Sunday, October 15, 2017

DOMINIKA YA ISHIRINI NA NANE YA MWAKA A

NIMETUMIWA HII NA RAFIKI NIMEONA NI VEMA NIIWEKA HAPA KIBARAZANI ILI WENGI TUPATE KUJUA ...

MASOMO.
Isa.25 :6-10.
Flp.4:12-14,19-20.
Injili Mt 22: 1-14.

WAZO KUU: HAITOSHI TU KUBATIZWA NI LAZIMA PIA KUUISHI  UBATIZO.
UTANGULIZI.
Ndugu zangu leo ni Dominika ya Ishirini na nane ya mwaka A wa kanisa.Tumefika tena siku ya Bwana ili kumsikiliza na kumwabudu.Leo Masomo yetu yanatufakarisha juu ya mwaliko wa Mungu kwa wanadamu wote.Bwana Mungu anawaliaka watu wote kushiriki furaha ya heri ya milele.Mwaliko huo ni wa bure,kuuitikia ni heri,na kuukataa ni hasara kubwa kwa kukosa vinono kwenye karamu ya Mbinguni.Tumuombe Mungu atujalie neema zake ili kukubali mwaliko wake na kubaki katika kanuni za mwaliko huo daima.Tutafakari masomo yetu tukiongozwa na wazo hili,Haitoshi tu kubatizwa ni Lazima pia kuuishi Ubatizo.

UFAFANUZI.
Ndugu zangu,katika somo la kwanza nabii Isaya anaeleza uzuri wa karamu ya Bwana aliyowaanadalia watu wake.Bwana Mungu anawaalika watu wote kwenye sherehe yenye vitu vingi vizuri.Kwanza Mwaliko ni kwa watu wa Mataifa yote.Kutakuwa na vyakula vingi vinono, vilivyandaliwa juu ya mlima wake Mtakatifu.Pili kutakuwa na  uchangamfu mwingi, maana utaji uliotandwa nyusoni mwa watu kwasababu ya huzuni utaondolewa.Tatu Kutakuwa na furaha tele maana hakutakuwa na mauti tena kwa sababu Bwana ataangamiza mauti, kuyafuta machozi ya watu wake,na kuwaondolea aibu yao.

Katika Injili tumesikia Yesu akitoa mfanano wa Ufalme wa Mbinguni kwa Mfano wa Sherehe ya Harusi.Anasema Ufalme wa Mbinguni umefanana na mwaliko wa mfalme aliyewaalika watu kwenye karamu ya harusi ya mwanae.Walioalikwa  walikataa.Akatuma tena watumishi wake kuwaita walioalikwa wafike,vinono ni tayari.Hawa  hawakujali,wakatoa udhuru kuwa wamebanwa na shughuli zao wakaenda kwenye shughuli zao na waliosalia wakawakamata na kuwaua watumishi wa mfalme.Mfalme alikasirika na kuwaangamiza waalikwa wale walitenda mabaya hayo pamoja na mji wao.Kisha aliwatuma watumishi wake kuwaita hata waliokuwa wapitaji tu wa Barabarani ili harusi ijae watu.Harusi ikajaa wageni.Hivyo waalikwa wa kwanza si tu walikataa mwaliko bali pia waliwaua wajumbe waliotumwa kutoa ujumbe wa mwaliko.Nafasi yao ikachukuliwa na waalikwa wa awamu ya pili.Hawa nao waliofika  mmoja hakuwa na vazi la harusi.Alipohojiwa na Mfalme kuwa ameingiaje kwenye harusi bila vazi la harusi? Huyu hakuwa na la kujitetea.Basi Mfalme akaamuru huyu afungwe mikono na miguu na kutupwa nje.

Katika somo la pili mtume Paulo anasema anafaulu kufanya mambo mepesi na magumu kwa sababu ya nguvu ya Kristo anayopata toka kwa Kristo mwenyewe.Anasema anayaweza yote katika Kristo amtiaye nguvu.Anawashukuru wafilipi kwa ukarimu wao kwake kwa msaada waliompatia na anawaombea baraka ya Mungu.

