Ndugu zangu,
Msanii Remmy Ongala alipata kuimba;
" Ukiwa na roho mbaya,kweli tutakuogopa,
Ukiwa na roho mbaya, huko unakokwenda nako ni kubaya!"
Siku zote, mwanadamu usijaribu kufanikiwa maishani kwa kuwa mbaya kwa wengine. Ndio, kuna waliofanikiwa maishani kwa kuwa wabaya kwa wengine.
Siku zote, mwanadamu aliyefanikiwa kwa kuwatendea maovu wanadamu wenzake hawezi kuwa ni mtu mwenye furaha na amani maishani. Ataandamwa na jinamizi la maovu yake mpaka atakapoingia kaburini.
Je, mwanadamu huyo afanye nini?
Ajitazame mwenyewe. Aache kuendelea kuwatendea mabaya wengine katika kiu yake ya kukifikia ’ kilele cha mafanikio’- kama kweli kipo humu duniani! Hivyo basi, mwanadamu huyo atakuwa amejitambua. Na kwa vile naye ni mwanadamu, basi, hakuna mwanadamu asiyetenda makosa.
Dhambi kwa mwanadamu huyo itakuwa ni hulka yake ya kuendelea kuwakanyaga wanadamu wenzake katika juhudi za kuyafikia mafanikio yake. Misaada kwa yatima na masikini haitasaidia kuzifuta dhambi zake, maana, amezifanya na bado anaendelea kuzifanya.
Je, kwanini mwanadamu anakuwa ni mtenda maovu?
” Kwenda huko, utakufa kwa roho yako mbaya!”. Hiki kilikuwa ni kibwagizo katika moja ya matangazo ya kijamii redioni miaka ya karibuni.
Nilipata kumwuliza msanii Mrisho Mpoto swali la kifalsafa; ”Je, binadamu tunakufa kwa roho mbaya au roho chafu?”
Mpoto ananijibu: ” Kaka Maggid, naiona mantiki ya swali lako. Kama nitakunjua viganja vyangu na kuitema roho yangu kisha nikaiangalia... lakini fafanua kwanza fikra zako.”
Nikafafanua, kuwa binadamu hatukuumbwa kuwa wengine wana roho mbaya na wengine nzuri. Sote tumeumbwa na roho nzuri isipokuwa mazingira ndio yanayotufanya wengine tukawa na roho chafu na wengine roho safi. Ndio, roho nzuri tulizoumbwa nazo zinachafuka. Tunakuwa ni binadamu wenye roho chafu. Na hakika, Watanzania wengi tunakufa kutokana na roho chafu, zetu wenyewe au za wenzetu.
” Mh!” Anaguna Mrisho Mpoto. Ananiacha niendelee.
Maana, ni mtu mwenye roho chafu tu anayeweza kujaribu kuyazuia mabadiliko yatakayomsaidia mwanadamu mwenzake atoke mahali alipo na apige hatua itakayomsaidia maishani.
Ni mtu mwenye roho chafu tu atakayeweza kuhujumu mradi wa kuangamiza Malaria inayosababisha vifo vya maelfu ya watoto na watu wazima ili apate mafanikio binafsi.
Ndio, kuhujumu mradi wa kuzuia malaria ili apate fedha za kufanya mambo ya fahari au hata kununua uongozi wa kisiasa au kuendelea kubaki madarakani.
Kwa mwanadamu, ni heri ufe kwa kupambana na anayehujumu mradi wa kuangamiza malaria kuliko kufa kwa malaria inayotokana na mbu anayesababisha malaria.
Naam, You do not win by being bad. Utakwama njiani. Na hilo ni Neno La Leo.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
0788 111 765http://mjengwablog.com/
Nimetumiwa na Maggid Mjengwa.....
Ahsante sana kwa neno la leo lenye mafunzo!
ReplyDeleteKiasili sisi sote tumeumba katika hali ya kukosa ukamilifu na kutenda ubaya ndiyo jambo kuu katika maisha yetu ya kila siku.Jitihada ni muhimu sana ili tuweze kutenda yaliyo mema.
ReplyDelete