Friday, March 26, 2010

Mgomo utamuathiri kila Mtanzania

Tanzania iko katika wasiwasi wa mgomo mkubwa ambao haujawahi kutokea nchini. Wafanyakzi wamekuwa na madai takriban matatu ya msingi ambayo wanataka Serikali iyashughulikie. Dai la kwanza ni Ongezeko la kima cha chini cha mshahara ambapo wameiomba serikali kupandisha kima hicho kutoka sh. 80,000 hadi 315,000 lakini Serikali iliongeza asilimia kidogo sana na ku[pandisha hadi sh. 84,000 tu. Dai lingine wanaomba kodi na makato mbali mbali yapunguzwe na ombi lingine serikali ipanue wigo wa kodi ili kumpunguzia mzigo mfanyakazi.

Kwasababu haya hayajatekelezwa kama walivyoomba sasa wafanyakazi wamedhamiria kugoma nchi nzima kuishinikiza serikali kutekeleza mahitaji yao. Jambo hili ni la hatari kwa mustakabali wa ustawi, maendeleo na usalama wa taifa letu. Hatua hii italeta adha kubwa kwa watanzania wote kuanzia wagomaji wenyewe mapaka ndugu zao. Na kibaya zaidi wananchi wengi wasio na hatia wataumia na wengine watakufa kutokana na madhara ya mgomo huo. Mama lishe wanaoishi kwa kuwauzia chakula wafanyakazi hawatafanya biashara, wanaopata riziki kwa kuosha magari hawatapata ridhiki kwa siku hizo. Wagonjwa watakufa kwa kukosa huduma. na kadhia mbali mbali zitaibuka.

Jambo lingine la hatari ni kuporomoka kwa uchumi wa Tanzania kwani siku za mgomo taifa litapoteza fedha nyingi sana. Madhara hayo yataendelea kwa muda mrefu hata bada ya mgomo huo kwisha Nilifanya mkutano na waandishi wa habari tarehe 22 machi mwaka huu, kuwasihi wafanyakazi wasigome, kuisihi Serikali iyashughulikie malalamiko hayo. Lakini hakukuwa na respond nzuri kutoka vyombo vya habari jambo ambalo limenifanya nihisi kuwa vyombo vya habari vinashabikia mgomo huo. Ni redio chache, na magazeti machache tu yaliripoti.

Kimsingi mgomo utayumbisha nchi na sekta zote. Maana mgomo wa nchi nzima, hata hivyo vyombo vya habari havitauza magazeti maana wafanyakazi ndio wanaonunua zaidi magazeti. Huwezi kukuta mama lishe, mmachinga, mfyatua tofali ananunua magazeti. Kipindi hicho kila mtu atakuwa anatunza hela yake isiishe mapema.

Makampuni mengi yataingia hasara na mwisho wa yote mgomo ukiisha kila sekta itaendelea na msukosuko wake na hatimaye upunguzaji mkubwa wa wafanyakzi utafuatia ili kuweka mambo sawa.

Kugoma ni sawa na kujilipua maana wafanyakazi watawatesa mpaka ndugu zao na watajiathiri wenyewe. Mgomo ni sawa na unamdai mtu halafu unamnyima mapato.

Malamiko haya ni ya msingi sana na serikali lazima isizibe masikio Ni wakati muafaka kwa wafanyakazi kufuta mgomo, kurudi mezani na Serikali ili kila upande ujue madhara na kuchukua hatua muafaka. Watanzania wanasifa kuu ya huruma, upendo na uvumilivu ni vema wajiangalie katika kioo hicho.



Na Jacob Malihoja

5 comments:

  1. Endapo tutshindwa kutatua kero ya leo, basi itakuwa kero ya kesho. Na ednapo tutashindwa kutatua kero ya kesho, basi itakuwa tatizo la leo.

    Kumbuka huu ni mwaka wa uchaguzi ni mwaka ambao do or die lazima serikali iwe kama kobe... lakini kwa maoni yangu, suala hili linaendeshwa kisiasa, limecha njia halisi ya kuwasilisha malalamiko na kugeuka kuwa malumbano.

    Ndiyo hakuna anayependa kuyaona yakiwa hivyo, lakini je sahihi ya kutanzua mzozo ni MEZA YA DUARA watu husikilizana na kukubaliana.

    lakini endapo tunafika meza ya majadiliano tukiwa hatuna hoja bali kumsikiliza mtoa hoja ili akikosea tu tuanze mashambulizi, basi hatujengi tutaendelea kulumbana daima.

    tufanye nini, ni lazima tuongeze shinikizo kwa serikali kukabiliana na hili, lakini shinikizo lenyewe halina maana ya kugomea tu, kwani ni suala la sera.

