Ndugu wasomaji wa blog hii ya MAISHA, katika kupitia mada mbalimbali nilizowahi kuweka humu ili kupata ile ambayo ilivuta hisia za wasomaji wengi na kuleta changamoto, nimevutiwa na mada hii ambayo ilileta vuta ni kuvute miongoni mwa wadau wa blog hii.
Kwa hiyo basi nimeichagua mada hii kuwa ndio mada iliyovunja rekodi kwa mwaka 2009.
Natoa shukrani kwa wadau wote mlioshiriki katika kuichangia mada hii.
Naomba muungane nami katika kujikumbusha kile kilichotokea katika mjadala huu.
MISHAHARA HAITOSHI+TUACHE UZEMBE KAZINI
Makala hii nimeipenda ndiyo maana nikaamua kumwomba http://hapakwetu.blogspot.com/ Kwani najua nakamilisha lengo lake la kuifanya isomwe na wengi.
Katika nchi yetu ya Tanzania, watu wanalalamika muda wote kuwa mishahara haitoshi. Gharama ya maisha ni kubwa kuliko mishahara. Hata kwa kuzingatia mahitaji muhimu tu, watu wengi wana haki ya kusema kuwa mishahara haitoshi.
Malalamiko ya mishahara kuwa haitoshi yanasikika duniani kote. Hapa Marekani, shida kubwa inayowakabili watu ni kulipa bili na madeni mbali mbali. Marekani ni nchi ya madeni. Kutodaiwa popote ni sifa nzuri katika utamaduni wa Tanzania. Lakini Marekani, sifa inakuja kutokana na umakini wa kulipa madeni. Mishahara ya Wamarekani wengi inaishia kwenye kulipa madeni. Kwa hivi, nao wanalalamika kuwa mishahara haitoshi.
Wako Watanzania ambao wana mishahara ambayo ingeweza kutosheleza mahitaji muhimu. Tatizo ni kuwa dhana ya mahitaji muhimu ina utata.
Tunaweza kusema mahitaji hayo ni chakula, malazi, mavazi, matibabu, elimu, na usafiri. Lakini, katika utamaduni wetu, orodha ya mahitaji muhimu ni kubwa zaidi ya hiyo. Kumlipia ada mtoto wa shangazi ni wajibu. Kuchangia gharama ya msiba kwa jirani ni wajibu. Kama una gari, kumpeleka mtoto wa jirani hospitalini ni wajibu.
Kwa msingi huo, hakuna Mtanzania ambaye anaweza kusema mshahara wake unatosha. Suala haliishii hapo. Je, ukitembelewa na marafiki, utakaa nao tu nyumbani na kuongea nao, au unatakiwa kuwapeleka mahali wakapate kinywaji? Je, unaweza kuacha kuchangia gharama za arusi ya rafiki yako?Tukizingatia hayo yote, mishahara haitoshi.
Watanzania wengi wana tabia ya kutumia fedha kwa mambo mengi mengine, ambayo umuhimu wake ni wa wasi wasi, kama vile bia. Kwa Watanzania wengi, bajeti ya bia ni kubwa sana. Kwa mtu anayekunywa sana bia, mshahara hauwezi kutosha. Lakini je, bia ni kitu muhimu namna hiyo?
Kwa upande wa pili, Watanzania tunapaswa kutafakari dhana ya mshahara. Mshahara unapaswa kuwa malipo muafaka ya kazi ambayo mtu anafanya. Kazi ndio msingi. Lakini, kuna tatizo kubwa Tanzania.
Watu wengi hawafanyi kazi kwa bidii. Muda mwingi wanatumia kwenye gumzo. Lakini wanategemea kulipwa mshahara, na wanalalamika kuwa mishahara haitoshi. Je, wanastahili hizo hela wanazopewa kama mshahara? Je, wakiongezwa mishahara, wataongeza juhudi kazini au wataendelea kukaa vijiweni na kupiga soga?
Huku Marekani, watu wanachapa kazi sana. Mshahara unatokana na kazi. Mtu asipofika kazini, halipwi. Akichelewa, malipo pia yanapunguzwa. Kwetu Tanzania mambo si hivyo. Mtu akishaajiriwa, anategemea kupata mshahara wake kila mwezi, hata kama anatumia masaa mengi kijiweni. Je, ni bora kuanzisha utaratibu wa kuwalipa wafanyakazi kwa yale masaa wanayokuwa kazini tu, na kupunguza mshahara kwa masaa wanayokuwa kijiweni?
Nami nataka kuongezea ni kwamba hapa Sweden ni karibu sawa na huko Marekani. Yaani hapa hata kama upo likizo hulipwi, inategemea ni likizo gani. Halafu kama unaumwa na halafu huendi kazini zile ziku mbili za kwanza hulipwi kitu kwa hiyo hapo ukiumwa basi ujue mshahara wako unapungua/unakatwa. Kwa hiyo kwa mtindo huo utakuta hata kama mtu unaumwa unajikaza na kwenda kazini. Kwani mshahara wanaokata ni mkubwa sana na ukizingatia maisha nayo yapo juu.
Na: Yasinta Ngonyani kl. 6:26 PM
NA HAYA YALIKUWA NI MAONI YA WADAU...........
kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...
nyie msituletee za kuletwa hapa kwetu tanzania.
yaani nyie kukaa sweden na marekani na kuona roho zao za kupenda na kuitukuza pesa basi mataka na kwenu tuige mambo ya wazungu? mtaiga mpaka lini nye wabongo msio fikiri?
mnadhani viwango vya mishahara vya huko utumwani mliko ni sawa na vya hapa tanzania?
boro kutawaliwa kimwili kuliko kutawaliwa kiakili na kiroho.
sasa kuna watu wanaolipwa shilingi lakini moja mpaka mbili kwa mwezi, huyu akiugua utakati shilingi ngapi kwa siku na abaki na kiasi gani na ataishi je?
kwa nini mnataka kuleta unyama wa huko utumwani hapa kwetu? mnataka kuleta mikono ya utumwa hapa ehe?
yaani mmewekewa mipaka ya kufikir kiasi kwamba hamna mwenye mawazo nje ya huo utumwa mnaouishi ehe?
kuweni makini mnapopendekeza upuuzi mwingine bwana. bongo binadamu wote ni sawa na ni ndugu na ndio maana unaweza kuwa huna ela lakini usife njee. kwa maneno mengine mshahra wa mtu mmoja unasaidia watu lukuki./
hapa ni ubinadamu kwanza mambo ya pesa na miliki za dunia hii ni baadaye. kaeni utumwani na mfurahie maisha ya utumwani na msituletee mizizi ya utumwa kwetu
na kama mnaona maisha ya uko ni sawa poa tu kivyenu.
March 18, 2009 8:25 AM
Yasinta Ngonyani said...
