Tuesday, May 21, 2013

Wanafunzi waliokatishwa masomo kwa mimba wafunguka



Mmoja wa wanafunzi alyepata mimba akiwa kidato cha tatu

Mada hii imenigusa sana,,,,nimekuwa muda mrefu nikulalamika sana kuhusu hili yaaani kwanini wasichana waachishwe shule na sio wavukana pia. na kwanini wasichana wasipate muda wa kusoma baaada ya kupata watoto. ..soma hapa  china...mada hii nimeiipata http://maendeleonivita.blogspot.se/ soma mwenyewe!!!!
----------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
WANAFUNZI wengi wanaosoma katika shule za sekondari wilayani Tunduru mkoani Ruvuma wanakatishwa masomo yao wanapofikia kidato cha pili na cha tatu baada ya kupata mimba na kuolewa wakiwa shuleni.
Hali hiyo inatokana na historia ya wakazi wa wilaya hiyo ambao ni kabila la wayao kutokuwa na mwamko katika elimu hasa kutokana na kutoa kipaumbele kwa desturi na mila za kabila hilo ambazo zinatoa fursa zaidi katika mila potofu za unyago,msondo na jando kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari hali ambayo inaathiri suala zima la elimu.
Takwimu ambazo zimetolewa na mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho zinaonyesha kuwa mwaka 2012 wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na sekondari mwaka huu walikuwa ni 2788 hata hivyo hadi kufikia mwezi Aprili mwaka huu ni wanafunzi 1710 tu ndiyo walioripoti hali ambayo inakwamisha maendeleo ya elimu.
Flavian Nchimbi kaimu afisa elimu msingi wilaya ya Tunduru anasema tatizo la mimba katika shule za msingi zimepungua ukilinganisha na miaka mitatu nyuma kulikuwa na mimba karibu 250 ambapo takwimu za mwaka jana zinaonyesha kuwa katika shule za msingi zililipotiwa mimba 16 na kwamba kuanzia mwezi Januari hadi Aprili mwaka huu imeripotiwa mimba moja tu.
Hata hivyo afisa elimu sekondari wilaya ya Tunduru Ally Mtamila amekiri tatizo la mimba na ndoa za utotoni kwa wanafunzi wa shule za sekondari kuwa ni kubwa ambapo wanafunzi wa kike wanakatishwa masomo kwa mimba au kuolewa.
Sarah Michael(15) mkazi wa Tunduru alikuwa anasoma katika shule ya sekondari Makita ambapo alipewa ujauzito akiwa kidato cha tatu na mwanaume ambaye alitoroka mara baada ya tukio hilo hali ambayo ilimfanya aishi kwa shida hadi alipojifungua salama mtoto wake wa kiume.
“Baada ya kupata ujauzito niliacha masomo wazazi walinipokea licha ya kupata misukosuko mingi hasa kutoka kwa baba yangu mzazi,nimejifungua naendelea kumlea mwanangu katika mazingira magumu sana kwa kweli nakumbuka shule mwaka huu ningekuwa namaliza kidato cha nne’’,alisema.
Sarah alisema anapenda sana kusoma lakini wazazi wake hawana uwezo wa kumsomesha hivi sasa hivyo endapo atampata mtu wa kumsomesha anaweza kuendelea na masomo ya sekondari na kwamba kitendo cha kupata mimba na kukatisha masomo yake kimetoa fundisho kubwa kwake hivyo hawezi kurudia makosa ambayo yameharibu ndoto za maisha yake.
Hata hivyo anasema baba yake ni mwajiriwa wa serikali anafanya kazi ya uaskari magereza wilayani Mbinga ambaye kitendo cha yeye kukatishwa masomo kilimchukiza na alitaka mtuhumiwa kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria,hata hivyo wazazi wa pande zote mbili waliyamaliza na kufuta kesi.
“Hivi sasa baada ya mwanangu kukua nimemwomba baba anisomesha ili niweze kuendelea na masomo,lakini baba bado ana hasira amekataa na kusema ningoje kwanza nijifunze maisha kwa kuwa mimi niliacha shule na kukimbilia mambo yaliosababisha kupata mimba naendelea kumuomba radhi baba kwamba sitarudia tena nikipata nafasi ya kusoma’’,alisema kwa huruma.
