Friday, December 18, 2009

BINTI YULE AKANILETEA KIDAMISI

Nimetumiwa barua hii ya kusikitisha na nimeona ni vema niwashirikishe na wenzangu. Haya karibuni kuisoma,


Kwa dada yangu Yasinta Ngonyani, mimi ni msomaji wa blog yako wa siku nyingi na nimekuwa nikijifunza mambo mengi sana katika blog yako hii ya maisha hususan juu ya maswala ya ndoa na mahusiano. Nimekuwa nikijifunza mambo mengi sana juu ya maisha na mambo ya kifamilia na malezi kwa watoto. Nakupongeza sana kwa hilo.

Dada dhumuni la kukuandikia email hii ni kutaka kufikisha dukuduku langu juu ya mkasa ulionipata hivi karibuni. Naomba nikupe ruksa ukipenda uweke email hii hapo kibarazani kwako ili watu wengine watoe maoni yao au wapate kujifunza katika uzoefu wangu huu.

Mimi ni mvulana ambaye nitatimiza miaka 30 hapo mwakani 2010, Januari. Nilioa mwaka jana na mke wangu ndio amejifungua hivi karibuni mtoto wa kiume, kwa hiyo sasa hivi naitwa baba Gabriel au ukipenda baba Gabby.

Dada Mkasa wenyewe uko hivi, mimi naishi maeneo ya Kijitonyama hapa jijini Dar na ninafanaya kazi katika kampuni moja binafsi inayojishughulisha na uuzaji wa vifaa vya teknolojia nikiwa kama meneja masoko na mke wangu ni mtumishi wa mojawapo ya benki zinazomilikiwa na wawekezaji hapa nchini.

Kabla mke wangu hajachukua likizo ya kujifungua, nilikuwa na mazoea ya kumpeleka kazini kwake, na ndipo niende kazini kwangu na jioni nilikuwa na kawaida ya kumfuata na kurudi naye nyumbani.

Alipochukua likizo nilikuwa naenda kazini peke yangu, lakini siku moja nilikuwa nimechelewa kwenda kazini kwa kuwa nilikuwa namhudumia mke wangu kwa sababu alikuwa anajisikia vibaya siku hiyo. Nilipofika maeneo ya kituo cha Sayansi kwa wale wanaoishi Dar wanapafahamu mahali hapo, niliwaona wanafunzi wawili wakisukumwa na kondakta wa daladala ili wasipande, kulikuwa na foleni na nililiona lile tukio vizuri sana.

Adha ya usafiri kwa wanafunzi hapa jijini Dar ni tatizo sugu, na afadhali watoto wa kiume wanaweza kugombea hadi wakapanda, tofauti na watoto wa kike hawajazoea mikiki mikiki, ya makondakta wa daladala. Nilishikwa na huruma na ilikuwa ni dhahiri kuwa wale mabinti walikuwa wamechelewa shule. Nilipaki gari langu pembeni na kuwaita wale mabinti. Awali hawakuniona, badala yake akaja binti mmoja mtanashati hivi, nilimuomba aniitie wale wanafunzi ili niwasaidie kwa kuwa wamechelewa shule, ni kweli aliwaita lakini alitumia nafasi ile kuniomba lifti na yeye nimsogeze mjini maana amechelewa kazini, nilisita, lakini nilimkubalia.

Wale mabinti ambao waliniambia wanasoma Shule ya sekondari Kisutu, niliwaambia kuwa nitawasogeza mpaka maeneo ya akiba walifurahi kwa ule msaada wangu. Njiani yule binti aliyeomba lifti aliaanzisha mazungumzo, na ilionekana alitaka kunifahamu zaidi lakini nilikuwa namjibu kwa mkato tu kwa kuwa siku udadisi wake.

Aliniambia kuwa anafanya kazi kampuni moja ya mawasiliano (Jina kapuni) na alitaka kujua kama huwa napita njia ile kila siku nilimjibu kuwa ile ndio njia yangu, alitumia nafasi hiyo kuniomba niwe namsaidia kwa kumpa lifti kwa kuwa usafiri ni mgumu kweli na hawezi kugombea daladala, nilimwambia kuw akama nikimkuta njiani nitampa lifti. Tulipofika mjini nilimshusha pamoja na wale wanafunzi nami nikaenda kazini kwangu.