Kamala ndugu yangu, Kuhusu maoni yako kwanza nasema asante. Halafu napenda kukuambia ya kwamba hakuna mtu anaishi utumwani, Hapa kinachozungumziwa ni jinsi watu wengine wanavyofanya kazi na matumizi yake na jinsi watu wengine wanavyolalamika ya kuwa mshahara hautoshi wakati hawafanyi kazi. Jambo jingine ni kwamba mimi binafsi nimeona na nimesikia watu wakisema afadhali waishio ughaibuni mna maisha mazuri. Lakini hawajui ni taabu gani zipo huku kwa sababu wao mara nyingi wamakuwa au niseme "sisi waafrika" tumezoeshwa sana kupewa misaada kutoka huko Ughaibuni. Je? tunajua hiyo misaada inatoka wapi? watu kwa huruma zao wanaacha familia zao na kwenda kufanya vibarua na pia zile pesa wanapeleka Afrika. na pia watoto wadogo wanatafuta pesa kwa mtindo wa kuosha magari na zile pesa wanapeleka kwa watoto wenzao Afrika. Je? hapo sasa nani ni mtumwa?
Ndiyo nakubaliana nawe ktk sisi waafrika hata kama mmoja katika jamii hana hela basi hawezi kulala njaa na hata kama una rafiki au jamaa. Sawa, ila kuna wengi katika akili zao wanafikiri watu huku wana mshahara mzuri na maisha mazuri na wana kila kitu na wao hawana shida na mshahara wao huwa unatosheleza mahitaji yote HAPANA.
March 18, 2009 11:39 AM
kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...
ysinta ndio maaana nakwambia kuwa huko ni utumwani. ni azima utumike vya kutosha sana.
wala usidanganyike na misaada itokayo ulaya. hakuna kitu kinachoitwa misaada ila kuna danganya toto. tangu uhuru afrika iliishi kwa misaada lakini hakuna maendeleo, unadhani misaada hiyo ina tija na hatuwezi kuishi bila yenyewe? mbona china sasa inakuja juu na kuwa super power, ulishawahi kuona inasaidiwa na nchi yoyote? si walijifungia na kuishi kivyao sasa hao wanaendelea wakati sisi tukipokea misaada kutoka utumwani na kuzidi kutuma watumwa wetu wakatumikishwe?
mbona kabla ya kuja kwa wakristo na waislilamu (wakoloni) afrika iliishi kwa amani, umoja na upendo bila ujinga wa kimsaada kutoka ulaya wala kupeleka watunwa huko?
sasa tumepeleka watumwa, wanazalisha na kuleta misaada mbona haupigi hatua yoyote?
muwe na macho mapana sio ya ndio mzee tu eti tunasaidiwa. waafrika hatuamini sana katika utajiri wa duniani japo tunao mwingi, tunajua kabisa kwamba dunia si chochote si lolote.
UTUMWA WA KIAKILI NA KIROHO NI MBAYA KULIKO HATA WAMIHEMKO.
March 18, 2009 12:13 PM
fred katawa said...
Yasinta,wazungu hawatupi misaada bali wanarudisha asilimia 0.00001 ya kile Wanachoiba Africa."THERE IS NO FREE LUNCH".Kuhusu kazi sisi tunafanya kazi zaidi ya hao wamarekani,hebu fikiria kubeba zege,kusukuma mkokoteni wenye magunia kibao ya viazi pamoja na kuendesha guta lililosheheni mzigo tani mbili.Huko wanaweza hayo?
Katika dunia hii ubinadamu umebaki Afrika ndo maana mshahara wa mtu mmoja unasaidia watu kibao.Haya mambo hayapatikani ulaya kwa kuwa hakuna binadamu huko bali kuna viumbe wanaofanana na binadamu.Usijaribu kutushawishi sisi tubadili maisha yetu yawe kama ya hao wanyama.
March 18, 2009 2:30 PM
Mbele said...
Ndugu Kamala, ninafuatilia maoni yako, kwani mimi hupenda kujumuika na Watanzania na wengine katika kufundishana na kuelimishana. Watanzania wanaonifahamu wanajua hayo, kama wanavyojieleza hao hapa.
March 18, 2009 4:29 PM
Bwaya said...
Ukimsoma Kamala haraka haraka unaweza pandwa jazba. Ila ukipunguza kasi ya kusoma, ukaongeza tafakari, unamwelewa. Mimi nimemwelewa. Anachotuzidi wengi, ni uwezo wa kusema wazi wazi anachoamini.
Hata hivyo ni kweli pia kuwa waswahili wengi hatufanyi kazi ipasavyo. Tunatumia muda mwingi kupiga domo maofisini. Nadhani tukibadilika, tukajiamini itatusaidia kwenda mbele.
March 18, 2009 4:53 PM
Mbele said...
Samahani, katika ujumbe wangu hapa juu, nilisahau kusema kuwa mimi ndiye niliyeandika makala ambayo Dada Yasinta ameiweka hapa kwake, kama aliyoelezea.
Kitu ambacho ningemshauri ndugu Kamala ni kufanya utafiti zaidi, ili aweze kuelewa fikra na misimamo ya watu asiowafahamu, kabla ya kuwadhania hili au lile. Kwa msingi huu, iwapo yeye ni mtu anayetafuta elimu, kama mimi, afanye hii juhudi, na anaweza kuanzia kwa kusoma blogu hii na hii.
March 18, 2009 5:08 PM
Anonymous said...
utajua tu nani ana hasira za kunyimwa visa, sijui tatizo ni lugha pale ubalozini! kufikiria kila aliye nje ya nchi anaishi utumwani ni utumwa na mwisho wa kufikiri pia! pole sana Yasinta, naona umevamiwa kijiweni kwako! ila ndio maisha hayo, kuna watu wanachukia sana habari za nje ya nchi kwa vile walishawahi kuwa na shauku ya kudaka pipa, wakashindwa kupata visa then wakaanzisha kampeni ya sizitaki mbichi hizi, kuna watu wapo nje wanaishi kama wafalme, na wengi tu hao wanaoitwa watumwa wanafanya kazi na kusaidia huko nyumbani. tunapotoa maoni ni vuzuri kuwa hekima fulani, hata kama tunachotaka kusema kina ukweli au ni lazima tuangalie tunawasilisha vipi ujumbe, zaidi ya hapo inakuwa ni upuuzi mtupu!!
March 18, 2009 11:29 PM
Anonymous said...
Uliyetoa maoni kuwa watu wakinyimwa visa ndo na kutokujua kiingereza ndo wanakuwa na hasira haupo sahihi hata kidogo.Hapa bongo kuna watu wanaishi vizuri zaidi ya wabongo waliohamia huko.
Na vilevile kuna watu wanayajua vizuri maisha ya huko na huku kwetu.Kuishi mbali na nyumbani haimaanishi kuwa una maisha mazuri kuliko uliowaacha nyumbani.
March 19, 2009 10:37 AM
Anonymous said...
