Friday, February 12, 2010

Ulanzi ukiwa mwingi ngono huwa nje nje!!

Unywaji wa pombe ya ulanzi unadaiwa kuwa chanzo cha kuongezeka kwa maambukizi ya Ukimwi Iringa!!

"KARIBU mchumba, karibu unywe ulanzi, unataka mtogwa (uliogemwa leo) au mkangafu (wa siku nyingi)? Njoo ukae nami hapa usiogope! Mama Anita, lete lita moja fanya haraka mrembo asije akaondoka," hivyo ndivyo nilivyopokewa katika klabu cha pombe cha Ndiuka, Iringa.
Nilikwenda kufanyia kazi utafiti wa wataalamu unaosema kuwa moja ya sababu zinazochangia kasi ya maambukizi ya Ukimwi katika Mkoa wa Iringa ni ulevi hasa wa pombe za kienyeji.
Mmoja wa wauzaji wa pombe hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe anasema wakati wa msimu wa pombe ya ulanzi, wanywaji wengi hushindwa kuzuia tamaa zao za ngono na kujikuta wakijiingiza katika vitendo hivyo bila kinga.
"Ulanzi ukiwa mwingi ngono pia huwa nje nje! Ndiyo maana msimu wa ulanzi ukiisha tu wanawake wengi huwa na mimba zisizotarajiwa. Ulanzi ni hatari, unasababisha watu washindwe kujizuia na hatuwezi kuuacha kwani ni asili yetu," anasema.
Pombe hiyo iligunduliwa wakati wa utawala wa machifu wa kabila la Wabena katika Wilaya ya Njombe baada ya mti mchanga wa mwanzi kukatika na kuanza kutoa maji matamu.
Tangu wakati huo, pombe hiyo imekuwa ikithaminiwa na wakazi wa Mkoa wa Iringa na tayari imeshambaa na kufika katika maeneo mengine mengi hasa kusini mwa Tanzania.
Wanywaji wengi wa ulanzi wanasema bila shaka kwamba pombe hiyo inachangia kasi ya Ukimwi.
"Msimu wa ulanzi huwa unauzwa bei rahisi ambayo hakuna inayemshinda ndo maana watu wengi hulewa hivyo kuwa rahisi kwao kufanya ngono bila kujiandaa kwani wanawake wengi wakishanunuliwa kinywaji hicho huwa wepesi kukubali," anasema Richard Mwenda.
Mtaalamu wa magonjwa ya ngono mkoani Iringa, Dk Paul Luvanda anasema pombe hiyo ndiyo kichocheo kikubwa cha ngono zembe hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa maambukizi ya Ukimwi.
"Ulevi hasa wa pombe ya ulanzi unachangia kuongeza hamu ya kufanya ngono zembe, wengi wamejikuta wakipata maambukizi kutoka na pombe hii ambayo inaheshimiwa na wenyeji," anasema Dk Luvanda.
Ulanzi siyo kichocheo pekee, Luvanda anataja mila na desturi potofu ambazo jamii nyingi mkoani humo bado inaziendeleza. Miongoni mwazo ni kurithi wajane, kukosekana kwa usawa kijinsia, kutakasa wajane na wasichana, kuoa wake wengi, imani za kishirikina na kutotahiri.
Nyingine ni umaskini wa kipato. Maisha ya wananchi wengi ni duni.
Anasema kutobadili tabia licha ya elimu ya ukimwi kuwafikia wananchi na wengine kuathiriwa kwa njia moja au nyingine na Ukimwi ni miongoni mwa sababu za kuenea kwa ugonjwa huo.
Anataja sababu nyingine kuwa ni muingiliano mkubwa wa watu kutokana na shughuli nyingi za biashara na ongezeko la taasisi mbalimbali mkoani humo.
Hali ya maambukizi ikoje?
Dk Luvanda anasema watu 17,555 kati ya 71,628 waliojitokeza kupima kwa hiari kati ya Julai 2008 hadi Juni 2009, walikutwa na maambukizi ya VVU. Hali inayoonyesha kwamba maambukizi yameongezeka na kufikia asilimia 24.5 hali ambayo ni hatari.
Anasema kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa hali ya ukimwi kitaifa mwaka 2003/2004, maambukizi yalikuwa asilimia 13.4 na mwaka 2007/2008 yakapanda na kufikia asilimia 15.7.
"Utafiti unaonyesha Iringa tupo asilimia 24.5, hii siyo hali ya kawaida hata kidogo." Anasema Wilaya ya Makete inaongoza kwa kuwa na asilimia 35.9, Njombe 31.9, Iringa 30.5, Mufindi 24.0, Manispaa 23.5, Ludewa 18.6, Njombe mjini 21.1 na Kilolo 12.2.
Hadi Juni 2009, wananchi walioandikishwa kweny mpango wa dawa za kupunguza makali ni 51,137 na walioanza kutumia dawa hizo ni 25,703.
