Tuesday, June 1, 2010

‘Housigeli’ anataka kuniharibia ndoa

habari yako. Nategemea mzima wa afya na hutasita kunisaidia kunipa ushauri unaonifaa. Mimi ni mwanamke mwenye watoto wawili. Tangu nimeolewa miaka sita iliyopita, nimekuwa na msichana wangu wa kazi mmoja ambaye nimempenda sana hasa kwa kuwalea vizuri watoto wangu na kuwa mwepesi wa kazi. Kutokana na kuishi vizuri na ‘housigeli’ huyu, amekuwa kama mtoto wa nyumbani na hata ndugu zangu na wa mume wangu wanampenda sana na wamemzoea kupita kiasi.

Tatizo hili la kuwazoea ndugu wa mume wangu sasa naona linataka kuharibu ndoa yangu kwani huyu msichana ameanza tabia mbaya na amemweleza mkwe wangu kuwa mimi situlii nyumbani na sina muda wa kumshughulikia mume wangu kwani kazi zote anafanya yeye, mimi kazi yangu kusafiri na kushinda kazini. Huyu mama mkwe wangu kusikia hayo, amekuja juu na sasa anamshinikiza mume wangu aniache eti nashindwa kuhudumia nyumba na badala yake amuoe ‘housigeli’. Mume wangu ameshtuka na amenieleza kila kitu hali iliyonikasirisha sana.

Sasa naomba ushauri wako kwani mama mkwe bado yupo kwangu, je, nifanyeje kabla hajaondoka kurudi kwake? Mama Kelvin Tabata, Dar es Salaam. Mama Kelvin pole sana kwani inaonekana huyo mama mkwe wako hajaelimika vya kutosha. Uzuri wa mwanamke haupimwi kwa kazi za nyumbani pekee, bali kuna mambo mengi na mkwe wako anapaswa kutambua kuwa wewe unafanya kazi hivyo huwezi kukaa nyumbani muda wote na ndiyo sababu ukatafuta msaidizi.

Lakini pia ni vyema ukiwa nyumbani ufanye kazi zilizopo ikiwamo kumpikia mumeo na kumhudumia ipasavyo. Usiwe na hasira za haraka kwa msichana wako wa kazi kwani inawezekana aliulizwa kimtego naye akajibu vizuri tu lakini mkweo akawasilisha kwa mumeo vibaya. Nadhani mumeo pia anapaswa amweleze mama yake kwa upole kuwa wewe unafanya kazi na huwezi kufanya kazi zote za nyumbani. Pia amweleze kuwa huyo msichana wa kazi kamwe hawezi kuwa mke wa mtoto wake.

Naamini mtoto wake akimwelimisha na akawa na msimamo, mama mkwe wako ataelewa au hata kama hataelewa, atashindwa kuendelea kusisitiza anachotaka. Ni vyema pia ukakaa na msichana wako na kumhoji ilikuwaje hata wakazungumza hayo na mkweo na ukiona kama alichokonolewa basi mtahadharishe akae mbali na mama mkwe na asiwe mwepesi kueleza mambo ya ndani ya nyumba kwa mkweo.

Hata hivyo fanya uchunguzi wako kwa siri na ukiona msichana wako anapalilia ili aolewe yeye, basi ni vyema ukatafuta msichana mwingine wa kazi na huyo kumwondoa ili asije kuharibu ndoa yako. Haina haja kugombana na mtu yoyote kwani naamini huyo mkweo ataondoka na nyinyi mtaendelea na maisha yenu. Pia jifunze kuvumilia kwani wakwe wengine uelewa wao ni mdogo.

Habari hii nimeipata Jamii Forum nimeona si vibaya kama tukijadili kwa pamoja!!

9 comments:

  1. KWANZA hatakiwi kukasirika anaweza kujiumiza tu. inahitaji akili na hekima ili afanye jambo ambalo linamridhisha kuwa anaweza kuihudumia ndoa yake.
    na haina haja ya kuzuka tu kwenda kumvamia mama mkwe kwakuwa kasema hayo, maana wanawake wanatabia hii ya kuzusha vurugu kwa madai ya kulinda upendo wao au kuonyesha wanajali. tulia kabiliana na hilo, panga taratibu zako za kila siku ijali ndoa yako haina haja ya kinyongo, onyesha UNAWEZA

    ReplyDelete
  2. Mama Kelvin, awali nikupe pole kwa mtanzuko na mparanfanyiko mkubwa ndani ya kichwa chako. Japo watu wanaweza wasinielewe kwa hili, lakini wacha niseme tu. Siyo salama kabisa kabisa kuishi na hausigeli kwa muda mrefu achilia mbali hiyo miaka sita.
    Unapoishi naye muda mrefu, watu tunadhani ndiyo ustaarabu ama utu wema sana.

