Thursday, February 3, 2011

KAZI YA UALIMU: TAALUMA MUHIMU ILIYODHARAULIWA

Mwalimu akiwa darasani anafundisha!!

Katika maisha yangu nimeishi na walimu sana . Kwa hiyo nimekuwa nikijiuliza miaka yote hii mingi. Na nimekuwa nikipatwa na uchungu sana nionapo watu/serikali jinsi inavyoiona kazi ya Ualimu kama isiyo na maana. Kila nikijaribu kufikiri, kazi zote hapa duniani naona hakuna kazi ngumu kama UALIMU.
Fikiria mtoto aanzapo shule hajui kuandika, kusoma wala kutamka a, e, i, o, u. Lakini mwalimu anahenya kwa kila njia na baada ya muda mtoto anaweza kusoma kuandika kutamka silabi zote bila shida kama mtoto si mgumu kuelewa. Na hii sio walimu wa shule ya msingi tu ni kuanzia chekea (vidudu) kule ndio kuna kazi kubwa zaidi.

Kwa nini walimu wanadharauliwa na pia mishahara yao ni midogo sana. Kwa kweli inatia huruma. Mshahara wa kima cha chini Tanzania hivi sasa ni laki moja kwa kweli hii ni halali/uungwana?

Ni juzi tu nimesikia ya kwamba idadi ya wanaoomba kusoma ualimu hapa sweden inapungua kwa kiwango kikubwa sana. Sijui huko tuendako kutakuwa na walimu. Na pia kuna kupunguzwa walimu katika kila shule watapunguzwa walimu 14. Sasa mbaya zaidi wanawapunguza walimu vijana na wazee wanaendelea kufundisha .

Awali nilidhani matatizo ya Waalimu labda ni kwa nchi za Africa pekee, lakini nilipokuja hapa nchini Sweden, ndio nikajua kuwa hata hapa matatiozo ni yale yale, yaani yanafanana kwa kiasi kikubwa sana. Kwa hapa Sweden walimu wanateseka sana na pia hawaheshimiwi kabisa. Wanafunzi wana dharau sana wanawaona waalimu kama ni watani wao, wanajibizana nao, na wakijaribu kuwaelimisha jambo ni wabishi ajabu, na kuwaadhibu kwa viboko hapa nchini Sweden ni makosa. Hapa hakuna viboko kabisa kwa hiyo kiboko ni maneno tu. Tena maneno yaenyewe inabidi yawe mazuri na ya unyenyekevu. Na kama Mwalimu akijaribu tu kupandisha sauti kumkaripia mtoto anaweza akachukuliwa hatua kali za kinidhamu na anaweza hata kupoteza kazi yake.

Kuhusu swala la mshahara:- Kima cha chini cha mshahara wa mwalimu hapa nchini Sweden ni 3,600,000TSh, kwa pesa ya hapa ni 20,000SEK. Kiasi hicho cha mshahara kwa huko nyumbani Tanzania unaweza kuona ni kiasi kikubwa sana, lakini ukilinganisha na maisha ya hapa ni pesa ndogo sana na usipokuwa makini unaweza kushindwa kumudu baadhi ya ghrama za maisha. Hebu angalia mchanganuo wa makato ya huo mshahara pamoja na matumizi ya lazima, kodi kwa ujumla anahitaji kulipa 1,200,000TSH. Baada ya hapo zinabaki 2,400,000TSH. Chakula, bili n.k ni kama 10,000SEK = 1,800,000TSH. Baada ya hapo zinazobaki kabisa ni kama 600,000TSH. Kwa kiwango cha gharama za maisha ya hapa Sweden, bado pesa hiyo ni ndogo sana.

Kwa kweli waalimu wanayo kazi kubwa, lakini mapato madogo wakati kazi ya ualimu ni nzito na ndio mwanzo wa watu kujua kusoma na kuandika. Bado najiuliza, hivi kwa nini waalimu wanadharauliwa kwa kazi hii ngumu ya kuelimisha.?

13 comments:

  1. hata mimi nimejiuliza sana kuhusu suala hili la kazi ya ualimu kudharauliwa. Ngoja tusubiri maoni mengine tuone wanasemaje. Hata katika masuala ya wao kulipwa mishahara yao katika wakati muafaka bado ni tatizo vile vile. Utakuta sehemu zingine walimu hawajalipwa hata mpaka miezi mitatu. je hawa waheshimiwa wanaishije? angalia hiyo picha!! bado mwalimu anajitahidi... kweli yataka moyo.

    ReplyDelete
  2. Ndio maana dunia haieleimiki..mama kama unamdharau muelimishaji utapata nini. Mimi ingekuwa nina uwezo watu makundi mawili ningewajali sana katika masilahi nayo ni WALIMU NA MADAKITARI!
    Sio kwamba wengine hawana umuhimu, lakini hawa naona umuhimu wao ni mkubwa kidogo...

