Thursday, October 1, 2009

KAZI YA UALIMU: TAALUMA MUHIMU ILIYODHARAULIWA

Mwalimu akiwa darasani anafundisha

Katika maisha yangu nimeishi na walimu sana . Kwa hiyo nimekuwa nikijiuliza miaka yote hii mingi. Na nimekuwa nikipatwa na uchungu sana nionapo watu/serikali jinsi inavyoiona kazi ya Ualimu kama isiyo na maana. Kila nikijaribu kufikiri, kazi zote hapa duniani naona hakuna kazi ngumu kama UALIMU.

Fikiria mtoto aanzapo shule hajui kuandika, kusoma wala kutamka a, e, i, o, u. Lakini mwalimu anahenya kwa kila njia na baada ya muda mtoto anaweza kusoma kuandika kutamka silabi zote bila shida kama mtoto si mgumu kuelewa. Na hii sio walimu wa shule ya msingi tu ni kuanzia chekea (vidudu) kule ndio kuna kazi kubwa zaidi.

Kwa nini walimu wanadharauliwa na pia mishahara yao ni midogo sana. Kwa kweli inatia huruma. Mshahara wa kima cha chini Tanzania hivi sasa ni laki moja kwa kweli hii ni halali?

Ni juzi tu nimesikia ya kwamba idadi ya wanaoomba kusoma ualimu hapa sweden inapungua kwa kiwango kikubwa sana. Sijui huko tuendako kutakuwa na walimu. Na pia kuna kupunguzwa walimu katika kila shule watapunguzwa walimu 14. Sasa mbaya zaidi wanawapunguza walimu vijana na wazee wanaendelea kufundisha .

Awali nilidhani matatizo ya Waalimu labda ni kwa nchi za Africa pekee, lakini nilipokuja hapa nchini Sweden, ndio nikajua kuwa hata hapa matatiozo ni yale yale, yaani yanafanana kwa kiasi cha kikubwa sana. Kwa hapa Sweden walimu wanateseka sana na pia hawaheshimiwi kabisa. Wanafunzi wana dharau sana wanawaona waalimu kama ni watani wao, wanajibizana nao, na wakijaribu kuwaelimisha jambo ni wabishi ajabu, na kuwaadhibu kwa viboko hapa nchini Sweden ni makosa. Hapa hakuna viboko kabisa kwa hiyo kiboko ni maneno tu. Tena maneno yaenyewe inabidi yawe mazuri na ya unyenyekevu. Na kama Mwalimu akijaribu tu kupandisha sauti kumkaripia mtoto anaweza akachukuliwa hatua kali za kinidhamu na anaweza hata kupoteza kazi yake.

Kuhusu swala la mshahara:- Kima cha chini cha mshahara wa mwalimu hapa nchini Sweden ni 3,600,000TSh, kwa pesa ya hapa ni 20,000SEK. Kiasi hicho cha mshahara kwa huko nyumbani Tanzania unaweza kuona ni kiasi kikubwa sana, lakini ukilinganisha na maisha ya hapa ni pesa ndogo sana na usipokuwa makini unaweza kushindwa kumudu baadhi ya ghrama za maisha. Hebu angalia mchanganuo wa makato ya huo mchahara pamoja na matumizi ya lazima, kodi kwa ujumla anahitaji kulipa 1,200,000TSH. Baada ya hapo zinabaki 2,400,000TSH. Chakula, bili n.k ni kama 10,000SEK = 1,800,000TSH. Baada ya hapo zinazobaki kabisa ni kama 600,000TSH. Kwa kiwango cha gharama za maisha ya hapa Sweden, bado pesa hiyo ni ndogo sana.

Kwa kweli waalimu wanayo kazi kubwa, lakini mapato madogo wakati kazi ya ualimu ni nzito na ndio mwanzo wa watu kujua kusoma na kuandika. Bado najiuliza, hivi kwa nini waalimu wanadharauliwa kwa kazi hii ngumu ya kuelimisha.?

11 comments:

  1. Cha ajabu mtu maarufu kuliko wote Tanzania alikuwa anaitwa Mwalimu Nyerere!Na inasemekana ndiye aliyeweka muelekeo wa nchi katika kilengeo kilicho tuweka hapa sasa hivi Tanania kama Nchi!:-(


    Umestukia jinsi kulaumu wengine ilivyokuwa tamu?