    Asikudanganye mtu, hawa watu after all siyo nduguyo. Akishazowea sana nyumba, anawazowea na wenye nyumba, kisha anajizowesha. Hili ndilo tatizo.

    Kuna mtu aliwahi kuandika katika riwaya moja niliisoma zamani kidogo. Akasema, kisaikolojia, hakuna mtu hususani mwanamke anayependa kwa moyo wake kumsaidia mwanamke mwenzake majukumu ya nyumbanu wakati naye anazo hisia za kuwa mwenye majukumu. Sijui nimeeleweka hapo?

    Nasema hivi, wasichana wa kazi, wakishakaa sana, kama huyo wa miaka sita, akili nazo huwa zinapevuka na wanaanza kujitambua. Kumbuka pengine alikuja kwako baada tu ya kumaliza std seven. Naye anataka.

    Nimeongea sana lakini sijatoa ushauri wangu. Sasa nakupa ushauri mama Kelvin.

    Chukua ushauri hapo juu wa dada Yasinta, kisha wa kaka Markus, kisha huu wangu. Wangu, huyo hausigeli si salama tena kwa ndoa yako (kumbuka ndoa si kitu cha masikhara) nakushauri umrudishe kwao. Kisha kama watoto wako wakubwa kiasi cha kwenda shule bora washinde shule. Wakirudi hawashindwi kujipikia. Ukirudi wampikia baba yao.

    Ingawa mi ni mtoto wa kiume, nilipofika tu drs la tatu, mama aliacha kuweka hausigeli. Kuanzia drs la tatu nilianza kujipikia mwenyewe. Na niliinjoi sana. Wafunze wanao kujitegemea.

    ReplyDelete
  3. Sina zaidi la kuongeza.
    Fadhy..... :-)

    ReplyDelete
  4. Fadhily wewe unafaa kuwa Kungwi hasa, na naona wanawake wengi watafaidika na ushauri wako. Kwa kuongezea tu hapo ulipoachia ni hivi sisi watanzania tuna matatizo ya kuweka mipaka ya kazi na familia. Kama mtu umeamua kuwa ni msaidizi wako wa kazi basi kuwe na mipaka hapo usimfanye tena yeye akawa ndio kama mke mwenzio katika nyumba. Inawezekana kabisa mama mkwe ameona huyo msichana amepita ile mipaka ya kuwa msaidizi wa kazi, pengine hata majukumu mengine ya mume anafanya yeye.

    Pili naomba nisikutishe sana utu uzima dawa huyo mama mkwe kuna kitu cha ziada amekiona humo ndani mwako pengine utani uliopitiliza mipaka kati ya mwanae na huyo binti na inawezekana tu amemuuliza kwa mtego baada ya kuona kuwa huyo msichana tayari amekwishajenga hisia za mapenzi kwa mwanae na hapo anakuamsha wewe uliyelala usingizi wa pono. Hapa naomba unielewe sina maana kuwa mumeo na huyo msichana tayari wana uhusiano la hasha lakini yawezekana msichana wa kazi keshamfia mumeo na mama ameona hizo dalili ndio maana kaamua kuchukua hatua kiutu uzima. Angekwambia direct kuwa msichana wako yuko hivi au vile ungekuja juu na kumuona mama mkwe mbaya lakini hiyo shortcut aliyochukua imekufungua macho wewe pengine na mumeo pia. Hivi mtu anawezaje kukaa ndani ya nyumba na mtu mwingine wa jinsia tofauti bila kujenga hisia za mapenzi, miaka 6? Bidada watafuta nini zaidi? Miaka miwili yatosha ukizidi wa tatu basi, ndio maana wanawake wengi wanatolewa kwenye nyumba zao ili hali bado wanazipenda na wanapenda waume zao. Utakaaje na mwanamke mwenzio ndani ya nyumba moja kwenye wazungu wanasema very confined space ya hivyo vinyumba vyetu jamani wakati sisi ni binadamu wenye viasili vya hisia?

    Mwambie huyo msichana kama amepata mchumba muandalie kitchen party na yeye akajenge unyumba kwake!

    Bi Mkora

    ReplyDelete
  5. Ushauri alioupata Mama Kelvin toka "Jamii Forum" ni wa kitaalamu katika kiwango cha juu sana, lakini akitaka kuongezea kidogo katika kuziba nyufa anazoona zinahitajika kuzibwa, ayachambue makini maoni ya Fadhy na Anonymous.

