STENDI ya Mabasi yaendayo Mikoani ya Ubungo, Dar es Salaam, kama lilivyo jina lake ndimo watu wanaosafiri kwa barabara kwenda mikoani na hata nje ya nchi wanapopandia na kuteremkia.
Shughuli zinazofanywa hapo si hizo tu, kuna biashara mbalimbali na hata huduma kama vile posta, simu, polisi na nyinginezo. Lakini kwa baadhi ya watu hayo ni makazi, ndipo wanapopategemea kwa kila kitu kuanzia malazi mpaka chakula.
Mmoja wao ni Rose Peter ambaye anasema huu ni mwaka wake wa tano akiishi katika stendi hiyo alifika hapo mnamo mwaka 2006 akitokea Same mkoani Kilimanjaro ambako alifunga safari hiyo kwa kile alichoeleza kuwa ni kufukuzwa na mjomba wake baada ya kupata ujauzito ambao wakati huo ulikuwa wa miezi mitatu.
Rose alililewa na mjomba wake baada ya mama yake kufariki wakati alipomzaa. Anasema hajawahi kumuona baba yake mzazi.
Rose anasema kwamba aliponzwa na kijana mmoja anayemtaja kwa jina moja la Jerome ambaye alimpachika mimba lakini baada ya kufukuzwa na mjomba wake, naye alimkana hivyo kulazimika kukimbilia Dar es Salaam... "Nilipomweleza kuwa ni mjamzito alinigeuka na kuniambia hanijui, nimtafute mwanamume aliyenipa mimba hiyo. Alinitisha na kuniamba nikiendelea kumfuata atanipiga.”
Kuona hivyo, alikwenda kwa shiga yake ambaye hata hivyo, hakutaka kumtaja jina ambaye alimshauri kwamba njia bora ni kwenda Dar es Salaam akatafute maisha ili aje kumudu kumhudumia mtoto wake atakapojifungua.
Aliondoka Same akiwa hana mbele wala nyuma, hakuwa na ndugu wala jamaa wa kumfuata Dar es Salaam na haikushangaza kwamba maisha yake Dar es Salaam mpaka leo yameanzia na kuishia hapo hapo stendi ya mabasi.
“Nilitegemea kwamba nikifika huku Dar es Salaam maisha yangu yangeninyookea. Ningepata kazi kirahisi nilijua kwamba kwa kuwa ni jiji kubwa si rahisi kukosa kazi matokeo yake maisha yangu yakawa magumu,” anasema Rose.
Binti mjamzito, anahitaji kula achilia mambo mengine kama malazi ambayo hadi sasa anayepata humo humo katika eneo ambalo limetengwa kwa ajili ya abiria wanaosubiri usafiri. Hali hiyo na ukizingatia kwamba kuna msemo wa hakuna cha bure, amekuwa wakati mwingine akilazimika kutumia mwili wake kupata riziki.
Baada ya maisha kuzidi kuwa magumu hasa baada ya mimba kufikisha miezi minane, aliamua kutoka 'nyumbani kwake' hadi katika Kituo cha Polisi Buguruni kuomba msaada wa kupatiwa mahali pa kuhifadhi walau kulala tu. Aliamini kwamba kwa hali aliyokuwa nayo wangemuonea huruma.
“Namshukuru Mungu walinikubalia nikawa nalala hapo. Kulikuwa na usalama zaidi tofauti Stendi ya Ubungo watu hawakujali hata ukiumwa wanakupita hapo utajijua mwenyewe. Nilikimbilia kule ili kama nikianza kuumwa wanikimbize hospitali,” anasema Rose.
Akiwa kituoni hapo, askari polisi mmoja wa kike anayemkumbuka kwa jina moja la Joyce alimuonea huruma na kumchukua kwenda kuishi naye kwake kwake Ilala.
Alipopata uchungum askari huyo alimpeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili na alijifungua salama mtoto wa kike ambaye alimpa jina la Inura Jerome.
"Afande Joyce alinihudumia vizuri hata baada ya kutoka hospitali. Nilipata huduma zote anazotakiwa kupawa mzazi bila kujali kuwa si ndugu yake. Mwili wangu ulirudi katika hali ya kawaida nilinenepa kama vile sikutoka kujifungua. Kwa kweli ninamshukuru sana ninamthamini kama mama yangu mzazi, hata ndugu zangu wasingenifanyia hivi.”
Baada ya kumaliza miezi miwili anasema mama huyo alimwombea kuishi kwa rafiki yake mwingine wakati huo akijikusanya kumtafutia nauli ya kurudi kwao Same.
Lakini anasema dada huyo alishindwa kukaa naye kwa kuwa mumewe hakuwa tayari kubeba mzigo huo... “Niliambiwa niondoke kwani angeweza kuachwa na mume wake. Niliondoka kuogopa kuachanisha ndoa ya watu.”
Hakuwa na pengine pa kwenda isipokuwa kurudi Stendi ya Ubungo. Lakini safari hii alipokewa kwa mikono ya huruma kwani anasema baadhi ya wasamaria wema walijitokeza na kumpa nauli ya kurudi kwao hasa baada ya kumwona akihangaika na mtoto.
Kwa kuwa maisha yale yalikuwa yameshamchosha, aliitikia wito huo na kupanda basi kurejea kwao. Hata hivyo, adhabu ya mjomba wake ya kumfukuza ilikuwa palepale alimwambia aende kwa mwanamume aliyemzalisha.