Ndugu Kamala, unatia aibu! Nafikiri hata wanaokunyamazia wamekustahi. U're such an idiot! Hivi unawezaje kuwalopokea watu usiowajua? Inasikitisha sana tena sana. Kwa nini usifikirie namna nzuri ya kuwasilisha maoni yako? Uwazi gani wa kijinga kiasi hiki?
Una bahati unajadiliana na watu wastaarabu wanaojua kuchagua maneno ya kumwambia mtu.
March 19, 2009 11:22 AM
Anonymous said...
Mdau uliyesema kwamba sipo sahihi niliposema kwamba hasira na kutokujua kiingereza, naona wewe ndio umenisemea habari za kutojua kiingereza, kwani sikusema tatizo kutojua kiingereza. Nimesema tatizo lugha. Hili lina mambo mengi mojawapo ni namna unavyojieleza. pia kumbuka kwamba kiingereza sio lugha pekee kwani kuna nchi nyingi ambazo hazitumii kiingereza. na pia sikusema kwamba bongo hakuna watu wanaoishi maisha mazuri hata kidogo, naomba kanisome tena vizuri. Mimi pia nipo bongo na nayajua vizuri tu maisha ya nje ya nchi kwa vile nimeishi sana tu huko, hivyo najua ninachokiongea. Ninapokuambia hasira za kukosa visa nina mifano mingi sana, nin jamaa ambao wanaponda sana habari za kwenda kujitafutia nje ya nchi kwa sababu wao walikosa visa, hao wapo wengi ninaowafahamu japokuwa siwezi kuwataja hapa. natumaini umenielewa!
March 19, 2009 11:30 PM
Mbele said...
Ndugu Kamala
Leo nina fursa ya kuongelea masuali yako, kwani nilikuwa nimezidiwa na shughuli.
Mimi ni Mtanzania, kama wewe. Tanzania ni yangu, kama ilivyo yako, na sote tunawajibika kuichangia kwa hali yoyote tunayoweza.
Popote tulipo, tunawajibika kutafuta fursa ya kuichangia Tanzania. Ukifuatilia mawazo ya Mwalimu Nyerere utakuta alitoa mfano wa kijana anayepelekwa mbali akatafute chochote kwa ajili ya kijiji chake. Ni fundisho alilotoa, wakati anaongelea suala la kuwasomesha vijana na wajibu wa hao vijana wa kuchangia nyumbani. Cha muhimu ni ule moyo wako. Kama unaipenda nchi yako, utaitumikia popote ulipo.
Kwa mzalendo, kukaa nje si hoja. Nje kuna fursa tele za kuchangia, kwani fursa zilizopo nje hazipo nyumbani. Ninawafahamu Watanzania wengi huku Marekani ambao wanafanya makubwa kwa nchi yao kwa kutumia fursa zilizopo huku Marekani.
Kwa maana hiyo, kama wote ni wazalendo, hakuna sababu ya kuwatenga waliopo nje na walipo nchini. Haya mawazo uliyotoa hayatatufikisha mbali. Nchi za wenzetu, hata hapa hapa Afrika zinatambua hayo. Kenya, kwa mfano, ina kitengo katika wizara ya mambo ya nje, kinachoshughulika na watu wao waishio nje. Nchi ya Mali inayo wizara kamili ya kushughulika na wananchi wao wanaoishi nje. Nchi hizi zinatambua faida ya kuunganisha nguvu za hao walioko nje na wale walioko ndani. Tanzania tunajiumiza wenyewe tukiendekeza fikra kama ulizotoa.
Sisi hatupigi kampeni kuwa tuige mambo ya wazungu. Tumelenga kwenye suala la mishahara na kazi. Ndio mada pekee ambayo tumeongelea. Si haki kudai kuwa tunapiga kampeni ya kuiga mambo ya wazungu. Wazungu mambo yao ni mengi, mengine mazuri na mengine mabaya.
Kuhusu kufanya kazi kwa bidii, hatuna hata sababu ya kuwataja wazungu. Tulipopata Uhuru, Mwalimu Nyerere alituhimiza kwa usemi wa "Uhuru na Kazi." Na watu nchini kote waliitikia, wakawa wanafanya kazi sana. Sio suala la kuiga wazungu. Taifa letu lilianza na maadili ya kufanya kazi kwa bidii. Baadaye tumeingiza uzembe, na sasa watu wengi wanakaa vijiweni na kungoja mishahara hapo hapo kijiweni. Hili ndilo tatizo, wala si suala la kuiga wazungu.
Mtu yeyote anayeipenda Tanzania anawajibika kuunga mkono dhana ya kufanya kazi kwa bidii. Kutetea vijiwe ambavyo vinafanyika wakati wa kazi ni kuhujumu Taifa. Vijiwe vije tukishamaliza kazi, wakati tumechoka na tunahitaji kupumzika. Hapo ni sawa kwenda vijiweni kusogoa.
Kama tunakubaliana kuwa msingi huo wa Uhuru na Kazi ambao tulianza nao, ulikuwa sahihi, sioni kwa nini leo mtu akisema tufanye kazi kwa bidii iwe ni dalili ya kutawaliwa kiakili. Je, huyu Mwalimu Nyerere aliposema Uhuru na Kazi, alikuwa ametawaliwa kiakili? Wananchi nchini kote waliosikia wito wa Nyerere, walifanya vibaya?
Dunia ya leo, ya utandawazi, ina ushindani wa kutisha. Tusipofanya kazi hatutafika popote. Na kazi hizo si za kuzalisha tu katika uchumi, bali pia kujiongezea maarifa na elimu. Tusipopunguza vijiwe tutaangamia.
Ni kweli mishahara ya wengi nchini ni midogo. Lakini, dawa ya tatizo hili si kukaa vijiweni. Kufanya kazi ni njia ya kuinua uchumi na hii ndio njia ya kuinua kipato. Badala ya kukaa kijiweni, ni bora watu wawe wanajiongezea ujuzi na elimu, ili kujiweka katika nafasi ya kupata fursa bora kazini au kuweza kujiajiri. Ujasiriamali ni wazo ambalo wenzetu duniani wanatumia. Badala ya kukaa na kulalamikia mishahara midogo, ni bora kutafuta maarifa na ujuzi na kutafuta fursa za ujasiriamali. Vijiwe si dawa.
Mwishoni mwa ujumbe wako, umekiri kuwa wewe unajipatia kipato chako bila kuajiriwa na mtu, bali kutokana na juhudi yako ya kufanya kazi. Hujatuambia kuwa unashinda kijiweni. Sasa kwa nini unatulaumu sisi ambao tunasema hilo hilo unalosema, kuhusu umuhimu wa kufanya kazi? Kwa nini unatuambia sisi tuna akili za kitumwa, au tumewekewa mipaka ya kufikiri? Na wewe ambaye pia unazingatia kazi, tukuite una mawazo ya kitumwa au umepangiwa mipaka ya kufikiri?
