Aaah wapi, mwisho wake lini mbona...
A-a-, mtani sikiza nikwambie, kwetu tumezaliwa ndugu kaka na dada, na kwa bahati, mzee wetu alikuwa na shamba lenye mali mingi, mifugo hene hene na ardhi yenye tuvimawe tudogo tudogo na thijakwambia tena tune visima vyenye maji chumvi na maji poa. Asa siku moja kadogo kangu 'Nkiki Iki' katundu sana hako, kakawa kanachimbua vijiwe na kwenda kuchezea mabento na watoto wa jirani zetu. Mzee 'Miiwi Alewode Soni', babake mtoto wa jirani, akaviona vile vijiwe, basi akamwambia Nkiki 'uwe unavichimbua na kuvileta muchezee halafu atakayemmanga mwenzie mi ntambadilishia nimpe gololi'. Ikawa ndo mchezo wao. Sa kumbe Mzee wetu akamstukia Nkiki ndo akamkamata Nkiki na siye wote akatuketisha chini akatwambia 'iwe marufuku kuchimbua vijiwe vile. Wakati wake bado na aliviacha kwa makusudi'. Ndiposa akatupa siri kuwa tule tivijiwe bwana kumbe mzee Miiwi (babake na mtoto wa jirani) alikuwa akivifanyia biashara Ng'ambo. Mzee akatwambia kuwa tule tujiwe tofauti na mazao ya nafaka, huwa hatuozi tule, hivyo hutwo utatufwaa sana kwa biashara tukishakuwa na akili mukichwa na ikiwa shughuli za mifugo ama nafaka itakuwa haikidhi mahataji yetu. Zaidi sana alitaka tujue jinsi ya kushirikishana na wadogo zetu na familia yetu yote ya baba mkubwa, mamdogo na shangazi hadi kijiji kiuzima tuviuze ili wote tuwe angalao na ubora fulani wa maisha. Aliamini hivyo kwa dhati marehemu Mzee wetu.
Mzee alituhenyesha kwenye elimu na akahakikisha tunasoma kweli kweli, yaani hata na wazee wenzie kijijini alihakikisha wanapelekwa shule kwa mwendo wa PUGU (Pata Ujuzi Gawia Umma). Lakini alitusisitizia pia kuwa elimu izingatie kilimo, mifugo, uvuvi na viwanda ghafi kwa sababu bado ni mali sana hivo, na vile vijiwe vibakie tu maana haviozagi hivo.
Kwa bahati nzuri ama mbaya, Mzee wetu aliugua na akafariki katika umri wa KiBiblia kama alivyojikadiria mwenyewe, sasa kumbe kaka zangu na dada zangu walikuwa wanamwonaga Mzee wetu mwanga na kauzibe flani katika mipango yao. Unaambiwa ile Mzee anakata roho tu, kwanza wao wakaanza na kuandaa zinga la sherehe kisha wakasherehekea kivyao kwa siri, alafu ndo wakaandaa bonge la mazishi na kwenye maziko wakihakikisha wanaweka sementi na kofuli kwenye kaburi la Mzee ili asijenyanyuka; si walijua fika kuwa makamuzi waliyopanga kuyafanya yanaweza kumwamsha Mzee kutoka ufuni?
Sasa mtani wewe ikiwa umeshawakalisha kaka zako na ndugu zako chini na ukawaita Wazee ili mzungumze kuhusu dhuluma wanazokufanyieni ninyi ndugu zao wa kuzaliwa damu moja wachilia mbali wale watoto wa shangazi, mjomba na kijijini, na Wazee waliokua na Mzee wetu hawasikiii, eeeh, yaani woooote ninyi mmegeuka kuwa ombaomba na hamjui kesho itakuwaje, eeeh, kaka zako na dada zako baada kusomeshwa na Mzee na kuachiwa urithi wamegeuka kuwa watoto wa mjini yaani siku hizi wao wanavaa kata-k, pullneck wananunua vitu supamarkiti, vekesheni udosini, watoto wao hawasomi tena Kamachumu, ninyi wadogo zao shule hamuioni na kama Mzee aliwaacha ndo mpo Sekondari mjue Chuo Kikuu mtaishia kukisikia tu, na kama mna watoto ndiyo hata haijulikani mliwazaa kwa sababu ipi, we unafikiri we uta...
..kwanza zamani si Mzee alikuwa anasema ni marufuku kufunga milango ya vyumba vyenu kwa kuwa sisi sote ni ndugu siri ya nini? Basi alipoitwa na Mungu tu, kaka zako na dada zako wamevuruga utaratibu siku hizi hata kupita korido ya nyumbani kwenu ni kwa mahesabu maana ukikaribia mlango tu ni kula mbata kwa kwenda mbele. Yaani umewekewa kauzibe huwezi kukaribia hata kizingiti cha chumbani labda uwe na cheti maalum! Cheti maalum cha kumwona kaka yako au dada yako tena kwa ruhusa maalum kutoka kwa Sektretari wake ambaye ni kutoka kijiji cha jirani. Kuingia chumbani kwao tena kama ilivyokuwa zamani kabla Mzee hajafariki ni ndoto tena macho yako uyageuzie kule mbali kila unapopita kuelekea kibarazani.
Sasa mtani, kweli kwa hali hiyo wewe utaendelea kuwa wa kawaida? Uvumilivu huo uwe labda umetunukiwa na Mwenyezi Mungu lakini kama ni mtu wa kawaida kabisa kabisa kama mdogo wangu mwingine 'Ote Kilemie Mnu' aliyefikwa na maji ya shingo, walahi nakuhakikishia akikujia nanihii akakwambia hii ishu ndogo sana kwangu naweza kuwasubiri kaka zako na dada zako siku moja wamekutana pale kwao kama kawaida yao WaChagga kuhiji kila Krismasi basi nasubiri wakitoka Kanisani wameshakula, wakati wanaendelea na mbege zao wakiteremshia na ndafu mi nawatumia salam kupitia vijana wangu, mtani we hapo utawaza mara mbili wewe?
We acha wewe mtani wangu! Mi nlivyowaza kuhusu maswahibu yangu basi ndiyo sababu iliyonifanya niwaze kununua bastola japo sijui kitako na kichwa vinatofautianaje. Ni mengi yamenichosha. We fikiria mtu unaposhindwa kutofautisha kati ya raha na karaha aisee, we unafikiri...
...ebu kwanza subiri kidogo kuna mdundiko unapita hapa sijui mtoto wa nani wanamcheza leo, hizi ni raha ndogo ndogo mtu huwezi kuziacha zipite hivi hivi. Yana mwisho haya! Na pia napenda kusema asante Da Subi kwa mada hii.
Hii mada imenifanya nimkumbuke mwl J.K Nyerere
ReplyDelete