Wednesday, April 28, 2010

Kuna wale wanaojikuta wanadanganya bila hiari!!!

Inasemekana wasichana wengi hudanganya juu ya umri wao

Inaweza ikatokea tukajikuta tumedanganya mahali ambapo wala hatukuwa na sababu ya kudanganya , tena mbaya zaidi tukawadanganya watu ambao ni wazi ingepaswa kutuuma sana kwa kuwafanyia hivyo. Watu ambao ni waelewa, wanaotuheshimu na kutupenda.
Hebu fikiria kuhusu bosi wako, mkeo, mumeo au hata rafiki tu ambaye anakuuliza juu ya jambo fulani ambalo ni wazi hata ukisema ukweli halitakudhuru wala kubadali chochote kwenye maisha yako. Unamwambia au kumjibu uongo, halafu baadaye anagundua kuwa ulimdanganya. Unaingia kwenye fedheha na aibu na kutokuaminika tena.

Kuna watu ambao wana laana ya uongo, yaani hujikuta tu wamedanganya juu ya jambo ambalo kwa kweli hawakupaswa kulidanganyia. Inaweza kuwa ni jambo dogo na la kawaida na watu wanaodanganya hawakupaswa kabisa kuwadanganya. Wenyewe (hao wanaodanganya) huwa wanajua kwamba wanafanya vibaya kwa kudanganya huko na kujisikiavibaya pia, lakini hawana uwezo wa kujizuia. Huwa wanajiuliza ni kwa sababu gani wamedanganya kuhusu jambo hilo na hujisikia vibaya.
Pengine kabla ya kuwazungumzia watu hawa wanaodanganya bilafaida au wanaodanganya bila hiari zao, ni vema tukabainisha kwamba kwa walio wengi kudanganya ni njia ya kuepuka matatizo. Mtu anapodanganya anafanya hivyo baada ya kuona kwamba bila kutumia uongo anaweza kuingia kwenye matatizo, ambayo angeweza kuyaepuka au kuyaepuka kwa muda kwa kusema uongo.
Uongo hata hivyo haupo kwa kila mtu. Kuna watu ambao hawawezi kabisa kudanganya, hata pale ambapo uongo mdogo ungeweza kuwaokoa kutoka kwenye adhabu kubwa. Lakini kuna wale ambao katika kauli zao kumi ni lazima zaidi ya tano zitakuwa za uongo.
Ni vizuri hata hivyo tutafafanua kwamba, hapa tunazungumzia kusema uongo na siyo kusema mambo ya uongo. Kuseama uongo ni kama huko ambapo mtu anaweza kusema kwamba alikuwa kwa dada yake wakati alikuwa kwa rafiki yake au kusema kwamba amelipia kitu fulani wakati hajafanya hivyo. Kusema mambo ya uongo ni kule ambako mtu anasema alipigana vita vya Kagera huku wakati huo hata meno alikuwa hajaota. Hivyo hatuzungumzii kusema mambo ya uongo, bali kusema uongo.
Kusema uongo ni tabia ambayo chimbuko lake kwa sehemu kubwa ni kutoka utotoni, kutoka katika malezi. Inaweza pia kuwa ni tabia ya kuiga, ambapo mtu huiokota katika mazingira anamokulia wakati wa makuzi yake. Hebu tuchukulie mtoto ambaye anakulia katika familia ambapo mzazi mmoja au wote ni wakali sana kwake. Kutokana na ukali huo, mtoto anajifunza kudanganya kama njia pekee ya kuepuka adhabu na kufurushwa mara kwa mara. Ni rahisi sana kwa mtoto huyu kuichukua hadi ukubwani amabako nako ataitumia kama silaha ya kujihami na adhabu au shutuma.

