Wednesday, January 25, 2012

Madaktari watangaza mgomo nchi nzima

MADAKTARI wametangaza rasmi kuanza mgomo katika hospitali zote za rufaa na vituo mbalimbali vya afya nchini kote hadi hapo madai yao yatakaposhughulikiwa na Serikali.
Pia wamepitisha azimio la kumtaka Rais Jakaya Kikwete kuifumua na kuiunda upya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kuwaondoa kwenye nyadhifa zao Waziri Dk Haji Mponda na Naibu wake, Dk Lucy Nkya kutokana na kile wanachodai kuwa ni kudhalilisha taaluma yao.Dk Uliomboka pia aliwataja Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa kwamba wanapaswa kuwajibishwa na Rais.
Akitangaza mgomo huo, Dar es Salaam jana Mwenyekiti wa Kamati ya Muda ya Jumuiya ya Madaktari hao, Dk Stephene Ulimboka alisema hatua hiyo inalenga kupata ufumbuzi wa madai waliyotoa kwa muda mrefu na kuongeza kwamba, leo wanatarajia kukutana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Dk Ulimboka alitaja baadhi ya madai yao kuwa ni kuwawekea mazingira bora ya kazi madaktari kwa kupeleka vifaa vya kazi hospitalini na kwenye vituo vya afya, kuboresha malipo ya posho na kuwapatia sitahili zote wanataalamu hao.
Hata hivyo, tafauti na ilivyokuwa awali, kikao cha jana ambacho kilikuwa cha majumuisho, kilitumika pia kupokea ripoti ya mikutano iliyokuwa ikiongozwa na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) na kupokea majukumu ya kuongoza harakati hizo.
“Kuanzia leo tunatangaza kuwa madaktari wote wanaoguswa na hili kote nchini kuacha kufanya kazi hadi hapo Serikali itakapotekeleza madai yetu, tunataka Serikali iboreshe mazingira ya kutolea huduma za afya, ili kumwezesha daktari kumpatia huduma mgonjwa katika kiwango kinachostahili,” alisema Dk Ulimboka.
Alitaja madai mengine matatu ambayo kamati anayoiongoza inasimamia kuhakikisha yanatekelezwa kuwa ni pamoja na madaktari kurejeshewa nyumba za kuishi kama inavyoelekezwa kwenye ‘Standard order’ ya Serikali, ambayo inasema daktari atapatiwa nyumba ya kuishi na Serikali na kama sivyo atapatiwa asimilia 30 ya mshahara.
Alisema kipengele hicho kiliondolewa kinyemela bila wao kushirikisha wala kuelezwa sababu za kuondolewa kwake, jambo linalowaongezea ugumu wa maisha na kuwafanya wadharaulike.
Madai mengine yalihusu nyongeza za mishahara, ambayo alisema kumekuwa na ugumu wa kutekeleza suala hilo kila mara hadi wanapofanya mgomo.
“Mwaka 2005 wakati tunaanza kazi, mshahara wa daktari ulikuwa unafikia Sh124, 000, lakini baada ya mgomo ndipo ukapandishwa hadi kufikia karibu ya laki 700,000 sisi tunataka suala hili lirekebishwe na nyongeza yake isisubiri shinikizo,” alisema.
Madai mengine ni malipo kwa madaktari pindi wanapofanya kazi katika mazingira hatarishi na kupendekeza walipwe asimilia 30 ya mshahara wao, posho wakati wa kazi ya ziada ambayo kwa sasa wanalipwa asimilia 10 ya mshahara wao.
Kuhusu mshahara, alisema yapo mapendekezo ambayo alisema wataitaarifu Serikali watakapokutana na viongozi wake.
Madaktari hao leo wanatarajia kuendelea na mkutano wao katika ukumbi wa Don Bosco.Rais wa MAT, Dk Namala Mkopi alisema alikabidhi majukumu kwa kamati iliyoundwa na wanachama baada ya kuonekana kuwa hadi sasa Serikali imekuwa ikiwazungusha.
“Wanachama wamesema hapo mlipofikia tunashukuru mmejitahidi vya kutosha na sasa tunaomba mtukabidhi majukumu ili shughuli hii iweze kusimamiwa na kamati ya madaktari,” alisema Dk Mkopi.
Hatua hiyo imelenga kuongeza wigo wa washiriki ambao watawahusisha madaktari wasio wanachama wa MAT na wafanyakazi wengine katika sekta hiyo ya afya.
Chanzo: Gazeti la Mwananchi.....kupitia http://simulizi.blogspot.com/.

2 comments:

  1. Kwa sasa hali ni tete na tulipofikia ni busara itangulie sheria.

    ReplyDelete
  2. Wanaoumia ni wagonjwa.
    Ingekuwa watu wote wakiwamo hao akina nanihii wanatibiwa hapahapa, nafikiri heshima ingekuwepo

    ReplyDelete