Wednesday, February 29, 2012

MADONGA/NATURAL TROPICAL FOREST FRUITS......



MADONGA/MATUNDA YA ASILI
Nimeamka nikiwa na hamu kweli ya matunda haya ya asili, nimekumbuka nilipokuwa mdogo ukienda mstuni kuokota kuni basi huko nyumbani wasahau maana chakula tayari kilikuwepo. Matunda haya yanakuwa kwanza kijana, na baadaye yanakuwa njano unapasua na ndani yake kuna mbegu. Mbegu hizo zina nyama nyingi tu basi unazimungĂșnyamungĂșnya kama vile pipi na mbegu unatema...weeeeeeeeeeeee ni matamu na sijayala miaka mingiiiiiiiiiiii nimetamani kwelikweli...kama vile LIKUNGU....Kuna mwingine amewahi kula matunda haya????

UPENDO

LEO NI ILE JUMATANO YA KIPENGELE CHETU CHA MARUDIO YA MATUKIO MBALIMBALI NIMEKUTANA NA HII NA HAPA

Upendo ni ukweli wa ndani ya moyo. Upendo ni msukumo wa ndanina si nje. Maana ya upendo huanza ndani ya mtu na kila mtu anao uzuri wa ndani uliobeba upendo ; hata kama mtu huyo anafanya mabaya kiasi gani, au hata kama anaonekana mbaya kimatendo – mimi naamini kabisa kuwa kila mmoja wetu anayo mazuri ndani mwake, mazuri yaliyobeba upendo.

Upendo ni hali ya mmoja kujitoa kwa faida ya ampendaye bila kudai fidia au malipo. Kwangu mimi: Upendo huvumilia, upendo hufadhili; upendo hauna wivu au majivuno.Upendo hauna kiburi na haukosi kuwa na adabu. Upendo hautafuti kujipendeza nafsi; haukasiriki upesi, hauweki orodha ya mabaya.Upendo haufurahii mabaya, bali hufurahia kweli.Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote.Upendo hauna mwisho.








Tuesday, February 28, 2012

JINSI JANA ILIVYOKUWA MJINI SONGEA:-SHEREHE ZA KUMBUKUMBU ZA MASHUJAA WETU!!!

Hapa ni baadhi ya wazee wa kingoni wakiwa wamevaa mavazi wakionyesha mfano JINSI MACHIFU WA KINGONI walikuwa wakivaa wakati wa ukoloni, kkabla ya vita vya majimaji. Hapa ni jana ilipokuwa sherehe hii ya kumbukumbu za mashujaa mjini Songea.

UJUMBE WA LEO!/AU NISEME NI WAZO!!

Ndo ndo ndo si chu ru ru; Ni kwamba ukiwa mwenye ndo ndo ndo au chu ru ru, si jambo la busara kubughudhi au kujigamba mbele ya wenzako. Kwa sababu hayo yote yanategemea uwezo wa Mungu. Na ndiyo tofauti iliyoko katika maisha

Sunday, February 26, 2012

JUMAPILI NJEMA KWA WIMBO HUU ULIOCHAGULIWA NA BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO:-)


NAPENDA KUWATAKIENI WOTE JUMAPILI NJEMA SANA NA NAPENDA KUSEMA TUPENDANE DAIMA KWANI SISI WOTE NI WATOTO WA BABA MMOJA. aMANI YA BWANA NA IWE NANYI NA ITAWALE KATIKA KILA KAYA.!!!!KRISTU NI TUMAINI LETU.

Friday, February 24, 2012

MVUA KUBWA YASABABISHA MAFURIKO MJINI IRINGA LEO

Hapa ni eneo la Zebra ambako mafuriko yameibuka katika maduka ya watu. Habari zaidi hapa.

UJUMBE WA LEO:- KILA BINADAMU ANA MAPUNGUFU YAKE!!!

Sisi binadamu tumeubwa na mapungufu, Hakuna aliyekamilika kila mmoja ni tofauti na mwingine. Kuanzia kimawazo, kimatendo pia kitabia. Na kwa kuwa kama tulivyo, hii ndio maana tuna hitaji pale jambo linapopinda, tuchukue jukumu na kujaribu kuliweka sawa na pia KUSAMEHEANA. Ila KUMSAMEHE mtu si jambo dogo maana kama kweli unamsamehe mtu basi umsamehe KIDHATI/TOKA ROHONI. Au hata kumpa yule mtu aliyekosea/uliyepishana naye mawazo nafasi ya pili/ajaribu tena. Sababu yeye ni banadamu kama wewe, yule, mimi na wao. NACHOTAKA KUSEMA:- KAMA UMEHITILAFINA NA MTU JARIBU KUONGEA NAYE ILI KUSHULUHISHA NA UTAOANA MAISHA YANAKWENDA SAFI. KWANI KUKAA NA KITU MOYONI HAISAIDII KITU. Binafsi kama kuna kitu nimemkosea mtu/nimemdanganya mtu basi NASEMA SAMAHANI SANA kwani hata mie ni binadamu na nina mapungufu.NA NINGEOMBA TUANZE UPYA/SECOND CHANCE. IJUMAA NJEMA!!

Thursday, February 23, 2012

BLOG YA MAISHA NA MAFANIKIO YATIMIZA MIAKA MINNE LEO!!!

Mmmmhh! miaka minne leo imefika kama mchezo!!!!

Blog ya maisha na Mafanikio kama mchezo leo yatimiza miaka minne (4) kamili. Napenda kuchukua nafasi hii na kusema:- Hii yote ni kutokana na uwepo wenu ulioambatana na upendo pia ushirikiano mzuri mlionao. Na kubwa zaidi ni kwa familia yangu kwa kuwa bega kwa bega nami. Pia napenda kusema kwa kupitia michango ya wasomaji na wanablog wenzangu nimeweza kijifunza mambo mengi sana. Na ndiyo kwa sababa hii napenda kusema:- AHSANTENI SANA KWA USHIRIKIANO WENU NASEMA TENA KWANI NAAMINI BILA NINYI, NISINGEFIKA HAPA LEO. KWA KWELI NAAMINI KUWA SISI SOTE NI NDUGU NA NI WATOTO WA BABA MMOJA.UPENDO NA UMOJA WETU UDUMU DAIMA NA PIA MILELE!!!!!

Wednesday, February 22, 2012

JESHI LA POLISI LATUMIA SILAHA ZA MOTO KUTAWANYA MAANDAMANO YA WANANCHI SONGEA

Polisi wakiwa katika gari lao wakati wakutuliza vurugu zinazoendelea wakati huu mjini Songea baada ya wakazi wa manispaa hiyo kuandamana kupinga mauaji ya raia wasio na hatia yanayofanywa na watu wasiojulikana.





Polisi wakiwatawanya na kuwakamata baadhi ya waandamanaji hao katika manispaa ya Songea baada ya wakazi wa manispaa hiyo wengi wao wakiwa madereva wa pikipiki kuandamana hadi ofisi ya kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma kupinga mauaji ya watu yanayoendelea kwa kasi mjini humo ambao hadi sasa jeshi la polisi halijafanikiwa kuwakamata wauaji.




MADEREVA PIKIPIKI WAKIWA WAMEFUNGA BARABARA YA SONGEA KWEWNDA TUNDURU KARIBU NA MLANGO WA KUINGILIA OFISI YA MKUU WA MKOA WA Ruvuma,wakilitaka jeshi la polisi mkoa huo kuchukua hatua dhidi ya mauaji ya watu yanayoendelea mjini songea ambapo hadi sasa zaidi ya watu 8 wameuawa na watu wasiojulikana wengi wao wakiwa ni madereva wa pikpiki.

