Wednesday, May 25, 2011

KUAMINI KUWA WAMEKAMILIKA NI KUJIDANGANYA BURE!

Tunayo mengi ya kujivunia


Ndugu zanguni kile kipengele cha kila Jumatano cha marudio ndio leo KARIBUNI!!
Wiki iliyopita na wiki hii nimekumbuka sana nyumbani, nadhani ni kwa sababu wiki iliyopita tarehe 17 ilikuwa ni tarehe ambao mama yangu alifariki na wiki hii 23/5 imetimia miezi miwili tangu Mdogo wangu alifariki. Kwa kweli nam-miss sana mama yangu pia mdogo wangu.

Nakumbuka ilikuwa kila nikienda likizo, nilikuwa natumia muda mwingi kuwa jikoni na mama yangu nikizungumza naye simulizi za kale za enzi ya utoto wangu.

Ni simulizi ambazo kwa kweli kila nizikumbukapo huwa natamani yale maisha yajirudie kwani kuna mengi ya kufurahisha na ya kuhuzunisha ambayo kwangu mimi nimejifunza mengi kwako.

Lakini lipo jambo moja ambalo nimelikumbuka, ambalo kwa kweli huwa linanifikirisha sana. Jambo lenyewe ni kuhusiana na baadhi ya marafiki zangu kule nyumbani.

Kusema kweli ule ukaribu niliokuwa nao na baadhi ya marafiki zangu umepungua kiasi cha kukatisha tamaa.

Sababu kubwa ni kutokana na kile walichodai kwa nimewatupa kutokana na kutowasaidia kupata wachumba wa Kizungu. Yupo rafiki yangu mmoja mbaye yeye aliwahi kunitamkia wazi kuwa mimi ni mbinafsi kwa kuwa ni mara nyingi ameniomba nimtafutie mchumba wa Kizungu kwa kuwa ninaishi huku ughaibuni lakini nimeshindwa kumtafutia.

Nakumbuka nilimweleza ukweli kuwa siwezi kumsaidia juu ya jambo hilo kwa sababu liko nje ya uwezo wangu, lakini kutokana na labda tuite ufinyu wa kufikiri, nilimpoteza rafiki huyu kwa sababu ya kushindwa kumtafutia mchumba wa kizungu……..yaani kaaaazi kweli kweli.

Hata hivyo nilijiuliza swali moja, kuwa hivi hakuna wanaume huko nyumbani mpaka mtu aamue kutafuta mchumba wa Kizungu? Je ni mapenzi au ni Uzungu unaotafutwa hapo?

Lakini kwa upande mwingine sikumshangaa sana kwa sababu kwa huko nyumbani ipo silka ya baadhi ya watu ambao wanaamini kwamba kuoa au kuolewa na Mzungu ni jambo la kujivunia sana. Huwa nimezoea kauli za baadhi ya watu kule nymbani kila niendapo likizo wakisema, ‘siyo mwenzako yule, kaolewa na Mzungu’ .

Yaani mpaka leo hii bado kuna baadhi ya watu wanaamini kuwa kuoa au kuolewa na mzungu ni jambo la kifahari na la kujivunia. Kinachotafutwa sio mapenzi tena ni huo uzungu..

Kuna baadhi ya watu wamefikia hatua ya kuamini kuwa sisi waafrika ni duni na wenzetu weupe ni bora na waliokamilika.

Lakini nadhani makosa hayo hayakuanza leo, yameanzia mbali sana. Kwani kizazi na kizazi tumekuwa tukiaminishwa kuwa wazungu ni bora zaidi yetu sisi.

Kwa mfano, mtu kufanya mambo yake kwa umakini na anayefuata muda huyo ataitwa ni mzungu, au mtu asiyependa majungu, uzinzi, uasherati na umbeya naye ataitwa kuwa ni mzungu. Nakumbuka wakati nikisoma kule nyumbani, ilikuwa kama kuna mwalimu ambaye ni mwadilifu kwa wanafunzi na anayewajali, utawasikia wanafunzi wakisema, ‘yule mwalimu ni mzungu’

Yaani kipimo cha kufanya mambo kwa uadilifu na kuwajali wengine kimekuwa kikihusishwa na uzungu, mpaka imefikia mahali kila mtu anatamani kuolewa au kuoa mzungu wakiamini kuwa hao wamekamilika.

Hata huko makazini napo watu wanaochapa kazi kwa uadilifu wanafananishwa na wazungu. Wakati mwingine huwa nacheka kwa sababu naamini hao wanaoamini kwamba mtu kuwa mzungu anakuwa amekamilika ni wazi kwamba hawawafahamu watu hao.

