Alikuwa ni Binti wa nne kuzaliwa hapo mnamo mwaka 1967 kati ya watoto nane katika familia hiyo, akiwa ametanguliwa na kaka zake watatu. Alipofikisha umri wa kwenda shule hapo mnamo mwaka 1974 alipelekwa kusoma shule iliyopo kijiji cha jirani takribani kilomita 4 akiwaacha kaka zake wakisoma shule iliyoko umbali wa mita 200 kutoka nyumbani.
Inasemekana kuwa eti aliandikishwa kusoma katika shule hiyo ya jirani lakini kutokana na shule hiyo kupokea wanafunzi wengi kupita kiasi ndipo walipogawanywa na wengine kupelekwa kijiji cha jirani ambapo kulikuwa na nafasi.
Kulikuwa uwezekano mkubwa wa baba yake kufanya mipango ya kuhakikisha kuwa mwanae huyo hasomi mbali na nyumbani lakini hazikufanyika juhudi zozote kufanikisha jambo hilo na badala yake aliachwa na hivyo aliendelea kusoma katika shule hiyo.
Alilazimika kuamka majira ya saa kumi alfajiri kila siku akiwa na wanafunzi wenzie walitembea kilomita hizo nne kwenda na kurudi na huku wakipigwa na baridi kali na wakati mwingine kunyeshewa na mvua, lakini alivumilia na baada ya miaka saba alimaliza darasa la saba mwaka 1980.Baada ya kumaliza masomo kama ilivyokuwa kwa kaka zake hakubahatika kuendelea na masomo ya sekondari, ingawa baba yake alikuwa na uwezo wa kuwaendeleza na masomo wanae lakini hakuona umuhimu wa kufanya hivyo ingawa yeye alisoma mpaka darasa la nane la mkoloni na kuajiriwa serikalini kama karani katika chama cha ushirika wilayani.
Mnamo mwaka 1981 kaka yake binamu ambaye alilelewa na wazazi wake na ambaye alikuwa ni dereva alimchukua na kumpeleka Moshi kwa madai kwamba amemtafutia chuo cha kujifunza mambo ya Typing.
Alipofika huko alifikia kwa mama mmoja wa kisomali ambaye alikuwa na familia ya watoto nane, watano wa kike na wakiume watatu. Cha kushangaza alijikuta akiamshwa asubuhi na mapema na mama huyo na kukabidhiwa furushi la nguo akafue. Binti wa watu akatahamaki, kulikoni apewe kazi ya kufua wakati alikuwa ameahidiwa kusomeshwa mambo ya Typing? Yule mama kama vile alikuwa akisoma mawazo yake akamwambia kuwa yeye pale ni House Girl, na akapewa ratiba ya siku nzima. Alikuwa akiamka alfajiri saa kumi na kuanza usafi wa nyumba akimaliza apike chai ya watu wote kisha achukue nguo za familia nzima kuzifua, akimaliza anaosha vyombo vilivyotumika kwa chai ya asubuhi, kisha anaenda sokoni na kadhalika na kadhalika ilimradi ilikuwa ni kazi mtindo mmoja.
Alikuwa akitukananwa na kudhalilishwa kama vile hakuwa na wazazi, lakini alivumilai kwa kuwa hakuwa na pa kwenda.
Hakuwahi kumuona yule kaka yake binamu kuja kumjulia hali wala nini alijikuta akiwa ametelekezwa ugenini asijue kwa kukimbilia.
Baada ya miezi mitatu ya mateso bila malipo ndipo siku moja akakutana na mjomba wake ambaye alikuwa ni mfayabiashara maeneo ya sokoni, walisalimiana lakini mjomba wake alimshangaa kutokana na kumuona akiwa amekonda sana, alimuuliza sababu ya kukonda kiasi kile na alitaka kujua anaishi pale Moshi na nani?
Yule binti alisimulia mateso anayoyapata na kutokana jinsi alivyokuwa amekonda mjomba wake hakuvumilia alilia sana na pale pale alikata tiketi ya basi na kusafiria naye hadi kijijini kwao ambapo alimlaumu sana dada yake kwa kitendo chake cha kumtoa mwanae na kumpeleka kufanya kazi za ndani na kuteseka kiasi kile, mama wa yule binti alishangaa sana kwani yule binamu yake aliyemchukua alikuwa kila akipita pale kijjini na gari alikuwa anatoa salamu kutoka kwa huyo binti kuwa ni mzima na anaendelea na masomo vizuri.
Mama wa binti yule alilia sana kwa uchungu, ingawa baba wa binti hakuonekana kujali sana, kwani wakikutana na huyo binamu aliyemchukua huyo binti hununuliwa pombe kwa hiyo hakuonekana kujali wala kumlaumu binamu kwa kitendo chake cha kikatili.