Maadili ya kwetu ya kusaidiana ni mazuri, kama unavyosema. Hapa tunakubaliana. Ni jadi ya kuihifadhi. Mimi ni mwandishi, na nimeshaandika kuhusu tofauti za utamaduni wa Mwafrika na ule wa Mwamerika, na katika maandishi yangu huwa nataja mazuri na mabaye ya pande zote. Yako ambayo Waafrika tunaweza kujifunza kutoka kwa Waamerika, na yako ambayo wao wanaweza kujifunza kutoka kwetu.
Mimi ninawafahamu Wamarekani. NI watu kama sisi; wako ambao ni wema, na wako ambao ni wabaya. Hakuna tofauti na wanadamu wengine.
Mfumo wa uchumi wa nchi yao ni wa kibepari, na huu tunaweza kuuita unyama, kama alivyouita Mwalimu Nyerere, lakini si sahihi kuwaita Wamarekani wote kwa jina hilo. Wengi wao wanaupinga mfumo huo, kwani unawaumiza.
Binafsi, nachukulia maisha kuwa ni fursa ya kufanya mambo ya manufaa kwangu na wanadamu, sio fursa ya kustarehe. Suala unaloliongelea, la kufurahia maisha, halinihusu. Muda wangu mwingi natumia katika kujielimisha, ili niwe mwalimu bora zaidi na zaidi. Nikichoka napumzika kidogo, halafu naendelea na kazi. Dhana ya kufurahia maisha haina umuhimu kwangu.
March 19, 2009 11:42 PM
Koero Mkundi said...
kamala, kamala, kamala,
duh!!!!
hapa naona umekutana na wanubi,
je una cha kuongeza?
ndugu yangu, kamala mada nyingine ni za moto kuzivamia, mimi nilijua tokea mwanzo kuwa maoni yako yatawaamsha waliolala, na ndio sababu nikakaa kando kwanza ili nione segere......
binafsi nilikuelewa na naamini hata dada yasinta alikuelewa kwa sababu tumezoea staili yako ya kuchangia mada, lakini ndugu yangu sio watu wote wanaokufahamu ki hivyo, kwa hiyo walikuelewa ndivyo sivyo.
kaka usicheze na walioko ughaibuni, kwani hujui kilichowapeleka huko, wewe kula ugali wako na maharage kisha mshukuru mungu kwa kukujalia pumzi ya bure usiyoilipia kodi halafu lala.
duh! poe sana......
March 20, 2009 4:18 AM
kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...
anony anayesingizia visa hajui mimi nimewahi kutembelea nchi ngapi mpaka sasa. anaona ni ukosefu wa visa tu na hajui nina uchaguzi gani katika maisha na labda sijui nini maana ya kuishi kama mfalme, wapi na vipi.
mbele, ni kweli uliyoyasema kwa kiasi kikubwa lakini mimi ninachokipinga ni tabia ya kuiga hata upuuzi na roho mbaya za wazungu.
kwa mfano kwanini tuanze na uwanyanyasa wafanyakazi kwa kuwanyima viisenti wanavyopata ambavyo hata hivyo haviwatoshelezi?
ni lazima tuanze na hiyo? kwani nyie mnaojiita wasomi na wataalamu wa dunia hii, hamna mawazo mapya na njia mpya za kujikomboa mpaka mfuurahie mfanyakazi wa bongo kunyimwa mshahara wake?
na je, pamoja na usomi wenu huo, unaonia ni sawa kwa bindamu mwenzako kunyimwa chakula (mshahala) wakati anaumwa? kama unaona nisawa, basi ukae tu ughaibuni.
na kama hayo ndio mawazo ya watu wa ughaibuni, basi mfilie huko huko hatuhitaji kuwa na wizara wala kitengo cha wakazi wa nje.
ninachosema hapa ni kwamba nchi kama yetu ambayo haina dira wala mwelekeo, watu watapata motisha gani wa kufanya kazi kwa bidii? watu wasiojitambua? wenye mawazo kama ya kwenu ya kukumbatia uzungu akija mzungu basi kuanzia kwa raisi mpaka mawazili wanachekelea?
kwani nyie hamuwezi kuja na njia mpya au hata kuwashauri wazungu kuachana na huo unyama wao na uuaji wakawa kama kwentu juu ya wafanyakazi wao wagonjwa, na kuwafikiria vyema kama watu wenzao?
upi utu kati ya wafanyiwavyo watanzania wagonjwa na wazungu au watumwa mlioko utumwani?
si kila kitu tutakiacha lakini ubinadamu wetu tutaondoka nao?
NB nayaongea haya lakini ninao ndugu wa kutosha huko utumwani, US na kanada na mipango yote ya mimi kwenda huko niliikataa mapema tu.
mdogo wangu koero, unaogopa nini? hujui tatizo la kusoma sana ni lipi?
ugali na hmaharage ndio chakula changu. sili vyakula vya viwandani wala vya wanyama. nikija kwenu we niandalia ugali maharage tena wa donna, mtenbele, mchiicha, njegele, mbaazi, karanga. lakini ukipika vyakula ya viwandani sitokula, am sory
March 20, 2009 1:59 PM
Mzee wa Changamoto said...
Alright!!
Amani, Heshima na Upendo kwenu nyote. Nami kama wengine ntawiwa kuikimbia mada na kutoa maoni kuhusu maoni maana ni sehemu kubwa na yenye nguvu kwenye ma-jamvi yetu haya.
Usomaji na utoaji wa maoni unatukutanisha na watu wenye uwezo, imani na mitazamo tofauti. Kwa hiyo kwangu naona kuna mawili kwa mtoaji na msomaji wa maoni hayo. Kwanza ni lazima kuzingatia kuwa hasira hupunguza busara. Namaanisha kuwa ukitoa ama kusoma maoni ukiwa na hasira kuna mengi utakayoshindwa kuwa nayo bayana. Na pili kwa msomaji kuna wakati yapaswa kuangalia zaidi "point of view" kuliko tone ya mtoa maoni. Na hili litasaidia maana kuna wengi wetu ambao huwa tunaandika kama tunavyoongea. Kwa hiyo kama hutazingatia hilo waweza kupata shida kiasi.
Na sasa nirejee ktk maisha ya kutatua tatizo kwa namna tulionavyo. Nilifundishwa kuwa katika kila linaloonekana kama jambo baya kuna uzuri ndani yake.
Nadhani wapo waliokerwa na maoni ya Kamala lakini nadhani kwa ujumla tunapaswa kujiuliza maswali ambayo yanapelekea kuwepo kwa mgongano wa mawazo hapa. Kwa mfano maoni ya Ndg Kamala yananipa CHANGAMOTO kujiuliza MAANA YA UTUMWA KATIKA ULIMWENGU WA SASA, YUPI MTUMWA NA VIPI UNATENDEKA.
