:-
Kuna mungu mmoja na baba wa wote ambaye yuko juu ya wote, afanya kazi katika yote na yuko katika yote. Waefeso 4:6

Wednesday, April 8, 2009

HERI KWA PASAKA WOTE/GLAD PÅSK ALLA


påskgubben

Påskkäringar

Haya wasomaji naona sasa pasaka inakaribia. Nimeamua niwaeleze kidogo mila na desturi wakati/kipindi hiki cha pasaka huku ninakoishi ni tofauti sana na nyumbani TZ. Ngoja nianze kuwaeleza kuliko kuanza kuwachosha. Ni hivi alhamisi kuu ni kama kawaida au nimesahau sijui yaani watu wanakwenda kazini kama kawaida. Ijumaa kuu baadhi ya watu hawafanyi kazi na JUMAMOSI KUU hapa ndio sikuuu kubwa sio kama nyumbani TZ sikukuu ni jumapili.

Haya sikiliza sasa siku ile ya jumamosi watu wote ni lazima kula mayai kadiri unavyopenda bila mayai basi si pasaka tena. Wana mila hii ya kula mayai kwa sababu hapo zamani kuku waliacha kutaga mayai. Na ghafla walianza tena kutaga na siku ile ya waliyoanza kutaga ilikuwa JUMAMOSI KUU. Hii ndio sababu siku hii ni lazima kuwe na mayai mazani.

Halafu kitu kingine siku hii ya JUMAMOSI KUU watoto wadogo wanavaa kama mababuna mabibi hapo zamani. Pia wanajichora usoni na kalamu za rangi .Na pia wanakuwa na barua ambazo wameziandika/chora wenyewe kwenye vikapu. Na wanapita kila nyumba na kubadilishana na pipi. Ni mila yaani ni kama jambo la kutakiana pasaka njema. Kwa hiyo kipindi kama hiki kila kaya inabidi iwe na pipi au matunda kama huna hivyo viwili basi uwe na hela. mwanzoni nilishangaa lakini sasa nimezoea. HERI KWA PASAKA WOTE!! GLAD PÅSK ALLA!!

Tuesday, April 7, 2009

KUTHUBUTU KUONYESHA MAPENZI/UPENDO=MAISHA


Kuthubutu kuonyesha upendo wako,
sio tu maneno mazuri,
Na sio tu upendo wa matendo
Au maua na chaklet.

Ni kuonyeshana heshima,uaminifu na imani.
Kuonyesha wepesi wa kuona huruma wakati mwanzako anapokuwa na msongo/matatizo.
Kuwa msaidizi mwema na mwenye kusema ukweli.

Kuthubutu kuonyesha masikitiko yako,
Sio kila wakati kujifanya mwenye nguvu(mvumilivu),
Tukae/kaeni pamoja, tuthubutu kuwa watoto ndani yetu.

Tuwe sisi(Kuweni ninyi) kwa dakika chache,
Tuwe na dakika chache za furaha,
Tuwe na dakika cchache za huzuni
Tufante siku iwe ya shangwe.

Tushirikiane katika raha na taabu katika maisha,
Tuwe waaminifu, tukaribiane na tupeane joto.

Monday, April 6, 2009

Friday, April 3, 2009

Video documentary : Taifa linalojengwa na wafanyakazi wa majumbani

Nimeichukua kwa Da Subi kwani najua kuwa wote tuna nia moja.





Nikiwa kama mzazi nimeguswa sana na maelezo katika vido hii kwa kweli ni dhurumana pia naweza kusema unyama kabisa. Soma na sikilizeni wenyewe na semeni mnawanza nini na je huu ni uungwana?

Ni imani yangu kuwa hakuna ubishi ya kuwa elimu ya darasani yenye malengo maridhawa ndiyo msingi mahsusi wa maarifa na maendeleo kwa jamii yoyote ile. Mtizamo huu ndiyo unaonisababisha nisikubaliane na kitendo cha watoto kufanyishwa kazi majumbani kwa kisingizio tu cha kuwa mzigo kwa kushindwa kuendelea na masomo ama ya sekondari au ufundi.