Wakati maambukizi ya Ukimwi mkoani Iringa yakiongezeka kwa kasi, takwimu za kitaifa zinaonyesha kuwa yamepungua kutoka asilimia saba mwaka 2003 hadi asilimia 5.8 mwaka 2007.
Hiyo ina maana kwamba Mkoa wa Iringa ndiyo wa kwanza nchini kwa kuwa na kiwango cha juu kabisa cha maambukizi, ukifuatiwa na Dar es Salaam yenye asilimia 8.9 na wa tatu ni Mbeya yenye asilimia 7.9.
Kutokana na kiwango hicho cha maambukizi mkoa unakisiwa kuwa na watu 246,935 wanaoishi na VVU/Ukimwi kati ya wakazi wake wote zaidi ya milioni 1.5 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2002.
Idadi ya watoto yatima nayo imekuwa ikiongezeka siku hadi siku kutokana na wazazi wengi kupoteza maisha. Watoto 67,915 wameshatambuliwa na 30,303 wanapatiwa misaada ya chakula, mavazi, malazi na elimu.
Mkoa unafanya nini?
Kupaa kwa takwimu za maambukizi ya Ukimwi kunaonyesha kuwa jitihada mbalimbali zinazofanywa na mkoa huo kupambana na janga hilo zimegonga mwamba.
Hata hivyo, Dk Luvanda anasema umeandaa mkakati wa kupambana na kasi hiyo ulioanza kutekelezwa tangu mwaka 2008 utakaomilika Septemba 2012 ukilenga kupunguza kasi hiyo kwa asilimia 50.
Anasema tayari Sh1.8 bilioni zimeshatumika kuanzia Juni 2008 hadi June 2009. Kati ya fedha zilizotumika, Sh953.9milioni ni kutoka serikali kuu wakati Sh870.1milioni ni michango wa wadau mbalimbali wanaoshiriki katika mapambano ya Ukimwi Iringa.
Dk Luvanda anasema Wilaya ya Makete ilitumia Sh 942.5milioni, Ludewa 150.7milioni, Manispaa 22.2 milioni, Iringa Vijijini 116.2 milioni, Kilolo 54.6 milioni, Mufindi 442.6 milioni na Wilaya ya Njombe ilitumia Sh114.8 milioni.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Ezekiel Mpuya anasema mkakati huo ni mwendelezo wa utekelezaji wa mapambano dhidi ya Ukimwi katika halmashauri za wilaya na kuwa umeandaliwa kwa kuzingatia vipengele vilivyomo katika Mkakati wa Pili wa Taifa wa Mapambano ya Ukimwi (NMSF) wa mwaka 2008 hadi 2012.
Mpuya anasema mpango huo umezingatia pia ushirikishwaji wa wadau mbalimbali walio katika mapambano ya Ukimwi mkoani Iringa, pamoja na maelekezo ya wataalamu wa ndani ya mkoa na taifa.
Anasema mipango iliyoibuliwa inatekelezwa katika kipindi cha mwaka mmoja mmoja na kutathminiwa kila mwaka kisha kuendelezwa na mipya kuibuliwa kulingana na matokeo ya tathmini.
Anasema huduma za tiba zinatolewa katika hospitali 16 zilizopo mkoani Iringa na vituo vya afya 14 kati ya 26. Lengo ni kufikia vituo vya vyote.
Ili kufikia lengo hilo, mkoa unatekeleza mikakati minne ambayo ni pamoja na kutoa huduma za majumbani kwa wagonjwa wa Ukimwi, tiba na huduma muhimu kwa wagonjwa wa Ukimwi na watu wanaoishi na VVU, kuanzisha mapambano dhidi ya Ukimwi sehemu za kazi katika sekta ya afya na kutoa misaada mbalimbali kwa watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mohamed Abdulaziz anatilia shaka takwimu hizo. Anawataka wataalamu kukaa upya na kuzitafiti ili kujua kama kweli ni hali halisi.
“Pamoja na mikakati yetu, wataalamu kaeni mfanye utafiti upya tujue kama kweli hizi ndizo takwimu au siyo na kama ni kweli, kuna kila sababu ya kutangaza hali ya hatari kwa mkoa huu,†anasema
Wananchi wanasemaje?
Wakazi wengi wa Mkoa wa Iringa wanataka mashirika yasiyo ya kiserikali kuendelea kutoa elimu ya ukimwi na kuhakikisha kuwa misaada na fedha zinazotolewa kwa ajili ya janga hilo zinawafikia walengwa.
Lakini wanashangazwa na kitu kimoja. Ikiwa wengi wanalalamikiwa kwa kufanya ngono zembe baadhi ya maeneo hayana kondom na mengine watalaamu hawajawaeleza kinagaubaga juu ya matumuzi na umuhimu wake
IMEANDIKWA NA TUMAINI MSOWOYA WA GAZETI LA MWANANCHI LA TAREHE 15/1/2010
Ijumaa njema wapendwa na kumbukeni kupunguza ugimbi(ulanzi= ulasi)