    Ninaaamini mgomo wa wafanya kazi umeanza kitambo sana ndiyo maana rushwa imeongezeka kupindukia..... kwasabau tu ya kukosa mshahra wa kutosha.... lakini je tuwalipe kama nchi Tajiri?

    ReplyDelete
  2. wagome tu kwani kuna nini wakati wakubwa wao wanajinufaisha?

    Mwalimu kwa mfano anayeanza kazi analipwa 169,000 bila makato na akikatwa NSSF, pay as you earn, earn as you pay, income taxi, tax income, CWT, health, blah blah blah anabaki na nini?

    Huyo kokngozi anayewakataza wasigome apewe sh 80,000 kw mwezi kisha akakae kijijini tuone kana hatarudi anataka kufa :-(

    ReplyDelete
  3. mimi naona wagome tu. nawasisitiza wagome

    mbona serikali ni tajiri na inaishi kitajiri tu??

    ila yawezekana wakaongezewa malipo harafu wakaongezewa kodi kwa mifumo mingine pia

    ila wagome bwana ukondoo wa watz ndo unaowaponza

    ReplyDelete
  4. MM BINAFSI NAONA WAGOME TU

    NYIE AMJUI MM NAONA TANZANIA MPAKA TU MWAGE DAMU NDIO TUTAPATA AKI YETU, LICHA YA HUCHUMI Tulio nao bado kuna watu wanaishi kwashida sana kule kwenye machimba ya barrck,
    KILE KIJIJI NITAJIRI SANA NA WATU WANAO ISHI KULE NI MASIKINI WAKUTUPWA, AMNA MAJI CHAKULA WALANYUMBA ZENYE MSIMAMO,JAMANIII!! TUPO WAPI WA TANZANIA ?WATOTO WANAO KUA KTK KIJII KILE AMNASHULE ZAKUTOSHA MAJI SAFI NA MBU WAPO WENGI SN ,TANZANIA ANNA AKI MPAKA DAMU HIMWAGIKEEEE,,

    ReplyDelete
  5. Madai ya wafanyakazi waTRL,hawakuwahi kukaa mezani na kuongea? Ni mambo mangapi yamekwama kwa sababu tu ya kufuatilia madai yao?

    Ni ndugu wangapi wa waalimu wameshindwa kupata huduma bora maospitalini kwa sababu ya kukosa fedha kutokana na kipato kidogo cha walimu?

    Wakati viongozi wa serikali wafikiria kujenga hoteli ya nyota tano,mfanyakazi wa kawaida anawaza namna ya kusimamisha vyumba viwili angalao apate pa kujisitiri.

    Wafanyakazi wangekuwa wanalipwa vizuri, hata bei za vyakula kwa mamalishe pengine zingekuwa ni zaidi ya ilivyo sasa,hata za kuosha magari vilevile.hivyo wangefaidika zaidi.

    Kwa sasa ni kina mama wajawazito na wagonjwa wengi tu wakosao huduma sahihi na kupelekea mauti kuwakuta kwa sababu tu ya kukosa fedha. Huu ni ukweli,na mshahara mdogo kwa mfanyakazi yawezekana ina mchango mkubwa sana.

    "dhana hii ya Tanzania ni nchi ya amani,binafsi sitamani wala sitaki kusikia yeyote akiitaja kwani inanipandisha jazba bure na kuniumiza moyo"

    Aliyeandika makala hii alitakiwa pia kuangalia upande wa pili wa shilingi, yani aangalie pia madhara yatokanayo na wafanyakazi kutotimiziwa haki zao muhimu kwani ni rahisi kupima kwani pengine madhara au hasara tayari zinaonekana.
    Na pia ajiulize itakuwaje kama ugomo huo utafanikiwa?
    Nadhani viongozi wa serikali ndio wanatakiwa wajiulize au wangalie hoja za aliyeandika makala hii kwa makini.

    Ninachoomba Mungu tu ni kuwa mgomo uwe ni wa haki ambao hauna chembe ya siasa.Uwe kweli ni kwa manufaa ya wafanyakazi na si vinginevyo.

    ....sasa ni nani atakayekuja kumfunga paka kengele.....


    .....au panya waendelee kuliwa na paka tu kama ilivyozoeleka?

    ReplyDelete