Binamu alipofika moshi aliambiwa kuwa binti ametotoka na ameiba nguo na pesa kiasi cha shilingi elfu ishirini, miaka hiyo ya themanini elfu ishirini ilikuwa ni kiasi kikubwa cha pesa, kumbe ilikuwa ni uongo kwani binti alikuwa ametumwa sokoni na alipewa shilingi hamsini za kununua mahitaji fedha ambazo hata hivyo alizisalimisha kwa mama yake mara alipofika tu.
Siku iliyofuata binamu alifika na kudai kuwa binti ni mwizi na kamfedhehesha sana, mama wa binti alimkata kalima, na kumuuliza sababu ya kumpeleka binti yake kuwa mtumishi wa ndani wakati alimuahidi kuwa atamsomesha Typing?Alimkabidhi ile shilingi hamsini na kumuambia aipeleke kwa msomali wake.
Kumbe huo ndio ulikuwa mwanzo wa mateso ya binti huyu.
Mwishoni mwa 1981 alichukuliwa na mama yake mdogo waliyechangia baba na mama yake na kupelekwa Dar kwa ahadi ya kusomeshwa, alipofika jiji Dar alijikuta akiwa ni muhudumu wa kuku wa mayai, kwani huyo mama yake mdogo alikuwa ni mfugaji wa kuku.
Mnamo August 16,1982, binti huyu alipata pigo la mwaka baada ya kupata taarifa za kufariki kwa mama yake ghafla kwa ugonjwa wa moyo.Ilimlazimu kurudi kijijini haraka ili kuhudhuria mazishi ya mama yake, ingawa hata hivyo alichelewa.
Baada ya mazishi Binti yule alimueleza baba yake kuwa alipokuwa Dar hakuwa akisoma kama alivyoahidiwa, safari hii tena akachukuliwa na mama yake mdogo tumbo moja na mama yake na kupelekwa Arusha alipokuwa akiishi huyo mama yake mdogo ili akasomee hayo mambo ya Typing, na alipofika kule kweli alijiunga na chuo cha kusomea typing, lakini mama yake mdogo alikuwa ni mkorofi kweli kwani ilikuwa kila akichelewa kidogo tu alikuwa akipigwa sana kwa madai kwamba alikuwa kwa wanaume, na pia alikuwa akitumikishwa kufanya kazi za hapo nyumbani kupita kiasi.Yule mama alikuwa na mradi wake wa mambo ya ususi, wakati huo kulikuwa hakuna mambo ya saloon. Kwa hiyo akimaliza kazi za nyumbani alikuwa anamsaidia mama yake huyo kazi zake za ususi.
Mateso yalipozidi ilibidi atoroke na na kurudi kijijini. Baada ya kutoonekana kwa siku mbili mama yake mdogo alisafiri hadi kijijini na kumkuta binti akiwa nyumbani kwao ametulia.
Baada ya mashauriano ikaamuliwa binti abaki pale kijijini.Miezi kadhaa baadae binti akapata mchumba, akalipiwa na mahari, haikuchukua muda hata kabla ya kufunga ndoa binti akapata ujauzito, na hivyo ndoa ikaahirishwa mpaka baadae atakapojifungua.
Baada ya miezi tisa binti alijifungua mtoto wa kiume, jambo ambalo lilifurahiwa na pande zote mbili. Hata hivyo swala la kufungwa kwa ndoa likawa linapigwa danadana hatimaye kijana muoaji akatoa taarifa kuwa haoi tena.Kisa, yalipenyezwa maneno ya fitna na baadhi ya ndugu ili kuvunja ule uchumba, mpaka leo sababu haijulikani.
Mnamo mwaka 1985 binti akalazimika kwenda Dar kwa kaka yake mkubwa ambaye alikuwa ni mtumishi serikalini ili kutafutiwa shughuli ya kufanya.Alipofika akatafutiwa kazi na kaka yake na hivyo kumudu kujitegemea kwa muda mfupi.
Mnamo mwaka 1990 akapata mchumba mwenyeji wa Singida ambaye alikuwa ameachana na mkewe na hivyo kuanza maisha mapya akiwa na mumewe huyo bila ya kufunga ndoa.Maisha hayakuwa mazuri sana kwani bwana huyo alikuwa na wivu sana, kwani alikuwa hataki kumuona akiongea na mwanaume yeyote, na ikitokea amemkuta na mwanaume ni lazima kutatokea ugomvi mkubwa ajabu.
Maisha na bwana yule hayakuwa mazuri sana, kwani kila siku hali ilizidi kuwa mbaya na kibaya zaidi ni pale yule bwana alipoachishwa kazi. Ilibidi binti aanzishe biashara ili kumudu kujikimu, lakini bwana yule wivu ulimzidi, kila akiongea na mteja ni bwana ake.