    ReplyDelete
  3. Suala si kudharauliwa bali ujinga wa pande zote! Viongozi walofikishwa hapo walipo na walimu hawaoni umuhimu wa walimu ama umuhimu unakuwepo karibia na chaguzi ambapo hutumika kuchakachua!

    Walimu kutojua umuhimu wao na kudai haki zao ama haki kugandamizwa na 'viongozi' wajinga!

    Kesi ya swedeni na kwingineko ambako huyo wa mshahara wa chini analipa kodi karibia nusu ya mshahara wake ni tofauti na sie huku. Huyo analipa kodi akijua baada ya kustaafu huduma atapewa na serikali lakini huku unakamuliwa kwa kodi halafu unadai vipesa vitakavyokusaidia kununua sanda tu!

    ReplyDelete
  4. Kaka Mrope yaani ukifikiria sana hata la kusema unakosa. Yaani sio miezi mitatu tu hadi sita yote lakini hata hivyo walimu hawakati tamaa.

    emu-3 kweli kabisa ddunia hii haielimiki kwel. Nakubaliana nawe kwamba wafanyakazi wote ni muhimu lakini hawa wawili mmhh....kazi wanayo kumuelimisha mtu na kumponya mtu...

    Kaka Chacha! ulichosema ni kweli baada ya kustaafu ulilipwa lakini zile pesa ni zile ambazo ulikuwa unaweka akiba wakati unafanya kazi.

    ReplyDelete
  5. Mimi ni mwalimu, na nilikuwa na wito wa kuwa mwalimu tangu nilipokuwa mdogo, sijaanza hata shule. Kila siku najitambua kuwa niliitwa na Muumba kuwa mwalimu, na sijawahi kutetereka hata siku moja, pamoja na magumu yake.

    Nitatoa mifano miwili ya magumu hayo. Nilianza ualimu katika chuo kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 1976, baada ya kuhitimu shahada ya kwanza. Baina ya mwaka 1980-86 nilikuja Marekani kusomea shahada ya uzamifu.

    Nilifanya juhudi masomoni, hadi kupata tuzo ya mwanafunzi bora, nikanunua vitabu vingi sana, kwa kuelewa kuwa ndio nyenzo nitakayohitaji wakati wa kurejea tena Chuo Kikuu Dar kuendelea kufundisha.

    Nilirejea nchini ule mwaka 1986 na shehena kubwa ya vitabu. Wa-Tanzania waliniuliza kama nimeleta gari ("pick-up"). Kwa vile sikuwa nimeleta gari, bali hivyo vitabu, waliniona nimechemsha.

    Hii ndio hali halisi, ambayo kwangu ni ngumu. Kwa mtazamo wangu, mwalimu si mtu anayefundisha darasani tu, bali anatakiwa kuwa mfano kimaisha. Nami nilijaribu kuonyesha mfano wa kuthamini elimu.

    Kinachonitatiza akilini ni kujiona ninajaribu kuwafundisha watu ambao akili zao ziko kwenye magari, na hapo darasani wanatafuta vyeti tu waende zao kusaka mali. Si kwamba wanathamini elimu kama elimu. Hawanioni mimi mwalimu kama mtu ninayewapa mfano wa kutambua nini kitu muhimu maishani, yaani elimu.

    Suala la kuwasukuma wa-Tanzania watambue umuhimu wa elimu lina usumbufu na kero nyingi, kama alivyoelezea Profesa Matondo hapa.

    ReplyDelete
  6. Wapendwa, nitapenda kuchangia kwa kutoa hadithi fupi. Hadithi hizo zinaonyesha ubovu uliopo si kwa serikali tu, bali kwa watu wa kawaida, kama Mwalimu Mbele alivyoelezea.
    Mimi pia nilijisikia kuwa na wito toka utotoni. Na baada ya kumaliza Kidato cha 6, nilikacha kazi ya ofisini nilikopangiwa na kujipeleka TTC kwa diploma ya ualimu. Hatimaye nikaingia Chuo Kikuu. Hiyo ni miaka ya 80 mwanzoni.
    Siwezi kusahau ubishi uliotokea baina yetu na jirani yetu wa hapo bwenini. Alidai huwezi kupata Division I na kwenda kusomea ualimu. Utakuwa huna akili. Hakuamini, mpaka tulipomwonyesha vyeti vyetu ambayo vilionyesha ni Division I isiyopingika.
    Wakati huo, nikiwatembelea jamaa hasa Dar es Salaam, wengine walinikatisha tamaa na kusema niachane na ualimu. Ualimu hauna fedha. Tafsiri, hakuna cha kuiba huko wa cha kuhonga. Utaiba nini, chaki?
    Kuna wizi wa mitihani uliokithiri. Na mkumbuke kwamba si watoto wanaoenda kuiba hiyo mitihani. Watu wazima, na pengine walimu wanasaidia. Je, tunawafundisha nini vijana? Jibu: usanii.
    Leo hii tunalaani kwamba matokeo ya mashuleni hayaridhishi, watu hawaandiki Kiswahili vizuri, wala usiseme lolote juu ya kimombo.
    Kila mtoto sasa anasoma kwa mikakati ya kujipatia nafasi ya kuchukua chake mapema, na wala si kufanya kazi hata kidogo.
    Kwa kiasi kikubwa jamii inathamini ufisadi na watu wanawachukia mafisadi kwa sababu tu wao hawajapata nafasi hiyo. La sivyo wangefanya hivyo hivyo.
    Maadili, ndugu. Maadili yetu ni yapi tena?

