Friday, May 28, 2010

Lucia: Uyatima umenifanya nisome kwa shida !!

Lucia, mwenye kitambaa chekundu kichwani akiwa na wadogo zake Jacqline na Elias nyumbani kwao katika kijiji cha Nyambiti Wilayani Kwimba mkoani hapa.


“Wakati baba anafariki aliniacha nikiwa darasa la tano katika shule ya Msingi Nyambiti mwaka 2003 na mwaka mmoja baadaye mama naye alifariki hapo ndipo hali ya maisha katika familia yetu ilipoanza kuwa ngumu,” anasema Lucia Juma (20).

Anasema kuwa kifo cha baba na mama yake kilimfanya aishi maisha magumu, kwani wakati akiwa na matumaini ya kupata elimu alilazimika pia kuwahudumia wadogo zake.

“Nilikuwa nimezoea kutegemea wazazi wangu lakini ilinibidi nianze kutegemewa na wadogo zangu licha ya kuwa sina uwezo na mimi nikiwa bado mwanafunzi tena wa shule ya msingi,” anasema Lucia.

Lucia ambaye ni mmoja kati ya wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka jana katika shule ya Sekondari ya Taro iliyopo katika kijiji cha Nyambiti wilayani Kwimba mkoani Mwanza anasema baada ya wazazi wake kufariki amesoma kwa shida sana na hali hiyo imesababisha hata matokeo yake ya kidato cha nne kutokuwa mazuri na hivyo kujikuta akipata daraja la nne hivyo kushindwa kuendelea na masomo.

“Mazingira ninayoishi yalinifanya hata nisiweze kwenda shule mara kwa mara kwa kuwa muda mwingi nilikuwa nikifukuzwa shule kwa kukosa ada,” anasema.

Lucia anasema mbali na kukosa ada pia alitumia muda wake mwingi akiwa hospitalini badala ya shuleni kutokana na hali ya afya ya mdogo wake kutokuwa nzuri.

“Mmoja kati ya wadogo zangu anasumbuliwa na ugonjwa wa kuishiwa damu, hivyo alipokuwa akiugua nililazimika kutokwenda shule ili nibaki naye na kumuuguza, hata alipokuwa akilazwa hospitali, nililazimika kulazwa naye…,” anasema Lucia na kuongeza kuwa;
‘Sikuishia kulazwa naye tu wakati mwingine nililazimika kutoa damu kwa ajili ya kuokoa maisha yake anapokuwa amepungukiwa damu na kutakiwa kuongezwa,” anasema Lucia.

Anasema kuwa analazimika kubeba jukumu hilo kutokana na ukweli kuwa hakuna mtu wa karibu ambaye anaweza kuwasaidia pindi wanapopata matatizo na hata kujitolea damu kwa ajili ya mdogo wake.

Ninapotoka hospitali ninakuta wenzangu wameishafundishwa sana, hivyo kwangu inakuwa ni vigumu sana kwenda nao sambamba, lakini sikuwa na namna ya kufanya kwa sababu mimi ndiye ninayegemewa na wadogo zangu, wanapopata shida nalazimika kubeba jukumu la kuwasaidia wadogo zangu,” anasema Lucia huku akitokwa na machozi.

Anaongeza kuwa mbali na kutumia muda mwingi hospitalini lakini pia hakuwa na uwezo wa kununua vitabu vya kiada wala ziada kwa ajili ya kujisomea hali ambayo ilikuwa ikimpa ugumu sana pindi anapohitaji kujisomea.

“Tangu nianze kidato cha kwanza hadi namaliza sikuweza kununua kitabu chochote wala mitihani iliyopita (Past papers) kwa ajili ya kujifunzia kama wanavyofanya wenzangu, kwa kuwa sikuwa na fedha ya kumudu kununua vitu hivyo,” anasema
Akizungumzia juu ya ulipaji wa ada anasema kuwa suala la ada na michango mingine ya shule hakuweza kulipa kwa wakati na hivyo alifukuzwa mara kwa mara.

