Kuna mambo mengi katika maisha ambayo kama wanaadamu tunakuwa tumeyapitia, hayo yote ndio huyafanya maisha haya tunayoishi yawe na maana. Miongoni mwa mambo au masaibu tuliyokutana nayo yapo ya kufurahisha na ya kuhuzunisha na mengine yenye kukera na kutia kinyaa, lakini yote ni maisha na yalikuwa ni lazima yatokee ili kujifunza jambo fulani.
Lakini hata hivyo si rahisi kusahau kila jambo ulilokumbana nalo katika maisha hasa kama lilikuwa ni la kuumiza kihisia, lakini kuna wengine wanasahau upesi na wengine si rahisi kusahau. Kwa mfano kwa upande wangu mimi kuna jambo moja, ambalo mimi SITALISAHAU. Nakumbuka nilikuwa na miaka 10 wakati huo. Baba na mama walikwenda hospital Litembo iliyoko katika wilaya ya Mbinga, mkoani Songea. Mimi na kaka zangu tulibaki kwa baba mkubwa.
Huyu baba mkubwa alikuwa na watoto wa kike 6 na mwanae mkubwa wa kike aliitwa Maria. Siku moja jumapili Nilimwomba dada Maria kanga kwani mimi nilikuwa sina, lakini hakunipa ALININYIMA na kuniuliza kwa nini baba yangu ambaye ni mwalimu asininnunulie. Kwani wakati ule nilikuwa mtoto wa kike peke yangu. Nayeye katika hali ya kinisimanga aliniambia "wewe uko peke yako mtoto wa kike inakuwaje wazazi wako wanashindwa hata kukununulia kanga" .(Mwana mdala nga veve vishindwa kukugulila nyula). Aliongea kwa Kingoni. Siku ile nililia sana, mpaka sasa nalikumbuka vizuri tukio lile na mpaka leo roho inaniuma sana kila nikikumbuka maneno yale.
Sikujua kama binadamu wanaweza kuwa wakatili kiasi hiki, na hasa ukizingatia yeye alikuwa dada yangu. Naomba nikiri kuwa tangu tangu siku ile sijawahi kuwasiliana naye, ingawa sina ukakika kama atakuwa analikumbuka tukio hilo. Kwani waswahili wanasema mtendaji hakumbuki ila mtendewa ndiye anayekumbuka.
Mimi kama walivyo binadamu wengine ninao udhaifu wangu, na udhaifu huo si mwingine bali ni kutomudu kufanya kazi ngumu tangu utototni mwangu. Nakumbuka nilipokuwa mdogo kule kingoli maisha yalikuwa magumu sana kwangu, kwani kulima mpunga na pia karanga na mihogo ilikuwa ni shughuli ambayo ilikuwa inanipa shida sana, ilikuwa kila tukienda shambani, mimi nilikuwa wa mwisho kumaliza ngwe yangu kule shambani.
Mazao ambayo tulikuwa tunalima sana ni karanga na mpunga tangu asubuhi mpaka mchana. Halafu kule kingoli tulikuwa tunakula sana ugali wa muhogo na kwa kuwa sisi tulihamia kule, tulikuwa hatuna shamba la mihogo. Kwa maana hiyo ilibidi tununue, ndugu yangu huko tulikokuwa tukinunulia hiyo mihogo kulikuwa ni mbali, yaani tunatembea mpaka miguu inauma. Tulikuwa tunachimba, kumenya kabisa ili uzito upungue.
Baada ya hapo tunarudi na mzigo kichwani na jua linawakia utosini. tukifika nyumbani na kutua mzigo, kuna kazi ya kuandaa chakula cha mchana. Tukishamaliza kula tunapumzika kidogo kisha tunaanza kazi ya kuchotelea maji ya kulowekea ile mihogo. Kwani kulikuwa hakuna maji ya bomba, tulikuwa tunachota kisimani. Jamani kweli maisha ni safari ndefu.