Kwamba kuwa mzungu ni kutokuwa na tabia mbaya, kama uvivu, udokozi, kutojali muda, kusengenya, umbeya, wivu, au kijicho, uzinzi, uasherati, ushoga na tabia zote mbaya tunazozijua hapa duniani, nikujidanganya bure.

Nasema kuamini hivyo ni kujidanganya, kwa sababu kwa wale wanaoishi huku ughaibuni au wale wanaofanya kazi na hawa wenzetu huko nyumbani, watakuwa ni mashahidi wangu.

Kama mlikuwa hamjui ni kwamba hawa wenzetu nakubali kuwa wapo waadilifu na wenye tabia nzuri, lakini pia wapo wenye tabia za ajabu kama uvivu, udokozi, kutojali muda, kusengenya, umbeya, wivu, au kijicho, kutojiamini, uzinzi, uasherati, ushoga na tabia zote mbaya tunazozijua hapa duniani.

Ule udhaifu tulio nao pia wenzetu hawa wanao tena wenzetu hawa wamepitiliza. Ila kutokana na kudanganywa na TV na hizo kauli za wazee wetu tumejikuta tukiamini kitu ambacho hakipo.

Mie wakati mwingine huwa nashangaa pale ninapokutana na baaadhi ya Watanzania wenzangu ambao wanaishi au wamewahi kuishi huku ughaibuni wanapozungumza kwa kubana pua kama hawa wenzetu. Wanashindwa kujua kwamba ile ni lafudhi ambayo inatokana na lugha yao. Ni kama pale unapokutana na Mmakonde, Mngoni au Msukuma au Mpare anapoongea Kiswahili kwa lafudhi ya lugha yao.

Mbona wenzetu kwa mfano Wanaijeria au Wakenya wanaongea kwa lafudhi ya lugha zao. Ni rahisi sana kumtambua Mkenya au Mnaijeria kutokana na lafudhi yake pale anapoongea Kiingereza, tofauti na sisi ambapo Tunajitahidi kubana pua mpaka tunajisahau hata pale tunapoongea Kiswahili.
Na ndio maana kuna baadhi ya wanawake huko nyumbani na hata huku ughaibuni wamefikia hatua sasa wanaukataa uafrika na kuanza kujichubua kwa mikorogo ili kuutafuta weupe.

Kuna wakati nilipokuwa huko nyumbani nilishangaa kuwaona baadhi ya wasichana ambao nawajua kabisa rangi zao kuwa ni weusi kama mimi lakini wamekuwa weupe mpaka wanatisha! Tabu yote hiyo ni ya nini?

Tumefikia hatua sasa kila jambo linalofanywa na hawa wezetu tunaiga, na ndio sababu siku hizi tabia kama za ushoga, usagaji na tabia nyingine chafu tunazozishuhudia huku zimetamalaki huko nyumbani.

Sisi kama Watanzania tunazo tabia nzuri ambazo hawa wenzetu wanazitamani sana tofauti na tunavyodhani. Kwa mfano, sisi ni kawaida mtu kuamka na kupita nyumba mbili tatu na kuwajulia majirani zake hali, au kuingia nyumba yoyote na kama akikuta chakula akala bila wasiwasi.

Kwa upande wa Misiba au harusi watu wamekuwa wakichangiana na kusaidiana kwa hali na mali, yaani tumekuwa na ushirikiano wa hali ya juu tofauti na wenzetu hawa.

Kuwa mzungu haimaanishai kuwa mwadilifu wala kuwa na tabia nzuri, bali tabia nzuri inatokana na tabia ya mtu na malezi kwa ujumla wake, hakuna mahusiano yaliyopo kati ya uadilifu, tabia nzuri na uzungu. Nasisitiza kuwa hakuna kitu kama hicho, ni kujidanganya bure.

Inashangaza kuona kwamba, badala ya kujivunia tabia hizi nzuri tulizo nazo ambazo hata hivyo wenzetu wanazitamani, tunatamani za kwao ambazo nyingi ni mbaya na zenye kuumiza.
Tubadilike………………

Tukutane tena Jumatano ijayo...

16 comments:

  1. Nyumbani ni nyumbani dada asikuwambia mtu. kwani hiyo inajulikana fika mkata kwao ni mtumwa.

    Kuhusu tabia inaendana na heshima ya mtu, na yote hayo yanakuja katika maisha, pale unapojiona babukubwa kuliko mwezako kumbe nikinyume na uonekanavyo. Hii inajinga hisia mbaya, pamoja nakufata maadili yaliokuwa hayopo kabisa katika jamii yetu.