Kwa hali ilivyo ntakubaliana kutofautiana na Kamala kuwa Utumwani ni huku. Na hata kama ni huku naamini kuwa utumwa ulioko nyumbani ni m'baya zaidi. Na pia sidhani kama kuna makosa ya kuiga mfumo unaoweza kuwa bora kutoka mahala ambapo unaamini si bora. Hata kama si masuala ya mshahara, lakini kuna mengi mema ambayo yanatendeka kuwawajibisha wanaofanya yasiyofanyika. Ukiangalia katika haki za wananchi, huduma za wateja (customer services), siasa na mengine mengi utagundua kuwa hatua waliyofikia huku ni kubwa ukilinganisha na nyumbani na sidhani kama tunaweza kupinga kujifunza kwa kuwa tu "tutaiga toka utumwani."
Utumwa unaofanywa na viongozi wetu kwa wananchi wetu nadhani ni wa kinyama kuliko uliofanywa na watu ambao lengo lao lilikuwa kuja kutenda hilo. Sasa hivi watu wanahenya kufanya kazi, kuonekana wanajenga nchi na kisha matokeo yake pesa inaingia kwenye akaunti za watu ambao wanatenda makosa hayo huku wakipindisha katiba tena kwa makusudi na kisha wanatumia kinga za kikatiba kutokwenda kujibu mashitaka. Huwezi fanya hayo huko unakokuita "utumwani".
Huku "uhuruni" ambako watu wanajilimbikizia mali kwa mshahara usiojulikana tena akiwa kwenye nafasi ya kuitumikia jamii na hakuna mwenye uwezo wa kumuuliza, huwezi kufanya hivyo ukiwa huku "utumwani."
UKWELI NI KWAMBA TAFSIRI YA UTUMWA IMEBADILIKA NA SASA TUNAKUWA WATUMWA WA KAKA NA DADA ZETU HUKU WANAOPANGA HAYO WAKISTAREHE NA KUSHEREHEKEA HAYO NJE YA NCHI.
Utumwa wa zamani ulikuwa nyumbani ukitendwa na wakoloni lakini UTUMWA ULIOSEMA KUWA NI M'BAYA ZAIDI ni huu unaotendwa na viongozi wetu wanaosema kuwa WANAWAPENDA NA WAKO HAPO KUTETEA MASLAHI YA NCHI YETU ilhali hakuna wanalofanya zaidi ya kuiba na kutumikisha jamii.
Naomba kuwakilisha kipande hiki. Ni mtazamo wangu kulingana na namna nionavyo tatuizo, na naendelea kutunza haki ya kukosea na kukosolewa.
Blessings
March 20, 2009 2:18 PM
kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...
mzee wa changamoto mimi binafsi sijawahi kuongozwa na hasira katika kujibu hoja zozote,. hisara ni sehemu ya hisia au mihemko muhimu katika maisha ya binadamu na bila hiyo twaweza tusiishi, hata hivyo ushujaa wetu unaonekana pale tunaposhinda hisia na mihemko yetu na hivyo mimi najitahidi kuwa bingwa katika hilo.
utumwa wa kwenu huko ughaibuni ni mbaya sana kuliko wa kwetu nyumbani hata katika miwani tofauti. watu wanaishi katika mbavu za mbwa, lakini wana amanai na wanaisha sasa (maisha waliyonayo) kuliko huko.
wale wanaoficha fedha huko ughaibuni (labda nyie mmezifuta) nao ni watumwa wabaya kwani wanamabwana wawili, wale wa kwenu pamoja na ujinga na roho mbaya.uhuru wa kusema nk ulioko huko na vitu vingine, inabidi uviangnalie kwa miwani mipana, sio uhuru wa kweli kama ukiangalia, utaona ila ukitazama, utaendelea kutizama bila kuona na utasifia tu majamaa yalivyo kuosha akili (brainwash).hata wale wanaojifanya mabwana huku, kuna vitu wanavikosa au vinawaumiza huko kwenu.
napinga kuiga eti kwa sababu ya usomi wenu wowote ule
March 20, 2009 2:52 PM
SIMON KITURURU said...
Kuna uwezekano watu wanaogopa kuitwa watumwa kwa sababu ya kutokuwa na uhakika wa WAO Uhuru.
Mimi tokea nizaliwe mpakaleopamoja na nchi zote nilizo wahi kuishi ambazo ni kadhaa , bado najihisi sijawa huru.
Na naamini kuna watu wanaongelea ya nchi wakati wako huru chooni tu na hata sebuleni au chumbani kwao hawako huru.:-(
Mimi bado mtumwa na nahangaikia uhuru!:-(
March 20, 2009 10:46 PM
Kissima said...
Kaka Simon samahani, wewe unasema ni mtumwa kwa maana hiyo hauko huru, utumwa unaouongelea ni upi? Kuna utumwa wa akili/mawazo, ambao unasababisha utumwa mwingine wa kukandamizwa,wachache kula jasho lako n.k.
Kwa mfano , miaka minne ya mateso huwa tunaisahau kabisa, kisa mwaka wa tano vibarabara vinarekebishwa kidogo, vizahanati vinajengwa, maneno matamu matamu yenye upanga mkali ndani yake,soda na bia mbili tatu, kisha miaka minne tena utumwani. Yote haya ni matokeo ya utumwa wa akili.
Naomba ufafanuzi kuhusu utumwa.
March 22, 2009 10:46 AM
Bwaya said...
Kamala,
Japo naweza kuwa sikubaliani na unachokisema, lakini naamini unayo haki ya kuutetea uhuru wako wa kusema.
Aidha, naamini kwamba katika kusema, una haki ya kusema kwa namna yoyote ile unayoona inafaa isipokuwa ile inayoweza kumletea msomaji hisia zisizo za lazima katika kukuelewa.
March 22, 2009 4:32 PM
Egidio Ndabagoye said...
Nibamize kwenye mada kwenyewe.Suala la mishara halian ubishi hamna sehemu duniani watu wanaridhika na mishahara.
Dhana la mshahara kuwa mdogo inatokana na majukumu uliyonayo,mfano majukumu yanapozidi mshahara unakuwa mdogo.
Wachumi wana kanuni zao za maisha kwamba kila kipato kinapoongezeka na matumizi yanaongezeka.Suala la kulia mshahara mdogo linabaki pale pale.
Suala la kazi halina ubishi sisi watanzania ni wavivu wa kutupwa kutwa kupiga domo vijiweni.Nenda maofisini leo hii utalia,utajiuliza huyu mtu kawekwa pale auze sura au afanye kazi?
Kuhusu utumwa nakubaliana na Simon.
March 22, 2009 6:42 PM
EVARIST said...
Prof Mbele umeleta mada ya moto...inanikumbusha makala moja katika gazeti la TIME (sikumbuki ni la mwaka gani ila ni 2000s ambapo gazeti hilo lilimtaja kuwa Man of the Year).Aliulizwa kuhusu upinzani uliosambaa ndani na nje ya Marekani kuhusu baadhi ya mitizamo yake hususan War on Terror.Jibu lake ndio nalotaka kuli-refer hapa:ukiona watu wana-react (positively or negatively) ina maana hoja ina mguso kwao,maana ingekuwa kinyume wasingeizunngumzia.