NA MUHIDIN AMRI,SONGEA



JESHI la polisi mkoani Ruvuma limelazimika kutumia mabomu ya machozi na risasi za moto kuwatawanya wananchi waliokuwa wakiandamana kuelekea ofisi ya mkuu wa mkoa wa Ruvuma na kituo kikuu cha polisi Songea mjini hali iliyopelekea shughuli mbalimbali kusimama.Hali hiyo ilianza kujitokeza majira ya asubuhi ambapo wananchi wa mtaa wa Lizaboni wengi wakiwa ni madereva wa pikpiki walianza kujikusanya na kuanza maandamano kuelekea kituo kikuu cha polisi kilichopo karibu na uwanja wa majimaji mjini hapa.Wananchi hao walikuwa wakiimba nyimbo za kulaumu jeshi la polisi wakidai kuwa limeshindwa kudhibiti mauaji yanayoendelea kujitokeza mjini hapa kila mara ambapo hadi sasa zaidi ya watu kumi wameshauawa na watu wasiojulikana.“Tumeamua kuandamana kwani kimsingi mauaji yamezidi kutokea mjini hapa jana ameuwawa mtu,juzi na usiku wa kuamkia leo ameuwawa mwendesha pikipiki na abiria wake”walisikika wakisema.Baada ya wananchi hao kukaribia kituo cha polisi walianza kurusha mawe na ndipo polisi walijihami kwa kutumia mabomu ya machozi ambapo wananchi hao na waendesha pikipiki walianza kukimbia ovyo na kupeleka maduka kufungwa kwa hofu ya kuibiwa.Licha ya biashara mbalimbali kusimama pia ofisi za serikali ikiwemo ofisi ya mkuu wa mkoa na ya mkuu wa wilaya Songea zilifungwa kwa kuhofia waandamanaji kuingia kwenye ofisi hizo na kufanya uharibifu.Kabla ya maandamano ya leo februari 20 mwaka huu wananchi kutoka kata ya Lizabon waliandamana hadi kwa mkuu wa wilaya ya Songea Thomas Ole Sabaya kulalamikia kukithiri kwa mauaji katani humo ambayo yamekuwa yakifanywa na watu wasiojulikana.Akijibu malalamiko hayo mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa serikali itahakikisha ulinzi unaimarishwa na kwamba aliwataka kuimarisha ulinzi shirikishi ili kukabiliana na matukio hayo maovu.Februari 19 mwaka huu mkazi wa Lizaboni Bakary Ally(20) aliuwawa kwa kukatwakatwa na mapanga na watu wasiojulikana ambapo februari 20 mwaka huu majira ya saa 3.00 usiku mtu mmoja mkazi wa mtaa wa Kipera shekhe Jamari(65) alikutwa ameuwawa kwa kukatwa mapanga kichwani na watu wasiojulikana wakati alipokuwa akielekea nyumbani kwake.Marehemu Jamari alikuwa ni mmoja kati ya viongozi wa msikiti uliopo katika eneo hilo la Kipera.Mauaji hayo yameendelea kujitokeza ambapo mwendesha pikipiki ambaye jina lake halikufahamika mara moja ameuwawa na watu wasiojulikana katika mtaa wa Mji Mwema mjini hapa usiku wa februari 22 mwaka huu na kupelekea wananchi mjini hapa kuishi kwa hofu kubwa.

NI NINI KINAFANYA MAISHA YAWE NA FURAHA?

NI JUMATANO NA NI KILE KIPENGELE CHA MARUDIO MBALIMBALI LEO NI MARUDIO YA November 25, 2008 NDANI YA MAISHA NA MAFANIKIO.
-----------------------------------------------------------------------------------------------
Hakuna kitu kitakacho weza kufanya maisha ya yako/yangu kuwa na furaha kama hatutakubali kujipokea mwenyewe na kupanga mfumo mzima wa maisha yetu. Wengi tunajikuta katika mahangaiko na mafarakano katika uhusiano iwe wa ndoa, au marafiki wa kawaida. Je? ume/tumesha wahi kukaa chini na kujadili kwa nini hili litokee, na je ni kweli kwamba katika haya yote hakuna jibu kwa matatizo haya.

Mpenzi msomaji katika kuchunguza hilo nimegundua kwamba tulio wengi hatuipi nafasi mioyo yetu kuchagua kile kilicho halali kwa matakwa yetu. Bali tunafuata mwelekeo wa mapendeleo yetu na tunaacha nafasi muhimu ya moyo kuupa nafasi ya kuchagua kilicho cha thamani zaidi ya furaha ya siku moja, ambao tulio wengi tumekuwa tukililia au kujionea fahari. Hapa nina maana kwamba kama mwanamke ameahidiwa kuolewa basi atataka haja hiyo itekelezwe wakati hana uhakika wa kweli kama mpenzi wake anampenda kwa dhati.

Kuna misemo isemayo kwamba:- mwanamke anapotoa uamuzi wa kuolewa anafanya hivi akitegemea kwamba mwanamume anayeolewa naye atabadilika baada ya wao kuwa mke na mume; poleni sana wanawake tumepotea, badili mwelekeo olewa na mtu mwenye mapenzi ya dhati na ambaye yupo tayari kutoa dhamiri yake kwa ajili yako.

Na kwa upande mwingine, Mwanamume anamwoa mwanamke na kumleta ndani ya nyumba akitegemea kuwa hatabadilika; Mungu ndiye ajuaye kuwa mwanadamu ni kigeugeu, sasa atutendee nini ndipo tulidhike? Naamini wanawake wengi wanavumilia katika mahusiano ila wapo ambao nao ni wasumbufu, kwa sababu tu ya tamaa, na wengine hujikuta wanabadilika kwa kuwa maisha ni magumu ndani ya ndoa, na wengine umaskini, wanataka kupata chochote au kuiga ufahali wa wengine.

Swali linakuja je? unafikiri kukamatana ugoni na kuonyeshana kwenye vyombo vya habari kwamba nataka kumshikisha adabu ajifunze ni njia sahihi ya kutatua matatizo katika jamii kama watu hawatatumia njia ya kuiweka wazi mioyo yao kwa kile wanachokipenda na kukitamani?

Ni changamoto kwamba kweli tulichokiamua pamoja na kukubaliana basi kiheshimiwe na kuthaminiwa kama kweli humpendi mwenzako sema tangu mwanzo liwe wazi tusitake maisha ya mtelemko kwa kuwa unayemwoa ana nafasi nzuri na wewe unavimba kichwa kwa sifa ya kazi yake na sio mapenzi ya kweli. Wewe utakuwa msaliti.

Maisha ya ndoa ni kuwa tayari kwa ajili ya mwingine wakati wa raha na shida, kwa furaha na amani bila majuto.

Tuesday, February 21, 2012

HONGERA KWA SIKU YA KUZALIWA BINTI YETU CAMILLA!!!

Ni miaka kumi na nne iyopita siku ya jumamosi tarehe 21/2 saa sita kasoro dakika tatu alizaliwa binti Camilla. Kwa pamoja twapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumlinda binti Camilla. Pia tunamshukuru Mungu kwa kutupa nguvu sisi wazazi za kuweza kumpa Camilla malezi yaanayotakiwa.HONGERA KWA SIKU YA KUZALIWA BINTI YETU!!!!

Monday, February 20, 2012

NAWATAKIENI JIONI NJEMA WOTE NA WIMBO HUU!!!


Leo nipo tu hapa nyumbani katika kusikiliza nyimbo angalau siku iishe haraka na pia kuondoa upweke, nimekutana na wimbo huu nimeupenda kwani ni kweli mambo ya kuchaguliwa mchumba ... ngoja niache...

KWA NINI WANAUME WANASHINDWA KULING'AMUA HILI?

Kuna wakati niliwahi kueleza juu ya wanaume kudhani kuwa kuwanunulia wake au wapenzi wao kila kitu kwa maana ya nyumba nzuri, magari ya kifahari na mavazi ya thamani, inatosha kupeleka ujumbe kwa mke au mpenzi wake kuwa anapendwa. Nilieleza kwa kirefu sana juu ya dhana hiyo jinsi isivyo sahihi na niliweka bayana kuwa, wanawake ni viumbe wanaohitaji kusikilizwa kuliko kitu kingine, bila shaka mlio wengi mnakumbuka makala hiyo.