    Raha ya dunia wadungu ni kujipendekeza kwa watu na watu wakakupenda, kama ulivyosema kusalimia jirani zako ni moja ya kutafuta upendo. kwani hujui nani atakae kufa.

    ReplyDelete
  2. Mdada uliyoyasema ni ukweli mtupu asante kwa kuliongelea hili.

    ReplyDelete
  3. Mimi nilishapoteza kumbukumbu, Je habari hii ni Mpya au unairudia?
    Nadhani ilinipitia kushoto.

    Nimesoma ni nzuri na inaelimisha kwa kweli.

    Ni ubunifu mzuri sana ulioufanya kubuni kipengele hiki ambacho kwa kweli kinatusaidia sisi tuliopitwa na makala zako huko nyuma.

    ReplyDelete
  4. Kabla marafiki zako hawajakukimbia ati kwa sababu hujawatafutia mume mzungu (nasikia kicheko kwa kweli)waambie wasome Warumi 12:9 "Mapendo yenu na yawe bila unafiki wowote..." Swala la ndoa kwa ujumla lihusishwe zaidi na mapendo kuliko mali.

    ReplyDelete
  5. hilo nalo ni neno dada Yasinta kwani hayo uyasemayo ni kweli yanatokea japo inawezekana ikawa siyo kwa sura hiyo bali hata kwenye nyanja nyingine kama elimu, ndugu zetu wengi wamekuwa wakitaka kuja kusoma ulaya, kila itwapo leo hupokea simu au message kutoka kwa ndugu na marafiki wakitaka kutafutiwa wafadhili ili waje kusoma na unapo wambia hali halisi huwa hawaelewi badala yake huishia kuchukia na kuona kama tuna wabania nafasi.
    Nadhani ukweli ni kwamba wakati umefika tubadilike na kujivunia vya kwetu lakini pale inapopatikana nafasi ya kubadili mazingira na itumike vizuri.Lawama zisizo na msingi hazijengi ila kuongeza fitina na kuvunja undugu.
    Kuwa na tabia njema au la ni tabia ya mtu bila kujali ni mzungu au mwafrika,nimekuwa nikishuhudia mambo machafu hata ambayo sikuwahi kuyaona ama kusikia kabla yakifanyika huku ulaya.
    Shime ndugu zangu wahenga walisema "mkataa kwao ni mtumwa" tuheshimu na kujali vyetu....naomba kuwakilisha.

    ReplyDelete
  6. mimi naona kwanza hawa wenzetu wanaongoza kwa usengenyaji, kutwa kusengenyana chini chini. Huku kila mmja wapo akiogopa kuonekana mbeya, hakuna watu wasengenyaji kama wazungu, wanasengenyana weee au watakusengenya, wakikuona wanajifanya kukuchekea, au kuchekeana kicheko cha unafiki

    ReplyDelete
  7. Dada mkubwa kwa darasa lako hakika nakuvulia kofia, yaani nakula somo huku najiona niko mbele nakutazama unaongelea somo hilo wakati umeandika. nashukuru kwa maarifa mkuu

    ReplyDelete
  8. haya mambo yapo dada yasnta yaani kuna watu wapo huku marekani wamepata uraia wa huku yaani ukikutanao hawataki kabisa waitwe watz yaani wanaukana uraia wao na utakuta wamekuja huku wakiwa watu wazima wengine na familia yao yaani wanajifanya kabisa wao ni wamerekani na huku wazi wanaonekana ni wakuja tu mimi sijuii kwanini watu wanaukana uraia wao au nchi yao waliyozaliwa nayo hili jambo lipo sana yaani hili jambo linatakiwa lizungumzuwe kwamapana sana

    ReplyDelete
  9. Asante da Yasinta kwakutukumbusha,nimeamini ukurudia kusoma na uhondo unazidi!Kazi nzuri dada.

    ReplyDelete
  10. Kwa upande wangu mimi huwa najivuna sana vile nilivyo, ukiona rafiki yako ana ndoto zinazovuka viwango kwa tamaa zake, ujue hapo ipo kazi kweli lweli maanake kwanza watu kama hao hawamjui mungu na ndiyo maana hawana matumaini. Maisha yako ukimkabidhi Mungu huwezi kuwa na shida/matamanio yanayokuvuka, kwa sababu mambo yote kwake yeye yanawezekana. Yeremia 33.3.

