Nimelipenda shairi hili na nimepewa idhini toka kwa aliyeandika Kaka Fadhy Mtanga kuwa niliweka hapa kwangu.
Nashika kalamu yangu, salamu nazituma,
Kwenu marafiki zangu, natumai mu wazima,
Nawaombea kwa Mungu, mjaliwe yalo mema,
Salamu wanablog.
Simon Kitururu, huzamia MAWAZONI,
Fikra zake ni huru, pia zina burudani,
Nasi tunamshukuru, hachoki tangu zamani,
Salamu wanablog.
Yupo dadetu Yasinta, yeye hupenda MAISHA,
Kamwe hawezi kusita, mazuri kutuonesha,
Sifa tele azipata, maana huelimisha,
Salamu wanablog.
Christian Bwaya yupo, hutaka tuJIELEWE,
Daima aandikapo, vichwa vyetu tusuguwe,
Ukweli daima upo, muhimu ujadiliwe,
Salamu wanablog.
Mubelwa Bandio pia, MZEE WA CHANGAMOTO,
Haishi kutuambia, mambo yalo motomoto,
Muziki hutupatia, yenye midundo mizito,
Salamu wanablog.
Subi dada yetu sote, wa NUKTA SABA SABA,
Ili mengi tuyapate, blog yake yashiba,
Asichoke asisite, ajaze hata kibaba,
Salamu wanablog.
Chib naye ni rafiki, hutumia HADUBINI,
Kazi yake haichoki, popote ulimwenguni,
Magharibi mashariki, hutujuza kulikoni,
Salamu wanablog.
MWANAMALENGA Kissima, hutuonesha MWANGAZA,
Makala zenye hekima, na mambo kuyachunguza,
Kwa ushairi ni vema, tungo zake zapendeza,
Salamu wanablog.
Serina Serina huyo, ana UPANDE MWINGINE,
Yale ayaandikayo, hupendwa nao wengine,
Kwa mawazo si mchoyo, hufanya tushikamane,
Salamu wanablog.
Koero Mkundi pia, hutuambia VUKANI,
Hachoki kutuletea, yatokeayo nchini,
Daima hukumbushia, tutoke usingizini,
Salamu wanablog.
Ndugu yetu Mumyhery, kabobea kwa MAVAZI,
Vitu vyake ni vizuri, hilo mbona lipo wazi,
Yupo kwenye mstari, hachoki kufanya kazi,
Salamu wanablog.
Kamala tunamjua, wa nyegerage KIJIWENI,
Fikra apambanua, ili tutoke kizani,
Sote tukajitambua, tujijue kina nani,
Salamu wanablog.
Masangu wa Nzunzullima, CHAKULA chake KITAMU,
Hatosahau daima, kutupa yote muhimu,
Ujuzi wake kisima, haisaliti elimu,
Salamu wanablog.
Markus Mpangala, KARIBUNI sana NYASA,
Yeye wala hajalala, mengi ameshayaasa,
Kabobea mijadala, ya jamii na siasa,
Salamu wanablog.
Lumadede mshairi, USHAIRI MAMBOLEO,
Mashairiye mazuri, tena yale ya kileo,
Huukuza ushairi, na kuupa mwelekeo,
Salamu wanablog.
Na MWANASOSHOLOJIA, siachi kumsifia,
Elimu kutugawia, na picha kutuwekea,
Mazuri hutuambia, ndani ya hii dunia,
Salamu wanablog.
Nami MWANANCHI MIMI, wa DIWANI YA FADHILI,
Tungo zangu siwanyimi, nawapenda kiukweli,
Tena mara kumi kumi, tena na kwa kila hali,
Salamu wanablog.
Ambao sijawataja, lipo shairi jingine,
Sote tungali pamoja, kwa mema tuombeane,
Tusichoke zetu hoja, hivyo na tushikamane,
Salamu wanablog.
Wow!! Sina ninaloweza kusema. Kaka Fadhy umedhihirisha u-Malenga wako na si kupanga vina, bali vyenye maana na ukweli.
ReplyDeleteBaraka kwako
Labda swali kwa Kaka Fadhy, hiki ni kipaji na ULIZALIWA NACHO AMA ULIRITHI?
ReplyDeleteAhsante sana da Yasinta kwa kulipenda shairi hili. Hakika nimejisikia furaha sana kwa rafiki zangu wanablog namna walivyolipokea.
ReplyDeleteKaka Mubelwa, niseme ahsante sana kwa baraka zako.
Kuhusu kipaji cha ushairi ni hadithi ya ajabu. Mi' mwenyewe hujiuliza sana. Ngoja nisimulie kidogo ili wewe utoe hitimisho kama ni kipaji ama urithi.