Kwa asili wanaume wanapenda sana kuwasikia wake au wapenzi wao wakikiri kuwa wanawapenda na kufurahia tabia zao nzuri wema walio nao, vipaji walivyo navyo na sifa nyingine lukuki. Wanaume wanapopewa sifa za aina hii na wake au wapenzi wao hufurahia na kupata nguvu na kuona kwamba wana thamani kubwa mbele ya wake au wapenzi wao, kinyume na hivyo wanaume hukerwa na kutowajali wake zao.

Pamoja na kuoneshwa upendo lakini hata hivyo hiyo haitoshi kuwafanya wanaume wawapende na kuwajali wake au wapenzi wao. Kuna wakati mwanaume anakuwa na kazi nyingi sana na anatumia muda mwingi kwenye kujisomea au kuangalia Luninga, hata pale mke au mpenzi wake anaponyesha kwamba anahitaji kuwa naye kwa muda fulani. Kuna wakati pia mwanaume anajali zaidi kazi zake kuliko mambo mengine ambayo mkewe anayataka na kuyaona ya maana.

Naamini wengi mtakuwa ni mashahidi wa kauli hizi, “Yaani niache kazi zangu nikae kukusikiliza wewe na upuuzi wako, subiri nikipata muda tutaongea mambo hayo” kauli hizi ni sumu kali sana katika uhusiano, na huchangia kwa kiasi kikubwa ndoa na mahusiano ya wapenzi wengi kuporomoka.

Ni kweli kuwa kuna wakati mwanaume anaweza kuwa bize na shughuli zake,lakini pale mke au mpenzi wake anapohitaji ukaribu na yeye ni wajibu wake kuonesha kujali.Kama mwanamke anahitaji kufanya jambo fulani ambalo inabidi mwanaume amsaidie, lakini inapotokea mwanaume kuonyesha kwamba hajali sana juu ya jambo hilo bila kujali kama yuko bize au hayuko bize, mwanamke huhisi kutothaminiwa na hiyo humuumiza sana kihisia. Lakini kama mwanaume ataonesha kujali hisia za mkewe na kumsikiliza kwa makini hata kama hatatoa ushirikiano hiyo tu inatosha kumridhisha mke au mpenzi kuhisi kuwa anapendwa na anasikilizwa.
Lakini utakuta wanaume wengi hawajali utashi wa kihisia wa wake zao na huamini kwamba wanawake wanachohitaji ni kupewa fedha au mali na kuhakikishiwa maisha ya kifahari basi. Ukweli ni kwamba wanawake wanahitaji sana kusikilizwa hisia zao na kupewa nafasi pekee na mume au mpenzi wake pale anapohitaji nafasi hiyo ya kusikilizwa. Kumuonesha mwanamke kwamba hana thamani na hana nafasi ya kusikilizwa na badala yake kazi na kusoma, au kuangalia luninga kukaonekana ndio kuna thamani kuliko yeye ni kosa kubwa.

Ni jambo la msingi sana kwa wanaume kulifahamu hili kwa ustawi wa ndoa au mahusiano yao na wake au wapenzi wao, kwani wanawake wanahitaji nafasi kutoka kwa wanaume au wapenzi wao zaidi ya kitu kingine, maana hayo mengine yatakuja kujazia tu

Sunday, February 19, 2012

LEO NI JUMAPILI MAALUMU KIDOGO KWA KAKA YANGU SAVIO /BABA AHSANTE ANATIMIZA MIAKA HONGERA KAKANGU!!

Huyu ni kakangu, Savio Ngonyani/baba Ahsante ambaye alipokea ziwa/titi baada ya mimi na leo ni siku yake ya kuzaliwa ametimiza miaka kadhaa. Savio napenda kukutakia kila la kheri katika siku yako hii ya kuzaliwa. Wote hapa katika kaya hii wanakutakia kila la kheri. Kwa vile najua wewe ni mwanakwaya na halafu Kwaya master basi nakuwekea wimbo huu halafu kikundi cha kwaya ni kama jina lako...

HONGERA SANA KWA SIKU YA KUZALIWA KAKANGU. NA KUMBUKA YA KWAMBA WOTE TUNAKUPENDA.

Saturday, February 18, 2012

FIKRA/WAZO LA JIONI YA JUMAMOSI HII!!!

1. Je?Kuna mtu yeyote amewahi kukuambia ni jinsi gani una umuhimu kwa wengine?
2. Unajua ya kwamba kuna mtu/watu wanatabasamu kwa upendo wako wa kweli?
3. Je kuna mtu yeyote amewahi kukueleza ni kiasi gani anakupenda? Basi, leo rafiki yangu nakuambia. Naamini ya kwamba bila kuwa na rafiki utakosa mengi. Uwe na jioni/siku njema , nina furaha ya kuwa sisi ni marafiki. URAFIKI UENDELEE NATUMAINI SIKU YAKO ITAKUWA/IMEKUWA NJEMA..NA ITAENDELEA KUWA NJEMA. KAPULYA.!!!

Wednesday, February 15, 2012

Jamani siku zinakimbia kweli leo tayari ni ile JUMATANO ambayo ni KIPENGELE chetu cha marudio. Na leo katika kupitapita nimekutana na hii habari hapa kwa mzee wa UTAMBUZI na KUJITAMBUA ambaye siku hizi amepotea kama shilingi ya mkoloni. Haya karibuni .....