    ReplyDelete
  7. Hata sehemu ya kuanzia inanikosa,mchango wa prof Mbele unabainisha wazi kuwa ualimu hauna uhusiano wa moja kwa moja na kujilimbikizia mali/kuwa nacho. Hivyo waalimu wanaonekana wanamchango mdogo katika jamii. Jamii inaangalia keki iliyoko mkononi na siyo vinginevyo. Hapa ndiyo mwanzo wa manyanyaso yao. Nakumbu wakati nikisoma walimu pale wele pale kijijini walikuwa wanatengeneza na kuuza pombe (local beer) wakipokezana na wanakijiji wengine ili kuyanusuru maisha yao, kweli ualimu umesahaulikan kwa miaka mingi. Sasa ipi ni njia sahihi ya kututoa hapa tulipo? Chama chetu kimetuacha, na wengine wametuacha! Naibu waziri mmoja mwaka jana aliwahi kusema kama mwalimu anaona mshahara hautosha aache kazi, akatafute inayo lipa zaidi!

    ReplyDelete
  8. Dhana ya walimu kuonekana watu duni, mimi nadhani inakuzwa kuliko uhalisia. Labda kwa sababu ya idadi yao kubwa.

    Madaktari wa tiba hawana kipato cha kuwatofautisha sana na walimu. Hata wanasheria waajiriwa wa serikali hawana kipato cha kutisha.

    Kinachowatofautisha watumishi hao ni fursa za kukwapua mali ya umma! Kwamba mwalimu hana fursa za moja kwa moja kuwa jambazi wa kodi za wananchi.

    Katika mazingira kama haya, tunapomwona kachelewa na heshima yeke haipo kwa sababu tu hana kipato cha kumtosha kumudu maisha wanayoyaishi wafanyabiashara na watumishi wezi wa mali ya umma, tunamjengea nini kichwani mwake?

    Kwa nini tunatafsiri mafanikio kwa kutizama "vitu"? Nini kusudi la maisha? Kushiba pesa?

    Kwa mtazamo wangu, tunawahitaji watu wanaoweza kuihudumia jamii pasipo kutazama wanachokipata. Na watu hawa ni wakupongezwa badala ya kuwaona watu wasio na mwelekeo kwa sababu tu uaminifu wao (unaoisaidia jamii hiyo hiyo inayowacheka) unawagharimu.

    Ukitaka kujua ikiwa jamii inathamini elimu ama la, angalia inavyomchukulia mwalimu.

    ReplyDelete
  9. Uliona wapi mwalimu anafundisha huku akiwa ananjaa,nyumbani hajui wanae watakula nini,kodi ya nyumba hajalipa mshahara hajui atapata lini na hata akiupata ameshakopa anatakiwa kulipa madeni,hawezi kufundisha vizuri na anaowafundisha hawawezi kufanya vizuri,kwasababu hawatafundishwa kama inavyotakiwa.

    ReplyDelete
  10. Fаntаstic goods frоm yοu,
    man. I've understand your stuff previous to and you are just too fantastic. I actually like what you have acquired here, really like what you're saying and thе
    wаy in which you say it. Υou maκe іt enϳoyable and уou ѕtіll care fοr tο keеp it smart.
    I cant wait to read far more from you. Τhis is actually
    a wondeгful websіte.

    Look into my blog post :: instant loans

    ReplyDelete
  11. Нi thеre cοlleaguеѕ, its іmpressive рiесe
    of ωriting сοncerning teаchingand fully explаined, keeρ it
    up all the tіme.

    Mу blog - payday loans

    ReplyDelete
  12. Post writing is also a exсіtement, if you bе acquаinted ωith after that you can
    write if not it is comрlex to wrіte.



    Heгe iѕ my web sitе - Payday Loans

    ReplyDelete
  13. Wonderful beаt ! I wіsh to appгenticе
    ωhile you аmend уоur site, how could i subѕcribе for a blog web site?
    The account aided me a acceptable deаl. I had been a lіttle bit
    acquaintеԁ of this your broadcast offered brіght cleаr iԁeа

    Look at my wеbpage - Same Day Payday Loans

    ReplyDelete