Salima Hamad(15) mkazi wa Tunduru anasema alikatishwa masomo yake baada ya kupata mimba akiwa kidato cha tatu mwaka 2012 na kwamba wazazi wake walichukizwa na kitendo hicho ,walifungua kesi ya mwanaume aliyempa mimba,alikamatwa na kutiwa ndani hata hivyo mwanaume huyo ametorokea nchini Msumbuji hadi leo.
“Wazazi walinisakama pamoja na viongozi wa serikali ya kijiji,nilitamani kutoa mimba lakini nilipiga moyo konde,nilivumilia kulea mimba katika mazingira magumu kwa kuwa wazazi wangu ni masikini hadi nikajifungua salama kwa kufanyiwa upasuaji mtoto wa kike,natamani kusoma lakini sina uwezo’’,alisisitiza.
Salima anasema wazazi wake wamekataa kumsomesha na kudai kuwa hawana uwezo wa kumpeleka tena shule na hivi sasa anaishi kwa kujitazamia na kuuguza kidonda ambacho kimetokana na kujifungua kwa upasuaji.
Hemed Ally mwanafunzi wa kidato cha nne shule ya msingi Frank Weston wilayani Tunduru anasema katika mafunzo ya msondo na unyago wanafunzi wa kike wanaelezwa faida za kuishi na mume lakini hawafundishwi madhara ambayo wanaweza kupata kwa kushiriki katika ndoa wakiwa wadogo hali hiyo ndiyo inawahamasisha wanafunzi kujiingiza kwenye ngono na kushawishika kuolewa na kupata mimba wakiwa wanafunzi.
Rehema Sara mwanafunzi wa kidato cha nne sekondari ya Mgomba anasema mila za unyago na msondo zimesababisha wanafunzi wengi wa kike katika shule hiyo kuacha masomo kwa kupata mimba au kuolewa ambapo hivi sasa katika darasa lao waliofanikiwa kufika kidato cha nne ni wanafunzi 106 tu kati ya wanafunzi zaidi ya 230 walioanza nao kidato cha kwanza mwaka 2010.
Sarah mkombozi wa kidato cha nne sekondari ya Mgomba ambaye alifanyiwa ngoma ya unyago na msondo akiwa darasa la tatu amekiri moja ya mambo ambayo wanafundishwa katika msondo na unyago ni kufanya mapenzi na watu wazima na kwamba kukataa kufanya hivyo ni kuvunja mila na desturi za wayao’’,alidai mwanafunzi huyo.
“wenzangu wengi ambao nilikuwa nao shule ya msingi na wengine ilitakiwa niwe nao sekondari wameacha masomo kwa kuwa wana watoto baada ya kupata mimba na wengine wameolewa na kuachika hivyo wanaangaika na maisha’’,alisisitiza.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho amekiri mila na desturi za kabila la wayao zinachangia wilaya hiyo kuwa duni kielimu hata hivyo amesema tayari serikali imeunda kikosi kazi cha kuonana na viongozi wa mila, makungwi na manyakanga kuwaelimisha juu ya utoaji wa elimu kwa watoto wa kike kupenda masomo tofauti na sasa ambapo kundi hilo limekuwa likifundishwa kukabiliana na maisha ya ndoa hali iliyosababisha kuwepo kwa matukio mengi ya ndoa za utotoni wakiwa shuleni.
“Mila na desturi za kabila la wayao kuwafanyia unyago wanafunzi ndiyo chanzo kikuu cha tatizo hili,sisi kama serikali ili kukabiliana na tatizo hili tumefanya vikao na viongozi wasiokuwa rasmi lakini wanakubalika katika jamii wakiwemo makungwi, mangariba, masultani,mamwenye,mashehe na maimamu kwa kuzingatia tumejadili kwa pamoja tatizo hili”,anasisitiza.
Kwa mujibu wa Takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, wasichana 8000 kila mwaka huacha shule kutokana na ujauzito. Kati yao 3,000 ni wanafunzi wa shule za msingi.
Kila siku, wanawake 24 hufariki dunia kutokana na mimba au wakati wa kujifungua. Wanawake watano mpaka sita wanaofariki kati ya hao ni watoto wadogo, watoto hao hufariki dunia kwa kuwa miili yao haijakomaa vya kutosha kwa ajili ya kujifungua.
Naibu mwakilishi mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa Linaloshughulikia Watoto (UNICEF), Mohamed Safieldin anasema mbali na athari hizo, pia virusi vya ukimwi (VVU), vinavyosambaa kwa kasi kwa wasichana hao. Tanzania kuna watoto yatima milioni 1.3 walioathirika kwa ukimwi.