Sio lengo langu kuwafundisha wanawake namna yakuachana na wapenzi au waume zao. Lakini hebu fikiria kwamba kila wakati wanandoa au wapenzi wako kwenye vita. Hakuna amani, hakuna masikilizano. Kutwa nzima mtu anawaza kuhusu uhusiano wake mbaya hadi anashindwa hata kufanya kazi. Je, hali kama hii ina maana kwa mtu kuendelea kuwa kwenye ndoa?
Hapa nazungumzia wale ambao wanashindwa kutoka kwenye uhusiano, ambao wanajua kabisa kwamba, unawatesa na kuwaumiza. Kuna sababu nyingi kwa nini watu hawa wanashindwa, lakini nyingine zinatokana tu na kutojua namna ya kutoka, sio utegemezi wa aina yoyote.
Moja ya sababu, ambazo ninaziona sana hasa kwa wanawake ni kujali jamii itasemaje. Mtu anaona kabisa uhusiano haufai na anatamani kutoka . lakini anajiuliza, hivi watasemaje? Kuna wakati ndugu wanamwambia, yeye ndiye mkorofi. Kama hii ndio sababu anachotakiwa kufanya mwanandoa ni kuhakikisha kwamba anajifunza kuishi kama yeye. Nijuavyo mimi, hata wanandugu au jamii hata ikisema vipi, anayeumia au kuepuka kuumia au kuuawa ni yule aliye kwenye mateso ya ndoa
Jambo la kujiliza hapa ni kama, jamii ndiyo inayopigwa, kutukanwa, kutelekezwa au kudhalilishwa? Lakini jambo kubwa zaidi la kufahamu ni kwamba mtu alishaolewa maana yake ni mtu mzima mwenye haki ya kuamua juu ya maisha yake. Akisbiri ndugu wamwamulie, basi huyo bado ni mtoto..
Jambo lingine ni lile la, je nikimwacha nitapata mwingine? kwani wanaume siku hizi ni shida sana? Ni ujinga unaowafanya wengi kuuliza swali hilo. Unahitaji mwingine wa nini? Unahitaji mwingine ili maisha yako yawe ya maana zaidi au? Kama hakuna mwingine ni vyema kwa sababu maana yake ni kwamba hakuna mwingine wa kukutesa. Lakini wanasaikolojia wanaamini kwamba, ‘kila bidhaa ina mnunuzi.’ Kama unataka mwingine, hata ukiwa na miaka sitini utampata. Huwezi kumpata wakati ukiwa ndani ya tanuru la mateso. Ni lazima utoke kwanza.
Kuna wale wanaoshindwa kutoka kwa sababu wanaamini kwamba mwanamke haruhusiwi kutoa talaka. Hi siyo kweli. Kuna wanaoshindwa kutoka kwa sababu dini zao zinakataza kuachana, hii pia siyo kweli. Mwanamke au mwanaume, yeyote anaweza kuomba talaka na ikatolewa, kama kuna sababu zenye kukidhi haja hiyo. Chombo pekee kinachoweza kutoa talaka au kuidhinisha wanandoa kuachana ni Mahakama, siyo dini au taasisi nyingine. Kinachoitwa ‘talaka tatu’ kwa mfano, ni ushahidi tu, na sio talaka.
Kuna wale ambao hawako tayari kutoka kwenye uhusiano mgumu kwa sababu ya mali. Wanaogopa watagawana mali na wenzao, jambo ambalo hawako tayari kulifanya na mara nyingi hawa ni wanaume. Wapo pia wanawake ambao wao ndio waliokuwa watafutaji wakuu. Swali la kujiuliza ni hili. ‘Ni kipi bora, ni mali au ni amani na utulivu na uhai wako?’ kama ni mali, basi hakuna anayeweza kukuingilia kwenye uamuzi wako.
Lakini, kwa ufahamu tu, ni kwamba, pasipo na amani, mali haina maana na pasipo na amani uhai ni wa kubahatisha pia.
Wengine wanashindwa kutoka kwenye husiano kwa sababu wazazi wa mume na ndugu wanampenda sana. Anaogopa kuwaudhi kwa kuondoka kwenye ndoa ya mateso ya mtoto wao na ndugu yao. Anataka wafurahi, hivyo hawezi kuondoka. Huu nao ni upungufu.
Hivi unakuwa umeolewa na ndugu na wazazi au na mume? Lakini, kwani ukiondoka utashindwa kuwa karibu na watu hawa? Hutashindwa na pengine urafiki wenu utakuwa wa kudumu. Ukiendelea kukaa kwenye ndoa ya mateso kuna siku utakosana hata na hawa, maana unaweza ukalipukwa ukamuuwa mtoto au ndugu yao.
Kuna wale wanaoshindwa kutoka kwenye uhusiano mgumu kwa sababu wana watoto na wanaogopa kwamba, watoto wao watateseka. Hivi ni kuteseka kupi kubaya, kule kwa utotoni au ukubwani? Mtoto anayeishi kwenye ndoa yenye vurugu, anaharibikiwa kuanzia utotoni hadi ukubwani. Lakini, hata hivyo kuachana kwa wazazi, sio lazima kuwe na maana ya watoto kuteseka.
Kuna wakati hata watoto wanamwambia mama atoke kwenye ndoa, halafu mama huyo huyo anadai anakaa kwenye ndoa hiyo kwa sababu ya watoto! Kuna haja ya kujiuliza maswali kwa upana zaidi.
Ukitaka kutoka kwenye ndoa ngumu jiulize maswali haya. Je, ndoa hii ni kwa faida ya nani? Je, niliolewa au kuoa ili kupata shida au amani na upendo? Je, bila ndoa,nisingeweza kuishi mwenyewe? Tafuta mifano ya wasio na ndoa ambao wanafurahia maisha.
Jiulize ni kwa kiasi gani wengine wanasaidia kukusukuma zaidi kwenye ndoa hiyo? Jiulize ukamilifu wako. Je, wewe ni nusu mtu au mtu kamili? Kama ni mtu kamili , basi ishi kama mtu kamili.
TUONANE TENA JUMATANO IJAYO PANAPO MAJALIWA!!!!!

Tuesday, February 14, 2012

NIMEUTAMANI MLO HUU KWA KWELI!!!

Leo nimetamani kweli mlo huu ningependa kweli kula mchana wa leo Ugali wa muhogo na samaki. Yaani nimerudi nyuma enzi zileee Lundo/Nyasa kila siku ugali na samaki. Katika picha hii ni samaki aina ya Tilapia "TILAPIA FISH CURRY" picha toka blog ya kaka Isaack yaani nimeiona picha hii tangu juzi nimemezea mate weeeeeeee nimechoka nikafikiri naota ndoto.



Ugali huuuo wote mnakaribiswa ila inabidi mharikishe maana jinsi ninavyopenda chakula hiki hasa hiyo samaki mtakuta imekwisha...LOL.
WOTE MUWE NA SIKU NJEMA UKIZINGATIA NI SIKU YA WAPENDANAO..NAMI NASEMA WOTE MNAPENDWA !!

Monday, February 13, 2012

Majambazi wawili wachomwa moto wakiwa hai mkoani Ruvuma Songea/Ruhuwiko


Baada ya kusoma makala hii nimepatwa na mshtuko pia woga na halafu maswali mengi sana. Binadamu wanaamua kufanya hivi kwa binadamu wenzao kuchukua sheria wenyewe je? nani hapa ni muuaji? Haya hebu soma mwenyewe...
........................................................................................................................................................................
Pichani ni miili ya watu wawili wanaodaiwa kuwa majambazi ambao walipigwa na kuchomwa moto hadi kifo katika eneo la Ruhuwiko manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.Baadhi ya wakazi wa eneo la Ruhuwiko ambao hawakutaka kutaja majina yao walidai kuwa kabla ya tukio hilo watu hao hawakuweza kufahamika majina yao waliwasili eneo hilo majira ya saa tatu asubuhi wakiwa na lengo la kuuwa na kuondoa viungo vya uzazi vya binadamu ambavyo inadaiwa vinauzwa kwa fedha nyingi.Wananchi hao walidai kuwa watu hao walifika kwa mama mmoja ambao walidai wanamtafuta hatimaye wakiwa wanakunywa katika klabu moja ya pombe za kienyeji inadaiwa wakazi wa eneo hilo waliwatilia mashaka watu hao na kuaanza kuwahoji ambapo inadaiwa baada ya kupata kipigo na kuanza kuchomwa walieleza kwamba wao ni wauaji na walipewa fedha kwa ajili ya kuuwa na kwamba tayari wamekuwa wamefanya matukio kadhaa ya mauaji .Chanzo cha habari kimebainisha kuwa wauaji hao walidai kuwa wapo 50 na wanatakiwa kuuwa watu zaidi ya 100 wakiwemo wanaume 60 na wanawake 40 kwa kuwaondoa sehemu zao za siri ambazo inadaiwa ni biashara ambayo inawapatia fedha nyingi . Baada ya wauaji hao ambao walikutwa na shilingi 500,000 kukiri kuwa kazi yao ni kuuwa ndipo wananchi wengi wenye hasira waliamua kuanza kuwapa kipigo kizito kisha kununua petroli na kuanza kuwachoma wakiwa hai .Hadi polisi wanafika katika eneo hilo miili ya watu hao ilikuwa inaendelea kuungua kwa moto.Uchunguzi umebaini kuwa wakazi wa Ruhuwiko waliamua kuchukua sheria mkononi baada ya matukio ya uharifu na mauaji kujitokeza katika eneo hilo na kwamba hii ni mara ya pili kwa wakazi wa Ruhuwiko kufanya mauaji ya kutisha ambapo miaka 25 iliyopita watu wengine wawili waliodaiwa kuwa ni majambazi sugu waliuwa na kisha miili yao kuchomwa moto."Mimi binfasi nimefurahia sana kitendo hiki labda sasa majambazi yataogopa kuendelea kufanya uharifu katika eneo hili,hivi sasa hatuna amani kabisa wizi imekuwa ni jambo la karibu kila siku ,mauaji nayo yanazidi kuendelea ,waharifu wengine wanakamatwa na kuachiwa acha wananchi wajichukulie sheria mkononi'',alisema mama mmoja ambaye hakutaka jina lake kuandikwa.Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na polisi bado wanaendelea na uchunguzi.
Habari hii nimeipata hapa.