Siku zikapita na nikasahau kabisa habari ile, lakini siku mmoja nikiwa njiani kuelekea kazini nilikuta foleni maeneo ya kituo cha Sayansi mara nilisikia mtu akigonga kioo cha dirisha nilipotazaa nilimuona yule binti wa lifti, nilifungua kioo na kumuuliza kama anashida gani, aliniomba lifti tena, nilimfungulia mlango akaingia ndani ya gari.

Aliniambia kuwa nimekuwa nikimpita kila siku pale kituoni na hata akinisimamisha nakuwa simuoni, nilimjibu tu kuwa sikuwahi kumuona, aliniomba namba ya simu, nikamwambia sina simu, lakini alionesha msisitizo na alidai kuwa haiwezekani nimiliki gari zuri vile halafu niwe sina simu, nilimpa namba yangu ya simu.

Nilimshusha pale Posta mpya kisha nikaelekea kazini. Mke wangu alipojifungua niliomba ruksa ya kumhudumia na nikapewa siku tatu. Siku ya pili yule binti alinipigia simu majira ya usiku akitaka kujua kama nipo maana hakuniona siku hiyo. Nilimjibu kwa kifupi kuwa sitakwenda na nilimuonya kuwa asije akanipigia tena simu usiku.

Siku mbili baadae nikiwa naelekea kazini alinipigia simu akitaka kujua kama naenda kazini, nilimjibu kuwa niko njiani, na kweli nilimkuta njiani na nikampa lifti, safari hii
Alianza kunikalia mikao ya ajabu ajabu huku akipandisha mini skirt yake kiasi cha kuacha mapaja yake wazi, nilijitahidi sana kutomwangalia lakini alikuwa akinisemesha kiasi kwamba kuna wakati nililazimika kumwangalia.

Alikuwa akinidadisi sana juu ya mke wangu na akitaka kujua mengi kuhusu sisi, sikumpa ushirikiano sana nililazimika kumdanganya mambo mengi kwani huyu binti alikuwa ni mgeni kwangu na nilikuwa nampa msaada tu lakini sasa nilianza kujuta kumfahamu.

Nililazimika kubadili njia kuanzia siku ile nikawa napita barabara ya shekilango ili nitokee magomeni na kisha mjini kwa kutumia Morogoro Road, kwa hiyo nikawa nimeepusha shari. Kumbe kulikuwa kuna bomu linakuja.

Wiki moja baadae tangu nimkwepe yule binti, nikiwa nyumbani mke wangu alikuwa akitumia simu yangu, kutuma meseji kwa rafiki zake kwani yakwake iliisha credit.

Kumbe yule binti alituma meseji akiniuliza mbona sionekani siku hizi, mke wangu alijifanya ni mimi na kanza kuchat naye, yule binti alituma meseji nyingi za kimapenzi huku akimponda mke wangu na kuniahidi kunipa penzi ambalo kamwe sijawahi kulipata.

Muda wote mke wangu alipokuwa akichati na huyo hayawani mimi nilikuwa nimeweka uzingativu kwenye luninga, na ili kuwa na ushahidi zile meseji zote zilizotoka kwa huyo binti alizi forward kwenye simu yake, kisha akanipa simu yangu na kuniambia nisome meseji za mpenzi wangu kisha akaingia chumbani kulala, awali sikumwelewa lakini niliposoma zile meseji, nilipatwa na mshituko, na nikajua kuwa leo patachimbika, nilikwenda kumwamsha mke wangu ili nimweleze ukweli lakini hakukubali alikataa na alikuwa akilia sana. Nilijitahidi sana kujieleza lakini haikusaidia kitu, nilijaribu kumpigia simu yule binti lakini simu yake ilizimwa.


Nilijikuta nikiwa na wakati mgumu sana na hatukulala usiku ule kutokana na malumbano kati yangu na mke wangu. Asubuhi niliamka na kumuaga mke wangu kuwa naenda kazini lakini hakunijibu. Niliondoka nikiwa nimechnganyikiwa.

Nilipofika kazini nilimpigia simu yule binti na alipoipokea simu yangu alinishambulia kwa matusi eti nimkanye mke wangu asithubutu kumpigia simu na kumweleza upumbavu na tena amkome na kam akiendelea atamfanyizia alijue jiji, alipomaliza kusema hivyo alinikatia simu. Nilishikwa na butwaa.