Kuhusu hoja iliyopo,binafsi sina comment bali naomba kugusia kasumba iliyojengeka muda mrefu huko nyumbani juu ya dhana nzima ya maisha ya Ughaibuni.Naomba kukiri kwamba dhana hiyo ndio ilinipa changamoto kubwa ya kuibatiza blog yangu jina hilo.
Kuna dhana (miongoni mwa wenzetu)kwamba Watanzania walioko ughaibuni wanapotoa uchanganuzi wao kuhusu masuala flani yanayoihusu nchi yetu basi wanafanya hivyo kama "kuwasanifu" wenzao walioko nyumbani Tanzania.Mantiki ya kinachoandikwa na Mtanzania aliyeko ughaibuni inafunikwa na na ukazi wake huko nje.Naomba kusisitiza kuwa si kila Mtanzania ana kasumba hiyo,na hapa nazungumzia zaidi uzoefu (experience) wangu binafsi na wa marafiki wachache waliokumbana na hali hiyo.
Naomba kusisitiza kwamba asilimia kubwa ya Watanzania walio nje ni watu wanaoipenda nchi yao,wanasikitishwa na baadhi ya yanayotokea huko nyumbani na pia WANAGUSWA (kwa sababu sidhani kama kuna yeyote kati yao ambaye hana family connection huko nyumbani).Again,hapa nawazungumzia Watanzania naowafahamu tu(ikimaanisha kuwa inawezekana kuwapo exceptions).
Kuhusu kasumba hiyo,nadiriki kusema angalau huku kwenye blogs kuna afadhali.Kuna wakati nilikuwa naandika makala katika baaadhi ya magazeti ya huko nyumbani,na ilikuwa nadra kwa wiki kupita pasipo msomaji flani kutoa tuhuma kwamba "aaah unataka kutwambia nini wewe?unadhani Ulaya ndio kila kitu..."na kauli kama hizo ambazo binafsi naziona ni za kibaguzi just like Mzaramo atapomwona Mndamba hana nafasi ya kuzungumzia Dar es Salaam,au Mporogo "kumkwida" Mmachame kuhusu masuala ya Mahenge.
Sote ni Watanzania,tofauti pekee ni mahala tulipo ambapo kimsingi hata kwa wale waliobadili uraia bado damuni mwao ni Watanzania hususan kutokana na connections za kifamilia,koo na kabila,vitu vinavyounda taifa letu pendwa.
Kuhusu "utumwa wa huku ughaibuni" naomba nichangie kwa mfano hai.Wakati flani rafiki yangu mmoja Mmarekani Mweusi aliwahi kunidadisi kuhusu ubaguzi hapa Scotland.Niliamua kuwa mkweli kwake na kumwambia upo na unanisumbua.Alichonijibu kilinifanya nifikirie mara mbili.Alisema "japo ubaguzi ni ubaguzi popote pale,lakini angalau wewe ni Mtanzania uliyeko kwenye nchi ya watu,wakikubagua wanaweza kuwa na excuse-hata kama ni muflisi.Vipi je kuhusu mie mzaliwa wa hapa Marekani na mwenye asili ya hapa lakini kuna nyakati nabaguliwa kwa vile tu mie ni mweusi?"
Majibu ya rafiki yangu huyo yanaweza kuwa muhimu katika ulinganifu wa "utumwa wa ugahibuni" na "utumwa wa nyumbani."Japo utumwa ni utumwa,na haupaswi ku-exist popote pale,lakini utumwa wa nyumbani unachukiza zaidi kuliko ule wa nje.Na hapa sitetei utumwa.Let's be realistic.Kuna mambo tunayokumbana nayo katika kutafuta maisha huku kwenye nchi za watu ambayo yanakera kupindukia,lakini tunajipa moyo kwa kusema aah hapa ugenini (kwa wale ambao hata wakiishi nje milele,Tanzania bado ni nyumbani) nikirudi nyumbani hakuna wa kunitenda hivi.Na unakanyaga pale Mwl Nyerer Intl Airport unatendwa maradufu ya kule ugenini!
Tujaribu kuiweka hivi pia.Mkoloni alitunyanyasa kwa vile alikuwa mgeni,hakuwa na uchungu na nchi yetu.Of course,ilikuwa inatuuma na ukoloni haukuwa sahihi.Lakini hebu tuangalie hawa Watanzania wenzetu wanaotutenda vibaya zaidi ya wakoloni.Wakoloni wangeweza kabisa kujitetea kuwa "ah sie sio Watazania ati!".Je vipi kuhusu mafisadi wanaoitafuna nchi yetu kwa jasho la walipa kodi masikini?
Ni dhahiri unyama unaofanyiwa na nduguyo unauma zaidi kuliko wa mtu baki,na hili halihitaji utafiti.
Mwisho,nimalizie kwa mfano mwingine mdogo.Majuzi nilikuwa nazungumza na mtu flani ambaye awali sikufahamu kuwa anaijua Tanzania vema.Yeye amezaliwa Mashariki ya Mbali na kuzunguka sehemu mbalimbali duniani,kwa sasa ni mhadhiri hapa chuoni.Kwa kifupi,nilizungumzia "WATANZANIA..." na yeye akaniuliza "hivi unaposema Watanzania kwa umoja unamaanisha watu gani hasa?Maana nchi yenu ina makabila zaidi ya 120 na ni dhahiri kuna tofauti za msingi miongoni mwao...maana nchi yenu ni moja ya nchi zilizo highly diversified kuliko nyingi barani Afrika....ni vizuri unapozungumzia Tanzania unyambulishe kwa makini ni watu gani hasa unaowazungumzia badala ya kuwajumlisha kana kwamba unazungumzia Rwanda ya Wahutu na Watusi ni makabila mengine machache nchini humo..."
Je tunapohitimisha kuwa "Watanzania ni wavivu...hawapendi kazi...wanataka mshahara pasipo kazi...walalamishi..." tunazungumzia wale mamwinyi wa Kiembesamaki,masamjo wa Kariakoo,maalwatan wa Makorora Tanga,nk au tunajumuisha pia akina Mwangaluka wanaopiga jembe kwa nguvu zote kule Mwanza na Shinyanga,Morani wa Kimasai wanaokabiliana na wanyama wakali maporini wakati wanatafuta lishe ya mifugo yao,Wandamba wenzangu pale Ifakara wanaopiga jembe robo tatu ya mwaka kuhangaikia na kilimo cha mpunga,nk?
Uvivu,uzembe,ulalamishi,nk ni tabia ya mtu mmoja mmoja na sidhani kama kuna kabila la wavivu let alone Watanzania wote kuwa wavivu.