“Nilirudi tena Dar es Salaam na kuendelea kuishi Ubungo Stendi. Pale ninalala sehemu wasafiri wanapokaa wakiwa kusubiri mabasi. Hakuna hata ndugu ninayemfahamu,” anasema.
Baada ya kurejea alipata bwana aliyekuwa akifanya kazi katika moja ya gereji ndani ya stendi hiyo... “Alinidanganya kuwa atanioa. Alikuwa anautumia mwili wangu kwa ajili ya starehe zake na alinipa fedha kidogo sana.
"Nikimwuliza mbona fedha unazionipa hazinitoshi hata mwanangu akiumwa nashindwa kumpeleka hospitali ananiambia haya mambo hayataki haraka.”
Ni dhahiri kwamba alikuwa akimhadaa kwani Rose anasema kila walipokuwa wakitaka kukutana faragha wala hawakutoka nje ya stendi hiyo bali kuvizia usiku hasa umeme ukiwa umekatika.
Ukweli wa mapenzi yao ulidhihirika mnamo mwaka 2009... "Nilimwambia kuwa amenipa mimba. Aliikubali lakini matokeo yake aliacha kazi na hayaonekana tena maeneo ya stendi."
Baada ya mimba hiyo ya pili kukua anasema alimfuata mama mmoja 'Mama Saidi' aliyekuwa anaishi Mbagala Kongowe na kumweleza shida zinazomkabili. Alimwomba aka kwake kwa muda na kwamba akishajifungua ataondoka.
Alimkubalia na kuishi hapo hadi alipojifungua mtoto wa kiume aliyempa jina la Gerard na siku nne tu baada ya kujifungua alirejea 'nyumbani' Stendi ya Ubungo.
“Nilikuwa na wakati mgumu fedha sina, ndiyo kwanza mwanangu ana siku nne tu. Ninatakiwa nile chakula cha nguvu ilibidi wakati mwingine kulala na wanaume hivyo hivyo ili nipate pesa ya kula.”
Baada ya kuona kwamba anahaingaika na watoto wawili, mama mmoja anayefanya biashara ya kuuza mikate katika stendi hiyo alijitokeza na kumchukua mwanae na kwenda kuishi naye kwake Buguruni hivyo kumpunguzia mzigo.
Rose hataki kupata watoto tena kwani anajua ugumu wa kuwalea ... “Kwa sasa nimejiunga na uzazi wa mpango ili nisishike mimba mwanangu bado mdogo ana miezi minane.”
Lakini siyo Rose aliyepageuza Stendi ya Ubungo kuwa ni makazi yake ya kudumu: “Pale tupo wengi siko peke yangu. Wanawake tupo zaidi ya 10 na tunaye mzee mwenye umri zaidi ya miaka 60 nimemkuta anaishi pale.”
Rose amechoshwa na maisha hayo. Lakini hana mtaji wala pa kwenda ingawa ndoto yake ni kupata angalau uwezo wa kupanga chumba chake na kufanya biashara halali itakayomwezesha kuwalea watoto wake.
“Nikisaidiwa fedha nitafanya biashara au nikitafutiwa kazi nitafanya, maisha haya ya sasa ni hatari kwani ninaweza kuambulia kupata Ukimwi na wanangu bado wadogo wanahitaji malezi yangu hasa ukiangalia hawana baba. Nikiupata Ukimwi wanangu watalelewa na nani? Hawana ndugu wanayemtambua kama kwetu Same hawatakiwi kuonekana.”
Na Pamela Chilongola wa Gazeti la Mwananch. Habari hii imenigusa sana na nimeona si vibaya nikiweka hapa kibarazani.
Hii story ni ya kusikitisha sana. Natumaini wasamaria wema watajitokeza kumsaidia. Ubovu wa serikali katika kutoa hudumA ya jamii nao ni wa kulaumiwa katika hili.
ReplyDeleteKwa jicho la ndani ninahisi Rose naye ni Mkorofi.
ReplyDelete1.Haiwezekani miaka mitano yooote tena na mimba unaishi nje, ina maana alishindwa hata kuomba kijishamba kwa mjomba wake akaanza kujitegemea. kama ameweza kujitegemea ubungo kweli atashindwaje kijijini ambako amezungukwa na ndugu?
2. Kwanini alikubali kutembea na wanaume hovyo bila kinga na magonjwa haya. Anaenda kuzaa mara ya pili, yaani hata kama mjomba alikuwa anataka kumsamehe ndo kwishne tena. Inawezekana mjomba wake anamfahamu sana mpwa wake huyu.
Bado sielewi ni kwa nini anang'ang'ania mjini ambako hana ndugu.
Mimi ninachoona haitaji msaada wa fedha, anahitahi msaada wa mawazo wa kuweza kujisaidia na wanae. Wazo langu ni kwamba arudi Same alime na kuuza mazao yake mikoani, polepole atasonga mbele.
Mheshimiwa Yasinta naomba kuwasilisha hoja.
Kaka Mrope ni kweli inasikitisha sana na jambo ambalo huwezi kuamini kama ni kweli linaweza kutokea Tanzania yetu yenye kuzoea kuishi kipamoja.
ReplyDeleteDa Mija nakubaliana nawe 100% kwa nini asishike jembe na kulima na kupata chochote hata kama sio cha kuuza lakini angeweza kulisha wanawe. Hata mie nimejiuliza kwa nini ashike mimba tena yaani hakujifunza tu kitu ile mara ya kwanza? Kwa kweli mara nyingine sisi wanawake tamaa zimetuzidi. Duh! kaazi kwelikweli!!