Kazi si adhabu wala dhambi, lakini kazi yenyewe inapofanyika bila kuzingatia mustakabali wa maisha ya wafanyakazi wenyewe, hasara inayopatikana kwa muda uliopotea na kudumaa mawazo ni kubwa kwa wahusika pamoja na Taifa lao. Nchi inakosa kuwa na raia walioelimika kwa kiwango cha kutosha kuchangia katika uchumi wa Taifa lenyewe.

Nadhani, nchi inayojengwa kwa vibarua na ufanyakazi wa huduma za nyumbani haiwezi kuwa na misingi imara katika mipango ya maendeleo. Mtapanga vipi mipango ya maendeleo ikiwa unaopanga nao wanafahamu shughuli za nyumbani tu? Ikiwa uamuzi wetu ni kusema habari ya maendeleo lakini hatuna nia ya kuendelea, basi hakuna sababu ya kuzungumzia mipango ya maendeleo, tuendelee kuishi hivi hivi tu. Lengo letu likiwa ni kuendelea, basi ni dhahiri kuwa inatubidi kubadilisha mifumo yetu na kuachana na kuendelea kufanya shughuli zile zile hasa zisizo za ushindani wa kimataifa huku tukitaraji kuona mabadiliko ya kutufikisha kwenye kilele cha maendeleo.

Kwa kweli tumebakia kuwa Taifa la wapokeaji na watendaji wa mazoea badala ya kuwa Taifa lenye wajuzi na wafikiriaji wa mambo mbadala. Hii haifai.
Film documentary hii inaonesha na kuelezea maisha ya watoto wanaofanya vibarua majumbani.

NGOJA LEO TUANGALIE:- UGONJWA UNAOMALIZA WATU WENGI AFRIKA YETU MALARIA

Malaria ni moja ya magonjwa hatari yanayoambukizwa kwa haraka sana. Gonjwa hili linaenea zaidi kwenye nchi za tropiki na (subtropical) juu zaidi kwenye joto duniani, zaidi ya yote Afrika. Dalili kubwa kujua una malaria ni joto la kupita kiasi(homa), baridi ya nguvu, maumivu ya kichwa, maumivu ya mwili, kutokwa na jasho. Pia kinyaa, kutapika na kuhara inaweza kutokea pia.

Wasiliana na daktari kama umepata joto baada ya kusafiri nchi za joto ambazo kuna uwezekano wa kuambukizwa na malaria, hata kama ulikuwa unatumia kinga. Mimi na familia yangu hapa juzi tulipokuwa TZ wote tumeumwa malaria na wakati huo huo tulikuwa tunatumia kinga. Kwa hiyo kula/kunywa kinga si kuwa hutapata malaria.

Watu zaidi ya milioni 300 kila mwaka huambukizwa na malaria. Zaidi ya milioni moja wanakufa na vifo vingi ni watoto hasa Afrika. Hapa Sweden kuna ripoti watu kama 100 husumbuliwa na malaria kwa mwaka. Wengi wao wameambukizwa Afrika

Ugonjwa huu husababishwa na protozo ambazo ni seli moja kutoka mnyama/mdudu ambaye ni familia moja na plasmodium na kuingia ndani ya mwili wa binadamu kwa kuumwa na mbu wa malaria. Vimelea(parasiter) vinaingia ndani ya seli za maini na humu wanagawana kabla maambukizo ya seli za dawa nyekundu(corpuscle)

Dalili nyingine
Muda kutoka maambukizo mpaka homa kwa kawaida ni kati ya wiki mbili mpaka wiki nne. Lakini inawezekana ikachukua miezi mingi kwa yale malaria ambayo si hatari sana, au muda mrefu zaidi.

Kuna ile aina hatari ya malaria ambayo dalili zake ni ngumu na maambukizi yake hajatibiki kwa hiyo watu wengi wanaweza kuzimia au kufa.
Aina ya pili ya malaria ina dalili ambazo zinaweza kuzuilika ila zinarudiarudia “baada ya siku mbili” au baada ya siku tatu.

