Wednesday, May 12, 2010

UKIKUTA MANYOYA, UJUE KESHALIWA!!!

Utotoni kuna michezo mingi ya kukumbukwa
Wakati wa utoto wetu yapo mambo mengi ambayo tumeyapitia, ambayo huwa wakati mwingine ukiyakumbuka unatamani sana kurejea utotoni.

Hivi karibuni mdogo wangu Koero aliweka mada yake aliyoipa kichwa cha habari kisemacho, ‘anaposema mwendawazima’.
Katika makala yake hiyo kuna kipengele alizungumzia kuhusu kuteka maji kisimani na jinsi yeye na bibi yake walivyowakuta mabinti wa pale kijijini kwa bibi yake walivyokuwa wakicheza na wavulana pale kisimani badala ya kuchota maji na kupeleka nyumbani.

Pamoja na kukemewa na Bibi Koero, lakini walimdharau ma kuendelea kucheza michezo yao na wavulana wale, bila kujali onyo la Bibi Koero, isipokuwa binti mmoja ambaye alimsikiliza bibi Koero na kuondoka kurejea nyumbani akiwaacha wenzie wakiendelea kucheza pale kisimani. Kama ungependa kujikumbusha makala hiyo unaweza kubofya hapa.

Kipengele hicho kilinikumbusha wakati wa utoto wangu kule kijijini Litumbandyosi/Kingoli wakati ule nikiwa darasa la nne.
Wakati huo tulikuwa tukienda kisimani kuteka maji na huko tulikuwa tukicheza michezo mingi ya kitoto.

Nakumbuka nilipokuwa likizo nyumbani mwaka jana, nilipokuwa naelekea sokoni, njiani nilikutana na kijana mmoja ambaye ningependa kumwita Mpetamanga (Sio Jina lake) kwa kweli nilikuwa nimemsahau, sijui ndio uzee unaninyemelea, maana nilishangaa alinikumbuka vizuri sana tofauti na mimi ambaye nilikuwa nimemsahau.

Mpetamanga nilisoma naye darasa moja na nakumbuka baadae familia yao ilihama pale kijijini na kuhamia kijiji cha jirani na huo ukawa ndio mwisho wa kuonana na kijana huyu.
Kukutana kwetu pale njiani kulitukumbusha mambo mengi sana ya utotoni ikiwemo ile michezo tuliyokuwa tukicheza kule kisimani tulikokuwa tukichota maji.
Mpetamanga alitumia muda huo kunikumbusha mambo mengi ya utotoni ikiwemo hiyo michezo tuliyokuwa tukicheza kule kisimani.

Kwa kuwa nilikuwa na haraka nilimuaga, lakini nilimkaribisha nyumbani, kisha tukaagana na nikaondoka kuelekea sokoni kununua mahitaji yangu.
Siku iliyofuata nikiwa nyumbani na mwanangu Erik, kwani Camilla alikuwa ametoka na baba yake kwenda mjini kununua mahitaji mengine ya pale nyumbani, nilisikia mtu akibisha hodi, nilipokwenda kufungua mlango alikuwa ni Mpetamanga.

Nilimkaribisha ndani kwa bashasha na kisha tukakaa sebuleni kwa mazungumzo.
Nilimwita mwanangu Erik na kumtambulisha kwa mgeni.
Mpetamanga alishtuka sana, na kuniuliza kwa hamaki, ‘Yasinta umeolewa?’
Nilimjibu kuwa nimeolewa na nina watoto wawili. Nilimjulisha kuwa ninaishi nchini Sweden na familia yangu, na pale nyumbani niko likizo tu.

Alishtuka sana na nilimuona dhahiri akiwa amenyong’onyea kabisa. Alinijulisha kuwa alipomaliza shule alikwenda nchini Malawi kundelea na masomo na amekuwa akiishi huko tangu alipoondoka nchini.
Na yeye kama ilivyo mimi aliamua kurudi nchini kuwasalimia ndugu zake na safari hiyo ilimlazimu kufika Ruhuwiko kumuona mjomba wake, lakini pia akiwa na hamu ya kuniona kwani aliambiwa kuwa familia yetu ilihamia Ruhuwiko siku nyingi.

Na pale tulipokutana ndio alikuwa amefika Ruhuwiko.
Aliniambia kuwa, nilipomkaribisha nyumbani alifurahi sana na alijua huo ndio wakati muafaka wa kuzungumza nami kwani ni muda mrefu alikuwa akiniwaza, na lengo lake ilikuwa kama akinikuta sijaolewa basi azungumze nami ili alete posa.

Nilicheka sana na kumwambia kuwa amechelewa kwani mie niliolewa na kuondoka nchini na kuhamia Sweden.
Nilimchekesha pale nilipomwambia, ‘Ukikuta manyoya basi ujue ndio keshaliwa’
Alicheka sana na kuniuliza kama nina maana gani, na ndipo nilipomfafanulia kuwa mpaka amekuta watoto basi ajue kuwa ndio nishaolewa hivyo……..

Lakini kitu kingine kilichomshangaza zaidi ni kuona jinsi ninavyozungumza kingoni na Kiswahili kwa ufasaha pamoja na kuishi nje ya nchi kwa muda mrefu, kwani hata nilipomweleza kuwa nimeolewa na ninaishi nchini Sweden alidhani namtania, hadi nilipomuonesha picha za familia yangu.