MAISHANI.
Ndugu zangu,mwaliko wa Mungu ni mwaliko wa neema.Tumealikwa kushiriki heri na furaha ya milele bila mastahili yetu.Kama wale walioalikwa toka mwanzo au wale  walialikwa toka  barabarani hawakutarajia kupata mwaliko ule wala hawakufanya chochote ili waalikwe,vivyo hivyo tunaalikwa kushiriki heri ya Mbinguni kwa sababu ya upendo wa Mungu kwetu.Masomo haya yanatutafakarisha maisha yetu ya kikristo.Baada ya kukubali mwaliko wa imani  na kuupokea ubatizo tujue kwamba tunapaswa kuuishi Ukristo wenyewe.Masomo yanatukumbusha kwamba:

Mungu anawaalika watu wote kwenye heri ya Milele Mbinguni.Pamoja na kuwa mwaliko huo wa Mungu ni mwaliko wa furaha kati ya waalikwa hao,wapo wanaokubali na wapo wanaokataa kama ilivyo kwenye mfano wa Harusi.Ni bahati,heri na furaha kualikwa na Mungu.Wale wanaokataa mwaliko wa Mungu wanapata hasara kubwa sana.Ubaya mkubwa wa kuukataa mwaliko wa Mungu si adhabu au mateso atakayopata aliyekataa mwaliko bali ni Kukosa uzuri na vinono vya sherehe ile.Mimi nafikiri ni mateso makubwa sana kukosa kupata kilicho kizuri kuliko vyote na bila tumaini la kukipata tena.Hilo ni teso baya.Pamoja na kuadhibiwa kwa kupata mateso ni kibaya zaidi kukosa vinono.

Tukumbuke kwamba vyenye uzuri visichukue nafasi ya uzuri Mwenyewe.Maana vitu vizuri vimetoka kwa uzuru mwenyewe yaani Mungu.Tusifikiri kwamba mambo yanayoweza kusababisha tusiitikie mwaliko wa Mungu si lazima yawe mabaya.Tumesikia kuwa waalikwa wengine wa kwenye harusi hawakujali mwaliko wa Mfalme,wengine wakaenda shambani na wengine kwenye biashara zao.Si jambo baya kwenda shambani kufanya kazi wala kwenda kwenye biashara,maana hizo ni kazi za mtu kujipatia mkate wake wa kila siku.Ni mambo yaliyo mazuri.Lakini tusisahau kwamba haifai kujishughulisha na mambo mazuri na kumuacha Mungu aliye uzuri wenyewe.Mambo mazuri yanashirikishwa tu sehemu ya uzuri wa Mungu.Mungu ndiyo uzuri wenyewe.Haifai kujishughulisha na kazi za Bwana tukimuacha Bwana wa kazi.

Haitoshi tu kubatizwa ni lazima kuuishi Ubatizo.Tumesikia kuwa wale waliokubali mwaliko wa Harusi na kuingia harusini ,mmoja hakuwa na vazi la harusi.Kilichompata ni kutupwa nje ya ukumbi akiwa amefungwa mikono na miguu.Tulipobatizwa tuliitikia mwaliko wa Mungu.Ni lazima kuendelea kuvaa vazi la ukristo kwa kuuishi Ukristo wenyewe.Vazi la Harusi,yaani vazi la Ukristo wetu ni matendo mema,maisha ya fadhila.Haifai kabisa kuingia katika ukristo na  kuendelea kuvaa mavazi tuliyokuwa nayo kabla ya kubatizwa yaani kuendelea na maisha ya matendo mabaya,maisha ya vilema.Mfalme aliyetualika anataka kutuona na mavazi ya harusi.Tukiingia na mavazi yasiyo,basi tutatupwa nje hata kama tulikubali mwaliko.Tutatupwa nje hata kama ni wakristo.Haitoshi tu kubatizwa ni lazima kuuishi Ukristo.

HITIMISHO.
Hatimaye ndugu,tumalizie tafakari yetu tukijifunza ukarimu kwa watu wote hasa masikini na fukara.Injili inaeleza juu ya mwaliko wa Mfalme kwa watu ili washiriki harusi.Aliandaa vinono vingi kwaajili ya wageni wake.Tunajifunza ukarimu mkubwa wa Mfalme.Jambo hili litukumbushe kuwa mafiga matatu ya kutusaidia kuuishi vizuri ukristo wetu ni kujisomea na kutafakari  Neno la Mungu,Kupokea Sakramenti za kanisa  hasa Ekaristi na kitubio mara nyingi ,na kutenda matendo ya huruma ya mwili na ya roho.Mimi nafikiri haya mafiga matatu ni msaada mkubwa wa kujivalia vazi la harusi ili tusije tupwa nje maana haitoshi tu kukubali mwaliko wa harusi,ni lazima pia kuvaa mavazi ya harusi.

Tumsifu Yesu Kristo!
Na Padre Augustino Kamnyuka.
Parokia ya Kristo Mfalme Bologna-Italia.
Tarehe 15.10.2017.

2 comments: