Baada ya kuisoma barua hii nimeona si mbaya kama nikiiweka hapa ili wengi waisome na na tujadili kwa pamoja.
KUJIAMINI ni jambo la maana sana katika maisha ya kila siku ya mwanadamu. Kujiamini katika kila uamuzi unaofanya na kila kitu unachofanya ndio siri kuu ya mafanikio ya mwanadamu yeyote. Bila kujiamini, hakuna chochote utakachofanikiwa na kila siku utakuwa 'mtumwa' wa wengine.
Kujiamini ni muhimu na chachu ya maendeleo si katika maisha ya mtu binafsi tu, bali hata katika taasisi kama vile serikali, mashirika ya umma na mashirika binafsi. Ili taasisi au shirika lolote liendelee, ni lazima kuongozwa na wataalamu waliobobea na wenye kujiamini kwa maamuzi na matendo.
Sababu kubwa ya nchi yetu kuendelea kuwa masikini ni kuwa na viongozi wasiojiamini na kuendekeza utegemezi hasa kwa wazungu.
Viongozi wetu bado wanaamini kuwa wazungu wanajua kila kitu kinachohusiana na nchi kupiga hatua mbele kimaendeleo. Wanaamini kuwa wazungu ndio wenye kujua mbinu na mikakati ya kufuta umaskini katika nchi yetu. Hawaamini kama Watanzania wana uwezo wa kujiendeleza wenyewe bila kutegemea usaidizi wa watu wa nje.
Viongozi wetu wanadanganyika kirahisi wanapoona nchi nyingi za Ulaya na Marekani zimeendelea, hivyo wanadhani kuwa wazungu ndio 'mwarobaini' wa matatizo yetu, ndio maana wakati wote wanajidhalilisha wao wenyewe na sisi wananchi wao kwa ujumla kwa kuwapigia magoti wazungu kuwaomba 'watuendeleze.'Wanaamini kuwa wao pekee (wazungu) ndio wenye akili hapa duniani, na sisi ni kama ‘misukule’ tu!
Kila kukicha viongozi wetu na Afrika kwa ujumla wanapishana katika nchi za Ulaya na Marekani kwenda kuomba misaada, wanaamini kuwa bila misaada hawawezi kuendesha nchi zao, wamekuwa akina 'Matonya,' wanatembeza kibakuli. Sijui wameona nani au nchi gani duniani iliyoendelea kwa kutegemea cha kuomba.
Viongozi wetu wanawaheshimu na kuwanyenyekea watawala wa Ulaya na Marekani kuliko hata wananchi tuliowaweka madarakani, wanakubali kila wanaloambiwa na ‘mabwana wakubwa'hawa.
Kwa mfano, wakati ule walipoambiwa wayabinafsishe (wayauze) mashirika na makampuni yote ya umma kwa hoja eti serikali haiwezi kufanya kazi mbili, yaani kuongoza nchi na wakati huo huo kufanya biashara, walikubaliana na ushauri huo bila hata ya kuhoji au kuja kwa wananchi kutuuliza maoni yetu, wakaanza kuuza mali zetu moja baada ya nyingine, na walipomaliza kuuza hawakuja kutuambia wamepata kiasi gani cha fedha.
Lakini ukiwauliza leo kama tumeendelea baada ya kuuza mashirika na makampuni ya umma? Hawatakujibu kitu, watabaki wanakutolea macho tu ingawa jibu wanalo, lakini wanapata kigugumizi kulisema kwa sababu wanaona haya kwa kuwa walitapeliwa au waliingizwa mjini na wazungu.
Tazama, wakati huu wa tatizo la kiuchumi lililowakuta wazungu hawa hawa ambao tunawaamini kuwa ‘waganga’ wa matatizo yetu ya kiuchumi, wakati makampuni yao mengi yakifilisika, wanakimbilia hazina za serikali zao na kuchota mabilioni ya dola, pauni na euro za umma ili kuyaokoa, wanadai wanalinda nafasi za kazi kwa raia wao, sisi makampuni na mashirika yetu yalipotetereka, wakatuambia tuyabinafsishe (tuwauzie wao).
Tatizo letu kubwa ni kutojiamini. Na hili halipo kwa viongozi wetu tu, bali pia kwa wananchi wa kawaida. Wengi wetu tunaamini kuwa mzungu ni mweledi kuliko sisi, hatujui kuwa wazungu wengi ni mbumbumbu wa masuala mengi tu kuliko waswahili.
Ninachojaribu kusisitiza hapa ni Watanzania na Waafrika kwa ujumla kujitambua na kujiamini kuwa tunaweza kufanya mambo makubwa kuliko hata wazungu, katika kila nyanja ya maisha ya mwanadamu, iwe ni kiuchumi, kisayansi na hata kiteknolojia.
Ipo mifano hai ya nchi zilizokuwa taabani kiuchumi na kijamii kuliko hata sisi, lakini kwa kuwa walijitambua na kujiamini, walichukua hatua ambazo leo zinawafanya kuwa tishio dhidi ya wazungu waliotangulia kupata maendeleo ya kiuchumi, kisayansi na kiteknolojia.
Nchi kama vile China na India ni mfano wa kuigwa na nchi nyingine zinazoendelea. Wachina kwa sasa ndio tishio pekee dhidi ya Marekani kiuchumi, na wakati huu wa mparaganyiko wa uchumi katika Marekani na Ulaya, China imetwaa uongozi wa uchumi duniani na inalitumia kikamilifu tatizo hili kukwea katika kilele na kuipiku Marekani. Wachina pia hawako nyuma katika maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Mwasisi wa Taifa letu, hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere, alikuwa kiongozi pekee wa nchi hii aliyekuwa na nia na maono ya dhati ya kujinasua kutoka katika minyororo ya ukoloni wa wazungu.
Mwalimu alitaka Tanzania ijitegemee kwa kila kitu, ndio maana alianzisha siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, ambamo Watanzania tulishuhudia viwanda vya huduma mbalimbali vikijengwa nchi nzima.
Mtazamo wa mbali wa Mwalimu ulikuwa kuhakikisha kuwa ifike wakati Tanzania iwe na ‘viwanda-mama,’ yaani viwanda vya kuzalisha malighafi kwa ajili ya viwanda vingine, haya yalikuwa malengo thabiti ya kujitegemea.
Mwalimu alifanikiwa kwa sababu alikuwa kiongozi mwenye kujitambua na anayejiamini, na alitaka pia Watanzania wote wajitambue na kujiamini. Lakini kwa bahati mbaya waliompokea wawakuliona hilo.
Ndio maana miaka 24 imepita sasa tangu Mwalimu ang'atuke uongozi, lakini hakuna chochote walichoongeza, zaidi ya kuuza kila kitu tulichokuwa nacho na kujaribu kufisidi hata kile kidogo tulichobaki nacho.
Kwahiyo, kama kweli tunataka kuwa taifa huru na kukomesha ukoloni wa wazungu, hatuna budi kuchukua hatua sasa. Viongozi tuliowapa dhamana ya kutuongoza wanapaswa kutuongoza katika jitihada hizo za kujikomboa, vinginevyo tutaendelea kutawaliwa na wazungu
Na George Maziku, Sundsvall, Sweden toka gazeti la mwananchi
umesema vema mkuu
ReplyDeletebila kujitambua ni vigumu kujiamini na usipojitambua/jiamini, utadharaulika na kupangiwa na kuamriwa killa kitu maishani mwako au unabishi yasinta?
ReplyDeleteUmesema yote.
ReplyDeleteLakini tatizo la viongozi wetu siyo tu kutojiamini, bali pia ni ubinafsi na kutoona mbali.
tatizo la nchi zetu kwa mfano nichukulie mfano tanzania..ikiwa rais wetu mwenyewe anavaa suti zinazotengenezwa ufaransa,
ReplyDeleteje ataamini kweli kuwa hapa tanzania kuna watu wenye uwezo mkubwa tu wa kushona suti?
ikiwa jambo dogo kama hilo linapewa kupa umbele ulaya.ijekuwa kuwaamini wa tz kuwa wana uwezo wa kufanya kazi,wakabuni mbinu mbali mbali,wakajenga barabara.ikiwa wamewezeshwa..ana diriki kuwaamini wahindi?..tatizo letu ni serikali bado ina mtazamo wa kimaskini
Fadhy. Hapo umenena. Pia kuna wengine ni ufinyu wa mawazo.