12 comments:

  1. Sina ukakika kama Ulanzi! Pingu!, Safari! Olvi! zote ni ubatili kama ulivyo UFISADI :-(

    Kama kondomu haziko ama ziko na hakuna wa kuzitumia, unadhani sheria zetu tulizo nazo zinakidhi mahitaji ya kuondoa umaskini Tanzania na kuwezesha ile 'sera mfu' ya MAISHA BORA KWA KILA MTz kutimia?

    Bwana mkubwa alisema zamani 'usipokuwa mwaminifu katika madogo makubwa utayaweza?'

    Je unadhani pia kuwa UKIMWI ni tatizo ama tatizo ni sisi wenyewe?

    ReplyDelete
  2. Ulanzi, ulasi kwa Kibena. Nakubaliana nawe da Yasinta. Wakati fulani nilifanya kazi na taasisi isiyo ya kiserikali mkoani Iringa. Nikapelekwa Lupembe huko Njombe. Moja ya mambo tuliyojifunza huko juu ya sababu za maambukizi ya UKIMWI ni pombe ya ulanzi. Wao wanywaji wanadai huwa inakimbilia 'chini'
    Maana yake inastimulate hisia.
    Na ukitazama maeneo yanayoongoza kwa ngono zembe mkoani Iringa, ni yale yenye kupatikana ulanzi kwa wingi.
    Ni hayo tu.

    ReplyDelete
  3. Papa Fadhy, wakati fulani napingana na dhana kuwa POMBE INAKIMBILIA CHINI! :-(

    Kama ingekuwa kweli hujawahi kushangaa kwa nini viongozi wakuu wa serikali wanakimbizana kuwekeza (kwa maisha ya baadaye) ilihali serikali itamtunza mpaka akufe (makazi, afya, usafiri nk) na majority kati yao wana watoto machizi ambao hawawezi ku-handle hiyo mali wanayolimbikiza baada ya wao kufa? :-(

    ReplyDelete
  4. NIMEFURAHI sana kuona kuwa unaendelea na kuhabarisha watu kwa njia mbalimbali big up sana remember wanasaikolojia kama vile Skinners, Edward Thondike na Ivan Pavlov wanasema stimula lead responses kwahiyo big up sana

    ReplyDelete
  5. Kuna msemo unasema Beer help ugly people to have sex.