Sunday, February 12, 2012

NI JUMAPILI YA PILI YA MWEZI HUU NA TUSALI SALA HII!!!

Ee Mungu unifanya niwe chombo cha amani yako. Penye chuki nilete mapatano, penye kukata tamaa nilete matumaini, penye huzuni furaha, Amina
JUMAPILI NJEMA KWA WOTE!!

Saturday, February 11, 2012

JUMAMOSI NJEMA JAMANI LEO TUSIKILIZE NGOMA YA ASILI YA WAHAYA WA KAGERA NA DADA SAIDA KAROLI


Saida Karoli ni mmoja wa wasanii niwapendao sana hata kama kuna nyimbo nyingine anaimba kilugha na sielewi lakini naridhika kabisa. Nadhani ndio maana napenda, halafu ni ule uasili, utamaduni wetu au niseme kwa ujumla napenda sana vitu vya ASILI. Na naamini kuna wengi wa aina yangu. Je wewe kuna msanii umpendaye?

Friday, February 10, 2012

Je? ulijuwa maana ya jina la mji wa MOSHI/Sala za Wachagga kulingana na eneo wanalotoka (utani)

Sala Kuu:
MOSHI: Mungu Onesha Sehemu Hela Iko

Viitikio:
1. Hata Ikipungua Mungu Ongeza! (HIMO)
2. Mungu Angalia RAia NGawira Utuhakikishie! (MARANGU)
3. Mungu Ahidi Mapesa Bila Ajira! (MAMBA)
4. Mungu Wekeza Ishara Kwenye Akaunti! (MWIKA)
5. Kristu Imarisha Leo Elimu na Mapesa Akauntini! (KILEMA)
6. Kristu Imarisha Riziki Ujaze Akaunti! (KIRUA)
7. Usitunyime Riziki Uchumi! (URU)
8. Kila Ikipungua Baba Ondoa Siasa Hela Ongeza! (KIBOSHO)
9. Mungu Atupe Chanzo Halisi Ambacho Mapesa ni Endelevu! (MACHAME)
10. Kwetu Ikikosekana SHIlingi MUngu Nakuapia Dunia Utaichukia! (KISHIMUNDU)
Kaaaziii kwelikweli!!Nimecheka kweli mpaka nimepata maumivu kwenye mbavu hii chanzo chake ni Subi

HAPPY 1ST BIRTHDAY BENEDIKT

YOU ARE THE REASON, BENEDIKT


HAPPY 1ST BIRTHDAY



Nimetumiwa picha na ujumbe huu maaalumu toka kwa wazazi wa mtoto Benedikt. Nami nimeupokea kwa mikono miwili. HONGERA BENEDIKT KWA KUTIMIZA MWAKA MMOJA.

-------------------------------------------------------------------------------------------------

Dear Benedikt Fulbright Makulilo,
Today is Friday February 10th, 2012. It marks your 52 weeks (1 year old) journey since you were born at Los Robles Hospital in Thousand Oaks, CA. It was on Thursday at 5:42 pm Pacific Standard Time when you showed up. I exactly remember how happy both Marie and I were at that minute. We thanked God for Blessing, and you are that Blessing, Benedikt.
I would like to quote one of my favorite Bible verses which tells you were not born by accident. “Before I formed you in the womb I knew you, before you were born I set you apart; I appointed you as a prophet of the nations” [Jeremiah 1:5]. Those God’s words are applicable to every child. Your birth is predetermined by God. God knew you before He formed you in Marie’s womb. You have the purpose to be here. You are a very special, unique and talented kid.
When I was growing up, I had a dream – and the dream is you, Benedikt. I had a road map, worked hard to make sure I would come to America one day. Coming to America was not neglecting my roots as African and specifically Tanzanian. The main purpose was my children could have all opportunities I could imagine and provide to them. All these could not be realized, in my perspective, if I could stay in Tanzania, my home country. But I promised myself, even if I will be living in America, I would do my best to help many people in Tanzania and other developing countries to reach their dreams. My current contribution is helping thousands of people on how to get admissions and scholarships for their studies in Developed World like in USA, Canada, Europe, Australia, New Zealand etc. That’s why now I am well known scholarship blogger, founder and director of the Makulilo Scholarship Foundation.
In 2008 I arrived in America as Fulbright Scholar – teaching at Marshall University, WV. That journey didn’t end there. After one academic year of teaching, I moved to California for my Master’s Degree in Peace and Justice Studies – University of San Diego. Being in California, I met one beautiful lady, Marie Anna Makulilo (formerly Mowery). She is your mother. Both Marie and I love so much. We are so happy to be your parents.
Benedikt, it is a great privilege of being born in America. But that should not make you more special than others. It should make you stronger, hard working and helping others. The privilege of being American comes with great responsibility. I truly believe in you. Marie and I will start a special scholarship under your name, BENEDIKT FULBRIGHT MAKULILO SCHOLARSHIP to help orphans and albino children in Tanzania to go to school. When you grow up, you will be in charge of the program, and many children will benefit from your generosity.
Every child is talented. You are talented, Benedikt. God does not create a damn kid. It takes time, patience and a lot of trials to discover that talent. Some people even become old and do not discover their talents. Marie and I will try our best to let you discover your talents at your early age and enjoy what God has given you. We will give every opportunity available to make sure your talent is discovered, seen and appreciated. We don’t care whether you will engage in soccer, swimming, music, American football, basketball, running, arts etc as long you are happy with what you are doing and enjoy it, you have our full support.
One last thing to remember – the meaning you GREAT name. Your name BENEDIKT FULBRIGHT MAKULILO has a special meaning. Your first name Benedikt is after Pope Benedikt XVI (Formerly Joseph Ratzinger). In spelling Benedikt there is “K” instead of “C” as many people are used to English spelling of that name. Since Pope Benedikt is from Germany and in German language the name Benedikt is having “K” so Marie and I did not want to change that. In addition to that, in Kiswahili, there is no usage of “C” to mean “K” that’s why you’re Benedikt with letter “K”. And for your middle name Fulbright, my dream to come to America was fulfilled by Fulbright Scholarship. The scholarship was named after William James Fulbright. So we chose Fulbright in honor of the dream and more importantly your life will be Full and Bright. Your surname is Makulilo. Makulilo is unsung hero. He is you Grandpa. You will meet him one day and I know you will admire his life and principles.
Benedikt, you are the reason I came to America. I came here for you. You are The Dream. May God bless you.
HAPPY 1ST BIRTHDAY BENEDIKT
I love you more than you can imagine.
It’s your loving Baba,
Ernest Boniface Makulilo (MAKULILO, Jr.)

Thursday, February 9, 2012

HIVI KWANINI WANAPOJENGA/TENGENEZA HIZI BARABARA HAWATENGENEZI NA BARARA ZA BAISKELI.....

.....Maana hii ni hatari kwa wananchi kuendesha baiskeli hivi fikiria sasa hapa magari mawili yanakutana je huyu kijana maisha yake yataweza kuokolewa kweli? Ni wazo tu la leo.....

Wednesday, February 8, 2012

Ni nani anayechangia kuvunja ndoa mke au mume?

Habari hii imenisikitisha sana na imeniuma sana nikiwa kama mwanamke. Na nimeshindwa kuvumilia kutoisambaza hebu soma mwenyewe. nimeipata hapa.

Ndugu mpendwa, nakusalimu kwa amani na upendo.