Anasema hatua ya kufukuzwa shule ilikuja baada ya kushindwa kulipiwa ada na Serikali wala halmashauri kwa kuwa hakuwa miongoni mwa wanafunzi ambao majina yao yalipelekwa kwa ajili ya kulipiwa ada.

“Mwaka 2006 nilipoanza kidato cha kwanza nilikwenda kwa Mtendaji wa kata ili na mimi niingizwe kwenye utaratibu wa kulipiwa ada na serikali lakini Mtendaji alidai majina yetu yalicheleshwa kupelekwa Halmashauri na hivyo hatuwezi kulipiwa ada na serikali wala Halmashauri,” Lucia anaeleza.

Anasema kutokana na hali hiyo alilazimika kujilipia ada na kutokana na kutokuwa na uwezo ulipaji wa ada ulikuwa ni mgumu sana kwani hakukuwa na mtu wa kumsaidia.

“Hapa nyumbani tupo na mjomba ambaye anasimamia Saloon iliyoachwa na baba nilipokuwa namwambia juu ya suala la ada alidai hana uwezo wa kunilipia, kwangu ilikuwa ni vigumu sana na wakati mwingi nilifukuzwa shule na hivyo kulazimika kukaa nyumbani hata wiki nzima hadi niende tena kwa mtendaji wa kata aende kuniombea shuleni ndipo niruhusiwe kusoma,” anasema

Anasema kuwa malipo ya fedha ya mtihani wa mwisho wa kidato cha nne alilazimika kwenda kukodisha mashamba yaliyoachwa na wazazi wake ili kupata fedha za mtihani baada ya mjomba wake kukataa kumlipia Sh35,000 za kulipia mtihani.

“Hadi sasa ninavyokwambia nadaiwa shilingi 85,000 shuleni ambazo ni madai ya michango mbali mbali pamoja na ada ambazo nilikuwa silipi kwa kuwa sikuwa na uwezo,” anasema.

“Kwa mazingira ambayo nimesomea naiomba Serikali iweke utaratibu wa kuwasaidia watoto yatima, kwa kweli watoto waliofiwa na baba na mama wanaishi na kusoma kwenye mazingira magumu kwani hata kama kuna ndugu, wazazi wanapokufa ndugu hawawathamini wale watoto,” anasema Lucia huku akilia.

Anasema kuwa maisha ambayo walikuwa wakiishi na wazazi wao na ya sasa ni tofauti kabisa, kwani hata ndugu wamekuwa mbali nao tofauti na walivyokuwapo wazazi wao, hivyo Serikali iangalie watoto yatima na kuwasaidia kwa hali na mali ili waweze kupata elimu kama ilivyo kwa wanafunzi wengine.

Akiwazungumzia wadogo zake anasema kuwa hivi sasa mdogo wake Elias ameanza kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari ya Taro baada ya kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka jana na kufaulu hivyo naye bado anahitaji msaada wa hali na mali ili aweze kusoma na pia anahitaji uangalizi zaidi kwa kuwa ana tatizo la kupungukiwa na damu.

Anasema kwa upande wa mdogo wake Jacqline, yeye hivi sasa yupo darasa la saba na kudai kuwa kulingana na uwezo wake darasani ana matumaini makubwa hata yeye anaweza kufanya vizuri katika mtihani wa darasa la saba mwaka huu.

Akizungumzia jinsi jamii inavyochukua jukumu la watoto yatima, Lucia anasema kuwa jamii bado haijaona umuhimu wa kuwasaidia watoto yatima licha ya kuwa inafahamu kuwa watoto hao hawana uwezo wowote wa kuweza kuendesha maisha yao.

