Karudi Baba mmoja, toka safari ya mbali
Kavimba yote mapaja, na kutetemeka mwili
Watoto wake wakaja, ili kumtaka hali
Wakataka na kauli, iwafae maishani.
Akatamka mgonjwa, ninaumwa kweli kweli
Hata kama nikichanjwa, haitoki homa kali
oho naona yachinjwa, kifo kimenikabili,
kama mwataka kauli, semani niseme nini.
Yakawatoka kinywani,maneno yenye adili,
Baba yetu wa thamani,sisi tunataka mali,
Urith tunatamani,mali yetu ya halali,
Sema iko wapi mali, itufae maishani.
Baba aliye kufani, akajibu lile swali,
Nina kufa maskini, baba yenu sina mali,
Neno moja lishikeni, kama mnataka mali,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.
Wakazidi kumchimba, baba mwenye homa kali,
Baba yetu watufumba, hatujui fumbo hili,
Akili yetu nyembamba, haijajua methali,
Kama tunataka mali, tutapataje shambani.
Kwanza shirikianeni, nawapa hiyo kauli,
Fanyeni kazi shambani, mwisho mtapata mali,
Haya sasa buriani, kifo kimeniwasili,
Kama mnataka mali mtayapata shambani.
Alipokwisha kutaja, fumbo hili la akili,
Mauti nayo yakaja, roho ikaacha mwili,
Na watoto kwa umoja, wakakumbuka kauli,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.
Fumbu wakatafakari, watoto wale wawili,
Wakakata na shauri, baada ya siku mbili,
Wote wakawa tayari, pori nene kukabili,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.
Wakazipanda shambani, mbegu nyingi mbalimbali,
Tangu zile za mibuni, hata zitupazo wali,
Na mvua ikaja chini, wakona na dalili,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.
Shamba wakapalilia, bila kupata ajali.
Mavuno yakawajia, wakafaidi ugali,
Wote wakashangilia, usemi wakakubali,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.
Wakawanunua ngómbe, majike kwa mafahali,
Wakapata na vikombe, mavazi na baiskeli,
Hawakuitaka pombe, sababu pombe si mali,
Kama mnataka mali, mtayapata shambani.
Wakaongeza mazao, na nyumba za matofali,
Pale penye shamba lao, wakaihubiri mali,
Walikiweka kibao, wakaandika kauili,
KAMA MNATAKA MALI, MTAYAPATA SHAMBANI.
Ahsante kaka Mjengwa kwa kunikumbusha shairi hili ni kweli mimi nizikumbuka beti zote na ilikuwa darasa la nne nikumbukavyo mimi. kulikumbuka Shairi ni kutokana na hapa.
Hakika leo ni moja ya zile siku ambazo huwa nakuwa na furaha sana. Maana shairi hili lilikuwa ni kama vile sala ya baba yetu kwangu mpaka nikawa nakatazwa kuliimba/kulisema. Ahsante kwa kunikumbusha nashangaa sijui kwanini sikukumba mapema?
ReplyDeleteKweli dada Yasinta, shairi hili , enzi hizo....lilikuwa kama nyimbo, na kumbuka enzi hizo vitabu vichache...lakini mambo ya makubwa.
ReplyDeleteShukurani ndugu yangu!
Binti Nangonyani asante mngoni wetu kwa kuonyesha kuwa wa kulekule kwa akina monile.Wangoni kwa sanaa ya ngoma,nyimbo na mashairi wapo katika chati ya juu kabisa.Nakumbuka mara ya kwanza kuwafaidi nilipokutana nao kwenye msiba wa watani zao wamakonde.Waliingia usiku mkubwa wako safi na mirindimo yao huku wakiuvamia uwanja kwa ngoma nzito na kuvuruga kila walichokiona mbele yao.Maji yote yalimwagwa na uwanjani pakawa hapatamaniki tena kwa kulala.Kwa hiyo wewe mrembo wao uliyehamishiwa ughaibuni katika ardhi ya waswedi leo hii kuja na mashairi kila ukiamka hainipi homa wala presha na zaidi sana ni vunja mbavu hadi Ruhuwiko.Wasalimie sana shemeji zetu huko na waambie kuwa:"JASIRI HAACHI ASILI NA MUACHA ASILI NI HASIDI NA HANA AKILI".
ReplyDeleteDada hili shairi nimelipenda na linanikumbusha miaka ya nyuma nilipo kuwa darasa la tatu kama siko sahihi basi mtanirekebisha kwani kipindi hiki elimu ilikuwa raha kwani hata ukienda bila kuvaa viatu huulizwi na pia vitabu hivi vilikuwa vikitufanya tupende kuhudhuria shule na kusoma vitabu malimbali.KAMA NINGEKUWA MSEMAJI KWENYE IDARA YA ELIMU NENGEPENDEKEZA MITAALA YA ZAMANI IRUDI NA KUTUMIKA.ASANTE!
ReplyDeleteNi kweeli na niraha sana kusoma shairi hili nakumbuka mbali sana enzi hizo nilikuwa napenda kachori za sh.10 sinabudi kusema litaendelea kudumu na kywa shairi bora miaka yote kwa kitabu cha kiswahili darasa la nne(4)
ReplyDeleteSijui nimewaza nini Leo mpaka nimefika hapa.
ReplyDeleteShair hili huwa nawaimbia wanangu
ReplyDeleteKuna lile Shairi la 'Bendera ya Taifa' maarufu "NDEGE HUYU NDEGE GANI?"
ReplyDeleteTafadhali kama kunaanayelikumbuka au linapatikana pahala fulani aweke link hapa,
Pia kuna shairi lingine ilikuwa ni beti tatu tu ikiwa inamalizia habari fulani ktk kitabu cha kiswahili darasa la sita kama sikosei, beti mbili za mwanzo ni hizi;-
"1_Sisi vijana hodari, tulio hapa kambini.
Twaishi bila jeuri, ingawa tuko porini.
Twalijenga Jamhuri, kwa jasho letu
Nchini.
Jamhuri letu tukufu, nguzo ni sisi vijana.
2_Nguzo ni sisi vijana, tujengao
Jamhuri.
Hatutaki kupigana, wala kufanya kiburi.
Tunataka kuungana, tutende mambo vizuri.
Jamhuri letu tukufu, nguzo ni sisi vijana.
3_.......!"
Ubeti watatu nimeusahau.
Habari ilikuwa inawahusu vijana waliokuwa kambini, sijui ni vijana wa jeshi la kujenga Taifa wale hata sikumbuki....
Kweli "YA KALE DHAHABU"
Tupo tayari vijana kujenga taifa letu
DeleteHatutaki kupigana wala kufanya kiburi
Tunataka kuungana tutende mambo vizuri
Jamuhuri yetu....
Ama kweli ya kale ni dhahabu,nakumbuka nilikuwa napenda sana shule kwa sababu ya kuimba mashairi na walimu walikuwa wanajituma sana
ReplyDeleteShairi
ReplyDelete