Saturday, October 30, 2010

Uchaguzi wa amani

Wakati umeshafika, uchaguzi Tanzania,
Kura zetu kutumika, viongozi kuchagua,
Umakini na hakika, ni wakati kuamua,
Naombea Tanzania, uchaguzi wa amani.

Vurugu hatuzitaki, tunapaswa kutulia,
Chaguzi iwe ya haki, uhuru wa kuamua,
Matokeo yale feki, amani itapotea,
Naombea Tanzania, uchaguzi wa amani.

Tuutimize wajibu, kuijenga Tanzania,
Kura zikawe majibu, nani kututumikia,
Hatuhitaji ghilibu, mabaya kutufanyia,
Naombea Tanzania, uchaguzi wa amani.

Kila aloandikisha, aende kupiga kura,
Tushiriki sababisha, ndoto ya maisha bora,
Ubovu kuuondosha, utufanyao dorora,
Naombea Tanzania, uchaguzi wa amani.

Kumekucha Tanzania, la mgambo lishalia,
Chaguzi imewadia, tuijenge Tanzania,
Makosa kutorudia, Mola atutangulia,
Naombea Tanzania, uchaguzi wa amani.
Shairi hili limeandikwa na Fadhy Mtanga

5 comments:

  1. Wenye dhamana ya nchi kwa sasa ni wapiga kura. Wachague kusuka au kunyoa

    ReplyDelete
  2. Thanks kwa utenzi

    ReplyDelete
  3. aHSANTENI SANA KWA KUTOCHOKA KUTEMBELA MAISHA NA MAFANIKIO. nI KWELI FADHY NI KIBAKO ANA KIPAJI CHA AINA YAKE KWA KWELI. AHSANTE MTANI.

    ReplyDelete