Thursday, January 9, 2014

UNAKUMBUKA HABARI/HADITH HII KITABU CHA DARASA LA SITA:- MVUMILIVU HULA MBIVU? KUMBUKUMBU!!

Hapo zamani za kale Sungura na Mbwa Mwitu walioa mabinti wa jamaa mmoja. Mbwa Mwitu alimwoa kifungua mimba na Sungura kitinda mimba. Mbwa Mwitu  alikuwa mvivu sana tena mlafi. Sungura alikuwa hodari wa kutega ndege. Kila siku nyumbani kwa Sungura kulikuwa hakukosekani kitoweo kizuri. Mbwa Mwitu akaanza kumwonea wivu Sungua kwa sababu alipendwa na watu wote wote kijijini.
Mwaka fulani njaa ilitokea katika kijiji chao. Mbwa Mwitu na Sungura wakamwendea mkwe wao kuomba ardhi ya kulima. Akawaonyesha mwitu mzuri wenye rutuba nyingi. Sungura hakupenda kufyeka msitu pamoja na Mbwa mwitu. Alikataa kwa sababu aliuelewa sana uvivu wa Mbwa Mwitu.
Kila siku asubuhi Mbwa Mwitu alipokwisha pata kifungua kinywa alikwenda shambani. Alipofika huko alikata mti mmoja, miwili au mitatu, kisha akakaa chini ya mti. Kwenye mti kulikuwa na mtambazi uliotambaa juu na kushikilia matawi imara kabisa. Mbwa Mwitu alitengeza pembea nzuri sana juu ya mtambazi huo. Ikawa kila afikapo shambani kukata miti miwili, mitatu, kisha hurukia pembea yake akijiningíniza.
Kila siku Mbwa Mwitu alirejea nyumbani mapema na kufanya fitina kubwa nyumbani kwa Sungura. Alimwambia shemeji yake kwamba Sungura hafanyi kazi yo yote ya kutayarisha shamba. Kazi anayoifanya ni kutege ndege tu. Kwa kuwa Sungura alikuwa hodari, kila siku alileta ndege aliowanasa kwa mitego yake. Jambo hili lilimfanya mke wa Sungura aamini maneno ya Mbwa Mwitu. Mke wa Sungura alipoona hayo, ugomvi ukazuka kati yake na mumewe. Ugomvi huu ukaendelea siku baada ya siku. Mbwa Mwitu alikuwa ibilisi mbaya sana. Sungura alijua haya yote yalitokana na fitina ya Mbwa mwitu. Hakusema neno. Alivumilia kwa sababu alifahamu kuwa njia ya mwongo ni fupi.
Majira ya kupanda yalipowadia Mbwa Mwitu alimwendea tena mkwewe kuomba aina mbalimbali za mbegu akapande shambani mwake. Akapewa. Mbwa Mwitu alipokwenda shambani, alichukua kigae. Akakoka moto, kisha akakaanga zile mbegu kwenye kigae, akala akashiba , halafu akalala fofofo. Mbegu zilizobaki akaziweka akiba mpaka kesho yake. Asubuhi ya siku iliyofuata aliendelea na mambo yale yale. Kama waswahili wasemavyo, "Chovya chovya humaliza buyu la asali", hivyo Mbwa Mwitu alimaliza mbegu zote.
Sungura hakwenda kwa mkwewe kuomba mbegu. Hii ilimfanya Mbwa Mwitu azidi kutia fitina, hata Sungura akawa anachukiwa sana. Hata hivyo akaendalea kuvumilia. Baada ya kununua mbegu za kila namna kwa fedha alizojiwekea akiba, Sungura alikwenda shambani mwake akapanda. Punde si punde, mvua kubwa ikanyesha na mbegu zote zikaota vizuri sana.
Wakati wa kupalilia ulipotimia, Mbwa Mwitu akaendelea na mchezo wake ule ule wa pembea. Lakini Sungura alifanya bidii mpaka shamba lake likawa safi kabisa. Alifanya kazi hiyo kwa juhudi kubwa, akayafuata mashauri ya wataalamu wa kilimo. Juhudi yako pamoja na maarifa ndivyo vilivyokuwa msingi wa kulipata shamba kubwa lenye mimea mizuri.
 Mbwa Mwitu alikwenda kisirisiri kuangalia shamba la Sungura. Uzuri wake ulimshtua sana, naye akazidi kumwonea wivu. Alikata shauri kuliharibu. Akakusanya majani makavu na kueneza katika shamba ya Sungura, ili ayatie moto na kuliunguza shamba. Lakini kwa kudura za Mungu; Sungura aliwahi kugundua hila hiyo. Mbwa mwitu alipotaka kulichoma moto, Sungura aliwahi mapema shambani mwake. Mbwa Mwitu akashindwa kuliharibu shamba la Sungura.
Mbwa mwitu hakuchoka kumfanyia Sungura hila. Baada ya miezi kadhaa alipeleleza habari za shamba la Sungura akafahamu kuwa mazao yalikuwa tayari kuvunwa. Akakusudia kuyaiba mazao ya Sungura. Alijidai kwamba shamba lile lilikuwa lake. Akawaomba mkwe na jamaa wajitayarishe kwenda shambani kuvuna, lakini Sungura akazipata habari hizo.
Kesho yake asubuhi na mapema, Sungura akawahi shambani mwake akiwa na jamaa. Mbwa Mwitu alipogundua kwamba Sungura amewahi, akalazimika kuwapeleka wale aliokuwa nao shambani kwake. Walipowasili mahali Mbwa Mwitu alipopaita shamba lake, hawakuona dalili y yote ya mazao. Mkwe wake alihamaki, akamsaili kwa nini hakukuwa na mazao. Mbwa Mwitu alifedheheka akashindwa kujibu kwa aibu. Karibu na shamba chini ya mti mkubwa, wakaona mahali alipokaangia mbegu. Waligundua maganda ya karanga na mpunga yametapakaa huku na huko. Mkwe wa Mbwa Mwitu na jamaa wakarudi nyumbani wamekasirika sana.
Jioni ileile, Sungura alimwendea mkwe wake akamweleze kwamba angefurahi sana kama yeye pamoja na jamaa wangefika kuliona shamba lake. Mkwewe alikataa shauri hili. Akaeleza jinsi alivyotendewa na Mbwa Mwitu. Sungura akambembeleza sana mkwewe mwishowe akakubali.
Waliondoka asubuhi na mapema kwenda kuliona shamba la Sungura. Walipofika shambani wakaona mazao mengi yaliyostawi vizuri. Sungura akamweleza kwamba hilo ndilo shamba lake. Akawaomba waingie shambani kuvuna. Wote waliofika walifurahi sana. Zaidi ya hayo walishangaa jinsi Sungura alivyokuwa mvumilivu kwa fitina za Mbwa Mwitu. Mkwe wa Sungura akaona ni kweli kwamba matendo hukidhi haja maridhawa kuliko maneno. Mbwa Mwitu alikuwa amesema maneno mengi kujisifu na kumfitini Sungura lakini hakuna alilokuwa ametenda.
Jioni ile mkwa wao aliwaita Sungura, Mbwa Mwitu na jamaa wote, akasema, "Leo tumepata fundisho kubwa kwa vijana hawa wawili, Sungura na Mbwa Mwitu. Kwa juhudi na uvumilivu, Sungura amejipatia chakula cha kutosha. Kwa ajili ya fitina, Mbwa Mwitu hakuambulia cho chote. Nataka wote mjifunze kuwa "Juhudi ni Shina la Maendeleo," na ya kuwa kwetu tunayo ahadi isemayo " Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko," Kwa hiyo anamwonya Mbwa Mwitu aache fitina, uchochezi na uvivu. Badala yake afanye kazi ili afaidi matunda ya jasho lake."
Tangu siku ile Mbwa Mwitu alianza kujirekebisha. Akashirikiana na wanakijiji wenzake kuendeleza kijiji chao. Kutokana na hadithi hii twakumbuka maneno ya wahenga wetu yasemayo "Asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu."
UJUMBE:- Hii  hutokea mara nyingi sana ..Tuache uvuvi, fitina na tufanye kazi ili kuendelea..Akina Sungura wapo wengi sana katika dunia hii.

3 comments:

  1. Da Yacinta unanitia uchuro. Juzi niliagiza vitabu nikaletewa vya kisasa visivyo na kichwa wala miguu. Hebu ulizie Ruhuwiko kama kuna anayeweza kunipata lau vitabu hivi kuanzia la tatu hadi saba afanye hivyo nitamjalia uchache wake dada yangu. Namiss Sikiri mimi maskini,Karudi Baba mmoja sizitaki mbichi hizi, Kibanga amchakaza mkoloni na Dadi motto wa Mahurunga.

    ReplyDelete
  2. Mwal. Mhango...pole kwa kukutia uchuro na zaidi kws kupata vitabu visivyo vintewe. Nitajaribu na maktaba ya Ruhuwiko....ingawa yangu hspa ninavyo...ohhhh sikiri na sadiki....ngokja

    ReplyDelete
  3. vimax thanks gan infonya vimax asli di tunggu info selanjutnya gan obat klg

    ReplyDelete