Kusema kweli kila nikikumbuka maisha niliyopitia kule kijijini kwetu, kuna wakati ninalia na kuna wakati huwa ninacheka sana. Kwa simulizi hii sio kwamba nilikuwa namlaumu dada yangu mkubwa kwa kitendo chake cha kunisimangia kanga yake, kwani ilikuwa ni hiyari yake kunipa au kutonipa, kilichoniuma ni yale masimango, hata hivyo simlaumu kwani kuna jambo nilijifunza, kutokana na kitendo chake kile.
Kama kuna mtu yeyote ambaye ataumizwa na simulizi hii basi anisamehe, kwani sio nia yangu kumuumiza mtu bali nilitaka kusimulia uzoefu wangu juu ya maisha haya tunayoishi, kwamba, kumfanyia mtu wema ni sawa na kuweka akiba ambayo inakufaa kesho..
Pole sana da Yasinta. Wengi katika safari za maisha tumekutana na ndugu na jamaa ambao walionesha dhahiri chembe za kutotuthamini katika namna moja ama nyingine.
ReplyDeleteTena wengine leo pengine sisi nd'o tumekuwa msaada kwao.
Lakini hatupaswi kuyahesabu hayo yote. Mungu ndiye apangaye kila jambo katika maisha ya mwanadamu.
Mi naomba Mungu awasamehe kwani hawakuwa wakiyajua wayatendayo.
Ni vitu vingi sana katika maisha ambavyo vinaumiza roho kwakweli, Pole kwa yaliyokutokea. Hakuna kitu kibaya kama masimango kweli kama ulivyosema, bora mtu akupe or akunyime kuliko kukusimanga,inauma sana.Nakutakia kila la kheri.
ReplyDeletepole kwa kovu hilo dada yangu, na hongera kwa kuwa wasema ulijifunza jambo, kama nipendavyo kuwaambia watu KAZA BUTI TWENDE bado life has so many in store for us, be blessed.
ReplyDeleteLeo hii ukikutana na huyu dada kwa namna ya upendo atayokupokea nayo utashangaa mwenyewe na bila shaka atakuona wewe ni wa dhamani ajabu.
ReplyDeleteKumtendea binadamu mwenzio wema ni kuweka akiba.
ReplyDeleteUkweli ni kwamba sisi wote hapa duniani tunajua tulipotoka lakini hatujui tunapokwenda. Ingawa simulizi hii umesema ni uzoefu wako juu ya maisha, lakini inatufaa, wote tuliopata wasaa wa kupitia maandishi haya kuanza kujiuliza, ni mara ngapi tumewatendea binaadamu wenzetu wema? au ni mara ngapi tumewahi kuwaumiza wenzetu kihisia? Naamini iwapo tutatafakari kwa kina kuna jambo tutaligundua juu ya mahusiano yetu na binaadamu wenzetu.
Hili ni darasa zuri sana ambalo dada yetu Yasinta katupa bure kabisa......
Ni vyema tukatumia nafasi hii wakati bado tunaitumia pumzi hii ya bure ya mwenyezi mungu kujikagua na kuonesha uadilifu kwa wenzetu.
Si hivyo tu, hata viongozi wetu na wanasiasa, nao yawapasa kujiuliza, Je ni kwa kiasi gani maamuzi na kauli zao zinawaumiza wananchi wanaowaongoza? Je tuwakumbuke kwa lipi baada ya kustaafu? Ni vyema nao wajue kwamba maisha tunayoishi ni mafupi sana, kujilimbikizia ukwasi huku jamii inayokuzunguka ikiwa katika lindi la umasikini, hilo sio jambo la kujivunia, ni kutafuta laana ya mwenyezi Mungu, na mara nyingi malipo yake ni hapa hapa duniani......
Naomba nisiseme sana nikamaliza hoja zangu kwani leo nina mazungumzo na rais kupitia kipindi maalum.....
Pole sana Yasinta katika maisha mengi tunapitia,umenikumbusha mbali sana,hata mimi kuna kitu sitakuja kukisahau,ktk maisha jamani usimtendee mtu ubaya.