    ReplyDelete
  2. Sikuwa najua na huko walimu wanapimiwa mshahara (kidogo), nafikiri ukimwambia mtu wa Songea kuhusu huo mshahara ataona huko ndio peponi, maana hana habari na mambo ya makodi makubwaaa

    ReplyDelete
  3. Da Yasinta, naomba unitafutie kazi ya ualimu wa chekechea huko...lol!!

    kazi ya ualimu inasahaulika kwa kuwa hakuna jambo la maana analofanya katika nji hii...akishakufikisha kwenye u-profesa (samahani matondo na mbele) hana maana tena. Angalia maprofesa wetu walioko wizara za elimu. wakati fulani wanafunzi waliomba waongezewe mikopo.

    waziri ambaye amesoma kwa jasha na mikopo ya walala-puuu akasema hakuna mikopo saidi!!!

    halafu wazazi wetu hatutaki watoto wetu wenye akili wasomee ualimu badala yake tunataka wale ambao wame-feli...utamsikia kamala anamwambia mwanaye...'yaani umefeli fomu foo/siksi? yaani hata ualimu umekosa?'

    hatujawa na mifumo ya kuwaenzi watu hawa

    ReplyDelete
  4. Kinyume na huko Sweden walimu hapa Marekani naweza kusema wanaheshimiwa na jamii na mishahara yao siyo mibaya sana (pengine dola 50,000) kwa mwaka (miezi 9) kutegemea na jimbo. Matatizo ya watoto hata hivyo ni yale yale kama ya hao wa huko Sweden - hakuna adabu, heshima - kila mtu kivyake vyake na tineja akikasirika basi anakwenda kuchukua bunduki ya baba yake anakuja ili myamalize "once and for all". Kufundisha High school hapa ni kazi ngumu mno kwani hawa ni matineja na ni watukutu hujaona. Kwa miaka 7 niliyofundisha chuo kikuu hapa sijaona matatizo makubwa sana ukiachilia mbali matatizo madogo madogo kama wanafunzi kukaa wazi madarasani na mengineyo....

    Kwa Tanzania kuna ule msemo wa "Ualimu ni wito" na pengine serikali inauchukulia ualimu kama kazi ya kujitolea tu ambapo mtu unalipwa kiposho kidogo cha kujikimu na siyo mshahara ambao utakusaidia kuendesha maisha yako.

    Kuna kipindi walimu wa shule za msingi walitishia kugoma nchi nzima na waziri wa elimu wa wakati ule (nadhani alikuwa Profesa Philemon Sarungi) akasema kwamba kama wanataka kugoma ni sawa na yeye anaweza kuchukua watu wanaotembea mabarabarani waingie madarasani wakafundishe. Ndivyo mwalimu anavyoonwa. Huyu ndiye mwelimishaji wa jamii, huyu ndiye anatakiwa atoe madaktari, wahandisi na maprofesa. Anaweza kufukuzwa wakati wo wote na nafasi yake ikachukuliwa na "watu wa barabarani"

    Chacha - mimi naheshimu sana walimu kwani ndiyo msingi hasa wa ukombozi wa jamii.

    ReplyDelete
  5. Ili elimu iende mbele shurti ama sharti watoa elimu wawe wenye sifa za kiushindani.

    Mwalimu atafundishwa vizuri kama, haki zake zitalindwa (ikwemo mshahara mzuri), maslahi yake yatalindwa, na heshima yake pia,kwani ni rahisi kuendelea kiuchumi kama una watu waliosoma na zaidi ya yote ni rahisi kumuongoza aliyesoma na ni ngumu kumbuluza.
    kama tuna majinga tu tutaburuzwa na wanyonyaji.asante kwa mada kuhusu elimu ina mashiko.waende mbele walimu, iende mbele elimu.