Binti yakamshinda, mnamo mwaka 1993 mwishoni akaondoka na kurudi kwa kaka yake akiacha vitu vyake vyote kwa yule bwana, kwani yule bwana ndiye aliyehamia kwa binti lakini alizuia vitu vyote kwa madai kuwa ni vya kwake.
Baadae binti akjikuta ni mjamzito, lakini hakutaka kumwambia yule bwana ingawa alikuwa na uhakika kuwa ule ujauzito ni wa yule bwana.Mwanzoni mwa mwaka 1994 binti aliamua kurudi kijijini kwao, wakati huo ujauzito wake ulikuwa na miezi mitano.
Ujauzito ulipofikisha miezi sita binti yule alipotea akawa hajulikani alipo. Ndugu zake walifanya juhudi kumtafuta bila mafanikio, lakini baada ya siku mbili alirudi mwenyewe akiwa amechoka sana, lakini alikuwa kama amechanganyikiwa, alipopelekwa hospitalini hakuonekana kuwa na ugonjwa wowote na mapigo ya moyo ya kiumbe kilichokuwa tumboni yalikuwa yanaenda vizuri.
Ilibidi awekwe chini ya uangalizi wa bibi yake mzaa mama kwani ilihofiwa kuwa angetoroka tena na kupotelea porini.Mwezi mmoja baadae, ujauzito ulipokuwa na miezi saba, binti yule alipata kifafa cha Mimba na hatimaye roho yake ikaachana na mwili, ilikuwa ni May 12, 1994.
Huo ndio ukawa ni mwisho wa binti huyu.
Simulizi hii ni Dedication kwa binti huyu ambaye ni dada wa rafiki yangu.
Inauma, inahuzunisha,inasikitisha na inasononesha......
ReplyDeleteNimesoma habari hii nikiwa na mchanganyiko wa hisia, kwanza mwili ulikuwa ukinisisimka kila nilipokuwa nikiendelea kusoma habari hii.
inasikitisha kuona kwamba kumbe hapa duniani kuna watu ambao tangu wazaliwe wao ni taabu tu mpaka wanaingia kaburini!
Hivi maisha yana maana gani kwetu?
Tuanaishi katika ulimwengu ambao wakati wengine wakiyafurahia maisha kwa ukwasi waliojilimbikizia, kuna wengine tangu wazaliwe ni taaabu tu mpaka kufa kwao ni taabu tupu, kama jamii tunaisaidiaje jamii inayoishi katika mazingira magumu, je ni kuwachukuwa na kuwageuza watumishi wa ndani na muwatesa, kuwadhalilisha na kuwanyanyapaa huku sisi tukifurahia maisha haya mafupi ya duniani ambayo ni matupu kabisa na yasiyo na maana yoyote mbele za mungu au ni kuwasaidia nao kufikia malengo yao?
Pole sana dada kwa kuondokewa na binti mumpendaye.
Ni matarajio yangu kuwa wengi tumejifunza hapa.
Hata sijui, ila nimesoma simulizi hii kwa mchanganyiko wa hisia za huzuni na huruma.
ReplyDeleteNaweza kusema kuwa binti hakuwahi kuyafurahia maisha yake.
Tangu akiwa shule, baba yake hakumwonyesha thamani yoyote.
Maisha hayakuwa rafiki mzuri kwa binti huyo.
Ni fundisho zuri kwetu wanadamu.
Mi nadhani tunapaswa kuyajali sana maisha ya watu wengine.
Pia nitumie fursa hii kueleza simanzi yangu kwa masahibu yaliyoyaandama maisha ya binti huyo.
Nimalizie kwa kumwomba Yeye Aliye Juu, Muumba wa mbingu na nchi aiangazie roho ya binti huyo mwanga wa milele.
Amina.
Inasikitisha sana. No comment.
ReplyDeleteSina chakusema :-(
ReplyDeleteKweli inasikitisha sana ila yote ni mipango ya Mungu
ReplyDeleteNimesoma hii habari nimeumia sana,maskini huyo dada maisha yake yote aliyoyapitia hapa duniani hakuwahi kuyafurahia ni mateso na matatizo ndiyo aliyopitia inauma sana,kwa upande mwingine ni bora alivyo ondokana na mateso haya.
ReplyDeleteMungu alaze pema.
Asanteni wote kwa kutembelea blog ya maisha na kutoa maoni yenu. Ni kweli hapa dunianai kuna wengine maisha yao ni taabu tu tangu siku wanazaliwa hadi wanaingia kaburini.
ReplyDeleteNa kuna wengine ni raha tu tangu wapo tumboni mpaka wanazaliwa na mpaka wanaiacha dunia hii.