Thursday, July 16, 2009

UTALII SASA KUVUMA RUVUMA

Nafikiri wote mnajua kuwa mimi ni mtu wa kutoka kijiji cha Litumbandyosi.


WanaMbinga kuonyesha njia

Vivutio vya Kusini kutangazwa


WILAYA ya Mbinga, chini ya usimamizi wa Halmashauri yake, mkoani Ruvuma, imedhamiria kufungua mianya ya kitalii kwa kuanza na uhifadhi wa pori la akiba la wanyama la Liparamba lenye wanyama na ndege wa aina mbalimbali, imefahamika.

Pori hilo la Liparamba ni msitu mnene wenye maji yanayotiririka na linaweza kutajwa kuwa kati ya hifadhi chache zenye vivutio vya kipekee.

Pori hilo litaendelezwa na kutunzwa ili wanyama na ndege wengi waweze kuzaliana na hatimaye vijiji vinavyolizunguka vianze kufaidika na hifadhi hiyo.

Wakati Wilaya hiyo imefanikiwa kuanzisha pori la akiba la wanyama Liparamba, wananchi wa vijiji vya Litumbandyosi, Paradiso, Luhagara, Ruanda, Mtunduwalo na Ndongosi wilayani humo nao kwa kauli moja wameridhia pori la Litumbandyosi linalozunguka vijiji hivyo kuwa hifadhi ya wanyama .

Halimashauri hiyo imependekeza kutenga pori la akiba la Litumbandyosi wilayani humo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 320 kwa ajili ya hifadhi ya wanyama pori baada ya kuwashirikisha wananchi wanaozunguka vijiji vya hifadhi hiyo.

Vijiji hivyo viliridhia mpango huo tangu mwaka 2003, na kisha Serikali iliweka mipaka ya kutenga eneo hilo na maeneo ya wananchi.

Kijiji cha mwisho, cha Kingole, ambacho kilikuwa hakijatoa ridhaa ya kukubali pori hilo kuwa hifadhi, hatimaye nacho kiliridhia nia hiyo Novemba 2008.

Akizungumzia hatua hiyo hivi karibuni, Kamanda wa Kikosi cha kuzuia ujangili Kanda ya Kusini, Metson Mwakanyamale aliwasisitiza wananchi wanaozunguka vijiji hivyo kuwalinda wanyama waliopo katika hifadhi na kuhamasisha utalii katika Mikoa ya Kusini.

Mwakanyamale anasema utalii si kuona wanyamapori pekee bali ni pamoja na shughuli za kiasili na kipekee zinazofanywa katika maeneo yao pamoja na kuweka mazingira ya utalii endelevu.

Anasema kwa kuridhia mchakato wa hifadhi ya pori hilo sasa wananchi wataweza kupata maendeleo ya haraka kama wawekezaji watafika kuwekeza.

“ Sasa mtaingizwa katika uhifadhi shirikishi katika mamlaka zilizoundwa na Serikali za Vijiji za kuhifadhi wanyama, mtapangiwa wanyama wa kuwinda kwa kuwa ni haki yenu na ndiyo moja ya faida ya sekta ya utalii,” alisisitiza .

Aliongeza: “Utalii hauzungumzii jambo moja tu la kuangalia wanyama, bali pia ni pamoja na kusafiri kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine pamoja na kuona shughuli zinazofanywa na watu katika maeneo husika.”

Katika kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa endelevu katika kanda ya kusini na hasa mkoani Ruvuma, Kamanda Mwakanyamale anasema amefanya mazungumzo na Ofisa Elimu wa Mkoa wa Ruvuma kuhusu mikakati ya sera ya idara ya wanyamapori kuhusu utalii Kusini mwa Tanzania .

Anasema chini ya sera hiyo kuna utalii wa kuangalia wanyama bure unaofanyika katika hifadhi ndogo ya wanyama ya Luhira iliyopo Manispaa ya Songea.

Kulingana na Mwakanyamale, utalii huo wa bure katika hifadhi hiyo unaanza mwezi huu hadi mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka huu ambapo wameagizwa maofisa elimu katika wilaya zote mkoani Ruvuma kuhakikisha kuwa wanafunzi wanakwenda katika hifadhi hiyo ili kuwaona wanyama bure.