    ReplyDelete
  6. Kisichodharauliwa nyumbani ni SIASA.
    Yaani haijalishi inawagharimu wananchi maisha na mali kiasi gani, itabebwa tuuu. Bungeni hawawezi kugoma kama bajeti ya elimu ni mbaya ila ulisikia msukosuko walipoonekana kugomewa kupandishiwa mishahara yao.
    Sijui ni kwanini tunaendelea kuziona hizi HESABU za kisiasa zinazokwenda kinyumenyue?
    Na ndio maana tunaona gharama za gari la m'bunge (ambalo Waziri Mkuu alisema ni sawa na matrekta 20) likiendelea kuwekewa oda wakati wakulima wanakufa njaa. Sijui gari hilo ni sawa na majengo mangapi ya wastani kwa ubora wa shule zetu? Sitoshangaa kuambiwa kuwa magari mawili ya wabunge ni sawa na shule moja (kidato cha kwanza mpaka cha nne na ofisi yake). Lakini walimu wanadharauliwa na kazi yao haiheshimiwi na matokeo yake ELIMU NZIMA INAKUWA IMEDHARAULIWA.
    Lakini hii ndio tanzania yangu, yenye kujenga ghorofa ikipuuza ubora wa msingi.
    Yaani inataka taifa lililo na elimu lakini haiboreshi maslahi na mazingira mazima ya uelimishaji na hata zana za kuelimisha.
    TUTAFIKA TUUUUUU

    ReplyDelete
  7. Unajua dada ..nashindwa kukuelewa...kama mwalimu napataa kr 20.000 za sweden halafu unasema maisha bado magumu kwakweli nashidwa kuelewa...manayake...sweden flat ni kr 6000 na chakula ni bei rahisi sana...hapo hapo doctor ni bure...kama ndugu zako wa kitanzania wanasafisha na kupta kr 15.000 or 10.000 na wakaishi..unataka kubniambia 20.000 kr ni ndogo..????
    Naona una cha kuandika......Tutaikimbia blog yako dada..
    Na ukiandika uweke ppia daraja la walimu.....siyo walimu wote wanalipwa mshahara 1....
    Tupo wote dada scandinavia

    ReplyDelete
  8. Habarini wadau,
    Mimi naona bora hata huko Sweden mwalimu anapokea mshahara matumizi yakiwa ya juu unaisha, na matumizi yakiwa mazuri unabakiza chenchi flani. Na uzuri ni kwamba kila mwezi una uhakika tarehe fulani kupokea mshahara.

    Kwa Tanzania kwanza mshahara ni mdogo, na mbaya zaidi hauna uhakika lini unatoka. Cha kushangaza wanasema ualimu ni wito, unakuta eti kuna malimbikizo ya mshahara miezi zaidi ya 6 hajapokea mshahara...huu ni udhalilishaji wa fani za watu na kutothaminiana kama wanadamu.Hivi ikitokea siku moja mshahara wa wabunge au mawaziri uchelewe nao ulimbikizwe kwa miezi 6 si patakua hapatoshi hapo?????

    MAKULILO, Jr.
    www.makulilo.blogspot.com
    San Diego, CA

    ReplyDelete
  9. Mimi baba yangu aliukimbia ualimu kungali mapema, akarudi shule kuongheza elimu na sasa mambo yamemnyookea, na kama angekuwa malimu.......Duh!!!!!!!!!

    ReplyDelete
  10. Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wote mliochangia mada hii. Nimejifunza mengi kupitia maoni yenu. Pia naomba mjadala uendelee "Ualimu ni wito" mmmmh watu bwana.

    ReplyDelete
  11. Dada yacinter hongera sana kwa kuwakumbuka walimu.Ni ukweli kabisa walimu hawathaminiwi lakini vipi wakutubi(librarians) ambao huwawezesha hawa walimu kupata nondo za maaana za kufundishia???????????? Hawa pia hawathaminiwi hata kidogo. Ni vyema serikali yetu na jamii kwa ujumla ikatambua umuhim wa walimu na hawa ndugu zetu wakutubi. Hawa ni watu muhimu sana katika jamii yetu jamani..... bila hawa tusingepata marais, mawaziri, wabunge, madaktari na wengine wengi. TUZINDUKE NA TUCHUKUE HATUA ZA KUWAJALI NA KUWATHAMINIWENZETU HAWA.

    ReplyDelete