Monday, May 10, 2010

MFALME MROPE: HAYA NI MAJIBU KUHUSU UONGO WAKO.

Inadawa kuwa wanafunzi wa vyuo ndio wadanganyaji wazuri.


Hivi karibuni dada yangu Yasinta aliweka makala hapa ambayo aliitoa katika Gazeti la Jitambua, makala hiyo ilikuwa na kichwa cha habari kisemacho ‘Kuna wale wanaojikuta wanadanganya bila hiyari’ ukitaka kujikumbusha juu ya makala hiyo unaweza kubofya hapa.
Katika makala hayo kulitolewa maoni tofauti tofauti na wasomaji wa kibaraza hiki, lakini Mfalme Mrope ndiye aliyenisukuma kujibu swali lake ambalo aliliita la kizushi kuwa, ni upi ni uongo mzuri na upi ni uongo mbaya?

Ukweli ni kwamba, kila mmoja wetu husema uongo. kuna majaribio mengi ambayo yamefanywa, ya watu kujitahidi kutosema uongo, lakini wote walishindwa jambo hilo.

Uongo huvunja uhusiano na kuondoa kuaminiana miongoni mwa watu. lakini, kuna ukweli kwamba, uongo utaendelea kusemwa. Hata hivyo, wataalamu wanakiri kwamba, kuna uongo ambao ni muhimu katika kumfanya mtu kutimiza mambo yake muhimu ya kijamii, kukabiliana na hali zisizopendeza na kujilinda na udhaifu wa kinafsi.

Pengine ukijua ni kwa kiwango gani watu wanasema uongo unaweza kuwa kwenye nafasi ya kulielewa vema zaidi jambo hili. Mtaalamu mmoja wa saikolojia aliwahi kufanya utafiti kuhusu kiwango cha uongo kwa watu. Huyu bwana alibaini kwamba wanfunzi na hasa wanavyuo, husema uongo kwa wastani wa mara mbili kwa siku.

Ukikutana na mwanafunzi wa chuo ujue kama hatakudanganya wewe, basi kuna watu wawili au mazingira ya aina mbili tofauti ambapo amedanganya au atadanganya kwa siku hiyo.

Kwa ujumla kama mtu akikagua tafiti nyingi zilizowahi kufanywa kuhusu kusema uongo, atabaini kwamba, katika kila mambo matano anayosema mtu mzima, moja linakuwa ni la uongo.

Wanafunzi nao husema uongo zaidi, kwani inaonesha katika kila matukio au mambo matatu, husema uongo mara moja.

Watafiti wamebaini kwamba, uongo husemwa zaidi kwenye simu kuliko watu wanapokuwa uso kwa uso.

Kwa hiyo, watu wanapowasiliana kwa simu uwezekano wa kusema uongo ni mkubwa sana kuliko wakiwa wanazungumza uso kwa uso. maana yake ni kwamba mazungumzo ya kwenye simu hayaaminiki sana.

Imebainika pia kwamba uongo unaposemwa, ni lazima uongo mmoja kati ya kila saba ufahamike. Hii ina maana kwamba, uongo mwingi hupita bila kufahamika, lakini ina maana kwamba, mtu akisema uongo ni lazima kuna mahali atanaswa tu.

Katika kila mara kumi za uongo unaosemwa, uongo mmoja unakuwa ni wa kuongeza chumvi.

Yaani jambo ni la kweli, lakini kunakuwa na kuongezea chumvi kwingi sana. Kati ya kila uongo kumi unaosemwa, uongo sita ni uongo kabisa, usio na chembe ya ukweli. Kumbuka, kuna uongo mwingine hauna hata chembe ya kaukweli fulani ndani.

Uongo uliobaki yaani asilimia 30 ya uongo wote unaosemwa, una viraka vya ukweli na viraka vya uongo wao.

Hii ina maana kwamba akidanganya kuhusu jambo fulani sasa hivi, atarudia kudanganya kuhusu jambo hili kwa mara nyingine.

Ndio pale mtu anaposhtukiwa kwa sababu maelezo yake kwa jambo hilohilo hugongana.

Watu wanaosema sana uongo wanaelezewa kuwa ni watu wanaohisi kupungukiwa, yaani ndani mwao kihisia kuna kutokukamilika au wanahisi kuwepo pengo ndani mwao.

Kwa kutumia uongo hujipandisha au kuhisi nafuu. Watu wanaojiamini hawawezi kuwa na uongo, labda ule uongo, ambao inaelezwa kwamba ni wa lazima kwa sababu ya mazingira.

Huu ni uongo wa aina gani?

Niliwahi kusoma habari fulani ya kidini. Mtu mmoja aliyekuwa akitafutwa na maharamia alikimbilia kwenye nyumba ya watawa.

Huko alionesha uadilifu wake mkubwa hadi watawa wale wakampenda sana.

Siku kadhaa baadae, wale waliokuwa wakimtafuta waliivamia nyumba hiyo na kufanya fujo wakisema wamtafutaye yumo ndani.

