Monday, July 9, 2012

Neno La Leo: Vita Hii Ya Serikali Na Madaktari Ikome Sasa!!!!


Ndugu zangu,
NCHI yetu ingali katika huzuni ya uwepo wa mgogoro kati ya madaktari wetu na Serikali yetu. Ni huzuni iliyochanganyika na hofu na mashaka.  Suluhu ya kushikana mikono haijapatikana.
Inasikitisha, maana, hii ni nchi yetu, wanaogoma ni madaktari wetu na inayogomewa ni Serikali yetu. Ni wananchi wa nchi hii wenye kutaabika na hata  kupoteza maisha yao kutokana na mgomo huu. 
Hili ni jambo la kuhuzunisha sana. Ni jambo lenye kuitia doa nchi yetu. Huko nyuma kuna tuliosisitiza, na hapa narudia kusisitiza msimamo wangu kama Mtanzania ninayeipenda nchi yangu, kuwa hakuna njia nyingine ya kuumaliza mgogoro huu bali ni kwa njia ya mazungumzo ya kindugu na kirafiki. Wahusika wana lazima ya kukaa kwenye meza moja kama Watanzania na kuitafuta suluhu ya mgogoro huu kwa manufaa ya nchi yetu na watu wake.
Kwa sasa kila upande unamwona mwenzake ndiye mwenye makosa. Hivyo, kila upande umejichimbia handakini na kuendeleza ' vita vya kuviziana'. Ukweli, katika vita hivi hakutakuwa na mshindi, maana, kama taifa, sote tumeshashindwa. Na tunaendelea kushindwa zaidi, maana, watu wetu wanaangamia kwa kukosa tiba ya uhakika.
Kimsingi madai ya madaktari ni ya msingi na yanazungumzika. Na hoja za Serikali ni za msingi na zinazungumzika. Hivyo, pande zote mbili zinaweza kuzungumza na kufikia muafaka. Si jambo la hekima kwa sasa kwa madaktari kuendelea na mgomo wao wakati milango ya mazungumzo haijatiwa komeo la shaba, na si hekima vile vile kwa Serikali ' kugomea' kuzungumza na madaktari kwa kisingizio kuwa suala hilo liko mahakamani.  Naungana na viongozi wa kidini walioisihi Serikali kufuta shauri hilo  na kuimaliza kadhia hii kwenye meza ya mazungumzo.
Ni vema na ni busara sasa kwa madaktari wakatangaza, kwa manufaa ya nchi  yetu, kuahirisha mgomo wao mara moja na kurudi kazini  kuwahudumia Watanzania kwa moyo wote. Wafanye hivyo  hata katika mazingira magumu waliyonayo,  wakati juhudi za kufikia muafaka na Serikali zikiendelea.
Maana, mgomo wowote ni jambo la hasara. Kila siku inayokwenda kukiwa na mgomo ina maana ya hasara kwa nchi na watu wake. Ni hasara ya fedha na uhai.  Ndio maana ya pande zote mbili zinapaswa kuhakikisha zinakutana na kutafuta suluhu ya kushikana mikono.
Na huko twendako, endapo kutatokea hali ya kutoelewana baina ya Serikali na madaktari, basi, Chama cha Madaktari kianze sasa kufikiria namna njema ya kuendesha migomo tofauti na hii ya sasa. Mathalan, katika kuishinikiza Serikali ingewezekana kuanza na mgomo kwa Hospitali moja na si nchi nzima. 
Ingewezekana pia isiwe kwa hospitali nzima bali vitengo kadhaa huku huduma kwenye vitengo vingine zikiendelea. Hata hilo pia lingewaletea usumbufu wananchi na kufikia kuishinikiza Serikali kwenye kujadiliana na madaktari  katika kuboresha maslahi yao. 
Lakini hili la ' Wild Strike' kwa maana ya mgomo wa nchi nzima lina' hatari ya kiafya' kwa taifa.  Tusifike mahala tukachangangia kuifanya nchi yetu wenyewe iende kwa kutambaa kutokana na migomo. 
Nimepata kuandika, kuwa katika  nchi zetu hizi, mganga wa tiba aliyesomeshwa kwa fedha za walipa kodi  na kwa miaka mingi anahitajika sana. Mganga wa tiba msaidizi anahitajika  sana. Na hata kama angelikuwapo Msaidizi wa Mganga Msaidizi wa tiba ,  naye angehitajika sana. Vivyo hivyo kwa wakunga wakuu na wasaidizi,  wauguzi wakuu na wasaidizi wao. Wote hao anahitajika sana.
Na  katika nchi zetu hizi, Serikali hazipaswi kufikia hatua ya kuwatisha na  hata kuwafukuza kazi madaktari. Hilo la mwisho lifanyike tu pale ambapo  njia nyingine zote za kumaliza tofauti na kusuluhisha migogoro na  madaktari zitakapokuwa zimeshindikana. Na kwa nini ishindikane?
Naam, Watanzania tungependa kuona vita hii baina ya Serikali na madaktari ikimalizwa haraka kwa kutafutwa suluhu ya kushikana mikono. Inawezekana.
Habari hii nimetumiwa na Mwenyekiti Mjengwa......

2 comments:

  1. tena imalizwe mapema, wagonjwa na wanyonge ndo waumia zaidi

    ReplyDelete
  2. Hii nyumba ni yetu sote na wajenzi wenyewe ni sisi na kugombea fito iwe ni mwiko.
    Meza ya mduara ni muhimu kwa wadau wote na busara ziende mbele hatua moja dhidi ya sheria.
    Salamu!

    ReplyDelete