    Mimi hapa sina cha kuongeza, kila kitu kimesemwa na wenzangu. Ila namalizia kwa kumwomba Mama Kelvin kuwa, awe "Mama Mwema" kwa huyo "Housigeli" kwa kumtafutia kitu cha kufanya, ili kumpatia Maendeleo katika maisha yake, baada ya kumtumikisha ndani mwake tangu utoto wake.

    Amsaidie kumsomesha au kumpeleka japo "Veta" akasomee kitu cha kumsaidia maishani, badala ya kumrudisha kwao kuhangaika na maisha. Tuwe na huruma pia kwa wenzetu walio na maisha ya chini.

    This Is Black=Blackmannen

    ReplyDelete
  6. Ni kweli Mtani Fadhy amesema yote na Bi mkore pia amesema. Binafsi sijawahi kuishi na msichana wa kazi kuanzia mimi mwenyewe nilipokuwa mdogo. Tulikuwa tunajitegeme wenyewe, baba na mama walitufunza kujitegemea tangu wadodo. Na sasa najivunia sana malezi niliyopata. Ahsante baba na mama. Pia sasa nina watoto na watoto wangu hawajawahi kuwa na msichana wa kazi hata siku moja walipokuwa miaka miwili niliwapeleka chekechea na wakawa huko mpaka walipofikia miaka 6 na halafu walianza shule na baada ya masomo kuna aina ya chekechea pale shuleni wanakuwa hapo mpaka mzazi mmoja anapomaliza kazi na halafu anakwenda kuwachukua. Lakini sasa wamekuwa wakubwa na wanaweza kujitegemea wenyewe kwa hiyo wamalizapo shule ni kurudi nyumbani na kutafuta kitu cha kula yaani kama mlo wa katikati. Na maisha yetu yanaenda safi kabisa

    ReplyDelete
  7. Yeah, achunguze vizuri tabia za mama mkwe wake nahuyo house gal,
    Undugu huwa haufi house gal ni mtu wa kupita tu, hivyo basi kama anaona vipi bora atafute house gal mwingine kimya kimya na amwondoshe huyo, kwani house gal akizoea sana nyumba wengine wana kawaida za kutaka kuolewa humo humo.

    ReplyDelete
  8. Jamani msichana wa kazi anatakiwa alipwe mshahara unaostahili, afanye kazi masaa yanayostahili yaani kuwe na mipaka. Mara nyingi sisi watanzania huwa tunapenda mteremko ambao unakuja kuwa cost sana wanawake wengi maana kwa kutaka dezo unamgeuza msichana wa kazi, binamu yako, mdogo wako, dada yako, ili tu umpunje au umnyime haki yake. Sisemi kuwa ni vibaya kuishi vizuri na msichana wa kazi, hapana, ni vizuri sana lakini kuwe na mipaka, hii mambo sijui hata ndugu za mume wangu wanampenda sijui nini shauri yenu, unajua hao ndugu za mume wanampendea nini?

    Wanawake wengi hawajui kuwa iwapo waume zao wanauhusiano nje ya ndoa ndugu za mume ndio huwa wa kwanza kujua, na hata kumkaribisha huyo mwanamke mwingine kwenye sherehe na misiba pia ilhali na wewe unashiriki hapo hapo bila kujua kuwa kuna mwenzio hapo. Sasa huyo mama mkwe kuna kitu kaona hapo ndio kamshauri mwanae afanye kweli kuliko kujificha ficha. Jamani ee tuwafundishe watoto wetu kujitegemea wakishafika umri wa kuweza kukaa peke yao bila muangalizi, haya mambo ya kutegemea wasichana wa kazi yanatuka kututokea puani, mngelikuwa mnakaa nje ya nchi mngepata msichana wa kazi?

    ReplyDelete
  9. Fadhy Mtanga, yaani una akili sana. Sikuwahi kufikiri kabisa ulichosema.

    Lakini mimi naona umefika wakati kwa nchi yetu kuanza kuwa na day care kwa watoto wadogo, ili badala ya kukaa nyumbani masaa yote kushindia tv, bora huko chekechea kunakuwa na activities nyingi za kukuza akili.

    Mama na baba nao wanatakiwa wajifunze kujitegemea, waanze kupika,kufagia na kufua wenyewe. Hii itasaidia pia kuwa na mshikamano wa familia, kiasi kwamba hata Mamamkwe au ndugu wakija wanajua kabisa hii familia imejipanga, ina system. Huwezi tu kuikurupukia na kuleta maneno yasiyojenga maana kila kitu wanafanya wenyewe si baba wala mtoto.

    ReplyDelete