ReplyDeleteKujiamini sawa, lakini pia ni kuwa na true consciousness (ambako ni zaidi ya kujitambua), hii itawezesha wanyonywao (exploited- sisi watawaliwa) kuungana na kuwafanyia kweli wanyonyao (exploiters- wakoloni- hususani wazungu. Wengi bado wana false consciousness ndo maana hakuna jitihada za kujikomboa toka makucha ya kutawaliwa!
ReplyDeleteRangi nyeupe inatawala kila sehemu si kwa Africa tu hata kwa waarabu wenye petroli na utajiri bado wanatawaliwa na wazungu.
ReplyDeletemwanasociolojia true consious ni hatua ya juu kabisa ya kujitambua
ReplyDeleteKwa viongozi imetokea ikawa hivo si kwa bahati mbaya bali ili mjue wao ni watu wa aina gani...lol
ReplyDeletena sisi tunaowachaguwa hao viongozi ndo tuko katika mawazo na mitazamo hiyohiyo...lol
As you think ...so you are....lol pengine waTZ wote tunapenda ufisadi ndo sababu tunachaguwa mafisadi...lol
Habari ndo hiyo...lol
Utajiaminije wakati hujui unajua, na kuwa pia hata umlengaye kwa kufikiri anajua ili akufundishe, kuwa ukweli ni kwamba hajui?
ReplyDeleteCHA KUSIKITISHA ni kwamba hata wajuao hawajui na WANAJUA wajuacho NI wasichokijua wanataka wakijue, sio wote wanajua jinsi ya kukijua WASICHOJUA , ndio maana pia TUNA wenye akili maprofesa wajingaPUMBAFU!:-(
Jamani sasa mimi niseme nini?
ReplyDeleteKila kitu mmemaliza. labda niseme tu kwamba bado waafrika tunayo safari ndefu sana ya kuelekea kujitambua.
Naamini sijachelewa sana, lakini nami nina mtazamo wangu.... ukweli ni kwamba sio viongozi wetu tu ambao hawajiamini,hata wasomei wetu hapa nchini hawajiamini pia, utakuwa mtu msomi na shahada zake kadhaa lakini anashindwa kutumia elimu aliyo nayo kujiajiri, na hata wale walio na vipaji vya uongozi nao wanogopa kujiunga katika siasa ili kuleta mabadiliko. na ndio maana wengine kwa kuogopa vivuli vyao wamekimbilia ughaibuni na kuchangia pato la nchi hizo badala ya kujiajiri hapa nchini na kuleta mabadiliko ya kiuchumi. swala la kutojiamini linamgusa kila mtu na tusiwalalamikie tu viongozi wetu kwani hata hao waliosababisha kufilisika kwa viwanda vyetu vya umma ni hhao hao wasomi wetu waliosomeshwa na fedha za akina bibi Koero, baada ya kulima sana kwa jembe la mkono......acheni hizo.....
ReplyDeleteKoero, Koero, Koero......Mhh!! mie naogopa hata kusema,,ina maan mimi na akina kaka Mubelwa Bandio, KItururu. Yasinta....No, hapana huyu ameolewa huko ughaibuni.. dada Subi, Na wengineo wengi tulioko ughaibuni, hatujiamini?
ReplyDeleteKaaaaazi kweli kweli
Mimi nadhani kinachokosekana ni UZALENDO, basi!
ReplyDeleteKama wananchi wanaelements za uzalendo, na kwa sababu viongozi wanatoka miongoni mwa wamanchi, ni dhahiri kuwa hata viongozi watakuwa wazalendo wa kweli.
Nchi kama China, watu wake wanasifika kwa uzalendo wa nchi yao, na bila shaka hili limewasaidia sana kwa hatua waliyoifikia ya kimaendeleo.
Nashukua nafasi hii na kuwashukuru wote kwa maoni yenu na nawaomba mjadala uendelee.....
ReplyDelete