Saturday, October 20, 2012

Neno La Leo: Hakuna Ugumu Wa Kurudi Misri...

Habari hii nimetumiwa na kaka Mjegwa.....
-------------------------------------------------------------------------------------
Ndugu zangu,
Yanayotokea katika nchi yetu kwa sasa yanatutaka tufikiri kwa bidii. Kama nchi kuna safari tumeifunga. Na tulivyo Waafrika, tu mahodari wa kufunga safari, lakini si mahodari wa kupanga safari. Kufunga na kupanga safari ni vitu viwili tofauti.

Ndugu zangu,

Ni vigumu leo kwa Wana wa Israel kuamua kurudi tena Misri, hata kama, pamoja na chawa na kunguni walioaacha Misri, bado, kuna wanaokumbuka samaki na masufuria ya pilau waliyoayaacha Misri. Lakini, kijamii, na kwa kuingalia jamii yetu hii ilikotoka, ilipo sasa na inakoelekea, na tuone sasa, kuwa hakuna ugumu wa kurudi tena Misri. Na hapa nitazungumzia umuhimu wa sisi WaTanzania kujitambua.

Nahofia, kuwa moja ya kiini ya haya yanayotukuta sasa ni dhambi ya Ubaguzi iliyoanza kututafuna pole pole. Taratibu tunapoteza uwezo wetu wa kujitambua. Ni ukweli sasa, kuwa Watanzania hatujitambui, na kibaya zaidi, baadhi ya viongozi wetu wa kisiasa na kidini wanapoonyesha wazi wazi kuwa hawajitambui.

Maana, tumeanza sasa kuzungumza lugha za ' Wao Wakristo' na ' Sisi Waislamu'. Tunasahau, kuwa sisi ni ndugu wa damu. Kuwa SISI ni Watanzania Kwanza. Na lililo la kwanza kwetu ni ' Nchi Yetu' na maslahi yake.

Hii ni Nchi Yetu Sote. Kila Mtanzania kwa nafasi yake ana lazima ya kupigania Usalama wa Taifa letu. Usalama wa Nchi Yetu tuliyozaliwa. Hatuwezi kuilinda na kuijenga Nchi Yetu kwenye mazingira ya kubaguana. Kwenye mazingira ya kugawanyika kwa misingi ya udini, ukabila na rangi. Na hapa nitamrejea tena Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na dhana ya Ujenzi wa Umoja wa Kitaifa.

Ni Mwalimu Nyerere aliyeuanzisha na kuusimamia mradi mkubwa wa Ujenzi wa Umoja wa Kitaifa, hata hivyo, tunaona sasa unavyoporomoka na kuliacha taifa letu mashakani. Ndio, Mwalimu alijenga misingi imara ya Ujenzi wa Umoja Wa Kitaifa ( Nation Building).

Kuijenga jamii ya Watanzania yenye kuamini kwenye ukweli kuwa sisi sote ni ndugu. Kwamba Nchi yetu haina dini. Yenye kupiga vita ubaguzi wa aina zote, iwe wa rangi, kabila au dini. Ilimchukua Mwalimu na taifa letu miaka mingi sana kuijenga misingi hiyo iliyowawezesha pia Watanzania kuwa na mioyo ya uzalendo kwa Taifa lao.

Tunaona sasa, kazi hiyo iliyochukua miaka mingi, kutokana na ubinafsi na uroho wa madaraka ya baadhi ya wanasiasa wetu, wanapelekea kubomoka kwa misingi hiyo na kuliacha taifa letu kwenye hatari ya kuangamia.

Ndio, msingi wake ni ubaguzi wa kisiasa unaotokana na ubinafsi na tamaa ya mali kwa baadhi ya tuliowapa dhamana za kufanya maamuzi makubwa kwa niaba yetu. Ni hali ya baadhi ya tuliowapa dhamana za uongozi kuishiwa chembe chembe za uzalendo; mapenzi kwa nchi yao.Ni watu wenye kulinda maslahi yao na ya wanaowazunguka. Wako tayari hata kutumia mbinu za Umafia kutimiza malengo yao. Kuna Watanzania wengi sasa wanaopoteza mioyo ya uzalendo kwa nchi yao.

Kuna hata wenye kufikia kutamka; 'Nchi hii ina wenyewe'. Kuna anayetamka hilo kwa lengo la kumtishia mwenzake au kulazimisha kitu fulani kifanyike. Lakini, kuna wenye kutamka hivyo kuashiria kukata tamaa. Kuwa hata wafanye nini, hakuna anayewasikiliza ama kuwajali. Hizi si dalili njema kwa taifa. Kuna wanaoiba mali ya umma mchana wa jua kali. Hakuna anayewagusa.

Ukiuliza utajibiwa; “Ah! Nchi ina wenyewe!”. Kwamba kuna baadhi yetu hawajisikii kuguswa na nchi hii, hawajisikii kuwa na nguvu ya kupiga vita maovu yanayotusumbua. Baadhi yetu wameanza kupungukiwa na mapenzi na nchi yao.

Juni 16, 2004 nilipata kuandika hili kwenye gazeti la Majira; kuwa Tanzania ina vyote, kasoro Watanzania. Niliandika; kuwa Tanzania ni nchi nzuri sana. Ni nchi ya kujivunia. Kwamba Tanzania ni nchi kubwa sana kwa eneo. Ni nchi yenye rasilimali nyingi; ardhi yenye rutuba, mito, maziwa, milima, mabonde, bahari na vivutio vingi vya asili.

Hata hivyo, Tanzania ni moja ya nchi masikini sana duniani. Kwa nini? Ndio, kikubwa kinachokosekana Tanzania ni Watanzania. Tanzania tunayoijenga sasa ni mkusanyiko tu wa watu wa makundi mbali mbali wenye kwenda kwa staili ya 'kila mtu na lwake'. Idadi ya Watanzania wenye uzalendo na mapenzi kwa nchi yao inazidi kupungua. Ubinafsi umekithiri, na ubinafsi mbaya zaidi ni ule wenye kufanywa na viongozi.

Ndugu zangu, Hakuna ugumu wa kurudi Misri. Tuna lazima ya kupanga safari ya kurudi tena Misri. Inawezekana.

Na hilo ni Neno la Leo.

Maggid Mjengwa,

Iringa,

0788 111 765, 0754 678 252
http://mjengwablog.com

No comments:

Post a Comment