Ilibidi watu hao wapelekwa kwa mkuu wa nyumba ile ya watawa.

Ni kwamba, kwa mujibu wa mazoea na ufahamu wa eneo lile, watu walikuwa wanaamini kwamba, mtawa hawezi kusema uongo, na kubwa kabisa, kiongozi wao ndiye ambaye hata iweje hawezi kudanganya.

Wale watu wakorofi walipofika kwa mkuu wa watawa wale walimuuliza, kama mtu wanaye mtafuta yumo mle hekeluni.

Mkuu wa watawa alifikiri na kusema, 'hakuna mgeni humu ndani,vinginevyo tusingemficha' Kwa kuamini kwamba, mkuu wa watawa hawezi kudanganya, wale maharamia waliondoka wakiamini kuwa wamtafutaye hayumo mle.

Baada ya maharamia kuondoka , mkuu wa watawa alimwambia yule mgeni, 'kwa mara ya kwanza nimesema uongo kwa sababu yako. Lakini unastahili kuokolewa kwa mtu kusema uongo, ni uongo wa haki na wa lazima.'

Huo ndio uongo ninaouzungumzia. Na hapo ndipo unapogundua kwamba hakuna mtu asiyesema uongo.

Uongo mwingine ni ule unaotumiwa na madaktari, maarufu kama Placebo. Uongo huu unatumiwa na madaktari pale inapotokea kuwa dawa inayoweza kutibu tatizo hilo haipo au mgonjwa ameonekana kutokuwa na tatizo lolote hata baada ya vipimo vya kitaalamu, pamoja na kwamba ameonekana kuwa na matatizo ya kiafya.

Kinachofanyika ni kumpa mgonjwa dawa ambayo haina madhara na mara nyingi ni vidonge maalum ambavyo vinakuwa havina kemikali yoyote, pamoja na ushauri nasaha imeonekana kuleta mafanikio makubwa.

Huu nao ni uongo mzuri, kwani umeonekana kuponya watu wengi sana na kutokana na tafiti mbalimbali imethibitika kuwa uongo huu uitwao Placebo ni moja ya tiba zilizoonyesha mafanikio makubwa

Makala haya nimetumiwa na kaka Shabani Kaluse wa kibaraza cha Utambuzi na Kujitambua yakiwa ni majibu kwa Mfalme Mrope.

6 comments:

  1. Dada Yasinta, alichokisema Kaluse ni kweli. Kinachosikitisha ni kwamba mtu asemaye uongo (achana na huo mfano wa kumuokoa mtu) huwa hapimi madhara ya afanyalo ambayo yanaweza kusababisha madhila makubwa kwa jamii, na hii ni kaliba ya watu. Matatizo mengi katika mahusiano ya watu duniani kwa sasa yanachangiwa pia na uongo. Makuzi na kuchangamana kwa kiasi kikubwa kuna"mfinyanga" mtu na kumkomaza awe mwongo.

    ReplyDelete
  2. Ahsante sana dada Yasinta na Kaluse. Hii imewakilishwa ipasavyo. Nimependa sana kuhusu ilivyonenwa kuwa watu wengine huamua kusema uongo ili kujazilizia mapungufu ya nafsi zao... Hii ni kweli kabisa na nimeona ikitokea. Lakini mwisho wa siku ni bora tutambue kuwa tunaweza kusosovo bila kusema uongo. Jaribu kujizuia kusema uongo polepole. Ukiuzuia uongo ambao ulikuwa uuseme, jipongeze nafsini mwako na nakuahidi "it feels so good". Ni hoja tu wajameni...

    ReplyDelete
  3. Uongo wa madaktari ni sehemu ya tiba jamani.

    ReplyDelete
  4. Je, mtu anaposema uongo, hufanya hivyo kwa hiari yake mwenyewe ama kuna msukumo fulani uliofungamana na haiba/personality?

    Kama ni shinikizo la, tuseme haiba ya mtu, je, ni haki kumbebesha mzigo wote huyo anayetuhumiwa kusema uongo?

    Tuchukulie mfano, kama inavyosemwa mtu anasema uongo ili kuziba mapungufu yake. Je, kufanya vile ichukuliwe kuwa ni kosa lake mwenyewe?

    Ni sawa na mtu mwenye njaa. Anaposikia njaa, suluhisho ni kula. Kitendo cha kutafuta chakula si hiari yake, ni matokeo ya upungufu wa kimwili.

    Sawa sawa na huyu anayetuambia uongo! Anafidia upungufu wa haiba yake ambayo imeekuwa hivyo kwa sababu zilizo nje ya uwezo wake!

    Sidhani kuwa watu huamua kuwa waongo. Hujengwa kuwa waongo....

    ReplyDelete
  5. Kha UONGO!!!!,
    Wakati mwingine hughalimu na hata kutoa maisha kwa muongopaji. Inatakiwa kuwa makini unapoamua kuongopa na unaemwongopea.

    ReplyDelete