Wednesday, November 11, 2009

JE UPWEKE NI UGONJWA?/ UPWEKE

Wapendwa posti iitwayo JE UPWEKE NI UGONJWA hii niliandika 27/8/2009 naomba kama hukusoma basi ipitie ndo utajua kwa nini nimeweka shairi hili la kaka Fadhy Mtanga.

Upweke

Upweke jama adhabu, upweke unasumbua,
Upweke ni maghilibu, kukufanya kuugua,
Watamani wa karibu, nenolo taelijua,
Upweke.

Upweke hutesa sana, umpendaye awe mbali,
Utamuwazia sana, hata mara alfu mbili,
Kwa usiku na mchana, maumivu ni makali,
Upweke.

Upweke unakondesha, chakula hukitamani,
Upweke unahenyesha, simanzi tele moyoni,
Homa pia hupandisha, na mwokozi humuoni,
Upweke.

Upweke tele mateso, hata machozi kulia,
Moyoni ni manyanyaso, nao moyo kuumia,
Wala si kimasomaso, kwani huleta udhia,
Upweke.

Upweke ni kama jela, huleta nyingi simanzi,
Huwezi hata kulala, maisha tele majonzi,
Utapiga hata sala, uruke vyote viunzi,
Upweke.

Upweke sawa na shimo, mtu ukatumbukia,
Nako shimoni uwamo, wateswa nayo dunia,
Kwani hauna makamo, kuweza kuvumilia,
Upweke.

6 comments:

  1. da yasinta, ahsante kwa shairi. nilipoliandika sikujua kama lingegusa wengine kiasi hiki. Ni kweli upweke ni jambo linalohuzunisha mno.Mungu hakupenda mwanadamu awe peke yake. Soma Mwanzo 2:18 'BWANA Mungu akasema, si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.'

    ReplyDelete
  2. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!November 11, 2009 at 10:31 AM

    Yawezekana lakini inategemea na mtizamo...lol

    Kitu hakiwi kweli mpaka umekitafsiri hivo...lol

    Kwa hiyo inawezekana upweke uko mawazoni mwa mtu hisika na siyo reality...lol

    sorry kama nimewaboa lakini habari ndo hiyo....lol

    ReplyDelete
  3. nategemea ni upweke wa nini kwani kwenye vyakula kuna wenye njaaa na kwenye watu wengi, kuna waliopeke yao

    ReplyDelete
  4. Upweke sio ugonjwa, ila unaweza kusababisha ugonjwa.

    ReplyDelete
  5. Kaka Mtanga umegonga pointi, upweke haufai.

    ubarikiwe.

    ReplyDelete
  6. Fadhy shairi lako limenigusa sana na asante kwa maoni.

    Chacha sijui nini na nini! Inategemea :-(

    Kamala ! upweke ni upweke.

    Chib! ni kweli upweke unaweza kusabisha ugonjwa na ni hatari Ahsante Chib.

    Da Mija Hata mie niliona hivyo kuwa kaka Mtanga kagonga ndo maana nikaona niweke hapa kuwakumbusha watu. Na kweli kaka Mtanga Ubarikiwe. Na Ahsanteni wote kwa kutochoka kutembelea kibaraza hiki.

    ReplyDelete