Kuna wakati tunajikuta tukidanganya katika mambo madogo na kwa watu ambao hatukuwa na sababu ya kuwadanganya kwa sababu ya kuhisi kwamba ukweli utatushushia hadhi na kuogopa kwamba watu hao wataanza kututazama vingine. Kwa mfano, mtu fulani ametuuliza kama tumefanya jambo fulani ambalo hatujalifanya, tunaweza kumdanganya, hata kama kusema kweli kusingesababishia lolote baya.
Tunadanganya kwa kutokuwa na uhakika kama kusema kweli kwetu tusingeweza kutuletea matatizo. Lakini hisia kama hizo haziji tu zinakuja kwa sababu ya uzoefu fulani wa utotoni. Huenda tulizoea kila tukisema ukweli tunapigwa au kuadhibiwa hata kama ukweli huo ndiyo hali halisi. Lakini pia inawezekana tulipokuwa wadogo, kauli na vitendo vya wazazi wetu vilituonyesha kwamba, mtu anapokuwa mkweli katika mazingira au uhusiano wa aina fulani anajiingiza matatizoni.
Kusema uongo ni udhaifu, kusema uongo kunaashiria mtu kuwa na mambo mengi, migogoro mingi, malimbikizo mengi ya shida za utotoni, ambazo zingehitaji msaada wa kiulaalamu kuweza kuondolewa. Kama mtu unajikuta huwezi kujizuia kusema uongo hata kwenye yale mazingira ambapo hukupaswa kudanganya, ni lazima ujue kwamba una matatizo mengi ya kisaikolojia ambayo yanaweza kuwa yanakuharibia maeneo yako mengine ya kimaisha.

Ni vigumu kusema ni kwa namna gani unaweza kujitoa kwenye tabia hii ya kusema uongo, hasa uongo ambao wala huna sababu ya kuusema na kuusema kwa mtu ambaye wala huna sababu ya aina yoyote kumdanganya. Uongo ambao baada ya kuusema huwa unakukera, lakini unashindwa kuuzuia. Hii ni kwa sababu, kama tulivyobainisha mapema, vyanzo na sababu za mtu kuwa na tabia ya uongo wa aina hii ni vingi.

Njia iliyo bora kabisa ni kwa mwenye tabia hii kuwa mkweli na mhusika, yaani aliyemdanganya. Kuwa mkweli kwa kumwambia kwamba, amemdanganya kuhusu jambo fulani ambalo hana sababu au hakuwa na sababu ya kumdanganya. Kujiadhibu kwa namna hii kwa kujishushua mwenyewe kwa mtu aliyemdanganya, huweza kumfanya mtu mwenye uongo huu kuanza kuichukia tabia yake, kwani itakuwa inamdhalilisha, hivyo uwezekano wa kuiacha huwa mkubwa. Tukumbuke kwamba kuwaambia ukweli waliowadanganya hakuwezi kuwaathiri chochote waongo hawa, kwani uongo wao huwa hauna maana na hauathiri chochote hata kama ungekuwa ni kweli.
Habari hii chanzo ni Gazeti la Jitambue.......

13 comments:

  1. Duh!

    lakini niseme tu kuwa uwongo ni hulka ya mtu.

    Na pengine inatokana na mazoea ama kutaka kujinasua na lililo mbele yako.

    kuna wanaosema pia kuwa kuna wengine huwa hawamaanishi kile wanachokisema. km: akisema ndiyo ana maanisha hapana na akisema hapana anamaanisha ndiyo :-(

    Lakini niseme tu kuwa inawezekana kuancha kuongopa!!!!

    ReplyDelete
  2. Mada ya leo ya moto kweli. Huwa naamini watu wote tumewahi kusema uwongo mara kadhaa. Lakini uwongo si rafiki mzuri maana ni utumwa.

    Ahsante kwa somo hili zuri sana.

    ReplyDelete
  3. Mada ya leo kiboko. Ni mada pana sana ukiweza naomba utubadikie kipengele kwa kipenge ili tuchambue kwa undani kwani tunahitaji kujua vizuri faida na hasara za uongo. Mf unaweza ukatupa changamoto ya uongo wa mzazi kwa watoto wake au wanasiasa kwa wananchi n.k

    Nimeipenda mada inaamsha aliyelala.

    ReplyDelete
  4. Nilipata kufikiria kuhusu suala hili siku moja. Dondoo moja iliyokaa sana kichwani mwangu ilikuwa ni pale watoto wanaposhuhudia wazazi wao wanadanganya wazi. Mara nyingi watoto hukua huku wakiihalalisha tabia ya uongo. Pia wale wanaotuzunguka kama tabia zao ni za kusema uongo basi nasi hujikita huko. Binafsi husema uongo lakini nafsi hunisuta kila mara ikiambatana na majuto. Hii imenisaidia sana kuwa 'a better person' Swali la kizushi, upi ni uongo mzuri na upi ni uongo mbaya?