Niliporudi nyumbani nilimkuta mke wangu kafura kwa hasira, kumbe mke wangu alimpigia simu yule binti ili kutaka kujua ukweli kama ana mahusiano na mimi, yule binti alimshambilia mke wangu kwa maneno makali na kunisingizia kuwa eti mimi ndiye niliyemtaka na huwa nampa lifti kila siku kumpeleka kazini na kumrudisha na nilimuahidi kuwa nitamuao.

Nilimpigia simu yule binti ili athibitishe maneno yake lakini simu yake haikupatikana. Nilijitahidi sana kumwelewesha mke wangu na kumweleza ukweli wote bila kumficha. Kidogo amenielewa, lakini amepunguza sana mapenzi na mimi, kwani amekuwa tofauti sana na mwanzo.

Baada ya kuvutana sana na mke wangu alinitaka twende tukapime ili niisije nikawa nimeambukizwa Ukimwi na huyo mwanamke na baada ya kuonekana hana, mke wangua akaniambia kuwa hatashiriki na mimi tendo la ndoa mpaka nikae miezi mitatu kwa ajili ya kupimwa kwa mara ya pili ili kudhibitisha kama sijaambukizwa Ukimwi.( Kwa mujibu wa wataalamu kwa kawaida ukimwi hauwezi kuonekana kama maambukizi ni ya hivi karibuni, wataalamu wanadai mpaka ipite miezi mitatu baada ya maambukizi ndio vipimo vinaweza kuthibitisha kama umeathirika,) sijui hili lina ukweli kiasi gani.

Tulikuwa tumejiandaa kwa ujio wa mtoto wetu wa kwanza lakini sijui hayawani yule alitokea wapi na sasa kanitibulia kila kitu, na kuiacha ndoa yangu ikiwa katika hati hati.

Kwa sasa natumia muda mwingi kuwepo nyumbani kila nitokapo kazini na niwapo off, ili niwe karibu na mke wangu na mtoto wetu mpendwa.Gabriel. Nimeweka gari yangu vioo vya Tinted ili kuepuka kidamisi kingine.

22 comments:

  1. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!December 18, 2009 at 6:41 PM

    Da Koero alinionya kuwa vijibinti vya dar vina-emcheku wanaume....duh! Kumbe kweli!


    Kaka...Baba Gabby, hauko peke yako yashawakuta wengi tu hivyo hayo ni mapito tu yataisha...almuradi roho yako nyeupe ila kama ulitaka kumega duh!

    nadhani kwa mtizamo wangu hakukuwa na haja ya kuweka tinted ...lol

    ReplyDelete
  2. Kitururu upo hapo? Vipi ingekukuta wewe ungefanyaje?

    Baba Gabby kwa kweli pole, hapo inabidi usali tu maana duuh! hata kama ingekuwa ni wewe nadhani ungeamini mkeo kapata mwingine.

    Hata mimi nadhani hakukuwa na haja ya tinted. Next time ukikutana naye mpe sura ya kazi atakuheshimu.

    ReplyDelete
  3. ninajitahidi kujiridhisha kuwa anayosema Baba Gabby ni kweli. Binti atoe wapi huo ujasiri wa kubishana na wife wa mtu. Kama hakuna kitu kilichokuwa kinaendelea basi alionyesha dalali za wazi za kumtaka huyu binti. KWA UMRI WANGU WA MIONGO MITATU NA USHEE, hapa inakuwa ngumu kukubaliana na wewe. ILA NAMSIFU SANA WIFE WA MSHIKAJI, LAZIMA NI KICHWA SANA(BUSARA NA UELEWA) na sio mbinafisi maamuzi yake pia aliangalia familia yake haswa mtoto

    ReplyDelete
  4. Kosa ulilifanya pale ulipompa namba yako ya simu huyo binti, hapo umebomoa uaminifu uliojijengea kwa mkeo kwa muda mrefu na yeye anaamini kwamba mimba ndio imesababisha wewe ukatoka nje ya ndoa na kumsaliti.
    Huwezi kumbadili mawazo mkeo kwa mara moja tu, ila tabia uliyoanzisha ya kutumia muda mwingi kuwa karibu naye pamoja na mtoto vina mfariji sana, ukiendelea hivyo baada ya muda atakusamehe moja kwa moja

    ReplyDelete
  5. Objection, Objection, Objection kwa kaka Godwin......