4 comments:

  1. Kuna mtu mmoja wa hekima, alisema watu wawili mombaji na muombwaji,je wapo sawa?

    Muombaji akiomba, je ni lazima apewe?

    Na je muombwaji akiombwa ni lazima atoe?

    Muombwaji akitoa, na akapata madhara kwa kutoa kwake, anastahili adhabu sana na muombaji?

    Ukiangalia haya maswali yana maana yake.

    Lakini ninachotaka kusema ni kuwa ni wakati muafaka, akina mama, kuwa na lengo moja, hasa kuwafunda watoto wetu wakike, kukataa...kusema NOOOO. Pili kuwa na mikakati ya kuzuia vile vinavyosababisha ushawishi,....

    Huenda ni rahisi sana kuliongea hili kwa mdomo kuliko vitendo. lakini kwa wazazi linatuhusu sana, hasa tulio na watoto wa kike ambao ndio wanadhulumiwa. Kwani likitoka hilo la kutokea atakayeumia ni mwanamke, mwanaume, hayupo hapo. sasa kipi bora, kufanya yale yatakayokulinda au kujiweka huru, nusu uchi yakukute, eti kwa vile ni `uhuru', ni haki binafsi.

    Ni kweli watoto kuwafunda hadi wajue madhara ya hilo jambo, ni vigumu sana. Na hasa kwa kipindi hiki cha utandawazi, kwani vishawishi ni vingi sana, na ukizingatia maadili ya dini, hasa ya kujihifadhi ili kuondoa tamaa za kimwili, hayazingatiwi, na hili la kujihifadhi linachukuliwa kama ni kuzalilisha, tunasahau madhara yake, ambayo ndio huko kubakwa, kushawishi nk.

    Ni mtihani kwa kweli-kweli, lkn kijumla kunahitajika kubwa na hukumu kuwa sawa, kwa aliyempa huyo mtoto uja uzito. Mtoto wa kike yeye keshaadhibiwa kwani atafukuzwa shule, atabeba mimba miezi tisa.

    ReplyDelete
  2. Ni bahati mbaya kuwa rais wao aliyewaahidi maisha bora kwa wote alisema eti wanapata mimba kutokana na kiherehere chao. Ajabu hakuona kiherehere chake cha kupokea kila upuuzi wa sera toka nchi za magharibi uliomsukuma kuiweka rehani nchi yetu. Ni ajabu kuwa hakuona kiherehere chake cha kupenda kuzurura badala ya kutulia ofisini na kusoma na kutatua matatizo ya wananchi. Ni bahati mbaya kuwa hakuona kiherehere chake cha kuwateua marafiki zake katika kulipana fadhila ukiachia mbali kuwavumilia na kuwakingia kifua pale wanapovurunda. Hakuna kiherehere chake cha kuendelea kuwa na mwaziri walioghushi shahada kama vile Makongoro Mahanga, Mary Nagu, Emanuel Nchimbi, Matayo Matayo na William Lukuvi bila kusahau balozi Deodorus Kamala na Meya wa jiji la Dar Didace Massaburi almaarufu Makalio.

    ReplyDelete
  3. Hili ni janga letu sote na kwa pamoja tuwawezeshe wahanga wetu.

    ReplyDelete
  4. Habari kama hii nimeanza kuisikia tangu nilipopata akili, inasikitisha sana kusoma/kusikia bado mpaka leo. Kinachoniuma zaidi ni pale wasichana wanapopata mimba na kutelekezwa na wavulana kuachiwa na kuendelea na masomo. Na baada ya hapo msichana akisha zaa anataka kurudi tena shule anakataliwa eti yeye ni mama/amezaa nani alisema aliyezaa hawezi kusoma tena? ni sheria hiyo kweli?...Na mpaka ikajengeka katika jamii eti hakuna haja kumsomesha mtoto wa kike..

    ReplyDelete