Bwana wewe nikuambie siri moja ya maisha,…’Mzee mmoja alikuwa kakaa karibu nami
kwenye daladala kaniambia, tulikuwa tumekaa wote kwenye daladala na muda huo
nilikuwa nimechoka, sikupenda kusumbuliwa, hamu yangu ilikuwa kupata usingizi
kidogo, kwasababu najua nina zaidi ya masaa mawili ndani ya daladala hadi kufika
kwangu, siunajua tena foleni.
Nikamwangalia yule mzee, alikuwa
kaniangalia kuonyesha kuwa ana jambo muhimu nikaona nimsikilize na kumwambia ,
`Niambie mzee, huenda likanisaidia katika maisha yangu…’
‘Katika
mipangilioa yako ya maisha , fanya juhudi pangilia mambo yako, fanya kazi kwa
bidii na ipende dunia kama vile utaishi milele..siunaniona mimi hapa nimezeeka
nina miaka sitini, lakini najihisi kama nina miaka mingine sitini mbele,
sijipweteki, na kusema aah, mimi mzee basi tena, nasubiri cha kupewa, nani
atakupa hivihivi dunia hii. Najitosa hivyohivyo kama vile nitaishi milele,
ingawaje kwa kweli naukumbuka sana, na kuujutia ujana wangu…’ akaniangalia kwa
macho makali. Akaongezea kusema `wakati ni mali, lakini wakati ni ukuta,
unahitaji mipangilio…’ akatikisa kichwa na kuendelea kusema;
`Pili
muabudu sana mungu wako kama vile utakufa leo, au hata sasa hivi, huwezi jua,
hapa gari linaweza likadondoka, tukawa wote marehemu au nikafa mimi peke yangu,
au hata bila kudondoka gari unaweza ukakauka ghafla, na ukafa. Sasa ni bora
umwabudu aliye na mamlaka na hiyo roho yako kwasababu hujui muda gani ataichukua
roho hiyo. Omba, muabudu mola wako kama vile hapo unapoomba ni sekunde au dakika
yako ya mwisho…’ akainama chini na nilijua anamuomba mola
wake!
Nilijiukuta nimelala na nilipoamuka yule mzee akawa hayupo, ina
maana aliteremka kituo nyuma wakati mimi nimelala, nilijuta sana, kwani
alionekana ana busara na mengi yakunieleza, lakini nimechelewa
keshaondoka.
Mzee huyu namfananisha na mwaka huu, unayoyoma, ni muda
mchache umebakia tutauita jina jingine, mwaka jana au sio , na tutaukaribisha
mwaka mpya. Mwaka huu tulikuwa nao na tulikuwa na mengi ya kufanya, na sijui
mangapi tulifanikiwa kuyafanya na mangapi hatukufanikiwa, sidhani wengi wetu
tuna kawaida ya kuweka kumbukumbu hizo, sidhani. Kumbukumbu hizo tunaziona
kwenye bajeti za serikali, bajetiza makazini, lakini sio bajeti ya mtu mmoja
mmoja.
Mwaka huu tupo nao kwenye kiti una mengi ya kutuambia, lakini
tunajifanya tumechoka, tunajifanya tupo busy…labda tungelitulia tukatafakari na
kuwa nao bega kwa bega k wa mipango, huenda tungelifanikiw sana. Tumekuwa
tukikimbizana na hili na lile na huenda hayo tunayokimbizana nayo haya maana,
tunapoteza muda mwingi kwenye vilevi, kucheza bao, kuongea na kufanya mambo
ambayo ukiangalia ni ya kupotezea muda, muda uishe ulale, siku ipite. Ndio siku
inapita, umri unakwisha na mwaka huo unakwisha, tukiamuka tutaukuta haupo
tena!
Tukiangalia katika maisha yapo mambo mengi yanaharibu miili yetu
hasa vyakula, vinywaji, vipodozi, hasira zisizo na msingi na mambo kadha wa
kadha ambayo unayaona mazuri kwa umri wa miaka hadi telathini ujanani yaani,
lakini ukifikia zaidi ya umri huo, hayo hayo uliyokuwa ukiyaona mazuri yanageuka
kuwa sumu mwilini mwako. Mfano vyakula vya mafuta, pombe, starehe , madawa,
vipodozi na mambo anuai, ni mazuri, yanastarehesha katika umri wa ujanani,
lakini ikifikia uzeeni hayo matamu yanageuka kuwa machungu, yanakuwa sumu.
Tunajikuta tunaamndamwa na presha, kisukari, ugonjwa wa moyo, vidonda vya tumbo
nk, kwasababu ya yale matamu tuliyokuwa tukiyafadi ujanani. Kosa hatukua na
mipangilio, hatukuali kusoma na kujifunza uzuri na ubaya wa hilo unalilofanya au
kula!
Sasa wakati umefika kabla mwaka haujaisha kaa na huu mwaka kabla
haujaisha, kumbuka yale ya muhimu, panga matarajio ukiwa na malengo kuwa utaishi
milele. Na mipango hiyo haiwezi kuja kichwani tu, chukua karatasi pata muda,
hata ikibidi soma, tafuta , uliza, kaa na mkeo au mumeo, angalieni matarajio,
majukumu na mambo mbali mbali ya kimaisha yapangeni vyema na jinsi gani ya
kuyatatua matatizo, jinsi gani ya kupata kipato, jinsi gani ya kusaidiana na
hata kama huna kitu lakini kwa kujua nini kifanyike na kipi cha muhimu kwanza
inasaidia, kuliko kulala, au kunywa pombe, au kusubiri mwisho wa siku ukaanza
kupiga mayowe , kurusha mawe kwenye mabati eti unashagilia mwaka umekwisha,
lakini umekwishaje? Ulikuwa nawo kweli wewe au ulikuwa umelala…!
Mkumbuke
mola wako, kwani imani ni kitu muhimu sana, mola wako ndiye mwenye mamlaka na
mwili wako, wangapi ulikuwa nawo siku za karibuni au mwaka huu sasa hawapo, je
ina maana wao walikuwa na makosa na wewe uliyebakia huna makosa. Kumbuka wangapi
wapo mahospitalini wagonjwa, wengine hawana viungo, wengine wanaomba mola
awachukue kwa mateso wanayopata ya kansa au mengineyo, je wao walikuwa wanjua
haya, je wao walimkosea Mungu ndio maana wanapata mateso haya, na wewe ni mbora
zaidi yao ndio maana leo upo mzima. Hapana, wao hawajakosa, na wala wewe sio
mbora sana mbora zaidi ni yule mcha mungu, ni yule anayemuomba mungu kuwa sala
yangu hii huenda ikawa ya mwisho kuwa mzima, kuwa hai…nahivyo Sali kama vile
hutaiona sekunde inayofuata.
Ujumbe huu
nimetumiwa na msomaji wa Maisha na Mafanikio aishiye Arusha. Binafsi umenigusa
sana nimeona nisiwe mchoyo niwajumuishe na wenzangu.
Hapa ni stori ndani ya stori na ujumbe ndani ya ujumbe!
ReplyDeleteNimeupenda ujumbe huu NA mimi nitashare NA wana blogger wangu
ReplyDelete