Thursday, September 15, 2011

KUMBUKUMBU NILIPOKUWA MDOGO/KACHIKI!!!

Mti wa mbura ukiwa na matunda yake bado mabichi





Leo nimekumbuka nilipokuwa kabinti kadogo (kachiki). Wakati huo nikiishi Lundo kando ya ziwa nyasa. Lundo kwa asili kuna miti mingiii sana ya mibuni/mbura, hii ni aina ya miti inayozaa matunda madogomadogo ya njano.

hapa zikiwa zimeiva tayari


Matunda haya huliwa kama yalivyo, pia nakumbuka tulikuwa tukiyatwanga kwenye kinu ili kupata urahisi wa kupata juice yake ambayo ni tamu haswa.
Pia hizi mbura zikikauka ni karanga tamu sana zipo ndani yake. Namna ya kuzipata hizo karanga hizo, ni kwamba:- unaweza kuzibangua kwa kutumia shoka, au jiwe (kienyeji).
Sasa siku moja mchana, kama sikosei hata shule nilikuwa sijaanza maana nilikuwa bado kachiki, lilinitokea tukio ambalo kamwe sitakuja kulisahau katika maisha yangu.
Naomba muungane nami katika simulizi ya mkasa huo, maana naona mnaanza kujiuliza ni nini kilimtokea binadamu huyu?
Ilikuwa hivi…….Nilikuwa na rafiki yangu aitwaye Puna Mahecha, huyu alikuwani shoga yangu hasa maana tulikuwa kama Kurwa na Doto. Basi Bwana, siku hiyo ya tukio, nakumbuka ilikuwa ni baada ya kuushindilia Ugali kwa Samaki na Matembele, tukatoka na shoga yangu kwenda kutafuta hizo Mbura. Sasa baada ya kukusanya Mbura zetu za kutosha, si mnajua mambo ya kitoto, tukaanzisha mchezo wa kulenga shabaha kwa kutumia zile Mbura ili kupima kama ni nani mwenye shabaha zaidi ya mwingine. Tukawa tunawekeana zamu………Puna-Yasinta, Puna -Yasinta nadhani tulifanya hivyo zaidi ya mara mia moja.
Ikafika zamu yangu tena, mara hii Puna akalenga bwana… Tapu……... Weee bwana wee kulichirizika damu.! Hapo ujanja wote ukaniishia na kilio kikawa kikubwa kweli. Bahati mbaya zaidi ilikuwa ni mkono wa kulia. Kwa hiyo sikuweza kula ugali kwa siku kadhaa kwa kutumia mkono huo. Sijui kama ningekuwa nimeanza shule ingekuwaje?...Nimekumbuka kisa hiki kwa vile nilikuwa nafanya kazi fulani nikajitonesha na kuhisi maumivu……….Mweh…hata baada ya miaka yote hii? Kweli michezo ya utotoni ina raha na hasara zake.Puna kama upo popote pale na unasoma simulizi hii nitafute rafiki yangu. Nitafurahi sana. Rafiki ni bora kuliko Mwanasesere.

3 comments:

  1. Aisee mbona umenikumbusha mbali sana kuhusu hayo mabuni,nikiwa shule ya msingi nimekula sana na kutwanga kutengeneza juice.Lakini ajabu siku hizi nikienda nyumbani Peramiho siyaoni tena.Shukrani kwa kumbukumbu nzuri,usengwili!
    Rehema Mahundi

    ReplyDelete
  2. CHE JIAH ISSACK
    Nasema kwanza pole kwani hiyo inadhihirisha kuwa jina lako la kapulya ulianza zamani yaani udadisi siku hizi tungesema mtundu ,hivyo naomba tu tutengenezee juice na mimi nitapenda ile iliyochanganywa na masuku nilipoyaona kwanza nilijua masuku maana pale mlimani lipumba ukitoka kigonsera kwenda mbinga yapo mengi tulikuwa tukifunga kambi ya skauti basi matunda yetu ni masuku tulikuwa tunajisevia barabaraaa
    CHE JIAH ISSACK

    ReplyDelete
  3. Mlongo apa kwa kweli umenikumbusha kutale sana sana sijuwi hatá la kusema. Ubarikiwe sana

    ReplyDelete