    Nakupinga kwa asilimia mia moja, mkuu, labda kama huishi katika jiji hili, la Dar, lakini kama unaishi hapa Dar , basi utakuwa unaishi aidha kazimzumbwi au Kilapalang'anda huko Mkuranga.

    kaka Godwin Jiji la Dar haliko hivyo, siku hizi mabinti huwapapatikia wanaume wenye usafiri ili maisha yawe mepesi kwao, hivi ni nani asiyejua hali ya usafiri wa hili jiji la Dar jinsi ulivyo mgumu,ni nani asiyejua kuwa mabinti wa siku hizi hawapendi shida ya kugombea usafiri wa daldala ambao watu hukanyagana na kupumuliana visogoni.
    Unatoka nyumbani umejipamba kwa vipodozi makini, kuanzia mavazi, lipstik, pafyumn na vikorokoro vingine, halafu unafika mjini au kazini hutamaniki na unanuka samaki kutokana na kubanana na wachuuzi wa samaki, ni binti gani ataipenda hali hiyo.

    kama unaishi dar nunua gari uone utashangaa unapendwa na usiowafahamu na hata ukitoa msaada hata kwa nia nzuri utashangaa unakaribishwa mpaka chumbani, na kama wewe ni dhaifu, utawapanga foleni ile mbaya lakini na wewe kaburi la mapema litakungoja.

    Mabinti wa siku hizi wanadai kuwa ili mambo yako yawe mazuri, ni lazima uwe na bwana mwenye gari, bwana wa kukununulia Vocha na wa kutoka naye out kwa ajili ya kujirusha.

    Kama huamini fanya utafiti....

    Mimi naamini kuwa baba Gabby alisababishiwa na hiyo ni baada ya kuonyesha kutotaka kujiingiza katika mtego wa huyo binti.
    Mimi namsifu sana kwa ujasiri wake, na pia nampongeza mkewe kwa ukomavu, ila nampa ushauri wa bure kuwa hao watu wapo amuombe mungu amuepushe mumewe na tamaa.

    ReplyDelete
  6. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!December 19, 2009 at 9:18 AM

    @Baba Gabby, unaweza ku-bar ama kuiweka nambari yake katika rejected number ktk simu yako ili akikukong'oli haiwezi kuingia tena kwani hakuna haja ya kubadili namba kwani huo utakuwa uwoga usokuwa na msingi...lol

    @Mama Gabby: anaweza kumfanya huyo binti akawa 'rafiki' yake iwapo atampigia tena. Hapa haina maana ya kukutana naye isipokuwa ku-respond kwa kila ujumbe ama simu ya huyo mbinti. Hiyo itamsaidia ku-heal mapema. Alione tukio hilo kama lililopita. I know at the bottom of her heart anamuamini mumewe Ba-Gabby sipokuwa hili lilotokea limevuruga mambo. so take it easy Mamie just for Gabby's sake.

    ReplyDelete
  7. Nakubaliana na kaka Godwini.

    Huyu binti alipata ujasiri wa kubishana na wife baada ya wife kuchati naye ktk simu binti akidhani anachati na baba gabby. Kumbuka lazima wife alikuwa akichati akijidai anampenda na hicho ndo kilichompa binti yule kiburi hadi kumtukana wife.

    Mimi naona mama Gabby hapo alikosea. Angechati naye akijifanya yuko upande wa mkewe hapo mama gabby angepata ukweli maana yule binti kama kweli walishawahi kuwa pamoja lazima angekuja juu kwa baba gabby ambaye yeye ndo anadhani anachati naye.

    Sijui kama nimeeleweka vizuri..

    ReplyDelete
  8. Da’ Mija nadhani umesoma filosofi, maana kwa jinsi nilivyoisoma hii stori, ni kama mama Gabby alikuwa akilitengeneza bomu yeye mwenyewe.
    Huyu binti alikuwa mtega ulimbo na lengo lake lilikuwa ni kumnasa baba Gabby, kumbuka kwamba alianza kwa kumkalia mikao ya ajabu ajabu ndani ya gari lakini pia akitaka kujua maisha ya ndoa ya baba Gabby na mkewe, yote ilikuwa ni kutaka kuchimba ili apate mahali pa kuanzia…na kwa kawaida wanaume wenye uchu wa mabinti huwa ni rahisi sana kunaswa na mitego kama hiyo.
    Haijulikani kama yule binti alituma meseji ya namna gani kwa baba Gabby na haijulikani mama Gabby alianzisha vipi mjadala.m Ila kama atakuwa aliendeleza kile alichoanzisha yule binti inawezekana kuwa ilikuwa ni rahisi yule binti kuchangamkia bahati ile, na ikumbukwe pia kwamba alikuwa akiisubiri kwa hamu baba Gaaby aanze tu yeye amalizie.

