Tuesday, July 24, 2012

BIDHAA ZITOKANAZO NA UBUYU - Mafuta, Sabuni, Vipodozi, na Dawa"




Marietha Mkuya Aendesha maisha yake kwa kuuza bidhaa zitokanazo na Ubuyu
MAISHA ni kuhangaika bila kukata tamaa, kutumia kila aina ya ubunifu hasa ukiwa mjasiriamali. Hili limeonekana kwa Marietha Mkuya; mjasiriamali anayetengeneza bidhaa nyingi, zote zikitumia malighafi moja tu, Ubuyu.
Nikiwa kwenye Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba, ndipo nilipokutana na mama mjasiriamali huyu kutoka mkoani Dodoma.
“Karibuni mjaribu bidhaa za ubuyu kutoka mkoani Dodoma.” Ndivyo alivyokuwa akiwakaribisha watu mbalimbali waliokuwa wakipita karibu na banda lake.
Anasema kama ilivyo kwa zao mhogo ambalo lina faida nyingi, ubuyu pia unafaida nyingi kiafya na kitabibu pia.
Muya anasema ubuyu unaweza kutumika kama dawa na pia kama kirutubisho cha mwili na pia unaweza kutumia ubuyu kama kipodozi.
Mama Mkuya ni mmiliki wa Kampuni ya kutengeneza vyakula ya Geitana Food Processor iliyopo mjini Dodoma,ambayo inajishughulisha na usindikaji wa bidhaa zinazotokana na ubuyu.
“Kwa takribani miaka minne sasa, nimekuwa nikijihusisha na utengenezaji wa bidhaa za ubuyu, napata malighafi hii kwa urahisi zaidi hasa ikizingatiwa kuwa Mkoa wa Dodoma unazalisha ubuyu kwa wingi.” anasema mama Mkuya.
Mjasiriamali huyu, ameweza kutengeza unga unaotokana na kiini cha ubuyu, ambao hutumika kama kiungo cha mboga kama ilivyo kwa karanga.
Pia kwa kutumia mbegu hizo za ubuyu, ameweza kutengeneza mafuta ambayo hutumika kama dawa kupunguza mafuta mwilini.
Si hivyo tu, ameweza kutumia ubuyu kutengeneza sabuni ambayo ni nzuri kupambana na aina mbalimbali za magonjwa ya ngozi.
Kwa mujibu wa Mkuya, ametengeneza dawa kwa kutumia majani ya ubuyu, dawa ambayo husaidia kupambana na maradhi sugu na kuongeza kinga ya mwili hasa kwa wagonjwa wa Ukimwi.
Akielezea jinsi alivyoingia kwenye ujasiriamali, mama Mkuya anasema ujasiriamali kwake uko kwenye damu kwani kwani alianza akiwa msichana mdogo sana, wakati huo alikuwa akiuza biashara ndogondogo gulioni.
“Nilianza kwa kuuza maji ya kunywa kwenye gulio, kisha nikaendelea na kuuza viazi, kadri siku zilivyokuwa zikienda nilikuwa nikibadilisha biashara kulingana na soko langu.” anasema.
Anaongeza kusema kuwa, kila alipoona bidhaa Fulani inasoko kubwa, basi alibadilisha na kuanza kufanya biashara hiyo.

Kuwa mjasiriamali

Mkuya anasema alilazimika kuingia kwenye ujasiriamali akiwa na umri mdogo baada ya wazazi wake kumlazimisha kuolewa baada ya kumaliza elimu ya msingi.
“Baada ya kumaliza elimu yangu ya msingi, baba yangu aliona bora aniozeshe jambo ambalo nilipingana nalo vikali.” anaongeza.
Anasema kutokana na hilo aliamua kukimbilia kanisani na kuamua kuwa Mtawa. Hata hivyo hakudumu kwenye Utawa kwakuwa familia yake ilikuwa kwenye umasikini na yeye ndiye aliyekuwa akitegemewa, alishindwa kuendelea na mafunzo ya utawa na kurudi nyumbani baada ya vuguvugu la kutaka aolewe kwisha.
“Familia yangu ilikuwa ikikabiliwa na umasikini mkubwa, hivyo nikaona ni vyema nikaingia mtaani kwa ajili ya kutafuta pesa.” anaeleza.
Mafunzo
Mkuya anasema baada ya kufanya biashara ndogo ndogo kwa muda mrefu, alibahatika kupata nafasi ya kuhudhuria mafunzo ya ujasiriamali yaliyokuwa yakitolewa na Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO)
“Huko nilijifunza masomo kadhaa ya ujasiriamali kama vile usindikaji wa vyakula, ufungasahaji, uhifadhi na pia namna ya kutafuta masoko kwa ajili ya bidhaa ninazoweza kusindika.” anasisitiza.
Ujuzi alioupata Sido ulitosha kabisa kumfanya kuwa mjasiriamali ayekomaa kwani alianza kufanya biashara mbalimbali kama kusindika karanga na mama lishe.
“Sifa ya mjasiriamali ni kujifunza. Kila siku sikusita kujifunza vitu vipya, nilikuwa nikitamani kuingiza bidhaa mpya katika soko langu mara kwa mara, hapo ndipo niliposhawishika kuanza biashara hii.” anaeleza.
Anasema awali alianza kwa kuuza ubuyu na unga wake kwa wateja waliokuwa wakitoka Dar es Salaam.
“Wakati nikiendelea na ujasiriamali wangu,walipokuja Wajapani na kutufufundisha jinsi ya kusindika ubuyu, hapo ndipo nilipopata utaalamu wa kukamua mafuta ya ubuyu pamoja na kutengeneza bidhaa zake.” anaeleza.
Mafanikio
Anasema alianza akiwa na mtaji mdogo wa Sh50,000, lakini hivi sasa mtaji wake umeongezeka na kufikia zaidi ya shilingi milioni moja, huku akiwa ameajiri watu sita anaofanya nao kazi.
Mkuya ni mama wa watoto wawili, alizaliwa mwanzoni mwa miaka ya sabini akiwa mtoto wa kwanza kwenye familia ya watoto wanne.
Nimetumiwa na http://varsitycollegetz.ning.com Source: Mwananchi

2 comments:

  1. Hakika ajaribuye hufanikiniwa.Asante kushirikisha wadau katika uzoefu wako.
    @Yasinta asante sana kwa kuibua vilivofichika.

    ReplyDelete
  2. Nashukuru sana kwa maelezo yako. Nataka kuuliza kuhusu mafuata ya ubuyu. Nimesoma kwenye website sites nyingine za ndani na nje ya Tanzania. Inavyoonekena mafuta ya ubuyu wanatumia sana kwaajili ya vipodozi vya ngozi na nywele. Ila wachache wanasema pia unaweza ukanywa. je ni sahihi kunywa mafuat mabichi na je hayana madhara mwilini? kwa sababu ni mabichi na vile hatujui utengenezaji wake unapitia njia gani. Naomba ushauri tafadhali

    ReplyDelete