Mpendwa Baba mkubwa,
Salamu ama baada ya salamu mimi huku ni mzima na ninaendelea vizuri. Hofu ni kwenu huko mlio mbali na upeo wa macho yangu.
Madhumuni hasa ya barua hii ni kukushtakia kuhusu tabia ya kaka na dada zangu huko nyumbani. Si hao tu kwani akina shangazi na akina shemeji pia ningependa kuwashtaki kwako.
Baba kama unavyofahamu mwanao siku hizi naishi ughaibuni. Niliwasili hapa miaka kadhaa iliyopita ili niweze kupata kaelimu kidogo na kuboresha maisha yangu na ya ndugu zangu. Namshukuru Mungu kwakweli tangu niwasili hapa nimekuwa bukheri wa afya. Tangu kufika kwangu hapa baba nimejitahidi sana kufanya kazi kwa bidii na kutuma njuluku kidogo huko nyumbani kwa ndugu zangu.Orodha ya niliowatumia pesa hata wewe baba unaifahamu kwani ni ndefu sana. Kusaidiana katika jamii ndio utamaduni wetu kwani nami nakumbuka vizuri akina kaka,dada na shangazi jinsi walivyonisaidia wakati nikiwa sina kazi na bado mwanafunzi. Malalamiko yangu baba si kuhusu kuwasaidia bali jinsi ambavyo wamekuwa hawathamini mchango niutoao katika familia. Je inawezekanaje pesa zote nilizotuma ni mmoja tu ndie kafanya kitu cha maana?? Hata wewe baba unamfahamu ni nani ninamuongelea. Wengine wote pamoja na kuwapa pesa za mitaji waliyoomba hawakuweza kufanya kitu cha maana. Chonde baba nakuomba unishauri nifanye nini kwani nimechanganyikiwa. Nikiangalia katika familia, umaskini ndio unazidi kujikita. Hata pamoja na kuwa tumeweza kupata kauwezo ka kupata tumitaji lakini bado hali inazidi kuwa mbaya. Angalia lile duka pale Tandale, mpwa wangu kalifilisi. Hata lile duka la vipodozi kule Namanga limefilisikaje? Yule aliyeomba mashine ya kusaga kule kijijini ana maelezo gani kuhusu kupotea kwa hizo mashine? Lile pick up kule Kibaha iweje liwe juu ya mawe na lilikuwa linazalisha pesa nzuri tu? Kaka Ubwa yeye ndie alinichosha kabisa. Ati kaenda posta kuchukua pesa za mtaji alizoniomba, akapotea nyumbani wiki mbili. Karudi baada ya pesa kwisha. Jee huu ni uungwana? Je nitaendelea kutuma ada za watoto wa ndugu zangu mpaka lini? Je ulisikia shemeji Makame haongei na mimi ati kwa kuwa nilimuomba anivumilie nimalize mitihani ili nimtafutie pesa aliyotaka? Eti ananiita mimi mpiga boksi!! je haki hiyo baba? Dada Hija huniita mimi ATM ati kila mara awapo na shida basi mimi humtatulia shida zake. Jee Huu ni Uungwana?? Sijasahau siku ile dada Hawa aliponieleza kaibiwa shilingi laki saba alizotoka kuchukua Western Union, ati aliziweka kwenye backpaki na kuiweka backpaki mgongoni. Watoto wanatakiwa shule wiki ijayo, nitatoa wapi pesa zingine? Namthamini sana dada yangu ndio maana watoto wake niliwatafutia shule nzuri?? Jee Baba huu ni uungwana??
Yaliyo moyoni ni mengi lakini kwa leo ni hayo tu. Chonde baba nishauri. Wasalimie wote hapo nyumbani.
Ndimi mimi mwanao
Kimenyanga Kaladamu wa Esimingori
Nimeipenda baraua hii nimekuwa nikipita kwenye kibaraza hiki na kusoma hata sijui ni mara ngapi na leo nimeona si vibaya nikiiweka hapa kibarazani ili wengi tufaidike. zaidi soma hapa . Ahsante sana kaka Mfalme Mrope.
Ahsante sana da Yasinta kwa kushea nasi.
ReplyDeleteUnajua mwandishi wa barua hii ama kwa hakika ana kipaji sana.
Nimesoma na kufurahi sana.
Kaazi kweli kweli, tusipojenga msingi imara, hata nyumba iwe nzuri kiasi gani itaanguka tu.
ReplyDeleteKwa haraka mtazamo wa barua hiyo unaweza ukatafsiriwa kwa namna moja tu, hasa kwa walio ughaibuni kuwasaidia ndugu zao hapa nchini. Lakini hilo linatokea hapa nchini pia .. walio katika miji mikubwa wanasaida ndugu zao walio vijijini, matatizo ni hayo hayo.
ReplyDeleteLakini pia tabia hii inatokea hata katika utendaji wa ngazi mbali mbali za Serikali. Serikali Kuu inaweza kupeleka Ruzuku katika Halmashauri Mbali Mbali .. lakini fedha hizo zisitumike ipasavyo .. Wahisani pia wanapeleka fedha katika Serikali mbali mbali zinazoendelea lakini pesa hizo hazitumiki ipasavyo.
Ni mfumo ambao umejikita katika akili za watu wengi hasa katika nchi masikini. Elimu zaidi inatakiwa na si kazi ya mtu mmoja kubadili fikra na hulka mbaya zilizokuwepo.
hata mimi ninangudu wa namna iyo fanya kwanza mambo ya maana ndipo uwasaidie unaweza kukosa hata pa kuishi kwasababu ya ngudu na ndio hao baadae watakucheka.
ReplyDeleteImenikumbusha mbaliiiiiii,
ReplyDeleteNi kweli sometimes inabore, mtu mmoja kutumika kwenye familia na ukoo mzima kisa eti anazo, jamani kumbuka kusaidiana hata kama hunacho na kuwa na nidhamu na kitu cha mwenzio, kitu kizuri sababu unampa moyo yule anaekusaidia. hebu wote tupendane na kuungana na tubebeane mizigo.sio kufanya uharibifu kisa unajua utasaidiwa tu. je umewahi kujiuliza utasaidiwa hadi lini?
Shukrani kwa wote na hasa kaka Mrope kwa hii barua.
ReplyDelete