    Kama Da’ Mija alivyosema kuwa, kama angesimama upande wa mkewe yaani kama mama Gabby alivyojifanya kuwa ni baba Gabby basi na meseji zake angezifanya ziwe za kuonyesha kumpenda mkewe na kumsifia, na hapo angeujua ukweli, maana kama kungekuwa na kitu kilichojificha kati yao kingejulikana tu.

    Napenda kuchukua nafasi hii kuwashauri wanandoa hao kuwa na moyo wa subira na kuaminiana, wasiingize negatives na kutuhumiana katika maisha yao ya ndoa, kwani hiyo ni sumu kali itakayoivuruga ndoa yao, wakati ndoa yao bado ni changa sana.

    Lakini lazima tukubaliane kuwa wakati mwingine matukio ya namna hiyo huja makusudi ili kuleta fundisho fulani katika ndoa, kwani hakuna tukio baya bali ubaya upo katika tafsiri zetu. Kama mama Gabby angemuuliza mumewe juu ya ile meseji naamini haya tunayojadli leo hapa yasingetokea. Lakini huenda pia limetokea ili wao na sisi tunaosoma hapa tujifunze pia kutokana na uzoefu wao.

    Jamani nisifungue darasa la utambuzi, ngoja niishie hapa ili niwapishe na wengine waje watoe maoni yao

    ReplyDelete
  9. Da Koero, Naona kwa hili tukubaliane kutokukubaliana. Inawezekana mkasa huu wa baba Gaby tumeungalia katika mitazamo miwili Tofauti.

    Nikiri mimi nina udhaifu wa kupenda kuangalia kwanza FANI(wahusika, mazingira nk) kabla ya kuanza kuangalia MAUDHUI. Hi mara nyingi inanisababisha kutofautiana na watu wengi kimtazamo.

    Kutokana na maelezo ya Baba, Gabby Mrembo huyu atakuwa anaishi mitaa ya makumbusho au Kijitonyama na anafanya kazi kwenye kampuni moja ya simu. KWA MAZINGIRA HAYO NAMTOA KWENYE KUNDI LA WASICHANA WENGI WA USWAHILI WASIO NA AIBU/UOGA WA ELIMU. Mimi naona kabisa mzee mzima baada ya kufanyiwa mambo ya MWANAMEKA(kumbuka wimbo wa mwanameka) Uzalendo ukamshinda mzee mzima. Baada ya kuharibu akataka kumkacha demu kiaina asiharibu ndoa yake.

    MARA NYINGI MADEMU WA MJINI UKIWAFANYIA HIVI LAZIMA WATALIPA KISASI.(huu ni mtazamo wangu). Ni bora kukubaliana kabla na baada ya... Ninauhakika hata namba ya simu baba Gaby ndio aliomba baada ya kulainika kwa kuona mikao ya kimtego mtego.(unacheza na Delila)

    WEWE UMEZUNGUMZIA UPANDE MMOJA, WANAWAKE WA DAR WA SIKU HIZI. VIPI ULISHAFANYA UTAFITI UKAONA NA WANAUME WA DAR WALIO KATIKA NDOA WA SIKU HIZI. Naamini ukiwa kama msichana tayari umewaona. Lazima wengi wameshakupigia " EE MCHEKUU" nyingi. KUNA MAKALA MOJA NILISOMA, SIKUMBUKI WAPI. "Inasadikika wanaume wengi wakware ni wazuri sana kuonyesha MALAVIDAVE kwa wake zao. na ni wepesi kuomba msamaha kwa gharama yeyote"

    Huyu baba Gaby ingekuwa ni mtu wa kutoa misaada kwa wanafunzi, angekuwa anatoa hata wakati yupo na mawaifu wake. Gafla tu kaanza kutoa huo ushirikiano wakati waifi amejifungua. HAPO SIJASEMA LIFTI KWA WATOTO WA KIKE TENA WA SEKONDARI WALA SI WA MSINGI WANAOHITAJI ZAIDI HUO MSAADA. Nina ushaidi mwingi wa mazingira unaosababisha nimshtukie huyu Kidume.

