Wednesday, August 18, 2010

Hatua za kuomba nafasi za masomo Ughaibuni

Naamini unaendelea vizuri kabisa na maisha.

Naomba uweke kwenye BLOG/Tovuti yako interview yangu niliyofanya na Gazeti la Mwananchi la August 10th, 2010 kuhusu NONDOZI Ughaibuni.
-------------------------------------------------------------------------------------------------



Makulilo
ALIHANGAIKA kutafuta nafasi za masomo ya elimu ya juu, hatimaye akaja kuipata nafasi hiyo
nchini Marekani. Baada ya kufanikiwa, Ernest Makulilo, Mtanzania anayeishi na kusoma
nchini… ameamua kuwasaidia wengine jinsi ya kuomba nafasi za masomo ya juu katika nchi za
Ulaya na Marekani ikiwa ni mchango wake kama anavyoeleza katika mahojiano haya na
mwandishi wetu.

Swali: Sababu zipi zilikusukuma kuwasaidia wanaotafuta nafasi za masomo nje ya nchi?

Jibu: Kwanza naomba niseme kuwa nilianza kuitoa huduma hii rasmi Julai mwaka 2007, na huu
ni mwaka wangu wa tatu. Sababu kubwa ya kuingia katika huduma hii ni kwa kuwa nilihangaika
sana kutafuta nafasi za masomo hadi kufanikiwa kuja hapa Marekani. Hivyo nikawa na taarifa
nyingi za mtu unawezaje kupata nafasi hizi kwa Marekani na Ulaya.

Sikuona kama ni jambo la busara kwa kuwa mimi nimehangaika basi na wengine nao
wahangaike, hivyo niliamua kurahisisha njia ya watu wanaopenda kutaka kusoma zaidi kwa
kupata udhamini ughaibuni.

Kitu kingine kilichonisukuma kujikita katika suala hili ni kuwa na blog (gazeti tando) mahsusi
kwa ajili ya kuweka taarifa za misaada ya masomo kwa watu wa nchi maskini.

Niligundua kuwa blog nyingi zilizopo Tanzania zina vitu mchanganyiko, nikaonelea ni vema basi
nianzishe kitu ambacho mtu akisema anataka nafasi za masomo basi ajue wapi pa kwenda na
kupata msaada.

Swali: Ukoje mwamko wa Watanzania katika kupata taarifa za vyuo ambazo wewe umekuwa
ukizitangaza?
Jibu: Mwamko wa Watanzania ni mdogo sana tofauti na mataifa ya Afrika Magharibi, Amerika
ya Kusini na Asia. Watanzania wengi bado wana ile dhana na kasumba kuwa ili mtu aende Ulaya
au Marekani kusoma ni lazima atoke katika familia tajiri au ya kisiasa. Hivyo wengi hukata tamaa
mapema. Kitu kingine kinachosababisha mwitikio mdogo kutoka kwa Watanzania ni wengi wao
kukosa ari ya ushindani kama ilivyo kwa Wakenya na watu wa nchi za Afrika Magharibi.

Ukiachilia hayo, wengi hudhani upatikanaji wa nafasi hizi ni kitu rahisi mno. Ninapompa mtu
taratibu za vitu gani ajiandae navyo ili aweze kuwa mshindani mkubwa na kufanikiwa kupata
nafasi, wengi hukata tamaa. Baadhi ya Watanzania tunapenda vitu mteremko sana wakati
uhalisia si huo tena. Dunia hii ni ya ushindani, inabidi Watanzania tubadilike, tuendane na
ushindani uliopo katika dunia ya kibepari. Tuachane na fikra za kijamaa)

Swali: Je wewe ni wakala wa vyuo au unaiendesha vipi huduma hii?
Jibu: Mimi si wakala wa chuo au taasisi yoyote ile. Na hakuna mtu, chuo au taasisi yoyote ile
inayonilipa kwa huduma hii. Naiendesha huduma hii kwa imani kwamba kuna watu wana ndoto
kubwa za maisha yao, lakini ndoto hizo mara nyingi hufa kutokana na ufinyu au ugumu wa
upatikanaji wa elimu ya juu Tanzania na katika nchi nyingi zinazoendelea. Hivyo ninachokifanya
ni kuhakikisha watu hawa wanatimiza ndoto zao za kielimu na maisha yao kijumla.

Aidha nimekuwa nikizipitia tovuti mbalimbali za vyuo na taasisi ambazo zinatoa udhamini wa
elimu kwa watu wanaotoka nchi zinazoendelea. Nikishapata taarifa hizi, nazichuja kwa umakini
na kuzihakiki kisha nazitangaza kwenye tovuti zangu ambazo ni www.makulilo.blogspot.com
na www.scholarshipnetwork.ning.com. Kwa wale wenye maswali zaidi kuhusu taarifa fulani
niliyoitangaza huniandikia barua pepe nami huwajibu kwa kutoa ufafanuzi husika.

Swali: Nani hasa walengwa wa huduma zako na kwa nini?
Jibu: Walengwa wakuu ni watu wenye nia na sifa ya kufanya shahada za Uzamili na Uzamivu,
kwa Kiingereza Masters Degree na PhD. Kuna nafasi nyingi za makundi haya mawili kuliko
wale wanaotaka kusoma shahada ya kwanza.
Kwa digrii ya kwanza, inakuwa ngumu kupata udhamini kwa kuwa sababu nchi zote ambazo
lugha mama si Kiingereza, hutumia lugha zao kama Kijerumani, Kifaransa na nyinginezo
kufundishia katika daraja hili.
Hali hii huwa kikwazo kwa waombaji wengi kwa kuwa wanalazimika kujifunza lugha hizi na
baada ya kufaulu mitihani ya lugha ndio upate nafasi. Nchi zinazotumia lugha zao za ndani ni
kama Sweden, Denmark na Ujerumani. Lakini kwa shahada ya pili na tatu, nchi hizi zimekuwa
zikitumia pia Kiingereza

Swali: Kwa hiyo unawaeleza nini Watanzania kuhusu hali hii?
Jibu: Ninachowaambia wasome shahada ya kwanza Tanzaniaa au katika nchi nyingine za Afrika
kisha shahada ya pili na tatu waende Ulaya, Marekani au nchi za mabara mengine.