Hata hivyo Mpetamanga alikubali matokeo, na kuridhika na maelezo yangu.
Kusema kweli kila niwapo likizo nyumbani nakutana na visa na vituko vingi vya aina hii na haviishii hapo, hata mtandaoni nako kuna visa vyake, hili sitalizungumza kwa undani maana mdogo wangu Koero amelizungumza hili kwa kirefu katika makala yake aliyoipa kichwa cha habari kisemacho, ‘Dalili hizi sio za kweli’ unaweza kubofya hapa kumsoma.

Kuna wanaume wakware ambao hawakubali kushindwa. Hata wakute manyoya lakini bado watapekuwa weeeee! wakiamini kukuta minofu. Jamani mmeshachelewa ndio keshaliwa huyoo…….LOL

18 comments:

  1. Da Yasinta: usemayo ni kweli lakini hata kama 'si vema kumpa mbwa chakula cha watoto, lakini hata mbwa hula makombo yanayoachwa na watoto'...lol

    nadhani hicho ndo alichomaanisha huyo mkaka....lol

    ReplyDelete
  2. Kaka Chacha umelonga nakuuunga mkonooooooooooooooooo.

    JASIRI HAACHI ASILI jamani da Yasinta hujui hilo??? Ila inauma aise eti ukikuta manyoya keshaliwa, yaani hata makombo hamna japo kulamba tu??? Lol Jamani hata kipapatio hakuna??? Lol angetia EMCHEKU

    ReplyDelete
  3. Jamani mnataka aonje asali akichonga mzinga je?

    ReplyDelete
  4. kweli kuna watu wanajua kuwaza,yaani miaka nenda rudi wanajua ipo siku tu.
    sasa yuko broken heart kweli kweli,nafikiri itachukua miaka mingine kama hiyo kupona moyoni

    ReplyDelete
  5. Yaani nimecheka kweli, Yasinta you have made my day, ni kweli wanaume wengine hata wakikuta manyoya hawaoni kama hayo ni manyoya wanafikiri labda kuku kanyeshewa na mvua tu akikauka watamkuta mzima!

    Na wengine hata wakimkuta mlaji mwenyewe wanakuuliza hivi kwani huwezi kunifanya na mimi niwe spare tairi? Sasa unabaki unashangaa kweli. Na kwako wewe ndio worse maana mwingine atataka kutumia mgongo wako kufanikisha safari yake ya maisha akiamini kuwa huko uliko huridhiki! Duniani kweli kuna mambo! Watu hata woga hawana. Waambie tu UKIONA VYAELEA JUA VIMEUNDWA NA WEWE UNDA CHAKO.

    ReplyDelete
  6. Banza stone anausemi wake anasema (ukikuta tangazo ulilolibandika limechanwa ujue lishasomwa) yaani naona zinakaribiana na hii

    ReplyDelete
  7. ANONY: WENGINE WANAPENDA manyoya badala ya KUKU...lol!

    ReplyDelete
  8. Yasinta Hello, I am very happy to read them, I hope you are well, a hug, thanks to my friend now in Sweden.

    Kisses

    Marlow

    ReplyDelete
  9. Yasinta unaona?...Nakwambiaga wewe una mwili mzuri husikii. Hebu ona huyu ambavyo alishindwa hata kugundua kama una watoto.

    Nampa pole.

    ReplyDelete
  10. nanukuu "Yasinta unaona?...Nakwambiaga wewe una mwili mzuri husikii. Hebu ona huyu ambavyo alishindwa hata kugundua kama una watoto.

    Nampa pole." Haha ha ha hahaha umenifanya nicheke na kushindwa kuacha. Da Mija unampa pole mimi Je?????

    ReplyDelete
  11. Yasinta sasa wewe pole ya nini? sana sana nakupa hongera.

    ReplyDelete
  12. Da Mija Da Mija pole kwa vile nami ni binadamu pia na nadhani ni mwanamke wa shoka pia....Lol

    ReplyDelete
  13. Haya Pole Yasinta, lakini umenilazimisha tu kusema hiyo pole ila kwa Mwanamke wa shoka kama wewe unatakiwa kupewa hongera.

    Natoka nje ya mada. Hakuna kitu Yasinta unanifurahishaga kama jinsi unavyowapelekaga wanao kijijini kwao Ruhuwiko, na kubwa zaidi ni jinsi unavyojitahidigi kuwavisha kulingana na mazingira.

    Yaani hilo tu huwa nasema Yasinta si Mwanamke wa mchezo.

    Sasa hapo hata kwa nini sikupi pole, ni hongera tu.

    ReplyDelete
  14. Mija Asante sana kwa hilo na nimepokea vyote pole na Hongera pia. Na åpia kumbuka usemi huu ukikuta sehemu wanatembea uchi basi nawe fanya hivyo. Na nakuambia sitaacha uta,maduni wangu mpaka naingia kabiurini. upendo daima.

    ReplyDelete
  15. leo hatusemi, kimisemo zaidi!!

    ReplyDelete
  16. nanukuu " leo hatusemi, kimisemo zaidi!!"

    usiye na jina naomba hapa unitafsirie una maana gani? we sema ulilonalo moyoni

    ReplyDelete
  17. Hadithi hii imenifurahisha. Literally: Chelewa chelewa utamkuta mtoto si wako.

    ReplyDelete