    Wengi wamejikuta wakifanya mapenzi baada ya kulewa. Wachambuzi wa mambo ya mahusiano wadai kuwa hiyo ni sawa na kubaka ama kubwaka.

    Zaidi nchini Uingereza wapo mbioni kupitisha sheria ya unywaji pombe na mapenzi. Sheria hiyo zaidi inalenga kupunguza ngono zinazotokana na unywaji pombe. Sehemu moja ya sheria hiyo inasema " Iwapo utafanya mapenzi na mwanamke aliyekunywa bia tatu, utakuwa umembaka"

    Pengine Halmashauri ya Manispaa ya Iringa itunge by-laws za kupunguza unywaji wa ulabu, ili kupunguza maambukizo ya Ukimwi

    ReplyDelete
  6. Kaka Chacha juu ya ulanzi kukimbilia chini si maneno yangu. Tulifanya utafiti tulikwenda vijiji sita vya kata ya Lupembe. Nimeshaanza kuvisahau majina. Lakini nakumbuka kuna Ihangana, Igombola, Lupembe yenyewe na vingine. Asilimia kubwa ya vijana walisema wanapata hamu sana ya kufanya ngono wakiwa kwenye vilabu vya ulanzi. Pia wasichana wakiwa bwii na ulanzi wanakosa assertiveness ya kusema no.
    Kuhusu viongozi, hako ni kaugonjwa sugu kwao.

    ReplyDelete
  7. Yasinta wewe ni mpiganaji mzuri, ninakufurahia na ninakupenda, pamoja na kuwa upo ughaibuni lakini unapenda sana nyumbani. Tunahitaji watanzania wote walio nje wawe kama wewe.

    Kwa ukweli kabisa tatizo la Elimu ya UKIMWI ni mtihani mzito kwa Taifa letu hasa katika maeneo ya Vijijini. Ulanzi ni moja tu ya sababu lakini kikubwa ni elimu yenyewe. maeneomyote wanayoendekeza saba pombe ndio maeneo yanayoendelea sana kuwa na maambukizi makubwa kwa sasa. Mkoa wa Iringa wanaendekeza sana Pombe, Kule Ruvuma, Wilaya ya Songea Vijijini wanakunywa sana Ugimbi (Pombe), Dar es Salaam wanakata sana Masanga (Vileo), baa kama miche ya mpunga kwenye majaruba! zilivyobanana!

    Maeneo hayo yanatisha kwa Ngoma kwa sasa, na Dar kama sikosei inashika nafasi ya pili! Pombe ikishapanda kichwani ni mtihani, msichana hata kama sauti inakwaruza ama nzito kama Umurheri wa DW, unaona kama ya Celine Dion, Mwanaume hata kama ana majeraha ya mapanga usoni na sura mbaya kama KingKong anaonekana kama Will Smith basi shida tupu! Wakisha bebana umuhimu wa Condom unachukua nafasi ya 12!! Labda akikumbuka kuvaa basi hata utaratibu wa kusex ili kusitokee na madhara ya kuvuka au kupasuka Condom unakuwa haupo!

    Mipango ni mingi, takwimu kila wakati zinatolewa, lakini ukweli ni kwamba ongezeko hilo la UKIMWI na matakwimu hayo mazito mazito Mkoani Iringa ama popote palenchini ni faraja kubwa kwa mafisadi. Mafisadi wametega mabomba makubwa ya kunyonyea kupitia tatizo hilo, wamekuwa wakichota hela nyingi sana za sSewrikali, na wahisani kwa madai ya kupambana na UKIMWI, kwa madai ya kuhudumia yatima na waathirika, kwa madai ya kuendesha upimaji nk.