Akizungumzia matarajio ya maisha yake ya baadaye anasema kama angepata mtu wa kumsaidia kupata nafasi ya kurudia shule angerudia ili aweze kutimiza ndoto yake ya kuaminika na hatimaye kuweza kupata kazi itakayomuwezesha kujikimu yeye pamoja na wadogo zake.

Naye Mtendaji wa Kata ya Nyambiti, Mathias Mayala, anasema kuwa tatizo kubwa ambalo lilikuwa likiikumba kata hiyo ni kutowatambua watoto yatima na maeneo ambayo wanaishi lakini hivi sasa wameanzisha utaratibu wa kuzunguka kwenye jamii na kuanza kuwatambua watoto hao.

Anasema kuwa hatua hiyo itasaidia hata kuweza kuwahudumia na zinapotokea nafasi za kusomeshwa basi inakuwa ni rahisi kuwafikia kwa kuwa watafahamika sehemu walipo na matatizo yao yatajulikana.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyambiti Joseph Stephen, anasema kuwa hivi sasa wanajipanga kubuni vyanzo vya mapato kupitia kamati za mipango na fedha ili angalau kupata fedha kwa ajili ya kusaidia watoto yatima.

Anasema kuwa suala hilo litafanyika kuanzia kila kitongoji katika kijiji hicho na kuwashirikisha wananchi kwa hali na mali ili waweze kuwasaidia watoto yatima ambao wanazidi kuongezeka kila siku.

Anaongeza kuwa hivi sasa wanaihamasisha jamii kuona namna ya kuweza kuwasaidia watoto yatima angalau kwa kuwachangia chochote ili waweze kuendelea na masomo kwani tatizo la watoto kufiwa na wazazi wao na kubaki peke yao limeonekana kuwa ni kubwa katika wilaya ya kata ya Nyambiti.

Akizungumzia suala la kusaidia watoto yatima diwani wa kata ya Nyambiti Peter Nyanda anasema kuwa ingawa kumekuwa na utaratibu wa halmashauri kuwalipia ada wanafunzi yatima lakini bado wanafunzi wanaolipiwa ni wachache.

Anasema kuwa hali hiyo inatokana na ufinyu wa bajeti kwenye halmashauri na hivyo halmashauri kujikuta zikichukua wanafunzi wachache kutoka kila eneo.

Afisa elimu wa Sekondari wilayani Kwimba Pancras Binamungu anasema baada ya Serikali kuu kurudisha shule kusimamiwa na halmashauri na kutaka halmashauri kuwalipia ada, baadhi ya watoto waliathirika na maamuzi hayo kwa kuwa Serikali kuu ilikuwa ikitoa fedha za ada ya shule na gharama mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya mtoto.

Hata hivyo Afisa Elimu huyo aliitaka jamii kuanzia ngazi ya kitongoji, kijiji na kata kuwasaidia watoto yatima kupata mahitaji yao ya msingi kwani tatizo hilo ni la kijamii na siyo la serikali pekee yake.
“Kuna watoto yatima ambao ndugu zao wa karibu wana uwezo lakini wanashindwa kuwasaidia watoto hao na kuisukumia Serikali,” anasema Afisa Elimu huyo.
“Kuna watoto yatima ambao ndugu zao wa karibu wana uwezo lakini wanashindwa kuwasaidia watoto hao na kuisukumia Serikali,” anasema Afisa Elimu huyo

Na Paulina David, Mwanza (Gazeti la Mwananchi) la alhamis 20/4/2010

7 comments:

  1. Habari hii inasikitisha sana....
    Ukisikia habari za watoto yatima, unaweza hata kutokwa na machozi, lakini mbona kuna hazina ya madini huko kanda ya ziwa , kwani hakuna mfuko unaotengwa kwa ajili ya kuwasaidai mayatima kama hawa na halmashauri za wilaya unaotokana na mrahaba wanaolipwa na wawekezaji?