    ReplyDelete
  5. Kwa Rwanda, wanawake ni mabingwa wa kudanganya umri wao, lakini ni kutokana na jamii kupenda kuoa wasichana wenye umri mdogo. Ukiwauliza wananume wengi, wanafahamu sana tatizo hili la kudanganywa umri.

    ReplyDelete
  6. Mfalme Mrope, nipe muda nitakujibu swali lako la Kizushi....

    ReplyDelete
  7. Hapo kipindi cha Mwanangu aliniuliza, Kwani mama mtoto anaingiaje tumboni? akimaanisha mimba. Nikamwambia kutoka kwa mganga hospitalini. Akanijibu kwa mshangao..,oooh! Kumbe si kweli kwamba anatoka kwa Mungu.
    Sasa na mimi kwa kuona jibu lake ndio bora zaidi nikamwambia kwanza anatoka kwa Mungu halafu ndiyo daktari.

    Haya wadau uongo huo vipi? Mtoto wa chini ya miaka kumi anakuuliza hivyo.

    ReplyDelete
  8. Mada hii ni pana ni bora ikajadiliwa kwa vifungu. Kusema uongo ni kinyume cha ukweli.Kwa waumini wa dini zetu wanasema msema kweli ni mpenzi wa Mungu, Hivyo uongo ni dhambi.Wakristo wanaambiwa The truth will set you free,yaani ukweli utakukomboa.Na ipo misemo mingi ya kutetea ukweli kama speak the truth and ashame the devil.Hivyo kuhalalisha uongo kwa namna mmoja au nyingine ni dhambi.Mahakamani unaapa kutoa ushaidi wa kweli,na ukweli mtupu(the truth and only truth).Achana na uongo wa kila aina ni kosa

    ReplyDelete
  9. Da Mija wewe kweli mwanamke wa shoka mpaka ukathubutu kujibu swali hilo. Mie nimekuwa nalikwepa sana kwani sikujua niseme nini? Ila nakumbuka nilikuwa mdogo, ilikuwa hivi mama yangu alikuwa na "kipaji" cha kupata watoto wa kiume tu na mimi nilikuwa mtoto wa kike pekee na kila akiwa na mimba siku za kujifungua zikifika alisema sasa nakwenda kununua mtoto na mimi nikwa nasema "mama safari hii huwezi kununu mtoto wa kike na mama alinijibu sawa, aliporudi cha kwanza nilichofanya ni kuangalia ni mtoto gani mara hii tena alikuwa mtoto wa kiume na nikamuuliza uliniahidi kununua wa kike sasa vipi na yeye alinijibu ya kwamba watoto wa kike walikuwa na bei sana au alisema alikuta wamekwisha na akaamua kununua wa kiume tena. ikawa hivyo hivyo. Je? mama yangu alifanya kosa kutoniambia ukweli kuwa watoto wanatoka wapi?

    ReplyDelete
  10. kwa swali la Damija, wewe ni mwongo, ilibidi umwambie atajua akikua, au ni mambo ya kikubwa au umwambie ukweli kwamba mkijifungia chumbani kuna nyakati huwa anasikiia mikiki mikiki na miguno, hapo ndo mtoto aja

    ila kuna ishu moja, mke wa jamaa alikuwa safari, sasa jamaa aamka asubuhi na mapema kuwaandaa watoto waende shule, katoto kakaona pensi imetuna na kumuuliza 'vipi baba umejigongo? Hapana! mbona hapo chini pamevimba (tuna)? sikumbuki alijibuje

    kuna nyakati uongo ni muhimu hata Yethu aliwahi sema yeye sio mesia

    ReplyDelete
  11. Nikigundua umeniongopea basi nakuwa sikuamini kwa kila jambo kwa sababu naamini kwamba wewe si mkweli kwa kila kitu
    Nikiwa nina shida nitashindwa kukuomba msaada na pia ukiwa na shida nitashindwa kukusaidia kwa sababu nitajua unaniongopea tu

    ReplyDelete
  12. uongo unamwisho na mwisho wake ni kuumbuka lakini pia naungana na wambula uongo ni hulka ya mtu...

    ReplyDelete
  13. ni kweli uongo sio mzuri ila kuna saa unahitajika sana tuu kwa wasoma biblia si mnakumbuka kilichompata samsoni baada ya kusema ukweli?

    ReplyDelete