Mimi ni mmoja wa wapenzi wa blog yako, na huwa sikosi kuifungua karibu kila siku, na nikiikosa ninakuwa sina raha, na raha yangu huzidi zaidi pale ninapoona umeandika kitu , hasa kwenye visa vyako, vimekuwa kama kitu ambacho nikikikosa siwezi kuishi…umenipa limbwata la visa vyako…lol
Nimesikitika sana kuwa huna vitendea kazi au sehemu ya kujishikiza, ili uweze kutupa visa hivi ikiwezekana kia siku, maana hasa sisi tunaoishi nje, tunatamani kusoma habari za Kiswahili na hasa visa vyenye ukweli ndani yake, kama vya kwako, ambavyo ukivisoma ni sawa na mtu anayeangalia movie. Na kwanini usiweke matangazo,…mbona wenye mitandao wenine wanaweka, na utakuta mitandao yao haina mengine zaidi …sana-sana ni picha, udaku au umbeya.Mimi leo nimeamua kukuandikia jambo moja linaloninyima raha,…kama halitifaa kuliweka hewani nirudishie, na kama litafaa lipitie vyema, kama nimekosea Kiswahili nirekebishe maana tumeloea Ulaya hata lugha sasa inatupiga chenga. Kwa ujumla nimekuwa nikipitia mitandao mingi, na mingi imekuwa haielezi ukweli kuhusu mwanamke na mwanaume, hasa NDOA, Naizungumzia ndoa, kwani mimi nipo ndani ya ndoa, nana bahati ya kuishi kwetu bongo kwenye manyayaso ya hali ya juu ya ndugu na mama mkwe na pia kuja kuishi Ulaya, ambapo maisha yetu sio mabaya, tunakula ….Sasa ubaya upo wapi, najua wengi mtauliza, nakuwaza, Ubaya upo ndani ya ndoa yenyewe, ubaya upo kwenye kusikilizana, ubaya upo kwenye maisha ya mke na mume, mimi huku ni kama mfanyaakzi wa nyumbani, ninaweza kusema mimi ni mmoja wa wahanga wa ndoa,ingawaje nipo dunia ya sasa, ninaishi Ulaya na mume wangu, lakini maisha ninayoishi na mume wangu ni kama tupo ile dunia ya mababu zetu ambayo mke hana usemi. Mke ni kama bidhaa, yote nimevumilia sikujali kuwa nipo Ulaya, na kama ningeliamua kufanya lolote ningeliweza, lakini bado naiheshimu ndoa yangu. Mimi hapa nipo kama mshumaa tu, siku yoyote unaweza ukazima, na ni bora niyasema haya ili watu wajifunze na waysikie, mwanga wa mshumaa huu usiishie kwangu tu, uwamulikie na wengine wanaoteseka kama mimi.
Najua wengi mtanilaumu kuwa natoa siri yangu ya ndoa, lakini nimeona ni heri kufanya hivyo, ili iwe chachu kwa wale wanaume wengine wenye tabia kama hizi waweze kubadilika, ila kwa mume wanu imeshindikana, imekuwa kama mbuzi kupigiwa gitaa. Hapa nilipo umri umeshapevuka, siwezi kusema niachane naye, nikatafute mume mwingine, nani atanioa mimi wakati sura imeshachujuka. Sitaweza kuwatelekeza watoto wangu kwa kuabdili wanaume, hapana, ila nahitaji mawazo yenu, ….Kwanini naandika haya : Nimeamua kuyaaandika kwasababu kuna mtu aliuliza swali, je kati ya wanandoa wawili mke na mume ni nani anayechania kuvunja ndoa. Ndio sisi wanawake tunakuwa na kitu kinachoitwa kitchen party, je inatusaidiaje kudumisha ndoa zetu, huyu mtu aliuliza hivyo, nikashindwa kumuelewa kwani ndoa ni watu wawili, kama mke atajitahidi sana na mume bado haelewi hiyo ndoa, au hayo mafunzo ya kitchen party yatasaidia nini.
Nimefikiri sana, na kufanyia utafiti ukianzia kwangu mwenyewe na kugundua kuwa kati ya mwanaume na mwanamke anayechangia kwa kiasi kikubwa kubomoa ndoa,ni mwanaume ila nchi za kwetu,hasa nchi za dunia ya tatu(maskini,afrika)wanamwangalia mwanamke kama ndiye chanzo cha kuvunjika ndoa, hasa wakisema, eti wanawake wengi haweze kumtuliza mume, hawajitahidi kumshawishi mume atulie nyumbani na ndio maana wanatafuta nyumba ndogo n.k swali hapa ina maana mke pekee ndiye anatakiwa kufanya jitihada hizo?
Hebu tuziangalie jitihada za mwanamke hasa wa Kiafrika, na tujiulize mwanamume anataka jitihadi gani zaidi ya hizo, kwani,mwanamke wa kiafrika,anamoyo ule wa kuvumilia,maudhi pamoja na manyanyaso ya kila aina,anayofanyiwa na mume wk.Mfano,kupigwa, kuishi na mwanamume mlevi, kumvumilia mwanamume hata akichelewa kazini kwa visingizio mbali mbali,kuletewa watoto wa nje,au hata kuletewa nyumba ndogo au vimada nk.Lakini yote hayo,anayabeba ndani ya moyo wake,na anaona kuwa ni aibu ya ukoo,yeye kurudi kwao,kwa kisa,ameshindwa kuvumilia ndoa.Wanawake wengine,hadi wanapata vilema vya maisha,kwenye ndoa zao na bado wapo kwenye ndoa wanavumilia na kuendelea na maisha kama kawaida.Wengine,wanawafumania waume zao,lakini,wanabakia na siri na kuwatetea waume wao,kuwa hakufanya jambo lolote baya na vitu kama hivyo, je uvu,milivu gani kama huo, upendo gani kama huo, uvuto upi mnaoutaka, kucheza sebene peke yake.Hebu chukulia upande wa pili kwa mwanaume mfano mwanaume,akufumanie,itakuwaje, wewe uchelewe kurudi nyumbani itakuwaje, ….ukosee kufanya jambo fulani, na mengine mengi, mwanamke atakiona cha mtema kuni.
Kwa ujumla Ndoa,inaumiza sana kwa wanawake.Na vidonda vya ndoa au majeraha ya ndoa,ni mengi sana kwa mwanamke na hayaponyeki, kwani kila siku yanatoneshwa…Kwa ujumla mwanamke wa Kiafrika anastahili kupewa heko, na hili nimejifunza nilipokuja kuishi huku Ulaya. Huku Ulaya mwanamke ana haki zake, hayanyanyaswi ovyo,na ole wako mwanamume umnyanyase mkeo halafu alifikishe hilo swala kwenye vyombo vya sheria….sio kwamba nawasifia kwa hili, lakini kwa kiasi kikubwa limemkomboa mwanamke na kujiona kumbe na yeye ni kimumbe kama mwanaume.Mimi nimeishi maisha hayo ya taabu hata vile nipo Ulaya, nimekuwa nikiishi na mume wanu na kumfanyaia yote kama vile nipo nyumbani, lakini ….nasema lakini ni ule usemi usemao penye miti mingi hakuna wajenzi…imefikia mume wangu hawajabiki kwenye swala muhimu la ndoa yake, swala ambalo wengi wanatulaumu kuwa sisi sio wabunifu, hatujui mapenzi, lakini utajuaje kucheza mpira kama hujaingia uwanjani…hayo ni visingizio vyao na kusema ukweli kama hilo wao ndio wakulaumiwa, kwani walitakiwa kushirikiana na mkewe wakafundishana na kuelekezana sio kukimbilia vimada.
Uvumilivu una mwisho wake, na majeraha yakizidi sana mwisho wake yanaweza kugeuka kuwa kansa, ndio maana nimeandika hilo swala kwako, uliweke hadharani watu walijadili na wanaume wasema ukweli wao, ili sisi wanawake tujue ni nini hasa waanume wanakihitaji kutoka kwetu, ili tuwatimizie,… ili tukiwafanyia hivyo waweze kutulia majumbani kwao, ili mwisho wa siku ndoa ziwe na amani.Humutaamini kuwa wengine tunamaliza miezi zaidi ya mitatu hatuwajui waume zetu, waume zetu huku Ulaya wanasingizia kuwa wanachoka kwenye kubeba maboksi, je ni kweli hili au ni kisngizio cha mume wangu tu, au na wenzangu wanafanyiwa hivyo hivyo, …je huko wanaposhinda na hata kulala na machangudoa hawachoki, au wanatufanya sisi ni wajinga tu hatjui nini wanachokifanya, je hii ni ndoa kweli, je na sisi tukiamua kutoka nje ya ndoa waatsemaje, na kwa hilo ni nani atalaumiwa, lakini tunaogopa kuja kuwaacha watoto wetu mayatima kwa kuugua magonjwa mabaya.Samahani sana kama nitakuwa nimewakwaza wengine kwa hayo niliyoyaongea lakini kama ilivyo kawaida ukweli huuma, …
Mimi mwenye majeraha ya ndoa Mama Wawili.