ReplyDeleteMimi kuna kitu kilinitokea sintakuja kukisahau,nilikuwa likizo tumefunga shule Tabora,kuna binamu yangu alikuwa anafanya kazi Shinyanga,mimihuyo safari Shinyanga nakumbuka kipindi hicho usafiri ulikuwa wa shida sana kipindi cha mvua,niliwahi mapema lakini basi likuwa limejaa sikupata siti,lakini niliambiwa nitapata mbele ya safari,bwana we!nilisimama mwendo wa masaa 3nikajisikia kuchoka,pembeni upande wa siti za watu 3 kulikuwa na mama mmoja na mtoto kama miaka 2/3 amekaa katikati upande wa dirishani mama yake mwisho alikuwa kaka mmoja.Basi nikamuomba yule mama mwenye mtoto nimpakate ili ni angalau nikae kidogo!jibu nililopata,SIKUTAKA APAKATWE NDIO MAANA NIKAMKATIA TICKET,KWANZA NAKUJUAJE MPAKA UMPAKATE MWANANGU?yaani ilikuwa ile ya jeuri hasa.
Basi bwana nikaendelea kusimama mpaka tulipofika karibu na Nzega,kaka mmoja upande wa pili siti za watu 2 akaniambia njokaa ukae hapa dada ngoja na mimi nisimame,nilimshukuru sana,kwani hata tulichukua muda!tukafika Nzega hapo ndipo utamu ulianza,kumbe yule mama jamaa aliekaa nae pale ni mwizi bwana,kufika Nzega katelemka kwenda kununulia mtoto chakula na kumpeleka kujisaidia,yule jamaa kumbe anampiga chabo tu,alipo ona mama kaishia kwenye kimgahawa akabeba mabegi yake 2 na box lilikuwa chini ya kiti,akatokomea zake utazani ilikuwa ni mizigo yake na mimi nilikuwa namuona anavyo shusha ile mizigo,nilizani ni yake kumbe ya mwenzanke.baada kama ya dk.20 watu wanaanza kurudi kwenye basi yule mama nae karudi kufika haoni cha mabegi yake wala kuina chini kucheki box nalo limechukuliwa,haaaaa palikuwa patamu hapo! hana mtu wa kumuuliza wengi walishuka ni mimi ndio nilikuwa karibu yake,akaniuliza eti yule kaka alikuwa hapa yuko wapi?mimi kimya! akaniuliza tena ulimuona kashusha mabegi yaliyokuwa hapa? mimi kimya!aliangua kilio utazani kafiwa na baba yake au mama yake mzazi,kumbe kwenye begi kulikuwa na kila kitu,na mbaya zaidi kumbe anakokwenda na mimi ndio nakokwenda, basi lilifika Shinyanga saa 2 usiku na yeye alikuwa uso umevimba kwa kulia,tumeshuka mimi nikamkuta binamu yangu ananisubiri akachukua taxi tukaondoka mpaka nyumbani kwake,nikamsimulia yaliyonikuta,tumeingia tu ndani baada kama ya nusu saa na yule dada anaingia na mwanae mikono mitupu,kumbe katembea toka stend ya mabasi mpaka nyumbani,nilipomuambia binamu yangu yule dada ndio huyu!alishangaa sana kumbe yule anae share nyumba na binamu yangu ni mdogo wake huyo mama nae alikuwa amekwenda tu kumtembelea anaishi Kigoma.UNGEKUWA WEWE UNGEFANYAJE?
Mmmh! Asante sana ndugu zangu kwa kuniliwaza. Mnajua hili jambo niwe wazi zaidi, ni kwamba tangu kipindi kile nimekuwa nafikiria ni vipi nimsamehe huyu dada lakini kila nikijaribu nashindwa kabisa. Hii ndio saabu ya kuliweka hapa ili nipate msaada wenu. Na nashukuru nadhani maoni yenu yatanisaidia na siku nitayomwona nitamsijitahidi kumweleza na kuona kama anakumbuka na ndipo nitamsamehe. Au sijui niache tu nisaidieni jamni sijui la kufanya.
ReplyDelete