Swali: Kuna watu wengi wanaotumia njia hii ya mitandao kutafuta na kuomba nafasi za masomo
bila mafanikio, nini sababu?
Jibu: Kuna sababu nyingi zinazomfanya mtu akiomba asipate. Hili nitalifafanua kwa
kirefu.Kwanza watu wafahamu kuwa kupata nafasi za masomo ughaibuni si jambo la bahati bali
vigezo na kufuata taratibu husika. Kwa kukosa vigezo au kwa kushindwa kufuata masharti, wengi
wamekuwa wakikimbilia kusema kuwa hawana bahati au kuna upendeleo.
Kwa mfano ili mtu aweze kupata udahili na kisha udhamini, vitu vifuatavyo ni muhimu:Mosi,
matokeo bora ya vyuo, vyuo vingi vinataka wastani wa daraja la pili la juu yaani Upper Sercond
kwa Kiingereza.Pili, mwombaji aandike malengo yake kwa umakini na ufasaha kupitia kitu
kiitwacho
Statement of Purpose/Interest. Ukiandika kwa kulipua hata kama una matokeo mazuri, sahau
kupata udhamini.

Tatu, kuna kitu kinaitwa Writing Sample, hii ni kazi ambayo umeshawahi kuandika kama insha
au utafiti wowote ule wakati unasoma. Lengo lake wanataka kujua uwezo wako wa kuandika
mambo ya msingi. Nne,ni barua ya kukupendekeza kutoka kwa walimu wako au mahala
unapofanyia kazi.Hawa nao wanapswa waiandike vizuri, waonyeshe uwezo wako wa taaluma na
kazi.

Pia kuna zoezi la kupima uwezo wa lugha kwa muombaji. Uingereza wana mitihani ya TOEFL na
IELTS, wakati Marekani wana mitihani kama GRE na GMAT. Waombaji wahakikishe vyeti vyao
vimethibitishwa uhalali na wakili au mahakama kama si nakala halisi.
Baada ya hatua hii na ukishakuwa na vigezo, omba vyuo ila kumbuka vyuo unavyoomba viwe
vimeshatangaza udhamini wa masomo kwa wanafunzi kutoka nje ya nchi husika.
Lakini pia mwombaji asitosheke kuomba chuo kimoja. Anatakiwa kuomba vyuo zaidi ya ishirini
ili kuwa na uhakika wa kupata udhamini mkubwa na ulio mzuri.

Swali: Unanufaika vipi kama mtu binafsi kwa kuendesha huduma hii?
Jibu: Mafanikio makubwa ninayopata ni kuwa na furaha ya kweli kutoka moyoni. Ninafurahi sana
watu wanapozipitia tovuti zangu, kuzifanyia kazi na kisha kufanikiwa. Furaha hii ni zaidi ya pesa
kwangu, maana mimi kujua mbinu hizi si kwa ujanja au werevu nilionao kwa wengine. Kwa
kuwa Mwenyezi Mungu kanipa maarifa haya, sina budi kuyafikisha kwa wengine wanaotafuta
elimu au maisha.Moyo huu ndio ulionisukuma pia kuanzisha mfuko wa kijamii utakaoitwa
Makulilo Foundation kwa lengo la kuongeza wigo wa taarifa na mbinu zaidi za upatikanaji wa
nafasi za masomo.

SOURCE: http://www.mwananchi.co.tz/magazines/33-maarifa/3780-hatua-za-kuomba-nafasi-za- masomo-ughaibuni.html

3 comments:

  1. Tunashukuru sana kwa watu kama hawa, na wewe dada yetu tunakupa shukurani kwa kukiweka hili hewani.

    ReplyDelete
  2. Da Yasinta,

    Asante sana kwa kuweka taarifa hii hapo kibarazani kwako.

    Naamini taarifa hii na nyinginezo za watu kuweza kufanikiwa zitazidi kusambaa na nina imani kabisa watu watazifanyia kazi.

    MAKULILO
    www.makulilofoundation.org
    www.makulilo.blogspot.com
    www.scholarshipnetwork.ning.com
    San Diego, CA

    ReplyDelete
  3. Kumekuwepo na maswali ya hapa na pale, moja ni suala la UMRI wa kuomba.

    Suala la umri ktk uombaji wa scholarships ni muhimu kuliangalia kwa mapana. Kuna scholarships za aina nyingi. Kuna zile ambazo hutolewa na vyuo husika uendapo kusoma. Mara nyingi hizi hazina masharti ya umri kwani kitu cha msingi ni kuwa na vigezo vya kwenda kusoma hapo, na kuwa admitted nk. Na kuna zile scholarships hutolewa na baadhi ya taasisi, sio lazima ziwe za vyuo husika. Hawa wanaweza kuweka kigezo cha umri kutokana na malengo yao ya udhamini wautoa. Hapa wanaweza kusema kwa mfano, mwombaji asiwe na zaidi ya miaka 55.

    Cha msingi kufahamu, hakuna kipingamizi kama kipingamizi kusema kama una umri flani huruhusiwi kuomba na kupewa.

    Note: Kama mtu una swali, usisite kuniandikia msauzi101@yahoo.com AU makulilo@makulilofoundation.org

    ReplyDelete