Sunday, July 4, 2010

NAPENDA KUWATAKIENI WOTE JUMAPILI HII YA KWANZA YWA MWEZI HUU WA SABA NA/ TAFAKARI YA LEO: IMANI KATIKA NENO TAKATIFU


Nabii Eliya katika maombi

Baada ya kutafakari kwa kina nimepata wazo la kuanzisha kipengele cha Tafakari ya Leo, ambacho kitakuwa kikuzungumzia neno takatifu la Mungu. Kipengele hiki kitakuwa kikiwajia kila siku ya Jumamosi ambapo ni siku yangu ya kupumzika na kumtumikia Mwenye enzi Mungu.

Katika kukumbushana huko, nitaelekeza fikra zangu juu ya maandiko matakatifu na hata nukuu mbalimbali kutoka kwa Wanafilosofia waliowahi kuishi hapa duniani wakiwemo Manabii.

Jana nilishindwa kuweka kipengele hiki kutokana na mtandao kupata kwikwi. Lakini kwa kuwa leo mtandao umetulia ninawaletea kipengele hiki kama ifuatavyo, naomba tutafakari kwa pamoja:

Leo ninaanza na somo la imani, hebu tuangalie 1Wafalme 18:42, nitanukuu,
“Naye Eliya akamwambia Ahabu, Haya! Inuka ule, na unywe; kwani pana sauti ya mvua tele”

Mwisho wa kunukuu.

Kama tulivyosoma fungu hilo hapo juu, Nabii Eliya akimwambia Ahabu ainuke ale na anywe kwani pana sauti ya mvua tele.

Ukweli ni kwamba kulikuwa hakuna mvua, pia mawingu yalikuwa hayaashirii kuwepo kwa mvua, pia hata upepo ulikuwa hauvumi kuashiria kwamba kungenyesha mvua. Lakini Nabii huyu wa Mungu Eliya alisema, “Nasikia sauti ya mvua tele”

Kwa kauli hiyo ya Nabii Eliya inanionyesha kuwa katika swala la imani, kusikia ni dalili muhimu kabla ya kuona kile unachokitarajia.

Tatizo la kwa nini sisi tunakuwa na imani haba kiasi cha kutofanikiwa katika kila tulitendalo ni kutokana na kutaka kuona kile tunachokitarajia kabla ya kusikia kwanza.

Nabii Eliya Alisema kuna sauti ya mvua tele, hebu tuliangalie kwa makini neno “Sauti” kwa sababu neno sauti anazungumzia kelele na matokeo yake.

Pia ni vyema ukijua kwamba sauti aliyokuwa akiisikia sio halisi bali ilikuwa ni ya rohoni.
Katika biblia tunasoma kuwa Nabii Eliya alimwagiza mtumishi wake kwenda kuangalia iwapo kuna dalili ya mvua, na mtumishi huyo alikwenda mara sita kuangalia, lakini alirudi na jibu lile lile kuwa kulikuwa hakuna dalili ya mvua.

Labda wewe unayesoma hapa leo uko katika hali hiyo hiyo, umeshajaribu kila kitu na una imani katika kufikia malengo yako lakini imani yako imekuwa ni bure kabisa.

Hakuna kinachotokea na maisha yako yamekuwa ni yale yale, kama vile ilivyokuwa kwa mtumishi wa Nabii Eliya alivyokwenda kuangalia dalili ya mvua mara sita lakini akirudi na jibu lile lile la hakuna dalili ya mvua.

Labda kwa upande wako imekutokea katika kazi yako, biashara zako, ujuzi wako, elimu yako, na unaanza kupoteza imani kwa mungu au unafikiria kuachana na mungu na kutomwamini.

Nataka nikwambie leo hii kuwa kama imani yako ikisema ndio, hakika hata mungu hawezi kusema hapana.

Nabii Eliya alisema,… “Nasikia…” na hakusema….. “Naona….” Hii inaonyesha kuwa Nabii Eliya alikuwa anajua kanuni ya kuwa na imani.

Kwa hiyo na wewe ili dalili ya imani yako kufanya kazi ni lazima kwanza usikie ile dalili ya kupata majibu kutoka kwa mungu ni lazima ujiandae kuisikia dalili hiyo kutoka kwa mungu.

Lakini tatizo walilo nalo waumini wengi ni la kusikia. Katika biblia tunasoma katika Warumi 10:17 “Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo”

Biblia haikusema kuwa “imani huja kwa kusikia neno” Kiasi gani utasikia inategemea na umbali unaoweza kuona.

Hebu tuangalie nyuma kidogo kwenye historia ya Abrahamu katika kitabu cha mwanzo 15:1. Mungu alimwambia Abrahamu “Usiogope Abrahamu, mimi ni ngao yako na thawabu yako kubwa sana”.

Lakini Abrahamu akamwambia mungu, “utanipa nini il hali sina hata mtoto”
Naamini kuwa tunafahamu kuwa hatimaye Abrahamu alikuja kupata mtoto.

Lakini hata hivyo kabla ya kupata mtoto, tuliona jinsi mungu alivyomchukuwa Abrahamu hadi ufukweni kuhesabu mchanga na pia alivyomchukuwa hadi nje wakati wa usiku na kumwambia ahesabu nyota. Unaweza kujiuliza kwa nini afanye yote hayo?

Naamini ni kwa sababu Mungu alitaka kubadili picha aliyokuwa nayo Abrahamu ya kutokuwa na mtoto.

Kwa somo hili naamini wote tumeona ni jinsi gani imani inavyoweza kufanya kazi iwapo tutafuata kanuni kama nilivyoeleza.

Tukutane Jumamosi ijayo……………

Mada hii nimeichukua kutoka kwenye kibaraza cha VUKANI, cha mdogo wangu Koero, nami nimevutiwa nayo nikaona sio vibaya kuirejea ili kujikumbusha. jumapili njema kwa wote.

3 comments:

  1. Aksante sana Sr. Yasinta kwa kutukumbushia NENO la Uzima!!!!!!

    Jumapili njema.

    ReplyDelete
  2. kwamba Eliya alisikia, hivyo hakuona. je tukisema alibuni tu ili kujiogopesha na kuwaogopesha wengine? neno takatifu linakuwaje maana hata mwanzo wa mafunzo ya LESSON ni upagani tangu enzi B.C lakini imekuwa takatifu sasa. Je nalo ni takatifu kwakua linajenga imani ya kusikia siyo kuona? sawa, biblia inasema twaenenda kwa imani siyo kwa kuona. Ni kwanini Yesu aliwajibu wanafunzi wa Yohana kwamba waende wakamsimulie kile walichoona na kusikia? hii ina maana kuona na kusikia ni vitu vinavyoambatana... lakini tunaweza kukitenga kimoja na kingine kwamba unaamini kwa kusikia au unaamini kwa kuona? kama ndivyo tunavyoamini MBONA FUMBO LA IMANI limekuwa na kusikia siyo kuona? maana tunaamini mafungu matatu lakini siyo ya kuona bali kusikia.

    Heeeee haya weeeeeee
    tunashukuru kwa kutuhimiza kusali na kujiombea kwa mungu.

    ReplyDelete
  3. Jumapili njema kwako pia dada Yasinta, mbarikiwe wewe pamoja na familia yako.

    ReplyDelete