Nikiwa darasa la tatu, kulikuwa na sherehe za CCM. Mimi nilikuwa nikicheza chipukizi. Nadhani sote twakumbuka kipindi cha chama kushika hatamu! Wakati wa mazoezi ya chipukizi, nilitamani kufanya jambo ili walionizidi umri wanistaajabie. Kitu nilichokitamani, ni kuandisha shairi. Sifahamu wazo lilitoka wapi.
Nikamwendea mama yangu. Alikuwa mwalimu wa lugha shule niliyokuwa nikisoma. Nikamwambia nataka kuandika shairi. Akacheka, akaniuliza "unaweza?" nikamwambia ndiyo. Akasema andika nione.
Sikujua mambo ya vina wala mizani. Nikaandika mawazo yangu kama insha. Muda mfupi tu, nikamfuata ofisini. Nikamwonesha. Akanitazama na kuona kiu yangu. Japo halikuwa shairi bali insha, akanitazama, nakumbuka mkono wake wa kushoto (nami ni left handed) ukawa begani. Kwa upole akaniambia, "utakuwa mshairi mzuri sana mwanangu" Hadi leo kila nikimaliza kuandika shairi huikumbuka siku ile.
Akaniambia sheria za kutunga mashairi. Akanifahamisha mambo ya vina na mizani. Sikuwa na utajiri wa misamiati, mizani haikuwa shida, nikaona ugumu kwenye vina. Akaniuliza kama nimeelewa. Nilipomwambia ndiyo, akasema nikaandike tena.
Nikaandika shairi la kwanza lenye kufuata sheria. Halikuwa la CCM tena. Sasa nikaandika kuhusu klabu ya Simba. Nikataja majina ya wachezaji, kina Mwameja, Idd Mkuki, Duwa Said, Damiani Kimti, Ramadhani Lenny, George Masatu na wengine ndani ya shairi lile. Niliporudi kumwonesha, mama akasahau yupo ofisini kwa shangwe aloyoipiga. Nilipata zawadi.
Hivyo, shairi la kwanza kuliandika, lilitaja majina ya wachezaji wa Simba. Hadi leo napenda sana kuwaelezea watu kishairi.
Kaka Mubelwa, baada ya hapo sijawahi acha kuandika mashairi. Namshukuru mama kwa hilo.
Hapo kaka Mubelwa na wengine, nadhani mtanisaidia uelewa kama ni kipaji ama urithi? Mama pia alikuwa akiandika mashairi, ni miaka mingi haandiki tena. Labda umri ama ameniachia.
Ni hayo, nisamehe kwa maelezo marefu mno.
Kweli Fadhy ni malenga aliyetukuka. Hongera sana na asante kwa kuwafagilia wakuu wa Blog.Yasinta asante kwa kutuwakilishia shairi tamu
ReplyDeleteShairi zuri sana inaonyesha kuwapenda wanablog wenzako wao pia lazima wakupende, Lakini mimi ingawa umenisahau si haba.
ReplyDeleteBorn 2 Suffer sijakusahau hata nukta. Nimeandika mstari wa kwanza ubeti wa mwisho;
ReplyDelete"Ambao sijawataja, lipo shairi jingine"
Hata kichwa cha shairi;
"Salamu wanablog I"
Chaonesha ni sehemu tu ya kwanza ya salamu kwa wanablog wenzangu.
Kiukweli kuna wanablog wengi sana. Hamu yangu ni kuwapa salamu wote. Lakini ingechosha wasomaji kuandika shairi moja beti 100 ama zaidi. Nikaonelea itapendeza kidogo kidogo baada ya tungo mbili tatu. Hivyo nategemea nitakuwa na Salamu Wanablog II, III, IV na zaidi kadiri uzima utakapokuwapo.
Eee Bwana Papaa Fadhy eeh! DUH!
ReplyDeleteUtalogwa shauri yako!:-)
Kwanza napenda kumshukuru mama kwa kukupa moyo kuwa uanze kuandika mashairi.Kwa kukupa mwongozo. Bila hivyo leo hatungemfahamu Fadhy na hatungesoma mashairi yake Fadhy.
ReplyDeleteAsante kwa kuwa na moyo wa upendo, kwa kutupenda sisi wanablog wenzako. Mungu azidi kukupa nguvu ili uweze kuandika mashairi zaidi.
nimekukubali
ReplyDeleteBw Fadili Shukran sana salaam zimefika, kila la kheri
ReplyDeleteleo imeamua kutembele blog hii n nikamua kusoma baadhi ya comment za watu. nimefurahi sana kukutana na mtu ninayemfahmu. hongera kaka Fadhy. nimekumic long time kitaa Njoss.
ReplyDeletebig up mkubwa. I hop hujaacha kutumia jina la Ras Muta.