Binafsi naamini kuna Watanzania wanaopenda sana kazi (angalia wenda/warudio kazini kwa miguu pale bonde la Jangwani,angalia wamachinga wanaokesha juani kuuza bidhaa za mabwanyenye wanaopigwa na viyoyozi,nk) lakini wanakwazwa na mfumo dhalimu uneoelekea kuzingatia kwamba "mwenye nacho ataongezewa na yule asie nacho atanyang'anywa hata kile kidogo alichonacho."Napo hapo nadiriki kabisa kusema kuwa kuna utumwa wa mchana mweupe katika maeneo mengi tu ya huko nyumbani.Angalia asilimia kubwa ya dada zetu baamedi wanaolipwa shs 30,000 kwa mwezi (ataishi vipi huyu kama "asipowachangamkia wateja"),wengi wa mahauziboi na mahauzigeli (wanaonyimwa sio tu haki yao ya kipato halali bali pengine hata uhuru wa kuingia sebuleni kwa tajiri au kuwasha redio au runinga),nenda "uhundini" uone jinsi wahindi wengi wanavyowadhalilisha wengi wa wafanyakazi wao (ambao kimsingi ndio wenyeji wao-wazawa)...huu ni utumwa m-baya zaidi kuliko huo mie na Braza Kitururu tulioufuata kwa hiari yetu kwenye nchi za watu.
Ni rahisi kuhitimisha kuwa Watanzania wanapenda sana kukaa vijiweni na kusahau kuwa mashirika waliyokuwa wakiyategemea kwa ajira yameuzwa kwa "wawekezaji",mazao yao kwenye vyama vya ushirika yanaendelea kukopwa kila mwaka huku yakiwaneemesha mafisadi wa co-ops,wamachinga wanaojiajiri wanamegeuzwa na askari wa jiji kuwa kama wako kwenye mgogoro wa Wapalestina na Wayahudi,respectively,mabilioni ya JK "kuleta maisha bora" yameishia mifukoni mwa wajanja (isomeke mafisadi,nk,nk....na wakikaa vijiweni kupoteza maumivu ya kufanywa watumwa ndani ya nchi yao wanaitwa wavivu.Tuwatendee haki,tafadhali
Samahani kama kuna niliemkwaza katika maoni yangu.
March 24, 2009 1:34 AM
Mbele said...
Ndugu Evarist, shukrani kwa mchango wako, ambao naona umetoa mwanga kwenye vipengele vipya katika suala linalojadiliwa. Kwa upande wangu, naafiki kauli yako kuwa tunapaswa kufafanua ni akina nani tunaowaongelea tunaposema Watanzania wanapenda vijiwe kuliko kazi. Hoja yako hii naiona muhimu.
March 24, 2009 4:52 AM
kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...
asante sana ndugu evarist kwa hoja yenye mifano hai na inayoelimisha. ndio maana nakaongelea hawa jamaa na kuseam wako utumwani. ni utumwa wa kiakili kwa kuwa wao wamezoea kila siku kuambiwa kuwa ni wazembe na kutumikishwa kama farasi, basi wakija nyumbani nao wanataka wawe kama mabosi wao wa halifanyi kazi hili liafrika!
natokea vijijini na hali za wazee wetu kuchwazika nazijua vizuri. yaani asilimia 80 ya watanzania kila siku wako mashambani, akina Mbele (eti ni professa, uprof. gani huo usiowezesha kuona hali halisi) wanakuja na kusema kila jitu ni livivu hapa na yanasingizia mishahala haitoshi!!!
yaani vitu vingine vinashangaza ehe? jamaa wamejaa negatives tupu wakija kwa watanzania wenzao. narudia utumwa wa akili kama watumikishwao akina mbele na yasinta, ni mbaya sana kwakweli!
evarist umenihakikishia kwamba kumbe kuna wasomi wanaofikiria na vizuri ba labda wanaweza kuleta mabadiliko. nilidhani kwamba natofautina na wengi kwa sababu ya kujikita katika maarifa ya utambuzi kumbe sivyo.
kwa kweli nilikuwa na mtizamo hasi kuhusu kusoma zaidi kwani kila niliposhauliwa kurui shule, niliona kama nikujipoteza na kupotoka kwani wasomi wengi wanafikiria ndani ya vijisanduku vya walimu wao tu na kukuza ego, kumbe sio.
bwaya, ulitaka niseme kile nilichotaka kukisema kwa njia inayonipendez mimi msemaji au wewe?
March 24, 2009 10:16 AM
Mbele said...
Ndugu Kamala, kwa vile unaongea kwa kujiamini sana, kwamba watu kama mimi tuna mawazo ya kitumwa na tumewekewa mipaka ya kufikiri, naomba kukueleza kuwa nimeandika vitabu, ambavyo baadhi vinapatikana hapa hapa Dar es Salaam. Kama ingewezekana ukavisoma, ungepata ushahidi zaidi wa utumwa wa mawazo yangu. Lakini kwa sasa, kwa vile tuko kwenye maandishi ya blogu, naomba tu unisaidie kwa kuichambua makala yangu hii hapa.
March 24, 2009 4:17 PM
Bwaya said...
Naam, mchango wa Evarist umeleta changamoto nzuri.
Evarist pamoja na uwezo mkubwa wa kujenga hoja, amefanikiwa kuchagua kwa makini kila neno alilolitumia. Si tu kufikisha ujumbe ulioukusudia, bali pia kumpata msomaji wake. Hili liwe somo la bure kwetu sote.
Kama alivyosema, watanzania walio ughaibuni wana fursa nzuri ya kuchangia mawazo yao katika masuala yanayoihusu nchi yetu. Na wanapofanya hivyo, hatutatenda haki kuwaona kama watu 'wanaotusanifu'.
Tusiruhusu mawazo mazuri kufunikwa na suala la ukazi, na kuwaona kama watu 'wanaotuchora' tu kwa kile wanachosema.
Mimi siamini kwamba mtu anaweza kuwa mvivu wa kufikiri kwa sababu tu hajasema ninachokijua. Nikifanya hivyo nitakuwa ninajijengea uzio wa kutokujifunza zaidi.
Utumwa hauna mahali. Wa ughaibuni anaweza kuwa huru kuliko sisi tulio nyumbani tunaoweza kuwa tunaogelea kwenye utumwa mbaya sana kuliko huo tunaouhisi huko nje.
Bado naamini kuwa wa-tanzania wengi (sio wote), hatufanyi kazi kwa bidii. Well, inawezekana pakawepo sababu nyingi kama alizoziainisha Evarist, lakini ukweli unaonekana. Sasa tufanyeje tuondokane na hali hii, huo ni mjadala unaojitegemea. Na mchango wa Evarist unatusaidia kupanua mjadala.
March 24, 2009 5:16 PM
Prof. Ngugi wa Thiong'o alishaandika kitabu a.k.a hadithi iitwayo 'Ngaahika nd'eenda' (kwa kikuyu) ambayo baadaye allitafsiri kwa kimombo akaipa taito 'I will marry when I want'.
