Wednesday, August 1, 2012

TUNAJENGA TAIFA LA WALEVI?


Ni ile JUMATANO YA KIPENGELE CHA MARUDIO YA MATUKIO MBALIMBALI NA LEO NIMETEMBELEA HAPA NA KUKUTANA NA HII HABARI NIMEIPENDA NA NIMEONA TURUDIE ILI KUJIFUNZA ZAIDI.

Mtu mmoja akiwa amelala porini baada ya kuzidiwa na kilevi

Pombe ni kiburudisho muhimu sana kwa walio wengi. Mamilioni ya wanaume na wanawake ulimwenguni wanatumia au wamewahi kutumia pombe wakati fulani katika maisha yao.

Umaarufu wa pombe bila shaka unatokana na uwezo wake katika kumfanya mtumiaji ajisikie vizuri na kusahau matatizo yanayo mkabili japo kwa muda. Pombe huondoa aibu, huufanya mwili kusisimka na kuleta furaha.

Kwa sababu hiyo pombe ni kimbilio la watu wengi wenye furaha, na wenye matatizo na shida za aina mbalimbali. Kwa mtazamo wa haraka haraka tunaweza kusema pombe ni nzuri na inafaa kutumiwa kama kiburudisho endapo mtumiaji atakuwa na kiasi na kuitumia kwa namna inayofaa.

Kwa upande mwingine pombe ni kitu kibaya sana kwani madhara yake yanazidi faida na hasa kwa kuzingatia kwamba ni watu wachache sana wanaoweza kufuata mashalti ya utumiaji kileo kama inavyotakiwa. Leo hii pombe ni chanzo kikubwa cha ajali za barabarani zinazo sababisha mauaji ya maelfu ya watu wasiokuwa na hatia.

Pombe ni hatari kwa wajawazito
Pombe pia ni chanzo kikubwa cha matatizo ya kijamii ikiwa ni pamoja na kusambaratika kwa familia, na ongezeko la talaka jambo linalosababisha mateso makubwa kwa watoto.

Aidha, pombe inachangia sana katika kuleta umaskini kwa mtu binafsi, familia na hata taifa. Pombe husababisha uzembe kazini, kupunguza uwezo wa kufikiri na kutoa maamuzi na kusababisha madhara katika ubongo hasa kwa watumiaji wenye umri mdogo (watoto).

Pombe pia husababisha matatizo ya kiafya kwa watoto walioko tumboni (ambao hawajazaliwa). Wanawake wajawazito wanaotumia pombe hujiweka katika hatari kubwa ya kuharibu akili (ubongo) za watoto wanaowabeba matumboni mwao.

Ni kwa sababu hiyo nchi zilizoendelea (kama Marekani na baadhi ya nchi za ulaya) zimepiga marufuku uuzaji wa pombe kwa vijana wenye umri chini ya miaka 18, na zinaendesha kampeni za kuwaelimisha akina mama kuepuka matumizi ya pombe katika kipindi chote cha ujauzito.

Pamoja na madhara makubwa yanayoletwa na unywaji wa pombe, ni ajabu kwamba nchini mwetu pombe tumeigeuza kuwa sehemu ya maisha. Watu wengi wenye kipato cha kawaida hujiingiza katika unywaji pombe wa kupindukia kutokana na kasumba iliyojengeka nchini mwetu kwamba watu wanaokunywa pombe kila siku wana pesa nyingi. Watu wanaojiingiza katika ulevi hufanya hivyo kwa kudhani wanainua 'status' zao.

Wengi wa walevi hawa hujikakamua kununua pombe zenye bei kubwa zaidi ili kuonesha kuwa wana pesa na kuwakoga wasiokuwa nazo. Baadhi ya wanywaji hufikia hatua ya kuweka bili katika mabaa na store zinazouza pombe ili waweze kunywa pasipo kukosa hata kama hawana pesa (na kulipa mwisho wa mwezi) jambo linalowaingiza katika umaskini wa kujitakia pasipo kujua.

Ni kutokana na ongezeko kubwa la wanywaji wa pombe makampuni mbalimbali yanayo tengeneza na kusambaza vileo yameivamia Tanzania kwa nguvu na kumwaga pombe za kila aina mitaani. Makampuni haya hujitengenezea faida kubwa isiyoelezeka.

Aidha wafanya biashara wengi nchini wameacha kuwekeza katika vitega uchumi vingine vya kimaendeleo kama kilimo, ufugaji, viwanda vidogo vidogo, elimu n.k na kugeukia biashara ya pombe ambayo inaelekea kutokuwa na mpinzani katika kuingiza faida. Si ajabu kwamba katika miji yetu kuna baa katika kila kona.