DUNIA YETU

Haya ndugu zangu ni JUMATANOnyingine tena na ndio kila KIPENGELE chetu cha marudio mbalimbali. Leo hii nimefika hadi Peramiho nilikuwa nikinunua mikate na nikafungiwa na gazeti la MLEZI.Kufika nyumbani sikulitupa lile gazeti nikawa nalisoma na kukutana na habari hii ambayo ilinivutia na sikupenda ninufaike mimi tu na ndio maana nikaona niiweke hapa leo. KARIBUNI.
Vitendo hivi msibani Mmmhh….!!

Kuna mambo yanayojitokeza na kuonekana wakati wa msiba na wakati wa kuzika. Kwa kweli, yanaleta huzuni Kubwa sana hasa unapowaona waombolezaji kwa njia ya nyimbo, baadhi yao wamelewa pombe, na kuomboleza kwa sauti kali yenye dhihaka isiyolenga hali halisi ya tukio lenyewe la msiba, kana kwamba wapo kwenye sherehe. Wapo watu wanaoitwa kwa jina maarufu “Watani wa jadi” wa msiba ule wakileta mizaha, vicheko na pilika pilika za hapa na pale ikiwa ni pamoja na masimango kwa marehemu. Kama marehemu alikuwa mtu wa Ibada, basi watawaambia wana familia kuwa ndugu yenu yupo kanisani kupeleka sadaka au kwenye Ibada ya jioni au Asubuhi. Kama marehemu alikuwa anakunywa pompe, watasema kuwa ndugu yenu mfuateni kilabuni. Hali kadhalika kama alikuwa mwindaji, watajaribia vile marehemu alivyokuwa akibeba mzigo wa nyama pori, na mambo mengine mengi. Na wakati mwingine huzua tafrani kati ya wanafamilia za marehemu na babu na bibi za marehemu kwa madai kuwa ndio waliomloga ili kulipa nyama waliokuwa wanadaiwa na wachawi wenzao. Kiasi kwamba watani hao wanawaweka wafiwa roho juu juu na hata kushikiana silaha za jadi kama vile rungu, panga, mkuki n.k.
Mnapofika makaburini eneo la kumsitiri marehemu, unawakuta watu wa aina nyingine wanaozungumzia habari za mpira wa Yanga na Simba kama watani wa jadi, kocha Marcio Maximo na timu ya taifa ya Tanzania kwamba yafaa abwage manyanga: mpira wa Manchesta, Chelsia, Arsenal na kadhalika. Watu hao hawasaidii kazi za kumsitiri marehemu na wala kuitikia nyimbo au sala za maombolezo. Wanajisahau kabila. Mikono mfukoni na misimamo ya kimikogo.
Utawakuta mabinti wamevaa nguo zao za kubana, tena fupi. Na juu kitovu kinaonekana wazi kabisa. Wao wenyewe wanajisikia fresh…Wamejipodoa kana kwamba wanaenda kwenye sherehe fulani au disko. Pamoja na kwamba kuna nguo nzuri za heshima, kwa mtu kwenda nazo msibani au kwa watu wa pwani huvaa nguo zao za heshima baibui. Si lazima uvae nguo nyeusi ili kuonekana kuwa umefiwa, lakini ni muhimu kuwa na mavazi yanayotofautiana kabla ya kufiwa na baada ya kufiwa. Hali kadhalika utamkuta mtu anasikiliza simu, tena anazungumza kwa nguvu bila huzuni yoyote, akizungumzia biashara zake zinavyoendeshwa.
Nawasihi wenzangu, tumsindikize mwenzetu katika safari yake ya mwisho kwa nyimbo na sala huku wenyewe tukiwa katika hali ya Ibada . Tena, haipo sababu ya kuanza kubishana wakati wa kuzika tunapomshusha marehemu kaburini. Kama kuna kitu hakipo sawasawa kwa mfano, kaburi halikuchimbwa kadiri ya vipimo vya sanduku, tuelezane kwa taratibu na heshima. Tusipige kelelse kama vile tupo kilabuni, sokoni au mnadani
Na Pius C. Nyoni: Likusanguse-Namtumbo.

Tuesday, February 7, 2012

Sakata La Mgomo Wa Madaktari; Tafsiri Yangu




Nimetumiwa habari hii na Kaka Maggid Mjengwa.


Ndugu zangu,
Mgomo wa madaktari wetu ni habari kubwa. Umeingia sasa kwenye wiki ya pili. Hata kama ungekuwa ni wa siku mbili, bado ungesababisha madhara makubwa kwa nchi. Kwamba sasa una zaidi ya siku kumi na nne ni balaa kubwa kwa nchi yetu.