    ReplyDelete
  11. Umasikini tu yasinta na ndoto za kuukata ndio zinafanya watu watamani kuoa au kuolewa na mzungu na wengine baada ya hio ndoa wanakuwa wanajuta sana ila tu hawawezi kusema ukweli kutokana na taswira waliyoijenga huko nyumbani kuwa wao sasa wameukata na maisha kwao mswano. Utakuta wengine kutokana na tofauti za tamaduni zetu na za wazungu wanashindwa hata kuwasaidia wazazi wao maana huku mzazi atajijua mwenyewe wakati nyumbani mzazi ni wajibu na jukumu la mtoto kwani pensheni na security yake ni mtoto wake. Sasa mtoto huyu anashindwa kutim,iza lile jukumu lake ama kwa kuwa pesa ziko kwenye joint akaunt au anabidi aakaunti kila senti inayoingia na kutoka kwenye familia. Na kwa wazungu wao kutokana na tamaduni zao za kujitegemea kivyao vyao inabidi asavu kila senti tano ili ikifika uzeeni awe na pensheni yake ya kutosha ya kumuwezesha kuishi bila ya kumtegemea mtu, na hapo ndipo mgongano unapotokea.

    Kwa wale ambao hawajaingia wanawaona walioko kwenye ndoa za wazungu wameukata na wanafaidi kwa sabau vitu vingine ambavyo ni necessity kwa mwanadamu kama friji, jiko la umeme, gari, hata baiskeli lazima awe navyo wakati kwa upande wa kwetu hivyo ni luxury na sio necesity.

    Ila kwa wazungu nawapendea kitu kimoja wanaweka maslahi au masuala ya familia mbele, lake ni yeye na familia yake mtu mwingine akiingilia ni non of his or her business, hakuna cha mie shemeji kwanini unaendesha gari la kaka yangu au kwanini hujazaa unajaza choo kwenye nyumba ya kaka yangu, hayo kwa wazungu hakuna. labda inabidi kuna vitu vingine sisi kama waafrika tubadilike hasa masuala ya unyanyasaji wa wanawake na uingiliaji kwenye masuala ya familia ya mtu mwingine, mambo yasiyokuhusu waachie wenyewe mke na mume, wewe kama kaka au dada huna nafasi kwenye nyumba hiyo.

    Bi Mkora

    ReplyDelete
  12. Du.
    Ni kazi kwelikweli

    Tatizo hapo ni kutokujitambua na kujiamini ,lakini ukienda kwa unadani zaidi kinachoonekena kwa huyo rafiki uliyempoze ni kuamini kwake kuwa akiolewa na mzungu mambo yake yatakuwa super bila ya kufikiria kuwa maisha yanahitaji kujipanga na nkutekeleza kile unachoamini kuwa kitaboresha maisha yako.

    Kuhusu kasumba ni suala lilelile la kutokujiamini na kuamini kuwa wngine kuwa wana thamani kubwa kuliko sisi waafrika wakati ukweli wa mambo kuwa wote tuna thamani sawa na kwa kutokulijua hilo ndo maana wengi wengi wanafanya mambo kwa kuiga mambo ya wazungu. Hawajui kuwa thamani yetu sis ibinaadamu ni ubinaadamu wetu maana wote tunahitaji mambo yaleyale ya msingi anayohiyaji hata mzungu,mfano chakula,malazi,mavazi na masuala ya kuvuta hewa na call of nature.

    Tuna kazi ya ziada kutoka katika kujishusha na kuamini katika sisi

    Kila la kheri,

    ReplyDelete
  13. Asante dada!
    umemaliza kila kitu.

    Kwanza pole kwa kuwa na huzuni ya kuondokewa na wapendwa (mama na mdogo) wako. Hakuna atakaye weza kuziba hiko pengo. Mungu azidi kukupatia nguvu.

    Mimi ni mfuatiliaji mzuri wa hii Blog yako. Kila siku nachota maujuzi humu! Ubarikiwe sana dada.

    ReplyDelete
  14. kama hapa arusha dad ayangu watu wamebezi sana kwa wazungu ili wasaidiwe wanashindwa hadi kufanya kazi ili wapate wazungu watoke kimaisha .hata mimi nashangaa sana kwanini inakuwa hivyo ,asilimia kubwa watu wa tours wa huku arusha wameadidiwa na wazungu kwahiyo hata ukimwambia mtu suala hilo awawezikuamini .Nimeona vijana wengi wakifa na ukimwi kwa ajili ya kusaidiwa na wazungu na wengine kupata magonjwa ya zinaa yaaanni aibu kwakweli.ssijua hata watakuja kubadilika lini maana mtu ukimwambia umepima naye huyo mzungu wanaamini kuwa wazungu hawana ukimwi kwakweli vijana hapa arusha wanakwisha mnooooo .nimeipaenda mada maana ndio uhalisia wa watanzania.asante

    ReplyDelete