Tuesday, May 5, 2009

NGOJA LEO NIWAPELEKE NA TUANGALIE SURA YA KIJIJI CHA LIKUYU FUSI SEHEMU YA KWANZA= KUNYUMBA

Kijiji cha Likuyu Fusi ni kijiji cha asili cha muda mrefu kilichoanzishwa na kundi la Wangoni wa Luyangweni ya malawi miaka michache baada ya vita vya Majimaji. Kabla ya kuanzisha kijiji hiki wakazi wake waliishi katika eneo la kijiji cha Kilawalawa-Luyangweni ya Mpitimbi, mahali ambapo Bambo Fusi, bin Zulu alihamia na kundi lake toka Malawi.

Kijiji cha Likuyu Fusi kipo upande wa kusini wa kanisa la Misheni Peramiho, umbali wa maili tatu na kipo kusini ya mji wa Songea umbali wa maili kumi na tatu kuelekea barabara iendayo Mbambabay.

Jina la Likuyi Fusi linatokana na mti uitwao “mkuyu” ambao unapendelea kuota katika bonde la mto Likuyu. Tunda la mti huo huitwa “Likuyu” na hupendwa sana kuliwa na baadhi ya ndege. Mto Likuyu unaanzia mlima wa Liwanganjahi na kupeleka maji yake hadi mto Ruwawazi. Urefu wake ni maili nne. Kabla ya kuvuka mto huu katika barabara itokayo Songea kuelekea Mbambabay ulikuwepo mti mkubwa wa mkuyu wenye kivuli kizuri chini yake. Wasafiri wengi walizoea kupumzika na kupika chakula chao chini ya mti huo. Kituo hiki kilikuwa kikubwa na kilijulikana kwa wasafiri wengi waliokitumia. Wasafiri hao walipita mahali hapo “Likuyu” kutokana na matunda ya mti wake. Toka muda huo jina la Likuyu limeendelea kutumika hadi sasa.

Jina la Fusi ni jina la baba mzazi wa Nduna Laurent. Kwa kuwa mto wa Likuyu ulikuwepo katika eneo la utawala wake, wasafiri waliamua kuita mto huo Likuyu Fusi kutofautisha na Likuyu nyingine iliyoko katika sehemu ya Undendeule, katika wilwya ya Songea, ambayo ilitawaliwa na Nduna Sekamaganga.

Kijiji cha Likuyu Fusi kimekuwa ni makao makuu ya utawala wa Nduna Laurent Fusi. Makao haya kwanza yalikuwa kijiji cha Luyangweni ya Mpitimbi na hatimaye yalihamishiwa Likuyu miaka michache baada ya vita vya majimaji.

Utawala wa Nduna Laurent Fusi ulijumlisha wakazi wa vijiji vya asili ya Parangu, Lihongo, Likuyu, Mkurumo, Ruwawazi, Mangúa, Chimbembe, Mlahimonga, Liboma, Mbatamira, Mapera, Litapwasi, Halali Magomera, Halali Fusi, Mhangazi, Matomondo, Kikole na Kilawalawa.

Kijiji cha Likuyu Fusi kina milima miwili na yote ipo upande wa kusini ya kijiji. Mlima Livánganjali upo karibu zaidi na nyuma yake unafuata mlima wa Namakinga. Pia katika eneo la kijiji ipo mito; Lihongo, Likuyu, Litapwasi, Chimbembe, Liboma, Mhangazi, Ruwawazi na Ruvuma. Mito hiyo ina mabonde mazuri kando yake yenye maji ya kutosha kwa wakati wote wa mwaka. Ardhi yake ni kidongo chekundu katika sehemu kubwa na mabonde yake yana udongo wa aina ya mfinyanzi wenye rutuba nzuri. Vilevile vya milima vina mawe mazuri yenye kuzuia mmongónyoko wa ardhi.