    NIHITIMISHE
    KIKUBWA DA KOERO HAKUNA UHUSIANO WOWOTE USIOKUWA NA SABABU. NDOA KARIBIA ZOTE(KAMA SI ZOTE) WAMEJIFUNGA KILA MMOJA AKIWA NA INTEREST FULANI KWA MWENZAKE. Kwa hiyo siwashangai hao mabinti wa Kisasa. Usafiri ndio sababu yao

    ReplyDelete
  10. Godwin...aisee maoni yako yamenifanya nitamani yule binti naye angeleta maelezo yake hapa ili tupate picha kutoka pande zote.

    ReplyDelete
  11. Da Mija hapo umesema. Si vizuri kuhukumu kwa kusikiliza upande mmoja.

    ReplyDelete
  12. Kaka Edwin naomba nikunukuu: "KWA MAZINGIRA HAYO NAMTOA KWENYE KUNDI LA WASICHANA WENGI WA USWAHILI WASIO NA AIBU/UOGA WA ELIMU" mwisho wa kunukuu.

    Naona sasa umekosa hoja ya kutetea hoja yako...hivi mpaka leo bado uanaamini kuwa wasichana wa uswahilini kwa kuwa hawana elimu ndio wasiojiheshimu!

    Kaka fanya utafiti, hivi hujui kuwa wasichan wanaosoma hasa vyuo vikuu ndio wasiojiheshimu kuliko wa uswahilini, hebu nebda pale Hosteli ya Mabibo au kule Kijitonyama, ukienda kwenye kumbi za starehe wanaoongoza kwa kujiuza ni hawa wasomi tunaowatarajia wawe wataalamu wetu kesho katika kulijenga taifa letu hili, japo naamini sio wote.

    Kaka swala la kuishi Masaki, Mikocheni au Mbezi Beach, hali Justfy kuwa na ustaarabu katu, mie naishi huko na ninafahamu ninachokiongea.

    lakini hebu turudi katika hoja ya msingi maana naona kuna kila daliliya Edwin kutaka kukandamiza baba Gabby, hivi unauhakika gani kama alijimegea kwa huyo binti?

    Labda tumuombe Da Yasinta amuombe mtuma habari atuletee maelezo ya mama Gabby ili tu balance hii stori na sio kupiga blah blah hapa!!!!!!

    ReplyDelete
  13. Napenda kuwashukuru wasomaji wote kwa changamoto zenu.Da Koero anasema nimenukuu"Labda tumuombe Da Yasinta amuombe mtuma habari atuletee maelezo ya mama Gabby ili tu balance hii stori na sio kupiga blah blah hapa!!!!!!"mwisho wa kunukuu. Nimefanya hivyo nimemtumia email mtoa habari na sasa nasubiri majibu. Ahsanteni.

    ReplyDelete
  14. hata kama nimechlewa, hata kama nipo nyuma kqwa wakti huu, bado nasema baba Gabby ni DHAIFU NA MZEMBE NAMBA MOJA ANAYESTAHILI KUADHIBIWA.

    KWANINI ALIKATAA KUTOA NAMBA ZA SIMU KWA KUSEMA HANA SIMU HALAFU AKATOA NAMBA HIZO? UJINGA MTUPU!

    UZEMBE UZEMBE SANA HUU, HALAFU UTAUIFITI MNAOZUNGUMZIA HAPA KWA MBWEMBWE NI UPI? WA DAR NA KUHITIMISHA TANZANIA KWA UTAFITI WA DAR?

    TOKA ZENU HAPA! BABA GABBY SIKUUNGI MKONO HATA KAMA NINAORODHA YA MADEMU WA AINA HIYO. MPEWA LIFT ANAFUNGULIWA MALNGO WA NYUMA KAKA, USINIDANGANYE SITAKI VISNGIZIO HAPA.......

    tena bora angekupatia adhabu kama Bill Clinton miezi 6 hakuna kuona uvunguni.....