“Licha ya burudani hiyo ya kuwaona wanyama bure pia wanafunzi na watu wengine watakaokwenda kutembelea hifadhi hiyo watapa elimu ya biolojia na ekolojia kuhusu utalii, lengo likiwa ni kuamsha utalii wa ndani kuanzia mtoto wa shule ya awali, msingi na sekondari.” Anasema.

Meneja Mkuu wa mradi wa pori la akiba la wanyama Liparamba, Mbinga, ambaye pia anasimamia hifadhi ya Litumbandyosi, Hashim Sariko anasema ya kuwa eneo hilo linafaa kuwa hifadhi ya wanyama kwa kuwa lina wanyama na ndege wa aina mbalimbali.

Anawataja wanyama waliomo katika pori hilo kuwa ni viboko, nyati, parahala, nyani, nguruwe pori, chui, pofu, swala, tembo, faru na aina mbalimbali za ndege wakiwamo kware, kanga na njiwa.

Sariko anasema kuwa eneo hilo lipo katika ukanda wa uhamiaji wa wanyama kutoka Hifadhi ya wanyama ya Selous ambako kuna wanyama wengi na kwamba wanyama hao wamekuwa wakiingia katika pori la Litumbandyosi kupitia ushoroba uliopo katika maeneo ya Lutukira, Hanga Gumbiro na Ngadinda wilayani Songea.

Anaongeza kuwa hifadhi tarajiwa hiyo pia ilipata kuwa kitalu cha uwindaji ambacho kilimilikiwa na kampuni ya Miombo Safari Hunting ambayo ilianza kuimarisha ulinzi na uendelezaji wa pori hilo ikiwa ni pamoja na kutengeza barabara, madaraja na camp site moja kabla ya kuacha kuendeleza pori hilo baada ya wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo kushindwa kutoa ushirikiano na kampuni hiyo na kusababisha wanyama kutoweka.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, malengo makubwa ya Serikali katika sekta ya utalii sasa ni kujaribu kupanua wigo wa utalii Kusini mwa Tanzania kwa kutambua vivutio vya utalii vilivyopo Kusini na kuviuza nje ya nchi ili wananchi waweze kunufaika navyo.

“Pori la wanyama Liparamba tayari limeendelezwa na watu wanaweza kwenda kutembelea na kuangalia madhari ya msitu mnene na namna maji yanavyotiririka kutoka milimani na kuingia katika mto Ruvuma, wanaweza kuangalia ndege na wanyama waliopo katika pori hilo,” anasema na kuongeza:

“Ni sehemu chache sana za hifadhi za wanyama hivi sasa ulimwenguni zinazofanana na uzuri wa pori la Liparamba, vivutio hivyo ndivyo ninavyouzwa sasa nje ya nchi na hapa Litumbandyosi baada ya kukamilisha mipaka ya hifadhi itanibidi nikae chini na kuangalia ni kitu gani kitawavutia wageni katika hifadhi hii na hasa wanyama.

Sariko anasema watalii wanaoingia nchini itabidi waje Kusini baada ya milango ya utalii kufunguliwa badala ya kwenda kaskazini pekee wakati Kusini kuna vivutio vingi vipya vya utalii ambavyo havijatangazwa.

“Lengo ni pamoja na kuboresha maisha ya wananchi wanaozunguka katika vijiji hivyo yawe bora kwa kutumia hifadhi ya wanyama ya Litumbandyosi baada ya mchakato wa kuifanya kuwa hifadhi ya wanyama pori kukamilika,” anasisitiza.

Anabainisha kuwa barabara za lami kutoka Masasi hadi Mbambabay zinatarajiwa kujengwa hivyo ni vema kujiandaa na watalii mbalimbali ambao wataingia Kusini kwa kuvitambua vivutio vya utalii na kuvitangaza sanjari na kusomesha vijana kozi mbalimbali za utalii.

Hii habari nimeipata kutoka raimwema http://www.raiamwema.co.tz


2 comments:

  1. Hii ni hatua kubwa sana kwa sisi wanamazingira na hawa wawindaji haramu wakome kuingia humo

    ReplyDelete
  2. Habari nzuri hii.

    Nami nitajitahidi kwa sisi tunaotoka kwenye visiwa vya ziwa Victoria tuanze kupigia debe vivutio vilivyoko huko, ila hatutaki mgogoro kama wa Migingo

    ReplyDelete