ReplyDeleteKutokana na hilo hapo juu mie huwa nachukia sana kuchaguliwa kitu na nshasema sitachaguliwa mke wala rafiki wa kuteta naye.
@Yasinta: imekuwaje umenichagulia mada bora ya mwaka bila kunishirikisha miye msomaji wako...? lol
Ama una mawazo kama ya che-nkapa kuwa waTZ wengi tuna uvivu wa KUFIKIRI?...lol
Anyway, kwa kuwa umitunyima fursa ya kuchagua basi...ama kwa hakika mjadala ulikuwa mkali kweli kweli. niliutazamaaaaaaaa nkanywea ili nione uwelekeo na nkafurahi kuona kuna baadhi ya watu walikuwa na mtizamo kama wangu na walileta mawazo ambayo yali-balance story nkawa sina la kuweka hapo.
tunatumai mwaka ujao ambapo miye ntakuwa nagombea kuwa fisadi niingie mjengoni kule idodomia kutakuwa na mijadala mingi motomoto itakayonisaidia kuleta changamoto mjengoni...lol
Chacahaaaaaaaaaaaaaaaaa. we ni mkuray kweli kweli
ReplyDeleteila huu mjadala ulikuwa mkali kweli kweli na mimi nilisema ngoja tuone itakuwaje, ulinitoa jasho mpaka koero akanipigia simu na kuipa pole na kutaka niombe radhi!! nikamwabia ashindwe, ntaombaje radhi wakati naisema kwweli? akawa mpole.
kaluse akasema nashambuliwa kama kibaka, nikaisimamia kweli
Dada Yasinta kweli wewe ni mbunifu, kumbe ulikaa na kupitia mada za mwaka mzima ulizowahi kuiweka katika blog ya MAISHA na kupata mada hii ambayo umeiona kuwa imevunja rekodi kwa mwaka huu.
ReplyDeleteNi kweli nakubaliana na wewe Mwanawane, hii mada ilikuwa ni kiboko, kwani ilimtoa jasho rafiki yangu na mpenzi wangu wa zamani japo kaoa hivi karibuni KAMALA OMWAMI LUTATINISIBWA……..LOL
Hii mada ilimletea KAMALA kizungumkuti cha nguvu mpaka akanyanyua mikono juu na kusema…….MAIWEEE……LOL.
Anya way naomba niseme tu kwamba hii mada ilileta changamoto na ilinifanya nijifunze mambo mengi sana….keep it up my sister.
Kusema kweli dada Yasinta mada zako nyingi unazoweka hapa zinafikirisha na zinaleta changamoto sana na naamini wengi wanajifunza kupitia kibaraza hiki ukiwepo wewe mwenyewe, kwani kupitia maoni ya wasomaji kuna mengi umejifunza..
Naomba nikubaliane na wewe kuwa hii mada ilivunja rekodi kwa mwaka huu wa 2009.
Kamala hii mada inakukumbusha maumivu ya kushambuliwa, dada Yasinta Nimekukubali wewe ni mbunifu kama alivyosema Da’ Koero.
ReplyDeleteHaka kamjadala mie niliishiwa na maneno nikabaki kuangalia mpambano, natamani huu mpambano urudiwe maana nimesoma mwanzo mwisho sijaona kupatikana mshindi.
Hili lilikuwa ni bonge la mpambano mpaka nikasema duh! Kaaaazi kweli kweli.
Nami napenda kukiri kuwa hii mada ilivunja rekodi kwa mwaka huu.
koero mpenzi wangu..................
ReplyDeletezamani hiyo iko wapi tena?
@Kamala & Koero: kale ka wimbo ka yule mkurya Jide kanasemaje? ati 'natamani niwe malaika...natamani niwe kama ntoto!!!' Je Koero, ungetamani iwe kama zamani japo kawowa?....lol
ReplyDeletena hapo sasa utakuwa nani..hawara, nke, kimada, serengeti girl ama shuga mami?...lol
Maweeeeeee,! Zamani zamani zamani, old is gold.!
ReplyDeleteHongera Da Yasinta..Mada na majadiliano yaliupamba mwaka 2009!
ReplyDeleteKamala Zamani ishaota mbawa, maana mjanja kaniwahi kwa kuwa mie nishazeeka.
ReplyDeletelakini kumbuka uzee dawa......LOL
Mmmh!
ReplyDeleteMada poa sana,tunamshukuru Kamala kwa ujasiri wake...bila kutuanzisha na maoni yake makala ya Prof. Mbele yangepita hivi hivi bila kuzaa matunda hayo sote tuliyoyaenjoy.
ReplyDeleteDada Yasinta, nimefurahi kuona taarifa yako kuwa makala yangu ndio iliyotingisha zaidi ukumbi wa "Maisha" mwaka 2009.
ReplyDeleteTuna wajibu wa kuchemsha bongo zetu, na changamoto kama hizi ni muhimu. Muhimu pia ni kulumbana kwa hoja, kwa lengo la kuelimishana. Binafsi naanzisha au kushiriki kasheshe hizi kwa lengo hilo.
Ni ajabu kuwa umeleta taarifa leo, ambapo leo hii nimechapisha kitabu kiitwacho "CHANGAMOTO."
Sawa na hii makala yangu, nategemea hiki kitabu nacho kitaleta songombingo la aina yake. Bofya hapa.
LIONE HATA AIBU HALINA!!!!!
ReplyDeleteMJADALA UNAhamu HUU
Mimi nakutakia heri ya mwaka mpya 2010
ReplyDeleteheri ya mwaka mpya mwee!
ReplyDeleteHabari zenu. Ilikuwa ngumu sana kwangu wakati mpenzi wangu aliniacha kwa mwanamke mwingine. Niliharibiwa kihisia, nilivunjika moyo na sikujua la kufanya ili kumrudisha. Nilihangaika kwa miezi mingi na niliendelea kutafuta msaada kutoka kila mahali hadi nilipopata kujua kuhusu DR DAWN. Niliwasiliana naye na kumweleza shida zangu. Alikuwa tayari kunisaidia na kunisisitiza nifuate taratibu ili aweze kurejesha penzi kati yangu na mtu wangu na pia kuhakikisha tunarudiana wote wawili. Nilipata mahitaji yote na ilifanya kazi hiyo. Baada ya saa 48, nilipata ujumbe kutoka kwa mpenzi wangu akiniuliza tarehe. Sasa tuko pamoja tena na shukrani zote kwa DR DAWN. Anaweza kukusaidia kumrudisha mpenzi wako,
ReplyDeleteAnaweza kukusaidia na uchawi wa ujauzito,
Anaweza kukusaidia kuponya aina yoyote ya ugonjwa.
ikiwa uko tayari kuamini na kubaki na matumaini. Watumie barua pepe tu kupitia: dawnacuna314@gmail.com
WhatsApp: +2349046229159