Katika maeneo ya vijiji nilivyovitaja ipo miti ya aina mbalimbali, kama miyombo, misuku, miwanga na aina nyingine ya miti midogo midogo. Kwa vile maeneo haya yalikaliwa na watu kwa muda mrefu sehemu nyingi zilizolimwa zamani sasa zimeota manyasi marefu na vichaka vya miti midogo midogo. Mitelemko ya milima na kando kando ya mabonde ya mito bado kuna miti mikubwa kiasi ya aina niliyoitaja hapo juu. Kabla ya matumizi ya mbolea ya chumvichumvi kuenezwa wananchi walikuwa wanafanya kilimo cha kuhamahama wakikata “matema” kila baada ya miaka mitatu au minne. Tabia hii imesababisha kupungua kwa miti katika sehemu zote za tambarare na kuwalazimu wananchi kuanzisha mashamba mapya kwenye mitemko ya milima na hata kwenye vilele vya milima. Mabonde ya mito iliyotajwa hapo juu ina sehemu nzuri ya kilimo cha kiangazi “madimba”. Manyasi, magugu na matete na mimea ya asili ambayo sehemu nyingi hufyekwa wakati wa kiangazi ili kulima mashamba ya madimba.

Wananchi katika sehemu za vijiji nilivyovitaja hulima mahindi, maharagwe,ulezi, mtama, mihogo, viazi vitamu, viazi vikuu mpunga na aina mbali mbali za kunde, kama mbaazi, nandala, fiwi, mangatungu, pia hulima karanga, ufuta, mazomba, aina mbalimbali za matunda kama mapapai, mapera na miembe.Inaendelea........

9 comments:

  1. Ama kweli leo umeturejesha kunyumba. Si tu kwamba ukisoma unajihisi nyumbani, bali nimekumbuka mengi niliposoma hiyo aya ya mwisho kuhusu maisha yao.
    Inafurahisha saana kuona tunaweza kurejesha fikra na mitazamo nyumbani.
    Sijui na mie niandike kuhusu kwetu???? Lol.
    Asante sana Dada

    ReplyDelete
  2. Da Yasinta, wala sikuwahi kufikiri kuwa wewe ni mkali wa Historia kiasi hicho. Hakika wewe ni noma. Nimependa sana staili yako hii ya masimulizi ya asili ya kijiji hicho. Hongera sana kwa kazi nzuri sana.

    ReplyDelete
  3. Kweli nyumbani ni nyumbani tu, na mkata kwao ni mtumwa! Umedhihirisha kuwa wewe si mtumwa dadangu!

    ReplyDelete
  4. Hapa nimepata darasa muhimu sana....
    Ahsante kwa elimu ya bure..
    Nitaifanyia kazi..

    ReplyDelete
  5. Chakusikitisha ni kwamba jinsi muda unavyokwenda ndio jinsi historia za vijiji mbali mbali zitapotea.

    Nilisha wahi kumuuliza mdau kuhusu kijiji chao akanikata kauli kwa kusema '' Kamuulize Nyerere na Kawawa na aidia zao za vijiji vya ujamaa isababishayo nisijihisi kijiji changu ni changu''.

    DUH!

    Asante Yasinta kwa historia.

    ReplyDelete
  6. Hii ni historia pamoja na jografia, hongera sana na ninatumai hii kumbukumbu haitapotea kwa jinsi ulivyo isambaza na kuna wengine ambao wataitumia kwenye mambo mengine

    ReplyDelete
  7. kwa hiyo wewe ni msauz, historia imetulia ila tuwekee na tabia za watu wa huko na ambayo labda wewe umeirithi

    ReplyDelete
  8. Mlongo kulikuyu, kweli apo umenifikisha nyumbani, nimekuja kukumbuka enzi za shule mashindano ya michezo ya kata na wilaya na tunapopitia likuyu kwenda kuperamiho kweli umenikumbusha mbali na umenielimisha sana.
    kazi nnzuri mlongo wangu,

    ReplyDelete
  9. Kazi nzuri sana Yasinta, basi usione hatari kujazia hapo juu,jina la huyo mtawala, jazia lile lingine, Fusi GAMA, usione hatari

    ReplyDelete