    Ikiwa kweli Srikali Kuu ina nia njema na watu wake, ina nia njema na Taifa kuna kila sababu ya kuwa na mkakati maalumu wa kuhakikisha NGO na taasisi zote zinatumia fedha kwa makusudio halisi. Kama ni kutoa elimu basi elimu itolewe, kama ni kuhudumia basi huduma zipatikane.

    Mkuu wa Mkoa hana sababu ya kuhoji kwasababu wanaotoa takwimu hizo wanachunguza nchi nzima kwanini ahoji kuhusu mkoa wake? ina maana hao watoa takwimu wana ugomvi na Mkoa wa Iringa. Anachotakiwa yeye ni kuingia kwenye vita na kuweka mikakati mizito.

    Inafika wakati inahitajika mikakati mizito hata kama itawakosesha raha watu, hili ni janga na watu wasitmatatizo ya wenzao kujineemesha. Hii ni sawa imetokea ajali badala ya kuokoa unaanza kupekua mifuko ya majuruhi na wlikufa uchukue kilichomo. Kama kipindupindu mama lishe wanamwagiwa chakula kwanini UKIMWI uisiwekewe mikakati mikali.

    Kama Serikali haina washauri wa mikakati gani itumike, wengine tupo tunaolipenda taifa letu, hata bure tuko tayari kufanya kazi ya kuishauri Serikali juu ya nini kifanyike.

    ReplyDelete
  8. kwa hiyo wajameni mtakubaliana nami kuwa tatizo si UKIMWI bali ni SISI wenyewe sivo?

    Kwa kuwa kama unajua kama ukilamba ugimbi CHINI kunaita na kuitika kwa nini uwende huko ilihali unajua huna mwenza ama unamuacha mwenza wako kunyumba?

    Aaagh! :-( Pengine sheria anayoipendekeza mkubwa Kibunango inatakiwa japo nina wasiwasi kama kutakuwa na mabadiliko ama yatatokea polepole

    kwani hamjaona waelimishaji wa uzuiaji maambukizo na magari yao DFP/STK yakiwa yamepaki katika vilabu hivyo wanagida ulabu? :-(

    ReplyDelete
  9. Watu wa Iringa wasifikiri wanasemwa wao tu, Kitu chochote kinachoitwa pombe, hupumbaza kama kikitumiwa kupita kiasi. Na mara nyingi huleta msukumo wa masuala ya ngono zembe

    ReplyDelete
  10. Ama kweli kila kabila linamambo yake ya hatali,hivi kuna ile pombe ya komoni yenyewe asili yake ni wapi?gongo je nayo inanywewa sana mkoa gani?zamani nilikuwa najua chibuku ndio ilikuwa maarufu sana Dar,lakini miaka ya hivi karibuni nazani gongo ndio imeshika nafasi ya chibuku,ukimuona mtu kalewa sana mitaani utasikia watu wanasema gongo hiyo alizani maji? kule kwa wenzetu utasikia Lubisi,kuna wengine utasikia mbege kila sehemu na mambo yake,haya Yasinta tujuze mwenzetu wajua mengi zaidi.

    ReplyDelete
  11. Huu ulanzi tulikuwa tunaunywa Mbeya miaka ya 97 - 99, ulikuwa utatu save sana wanachuo na bajeti zetu finyu, ukimaliza kunywa basi juu yake unaweka na safari lager moja (aka mbuyu)

    ReplyDelete
  12. Tulipokuwa high school Iringa, mwalimu alipofikia topic ya probability alikuja na swali moja la kutufanya tuvutiwe sana: "When do people enjoy themselves most?" aliuliza. Na akajibu "Of course, during ulanzi time." Halafu akaendelea kukokotoa sasa probability ya grafu ya kuzaliwa kwa watoto katika mwaka. Sasa tuta-calculate maambukizi!

    ReplyDelete