Kupinga/kuzuia
Kama unasafiri katika sehemu za malaria jaribu kujiepusha kuumwa na mbu kwa kutumia dawa (anti-mosquito), vaa nguo mbazo unajua zinafunika mwili mzima hasa wakati wa jioni na usiku na tumia chandalua.

Mbu mara nyingi wanauma jioni na wakati wa usiku. Kama unajua sehemu uendayo kuna mbu wa malaria ni lazima uwe na dawa kwa nia ya kuzuia malaria.

Hata kama matibabu ya kuzuia sio 100% yanakinga, ni muhimu kuzuia kwa kunywa dawa kwa sababu ukiacha inaweza kuhatarisha na kusabisha ugonjwa mwingine zidi ya malaria.

Uchunguzi
Utambuzi wa malaria unafanyika kwa kupima damu kwenye darubini.Lakini hapa nilipokuwa nyumbani nilishangaa sana nilipojisikia vibaya nilienda kupima. Nilikwenda kwenye kliniki ya mchina mmoja yeye hatoi damu anatumia komputa tu anaweka vifaa kwenye vidole na inachukua nusu dakika kugundua kuwa una wadudu wa malaria au sio.

Matibabu
Inasemekana kuna dawa nyingi zenye nguvu ambazo zinaweza kutibu malaria.
Kwa urahisi inabidi kunywa dawa mara mbili mpaka mara tatu kwa siku (usiku na mchana). Kama hali inakuwa mbaya sana ni lazima upewe dawa moja kwa moja kwenye mishipa ya damu.

Wengi wanaweza kutibiwa muda mrefu, wakati huohuo mgonjwa mwingine wa malaria anaweza kuhitaji matibabu ya uangalizi makini (intensive care) Muhimu ni kwamba matibabu yaanze mara moja uonapo dalili.

Thursday, April 2, 2009

NAMTAFUTA DADA PRIMROSE KALUNGI TUMEPOTEANA TANGU MWAKA 1999


Tulikuwa tunaishi vizuri sana hapa Sweden yeye ni mtu wa Uganda. Mwaka 1999 alihama hapa na kuhamia UK mtaa wa Croydon , tangu hapa hatujaonana tena isipokuwa nimeongea naye kwenye simu mwaka 2003 mara ya mwisho. Lakini kila nikijaribu kuwasiliana naye simpati. Kama kuna mtu anamfahamu au kama wewe mwenyewe utasoma hapa basi naomba uwasiliane nami. Primrose ni huyo dada aliyesimama upande wa kushoto na amevaa jeans ya bluu.

Wednesday, April 1, 2009

Hivi haya maswali hutokana na nini hasa?

Nimepita ktk kibaraza cha kwa kaka Ramadhani msangi http://www.uchambuzi.blogspot.com/nimeona maswali haya ni maswali mazuri na ni kweli hata mimi nimekuwa nimejiuliza "hivi haya maswali hutokana na nini hasa?" je mtu huwezi kuongea tu bila kuuliza maswali? (Pia yamenigusa kwani binafsi ni mtu wa maswali sana:-)

Limekuwa ni jambo la kawaida sana ambalo limeshazoeleka, kuwa unapokutana na washkaji zako mitaani wanakuuliza kwanini hiki, mara kwanini kile nakadhalika.

Chukulia mfano ulikuwa unafanya kazi, unapoacha au kuachishwa kazi, watu watakuuliza kwanini umeacha au kuachishwa kazi? Kama ulikuwa na demu, mchumba, mke au rafiki na ukaachana naye, watakuuliza kwanini uliachana naye.

Kama ulikuwa unatembea kwa gari na siku ukaamua kuzurura mitaani kwa mguu watakuuliza mbona huna gari leo, na maswali mengine kama hayo. Ninachojiuliza ni kuwa mbona uulizaji wa maswali haya huzingatia upande mmoja zaidi?

Mbona unapokuwa kazini hakuna anayekuuliza kwanini unafanya kazi? Mbona unapokuwa na huyo demu, mchumba, rafiki au mke, hawaulizi kwanini unaye? Mbona unapokuwa unaendesha gari hawakuulizi kwanini unaendesha gari au kwanini ulinunua gari?

Hivi aina hii ya maswali hutokana na nini hasa?