    ReplyDelete
  15. Markus unajua baba Gabby analo gari la aina gani, kumbuka katika maelezo yake hakusema analo gari gani.
    Je kama ni Pick Up je binti mrembo atakaa nyuma kweli?

    na wewe acha hizo, baba Gabby ana hikima nandio maana ametuletea hii mada tupate kujifunza, yuel binti alishindwa kumshawishi baba Gabby na ndio maana akaona amuharibie.

    tafuta hoja nyingine Markus hiyo umechemsha.....

    ReplyDelete
  16. Da Koero, kwanza kabisa naomba unitake radhi kwa kukosea jina langu. Mi naitwa GODWIN. na si EDWIN.(joke)

    Sijasema kuwa wanawake wa masaki na maeneo ya aina hiyo na waliosoma wanaustaarabu zaidi kuliko wa Uswahili. "ILA NIMESEMA KIDOGO WANA AIBU YA ELIMU". PIA NIMETUMIA NENO "WENGI" SIJATUMIA "WOTE" Kwa maelezo yako, wewe umeishi/unaishi maeneo hayo. Ya huku kwetu uswahili unahadidhia tu au unaona kwa kupita tu.

    Labda nikujulishe kuwa mimi nimeishi maeneo yote(UZUNGUNI na USWAHILI) kwa nyakati tofauti. Na niliishi pia Hostel za Mabibo kwa miaka miwili.

    Nimekuwa na mahusiano na wasichana wa pande zote mbili kwa nyakati tofauti. Kwa hiyo ninachokizungumza ni vitu nilivyoviona/ninavyoviona na ninavyoishi navyo.

    Labda nisubiri kwanza hiyo barua ya huyo Dada. WASIWASI WANGU NI KAMA KWELI HIYO BARUA ITATOKA KWA HUYO DADA KIUKWELIUKWELI. Nasema hivi kwa sababu barua hii imetoka kwa Baba Gabby, Na email aliyonayo dada Yasinta ni ya mtu aliyemtumia hichi kisa(NI WAZI NI BABA GABBY)

    Ninawasiwasi mkubwa kama huyu binti atatendewa haki. Labda tupate namba ya huyu binti toka kwa Baba Gabby, halafu upate maelezo toka kwake moja kwa moja(SIJUI KAMA MMENISOMA). Hapa naomba da Koero asishirikishwe. Nasema hivi kwa sababu nimemuona wazi ameegemea upande mmoja.

    ReplyDelete
  17. Da Koero baba Gabby ndugu yako nini?..(Natania jamani)

    ReplyDelete
  18. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!December 22, 2009 at 12:34 PM

    @Da Mija:labda alishampa 'emcheku' naye akaikubali....lol

    bado tunaisubiri hiyo majibu ya huyo mkaka ili mjadala uwendelee

    kaazi kwelikweli!!!!

    ReplyDelete
  19. Koero dadangu, nadhani unaelewa mazingira aliyosema baba Gabby, ni wazi gari yajke. Sawa nikubali kuwa anayo POick UP, halafu jiulize kwali unaweza kubabaika na mapaja jamani? najua ni mda tamu sana, lakini katika aina ya uandishi huo ninaweza kubashiri jambo(tuache hilo).

    Koero, tuache utani kiasi hivi kweli kweli kweli kweli kabisaa useme huna simu halafu baadaye unatoa? Unajua baba Gabby angeliweza kabisa kuepusha hilo. Inatosha kusema kuwa hata simu ingeliita, ni laziam aseme HAPANA. au labda hii ni STORI YA KUTUNGA? lol;;;;;;;;;;;;

    ReplyDelete
  20. I'm really enjoying the theme/design of your blog. Do you ever run into any web browser compatibility problems? A handful of my blog audience have complained about my website not working correctly in Explorer but looks great in Chrome. Do you have any recommendations to help fix this issue?

    my site; diets that work fast
    Also see my page > diet plans that work

    ReplyDelete
  21. I am regular reader, how are you everybody? This article posted at this website is truly fastidious.


    Here is my website: melissanichols423.blog.com

    ReplyDelete
  22. Woah this weblοg is magnificent i lοve studуing yοur articles.
    Keeρ up the gгeat work! You recognize, lots of persons aгe loοκing
    round for this infο, you can aіd them grеatlу.


    My pagе :: free Microsoft points codes.how to get Free microsoft points codes

    ReplyDelete