    ReplyDelete
  2. Ni kweli ni habari ya kusikitisha sana, Nilipoisoma nimeishoma na´dhani zaidi ya mara tano na kila niliposoma machozi yalinidondoka. Nasangaa serikali sijui kwa nini isianzishe mfuko kwa mayatima nao waweze kupata elimu. Kwa kweli iko haja ya kugombe urais au sijui nimechelewa? Ningependa mabaa yote yafungwa na ziwe shule na mahospitali inaumiza sana kuona wengine wanasoma, kula, kuvaa vizuri na mpaka kutupa chakula na wengine haswana kabisa. Kweli huu ni uungwana . Samahani naacha kwani naona hasira zinafumuka. Ngoja nitulie kwanza..

    ReplyDelete
  3. Inatia uchungu sana,yatima kweli wanateseka sana,na mbaya zaidi ni wengi mno,karibu kila familia au kila ukoo utakuta kuna yatima.Sasa kama hawa angalia hata hiyo nyumba wanayoishi jamani! du kweli maisha haya basi tu,sina la zaidi mungu ndie mpangaji.

    ReplyDelete
  4. Kama serikali ingeamua kuhamishia nguvu zake vijijini mambo yangekuwa shwari. Lakini wapi? Labda watu waishio vijijini wangeanza maandamano pengine hali huko ingebadilika.

    Hebu ona kituo cha watoto yatima cha mjini Kurasini kinavyopata misaada kila kukicha utadhani ni kituo pekee cha watoto yatima Tanzania.

    ReplyDelete
  5. Umefika wakati sasa wa wadau mbali mbali, badala ya kuililia serikali tu basi nasi tufanye kitu fulani. Habari kama hizi zinapowekwa kwenye mtandao ziwe ni kwaajili ya kuleta mabadiliko fulani. Kusoma tu habari na kutoa machozi bila kufanya jambo la maana kusaidia hao wanaokutoa machozi haisaidii kitu chochote. Sio kwa vile serikali haiwajali ndio basi hata sisi raia tusijaliane. Kwa mfano pesa anazohitaji huyo bint kwa wengi wetu ni pesa kidogo sana hizo kiasi kwamba uwezekano wa kuwawezesha upo tukiamua. Siku nyingine nitafurahi sana nikikuta habari kama hii ikiwa kwa lengo la kuomba tutoe msaada wetu, na nitakuwa wa kwanza kuchangia.
    Kusema baa zifungwe hiyo ni ndoto ya mchana wa jua, hivi unajua serikali inakusanya kodi kiasi gani toka kwenye makampuni yanayozalisha bia/pombe?
    Nakupa kazi, ukifanikiwa kumpata huyo bint njoo andika hapa nitajitokeza kumlipia deni lake la shuleni, pia nitamlipia ada ili aweze kurudia mitihani yake kama alivyoomba kwenye hiyo habari.

    ReplyDelete
  6. kwa kweli hii habari inanisikitisha
    sana hata mimi nikimuona huyo mtoto ambae ana daiwa ningejitolea japo £100

    ReplyDelete
  7. ni habari ya kusikitisha na kuhuzunisha,je kweli serikali za mitaa na ustawi wa jamii zinafanya nini?katika masuala kama haya?dada yasinta nitakuomba siku nyingine unapoweza kupata habari kama hizi ningependelea wewe na sisi wadau wengine tujitolee kwa kuanziasha au kuwachangia hawa watoto hasa upande wa vijijini naona wamesahauliwa na jamiikwa ujumla,mimi binafsi naishi america,nitakua nipo tayari kutoa mchango wangu kwa kupitia blog yako,pili ushauri wangu michango yetu ipitie kwenye mikono safi ya watu wenye huruma sio wasanii mafisadi ambao watatumia michango yetu mbali bila kujali mahitaji ya hao tunaowachangia...jaribu kufuatilia suala hili ,nitakua nipo radhi kuchangia saa yoyote na wakati wowote punde mchango wangu utapohitajika

    ReplyDelete