Tafsiri yangu;
Uliopo ni mgogoro kati ya madaktari na Serikali. Na kwenye mgogoro kama huu, siku zote,wenye kuathirika zaidi ni wananchi walio wengi.
Ni ukweli, kuwa karibu kila Mtanzania anayeamka asubuhi, ama nimgonjwa au ana ndugu, jamaa au rafiki aliye mgonjwa.
Hivyo basi, kuna mamilioni ya Watanzania wenye kutaabika kila siku na maradhi ya aina mbali mbali. Ni Watanzania wenye kutegemea sana huduma ya tiba inayotolewa na madaktari wetu. Na katika nchi zetu hizi, daktari ni rafiki muhimu sana wa mwananchi.
Ni jambo baya sana, pale Serikali inapoingia kwenye mgogoro namadaktari. Inapoingia kwenye mgogoro na marafiki wa wananchi. Hakuna mahali popote duniani wananchi wakatokea kuwachukia madaktari.
Hivyo basi, ni balaa pia pale Serikali inaposhindwa kumaliza tofauti zake na madaktari wawananchi kwa njia ya mazungumzo na hata kufikia hatua ya madaktari kugoma.
Katika nchi zetu hizi, mganga wa tiba aliyesomeshwa kwa fedha zawalipa kodi na kwa miaka mingi anahitajika sana. Mganga wa tiba msaidizi anahitajika sana. Na hata kama angelikuwapo Msaidizi wa Mganga Msaidizi wa tiba , naye angehitajika sana. Vivyohivyo kwa wakunga wakuu na wasaidizi, wauguzi wakuu na wasaidizi wao. Wote hao wanahitajika sana.
Na katika nchi zetu hizi, Serikali hazipaswi kufikia hatua yakuwatisha na hata kuwafukuza kazi madaktari. Hilo la mwisho lifanyike tu pale ambapo njia nyingine zote za kumaliza tofauti nakusuluhisha migogoro na madaktari zitakapokuwa zimeshindikana. Nakwanini ishindakane?
Tufanye nini sasa?
Taarifa kwamba Kamati ya kudumu ya Bunge inayohusika na masuala yahuduma za jamii imepanga kukutana na madaktari wetu ni hatua njema na ya busara. Maana, katika mgogoro huu taarifa zimekuwa zaidi za upande mmoja; upande wa Serikali. Niwakati sasa pande zote mbili zikasikilizwa na Kamati hiyo ya Bunge. Ndio, ni wakati pia hata madaktari wetu wakapewa nafasi tuwasikie.
Huu si wakati wa kufanya ’ propaganda’ za kisiasa kwenye masuala ya afya za wananchi.Na hata pale Waziri wa Afya alipokaririwa jana Bungeni akitamka kuwahali ya huduma za mahospitalini zimerejea katika hali yake ya kawaida ni mfano wa ’Propaganda’ za kisiasa ambazo Watanzania hatuzihitaji kwa sasa.
Hivi ni hali gani hiyo iliyorejea kwenye kawaida yake kwenye hospitali zetu baada ya mgomo huu wa madaktari unaoendelea sasa? Kwamba askari wetu wa Jeshi la Wananchi wamelazimika kwenda kutibu wagonjwa Muhimbili hiyo haiwezikuwa ni ’ Hali ya kawaida’. Kwamba madaktari wameripoti lakini hawaonekani mawodini hiyo haiwezi kuwa ’ hali ya kawaida’. Na kama ni kawaida, hivi ni nini tafsiri ya ’ kawaida’?
Hapa kuna ukweli unaopaswa kusemwa, na si kitu kingine bali ni ukweli. Watanzania tunatakakujua; ni kwanini watendaji wa Wizara husika wameshindwa kulitatua suala la madaktari wetu na hata kutufikisha hapa tulipo?
Yumkini, kulikuwa na hali ya kuyapuuzia madai ya madaktari katika hatua za awali. Yawezekana pia watendaji wa Wizara hawakuwa karibu na wawakilishiwa madaktari hao ili kutoa fursa ya kuongea na kutafuta ufumbuzi watatizo. Labda ndio maana tumefika mahali sasa mgogoro umekomaa na wahusika kuonyesha hali ya kutunishiana misuli. Kuna mahali kosa limefanyika. Ni wapi?
Ndio hapa, kuwa hata kama Kamati ya Bunge itafaulu kusuluhisha mgogoro huu, bado Watanzania tutahitaji iundwe Tume huru itakayochunguza namna watendaji wa wizara husika walivyolishughulikia suala hili kwa upande wao.
Tume hiyo itusaidie kuupata ukweli mzima ili kama taifa, tujifunze. Na wakati tume kama hiyo itakapokuwa ikifanya kazi yake, itakuwa ni busara, kwa watendaji wakuu wa wizara husika wajiweke pembeni kwa maana ya kujiuzulu ili kupisha uchunguzi huo.
Kama Tume itabaini kuwa hakukuwa na mapungufu makubwa katika utendaji wao na hususan walivyolishughulikia suala hili la mgogoro na madaktari, basi, itajulikana hivyo, na wana nafasi ya kurudi tena kwenye nafasi za utendaji Serikalini. Inahusu umma kurudisha imani yake kwa Serikali yao. Ndio maana ya umuhimu wa wahusika kupisha pembeni kuruhusu uchunguzi ufanyike. Maana, haitakuwa busara kuliacha suala hili likapita kama yanavyopita mengine ili hali limegharimu maisha ya Watanzania.
Na kubwa zaidi kwa sasa, ni kwa pande zote katika mgogoro huukutambua; kuwa kwa sasa mvutano unaoendelea hautatoa mshindi, ni kwa vile, katika kilichotokea na kinachoendelea kufanyika sasa, sote, kama taifa, tumeshindwa.
Huu ni wakati wa kutanguliza busara na hekima. Tufanye yote, lakini,njia mujarab ya kutanzua mgogoro huu uliopo sasa ni mazungumzo katika mazingira ya kuheshimiana, basi.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.
Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam, Jumamosi, Februari 4, 2012 http://mjengwablog.com/

Monday, February 6, 2012

Sunday, February 5, 2012

JUMAPILI NJEMA...KARIBUNI CHAI KWA MIHOGO YA KUCHEMSHA!!!!

Mihogo ya kuchemsha.......
Na chai ya rangi

Karibuni tujumuika, mimi napenda zaidi mihogo ya kuchemsha. kuna wengine wanapenda ya kuweka nazi, karanga au nyanya na vitunguu. Je wewe unapenda mihogo yako itayarishweje? Haya ngoja niwatakieni wote jumapili njema sana. Mimi nakunywa chai yangu hapa maana baridi si mchezo!!!!

Friday, February 3, 2012

NIMEWASIKIA WENGI WANASEMA UKITAKA KUJUA MENGI BASI NENDA KWENYE VILABU VYA POMBE.....

.....Lakini kumbuka pombe si maji kunywa kidogo isije ukashindwa hata kujua chochote kilichozungumzwa. Ukinywa kidogo utaepuka ajali na pia utatunza afya yako. Unajua kwamba mnywaji pombe sana anazeeka kwa haraka kuliko asiyekunywa?

IJUMAA HII NIMEONA TUIMBE KWA PAMOJA

Ni mwimbo mzuri sana kwa kuimba,kusikiliza pia kucheza. Nimejaribu kurekodi lakini mmmhh....yamenishinda:-(
Haya tuimbe sasa Ni wimbo wa lizombe:-

KISWAHILI:
Wageni karibuni mama aah x2
Karibu nyumbani wageni wetu,
mjisikie nyumbani wageni wetu x2

KINGONI:
Kamwali bwela bwela mama aaahx2
Karibu pa nyumba mgeni wetu,
hapa pa nyumba yangu mama aaah x2
IJUMAA NJEMA NDUGU ZANGUNI!!!!

Thursday, February 2, 2012

NATAMANI KUWA MDOGO NA MREMBO KAMA HAWA WATOTO

Natamani kuwa mdogo tena, angalia watoto hawa walivyopendeza NIMEIPENDA SANA PICHA HII NA NIMEONA IWE PICHA YA WIKI HII.

Kweli pamoja tunaweza tukazuia hali hii isitokee katika nchi yetu?



Kw pamoja naamini tunaweza kufanya hali hii isitokee katika taifa letu ingawa kuna maeneo kuna hali ngumu ambao hata huwezi kuizungumza, ndugu zangu wazalendo tuungane pamoja bila kujali wewe ni chama gani, dini au ukabila tuseme sasa inatosha na hali hii.

Wednesday, February 1, 2012

Ukipenda boga

KATIKA KIPENGELE CHETU CHA MARUDIO JUMATANO HII NIMEONA TURUDIE UJUMBE HUU MAANA KAPULYA NI MDHAIFU SANA WA MASHAIRI.NIMEKUTANA NALO HAPA.
-------------------------------------------------------------------------------------------
Pendo pendo mwapendana, nyie ni nyie wawili,
Pendo pendo mwashibana, lenu la jambo muhali,
Mwanoga mwaambiana, mwingine hatobadili,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Mapenzi yake matamu, wanogewa na mumeo,
Kamwe haiishi hamu, ana upya kila leo,
Penzi lashika hatamu, huwajali visemeo,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Mumeo umemkuta, anao na ndugu zake,
Binti unafurukuta, hutaki kwako wafike,
Wataka mume kufyata, lako tu nd’o alishike,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Siyo vema mwanakwetu, si tabia yenye sudi,
Nao waoneshe utu, upendo kwao si budi,
Mabezo si malikitu, siwoneshe ukaidi,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Kwa mumeo umekuta, tayari alishazaa,
Kabla hajakupata, akupe wake wasaa,
Mtoto wamkorota, zaidi wamkataa,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Nawe umepata mke, tayari ana mtoto,
Simfanye ateseke, kuiweka nyumba joto,
Haki yake apendeke, siyo kuleta fukuto,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Usipende nusu nusu, nani tena wamwachia,
Yake yote yakuhusu, nayo uyapende pia,
Sisite kumruhusu, nduguze kutembelea,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Mapenzi huleta raha, kwa dhati mkipendana,
Tena huipata siha, kama mwasikilizana,
Siyafanyie mzaha, mkaja kuumizana,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Cha mwenziyo kyone chako, halafu ukithamini,
Kipende moyoni mwako, sikitenge asilani,
Sikifanyie vituko, kamwe kamwe abadani,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

Ya kusema nimesema, ni vema kuyasikia,
Yatunze yaliyo mema, kazi ukayafanyia,
Pendo lijae hekima, nyote kulifurahia,
Basi ukipenda boga, lipende na ua lake.

TUKUTANE TENA JUMATANO IJAYO!!!!