Mbaya zaidi ni kwamba serikali haifanyi jitihada zozote kudhibiti uuzaji na matumizi ya kileo katika nchi yetu (pengine kutokana na kodi kubwa inayokusanya kutoka katika biashara ya vileo). Matokeo yake pombe huuzwa kwa mtu yeyote bila kujali umri wake, muda wala mazingira inapouzwa pombe hiyo.

Leo hii makampuni makubwa yanayouza vileo ikiwa ni pamoja na kampuni ya TBL yanafanya matangazo mengi ya kuwashawishi wananchi kunywa pombe bila kujali matangazo hayo yanawavutia watoto wadogo. Hebu fikiri yale magari yanayotangaza bia mitaani kwa kupiga muziki huku kina dada warembo wakicheza mayenu na kugawa zawadi za bia kwa wananchi waliokusanyika.

Ni hivi juzi tu kampuni maarufu ya bia nchini iliendesha tamasha kubwa la muziki ambapo kiingilio ilikuwa kopo la bia ambayo mteja alipaswa kuinunua uwanjani hapo. Katika tamasha hilo washiriki wengi walikuwa vijana wadogo wenye umri chini ya miaka 18 ambao waliuziwa pombe bila hofu wala aibu.

Ni lazima tukubali ukweli kwamba pombe ni hatali kwa afya na maendeleo. Ndio maana nchi zilizoendelea (Marekani, Ulaya na hata baadhi ya nchi za kiarabu) zimeweka taratibu kali za kudhibiti matumizi ya vileo ikiwa ni pamoja na kuzuia uuzaji wa pombe kwa vijana wenye umri chini ya miaka 21 (kwa USA), kuzuia unywaji wa pombe hadharani, kupanga masaa maalum ya uuzaji wa pombe na kuzuia aina zote za matangazo ya pombe yanayo walenga vijana wadogo.

Ni jambo lililo dhahiri kwamba ulevi ni adui wa maendeleo na hivyo kuendelea kujenga taifa la walevi ni hatari kwa maendeleo, afya na usalama wa jamii yetu. Ni kwa sababu hiyo tunaishauri serikali kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya utumiaji vileo.

Aidha ni vema serikali ikatunga sheria kali za kudhibiti uuzaji holela wa vileo ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku uuzaji wa pombe kwa watoto wenye umri chini ya miaka 18.Ni muhimu sheria hizo pia zifafanue aina ya matangazo ambayo makampuni ya uuzaji vileo yanaruhusiwa kufanya ili kudhibiti matangazo yanayowalenga vijana wadogo, na pia kutamka maeneo na muda unaoruhusiwa kuuza vileo kisheria.

Kama serikali isipochukua hatua za haraka kudhibiti ongezeko la walevi nchini, si ajabu nchi yetu ikaendelea kudidimia katika wimbi kubwa la umaskini wa kujitakia. Na watu wengi wataendelea kuamini kuwa serikali inaendekeza ulevi ili wananchi wengi wasione hali ngumu ya maisha iliyoko nchini na kuipigia kelele serikali.
Na Mwana Dikala
TUONANE TENA PANAPO MAJALIWA!!!

5 comments:

  1. kwakweli Taifa halitajengeka kwa namna hii

    ReplyDelete
  2. Pombe sio chai,inabidi kuwe na sheria, mtu akikutwa mchana kalewa achapwe viboko,....

    ReplyDelete
  3. Mimi sijaona kosa lolote alilofanya huyu jamaa, Kosa ni serikali na wauza pombe manake TZ viwanda vya kutengeneza pombe au bia ni vingi kuliko viwanda vya maana vya vyakula au nguo, halafu mabaa yamejaa kama mchezo kila kona na kila kichohoro isitoshe na pombe za kienyeji pia, watanzania bila kulewa hajafanya kitu hapo akose kula lakini aikose kulewa pombe.

    ReplyDelete
  4. 29 Ni nani aliye na ole? Ni nani aliye na wasiwasi? Ni nani aliye na ugomvi? Ni nani aliye na mahangaiko? Ni nani aliye na majeraha yasiyo na sababu? Ni nani aliye na macho mazito? 30 Ni wale wanaokaa muda mrefu kwenye divai, wale wanaoenda kutafuta divai iliyochanganyika. 31 Usiitazame divai inapotoa rangi nyekundu, inapochemka katika kikombe, inaposhuka taratibu. 32 Mwisho wake inauma kama nyoka, nayo hutoa sumu kama nyoka. 33 Macho yako mwenyewe yataona mambo mageni, nao moyo wako mwenyewe utasema mambo yaliyopotoka. 34 Nawe utakuwa kama mtu anayelala katikati ya bahari, kama mtu anayelala juu ya mlingoti. 35 “Wamenipiga, lakini sikuwa mgonjwa; wamenichapa, lakini sikujua; Nitaamka wakati gani? Bado nitaitafuta hata zaidi.” _Methali 23:29-35

    ReplyDelete
  5. karibu tunakusubiri.

    ReplyDelete